Dubois: Wakati wangu, zama zangu!
LONDON, ENGLAND: DAKIKA 30 baada ya Daniel Dubois kumchapa Fabio Wardley ndani ya raundi zisizofika mbili wikiendi iliyopita, promota wake Frank Warren alitikisa kichwa kwa mshangao kidogo alipokuwa akielezea kiwango cha umakini wa bondia huyo kabla ya ushindi huo wa kishindo.
“Nilikwenda kwenye chumba cha kubadilishia nguo kabla ya pambano kama ninavyofanya kawaida, lakini sikuweza hata kuzungumza na Daniel kwa sababu alikuwa ameelekeza akili yake yote kwenye pambano. Hilo lilionekana alipoingia ulingoni. Aliingia akiwa na dhamira ya kumtafuta mpinzani na kumwangamiza,” alisema Warren.
Dubois alifanana na Mike Tyson enzi za ujana wake, lakini akiwa na mwili mkubwa na mzito zaidi. Akiwa amevaa kaptula nyeusi na joho jeusi, alielekea ulingoni kwa dhamira ya kumaliza mchezo mapema. Hakukuwa na dalili yoyote ya hisia usoni mwake alipokuwa akitembea kwa kasi kumfuata Wardley katika pambano lao la marudiano la ubingwa wa dunia wa WBO.
Katika pambano lao la kwanza miezi mitano iliyopita, Dubois aliangushwa mpinzani wake huyo baada ya sekunde 16 tu. Aliangushwa tena katika raundi ya tatu kabla ya kuanza kushambulia kwa kutumia ngumi zake za moja kwa moja zilizokuwa na nguvu, kisha akaendelea kumpiga Wardley aliyepambana kwa ujasiri na kukataa kusalimu amri hadi mwamuzi alipoingilia kati na kusitisha pambano katika raundi ya 11.
Wengi walikubaliana kuwa Wardley alionekana dhaifu zaidi katika pambano la marudiano na kwamba matumaini yake makubwa yalitegemea ukweli kwamba bado ana ngumi zenye nguvu, huku Dubois akijulikana kwa kuanza taratibu katika mapambano yake, lakini bingwa alikuwa amejiandaa.
HUYU HAPA
“Nilikuwa na umakini mkubwa zaidi kuliko nilivyokuwa Mei, kwa kiwango kikubwa sana. Tangu nilipovaa vifaa vyangu vya pambano, nilikuwa tayari kwa kazi. Huenda nilifanya mazoezi ya kujiandaa kabla ya pambano kwa muda mrefu zaidi kuliko kawaida, lakini pia nilijiweka kwenye hali ya ushindani haraka zaidi. Kila mtu alikuwa akisema Fabio angeanza kwa kasi, kwa hiyo nilikuwa tayari kwa hilo,” anasema Dubois
Hata hivyo, je alitarajia pambano kusitishwa kwa haraka na kwa namna ya kikatili kiasi hicho?
“Siwezi kusema nilitarajia. Nilikuwa nimejiandaa kwa vita. Sikuwa tayari kukubali kukosa ushindi. Nilikataa kushindwa,” anasema Dubois akisisitiza kuwa hakuna bondia wa uzito wa juu duniani ambaye anaweza kustahimili makonde makali aliyomshushia Wardley.
Uhakika wake unaeleweka kutokana na jinsi alivyokuwa akionekana kuwa hatari, ingawa uwezo wa Wardley wa kustahimili makonde, ambao ulijulikana sana, ulionekana kupungua.
“Fabio ana kidevu imara sana,” anasema Dubois. Na ni kweli kwamba Wardley hajawahi kuangushwa. Hata katika pambano la majuzi lililokuwa na mashambulizi makali na ya haraka, alipewa hesabu ya mwamuzi akiwa bado amesimama baada ya sekunde 17 tu, kufuatia ngumi kali ya mkono wa kulia iliyomfanya ajikunje kwenye kamba za ulingoni.
Wardley alikuwa bado amesimama, ingawa akiwa ameinama kwenye kona moja ya ulingo, wakati kocha wake Ben Davison alipoamua kutupa taulo kuashiria kusitishwa kwa pambano. Baada ya ushindi wake, Dubois alitangaza kuwa, “huu ni wakati wangu, zama zangu.”
