Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dirisha dogo linavyoficha madudu ya usajili uliopita

Muktasari:

  • Klabu zinapambana kusajili baada ya kushindwa kutimiza malengo dirisha kubwa lililofungwa siku chache kabla ya msimu kuanza.

HUU unaonekana ni msimu wa kipekee na dirisha la usajili la mwezi Januari limegeuka kuwa kimbilio muhimu kwa klabu nyingi.

Klabu zinapambana kusajili baada ya kushindwa kutimiza malengo dirisha kubwa lililofungwa siku chache kabla ya msimu kuanza.

Kwa kawaida, dirisha hilo kubwa hutambulika kama msingi wa maandalizi ya msimu mzima kwa sababu huwapa makocha na benchi la ufundi muda wa kutosha kujenga timu, kufanya tathmini ya kina na kuunda mifumo ya kiuchezaji kabla ya ushindani kuanza rasmi.

Kwa misimu mingi iliyopita, dirisha dogo la Januari lilikuwa linatumika zaidi kama nyongeza ya kurekebisha mapungufu machache yaliyojitokeza baada ya mzunguko wa kwanza wa ligi, baada ya benchi la ufundi kuwasilisha ripoti ya mwenendo wa timu, ikionyesha maeneo yenye udhaifu yaliyohitaji kufanyiwa maboresho.

Hata hivyo, kwa msimu huu, hali imekuwa tofauti kabisa, kwani baadhi ya klabu zimejikuta zikitumia dirisha la Januari kama fursa ya pili ya kujenga upya timu, badala ya kufanya marekebisho madogo tu.

Sababu kubwa ya hali hiyo ni wachezaji waliosajiliwa dirisha kubwa walitarajiwa kubeba timu, kuongeza ushindani wa ndani na kuleta ubora katika maeneo muhimu, lakini kwa vitendo mambo hayakwenda kama ilivyopangwa.

Matokeo yake, baadhi ya klabu zimelazimika kuingia sokoni tena Januari na kusajili zaidi ya wachezaji watano, hatua ambayo kwa kawaida haikuwa ya kawaida dirisha dogo.

Wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa nao hawakuwa nyuma katika mchakato huu. Klabu zinazoshiriki mashindano ya CAF zimetumia dirisha la Januari kujiongezea nguvu ili kuongeza ushindani kwenye ligi ya ndani na pia kujipanga vyema kwa mechi za kimataifa.

Miongoni mwao, Azam FC imeonekana kuwa na pilika chache sokoni. Sababu kubwa ni faida waliyonayo ya kuwa timu pekee kati ya wawakilishi hao ambayo bado imeendelea na kocha aliyefanya maandalizi ya msimu tangu mwanzo.

Hivyo, mahitaji yake mengi yalishatimizwa mapema na kinachoendelea sasa ni maboresho ya taratibu, ikiwemo kusajili wachezaji wa ndani kwa kuzingatia zaidi mustakabali wa timu na umri wa wachezaji hao.

Kwa upande wa wawakilishi wengine wa Kombe la Shirikisho, Singida Black Stars wamejikuta katika hali tofauti. Baada ya kuondokewa na baadhi ya wachezaji muhimu, walilazimika kuingia sokoni ili kuziba mapengo na wakati huo huo kuongeza makali ya kikosi chao.

Hata hivyo, hali yao unaweza kuifananisha na mkulima anayetumia gharama kubwa kulima shamba, halafu baada ya kuvuna, anagawa mazao kwa wakulima wenzake badala ya kuyauza.

Ni picha inayoakisi changamoto ya uwekezaji usioendana kikamilifu na faida ya moja kwa moja uwanjani.

Bingwa mtetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga SC, naye hakusalia salama katika msimu huu.

Takribani asilimia 80 hadi 90 ya sajili zake za dirisha kubwa zimeshindwa kufikia matarajio. Hali hiyo imeilazimu klabu kutumia dirisha la Januari kuimarisha kikosi.

Bahati kwao ni ubora wa kikosi kilichomaliza msimu uliopita ulisaidia kuficha udhaifu wa wachezaji wapya kwa kipindi fulani.

Ndiyo maana mara tu dirisha dogo lilipofunguliwa, Yanga iliingia sokoni kwa kasi, ikasajili wachezaji watano wapya na kumrejesha kwenye mfumo mlinzi wa kulia, Kouassi Attohoula Yao, aliyekuwa majeruhi.

Mpaka sasa, Allan Okello, Mohamed Damaro na Laurindo Depu tayari wameanza kujitambulisha na kuleta matumaini mapya kwa mashabiki wa Yanga.

Depu ameibuka kuwa gumzo zaidi baada ya kufunga mabao matatu na kutengeneza moja ndani ya mechi nne za mashindano tofauti.

Kwa takwimu na mchango wake, anaweza kuhesabika kama ingizo jipya bora mpaka sasa, bila kupunguza heshima kwa Okello na Damaro ambao nao wamekuwa na mchango muhimu tangu kuwasili kwao.

Kwa upande wa Simba SC, nao hawana hadithi tofauti sana. Hata hivyo, kwao hali inachukuliwa kwa tahadhari zaidi kutokana na ukweli kwamba wako katika kipindi cha mpito cha kujenga upya timu.

Hivyo, karibu kila dirisha la usajili wamejikuta wakianza upya. Ukiangalia kikosi chao, wachezaji waliosajiliwa kwa ajili ya msimu uliopita waliobaki hawazidi watano.

Msimu huu, dirisha kubwa waliwasajili zaidi ya wachezaji 12, na dirisha la Januari tayari wameshasajili wachezaji saba, yote ikiwa ni juhudi za kuongeza ubora wa kikosi.

Hata hivyo, usajili ni jambo moja na kufikia matarajio ni jambo jingine kabisa. Mabadiliko ya benchi la ufundi pia yana mchango mkubwa, kwani kocha mpya anaweza kuwafuta au kutowahitaji wachezaji waliokuwa chaguo la kocha aliyepita.

Mfano mzuri ni suala la Antony Mligo na Miraji Abdallah, ambapo ilielezwa kuwa Kocha Fadlu Davids alimkataa Miraji, lakini leo kocha mwingine anamuhitaji Nickson Kibabage. Haya ndiyo maisha ya soka, na mara nyingi klabu hujikuta zikiingia hasara katika mchakato wa kujenga kikosi.

Kwa sasa, golikipa Mahamadou Tanja Djibrilla Kassali ameanza vizuri katika mechi yake ya kwanza akiwa na Simba, akitoa matumaini mapya katika eneo la ulinzi wa lango.

Wakati huo huo, Libasse Gueye na wenzake bado wanahitaji muda wa kujitambulisha kikamilifu. Hata hivyo, historia zao zinaashiria mazungumzo chanya, na endapo zitatafsiriwa vizuri uwanjani, basi klabu zitafaidika kwa kiwango kikubwa na dirisha hili la Januari.