Kwa sasa, ni mabondia watatu tu wanaoonekana kuwa na uwezo wa kutumia mwendo na ufundi wao kumzuia Dubois anapokuwa katika mashambulizi makali. Oleksandr Usyk bado ndiye bondia bora wa uzito wa juu duniani, na tayari amemshinda Dubois mara mbili. Hata hivyo, bondia huyo wa Ukraine ambaye hajawahi kushindwa anatimiza miaka 40 Januari na anataka kupigana mara moja tu zaidi nchini Marekani.
KUNA HUYU PIA
Kwa kuwa alionekana kuwa na nia ya kupambana na Deontay Wilder ambaye amepoteza makali yake, kuna uwezekano Usyk anataka pambano la mwisho lisilokuwa na ugumu mkubwa kabla ya kustaafu. Tyson Fury, ambaye anatarajiwa kumshinda Anthony Joshua, Desemba, anaweza kushawishiwa na fedha nyingi zitakazopatikana katika pambano jingine kubwa la mabondia wa Uingereza dhidi ya Dubois.
Akiwa katika ubora wake wa juu, Fury atamshangaza Dubois kwa mwendo wake usiotabirika na ufundi wa kukwepa mashambulizi. Lakini Fury ana umri wa miaka 38 na uwezo wake unaonekana kupungua.
Moses Itauma ndiye bondia wa tatu mwenye kasi na ustadi wa kumletea Dubois changamoto. Hata hivyo, bondia huyo mwenye kipaji cha hali ya juu akiwa na umri wa miaka 21 alipata pigo kubwa baada ya kushinda kila raundi dhidi ya Filip Hrgovic, lakini baadaye akachoka na kushindwa kuzuia mashambulizi ya mpinzani wake katika raundi ya tisa.
Hilo lilikuwa somo muhimu linaloonyesha kuwa Itauma bado ana mengi ya kujifunza kuhusu uhalisia mgumu wa mchezo wa ngumi.
“Ninachotaka kujua ni nani anayefuata, Frank?” anahoji Dubois kwa furaha.
Promota Warren anaeleza kuwa Hrgovic, bingwa wa IBF, anatakiwa kutetea taji lake dhidi ya Frank Sanchez nchini Croatia. Kwa upande mwingine, taji la dunia la WBC linashikiliwa na Agit Kabayel, bondia mzuri wa uzito wa juu ambaye huvutia mashabiki wengi na huuza tiketi nyingi nchini Ujerumani.
Hrgovic, Kabayel, Fury na Itauma wote wanasimamiwa na Warren, ambaye anasema: “Jambo zuri ni kwamba kila mtu anataka kupigana. Hawa ni watu wa mapambano. Kutakuwa na mapambano makubwa na, jambo ambalo Daniel atapenda kulisikia, kutakuwa na fedha nyingi.”
Hata hivyo, Dubois alicheka kwa furaha kabla ya kuulizwa ni bondia gani angependa kupambana naye zaidi.
“Nimesikia mazungumzo kuhusu Kabayel, lakini nitapambana na yeyote atakayefuata kwenye orodha ... yeyote atakayelipa fedha nyingi zaidi.”
Hrgovic alikuwa amekaa kando ya ulingo kutazama pambano hilo, na alidai kuwa alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa aliposhindwa katika pambano kali dhidi ya Dubois 2024. Bondia huyo mwenye kujiamini kutoka Croatia aliahidi kumchapa mpinzani wake watakapokutana tena.
“Kweli amesema hivyo?,” Dubois anauliza kwa mshangao na furaha, kabla ya kuzungumzia uwezekano wa kukutana na Usyk kwa mara ya tatu.
“Bila shaka. Ningependa sana hilo. Safari hii tutashinda. Tumefanya makosa yetu, lakini sasa mimi ni bondia tofauti,” anasema.
Warren anathibitisha kuwa anaweza kabisa kumuona Fury akikubali kupambana na Dubois, kabla jina la Itauma halijatajwa tena.
Itauma ndiye bondia wa uzito wa juu mwenye kipaji zaidi nchini Uingereza, lakini Warren anakumbushia kuhusu umri wake. Pia anasisitiza kuwa pambano la baadaye kati ya Dubois na Itauma atakapokuwa na uzoefu zaidi itakuwa “vita ya ngumi kali” inayoweza kujaza uwanja mkubwa.
Dubois alipoulizwa kama angependa kupambana na Itauma siku moja, alitikisa kichwa kwa msisitizo,“natumaini hivyo, kwa sababu nahitaji washirika wa kucheza nao dansi.”