Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dili za pesa nyingi zilizoshikilia rekodi England

MKWANJA Pict

Muktasari:

  • Hadi hapo, iwe kama italipwa pesa ya dau lililowekwa mezani na Liverpool la Pauni 120 milioni, au lile la Pauni 150 milioni inayotaka Newcastle, hiyo itavunja rekodi ya uhamisho England.

LONDON, ENGLAND: LIVERPOOL imeripotiwa kuweka mezani Pauni 120 milioni kunasa huduma ya straika Alexander Isak. Lakini, klabu yake ya Newcastle United inamthaminisha kuwa na thamani ya Pauni 150 milioni.

Hadi hapo, iwe kama italipwa pesa ya dau lililowekwa mezani na Liverpool la Pauni 120 milioni, au lile la Pauni 150 milioni inayotaka Newcastle, hiyo itavunja rekodi ya uhamisho England.

Kwenye Ligi Kuu England, ada inayoshikilia rekodi ya uhamisho kwa sasa ni ile iliyolipwa na Liverpool kunasa saini ya Mjerumani, Florian Wirtz kutoka Bayer Leverkusen kwa dau la Pauni 116.5 milioni.

Kwa maana hiyo ni sahihi kusema, Wirtz ndiye anayeshikilia rekodi ya kuwa usajili ghali kwenye historia ya uhamisho ya Uingereza.

Je, Liverpool itavunja rekodi yake ya kusajili mchezaji mmoja kwa pesa nyingi na kuandikisha rekodi nyingine kwa kumtaka Isak?

Lakini, ukiweka kando dili hilo la Wirtz kuna dili nyingi za uhamisho wa pesa nyingi zilizowahi kutokea kwenye Ligi Kuu England, huku zile zilizoshika nafasi ya juu ni hizi hapa.

Hawa ndio mastaa walizisababisha klabu za Ligi Kuu England kulipa pesa nyingi kunasa saini zao na kuwafanya kuingia kwenye orodha ya wanasoka ambao walinaswa kwa mkwanja mrefu.

MKWA 01

10. Josko Gvardiol (Man City, 2023) – Pauni 80 milioni

Beki Mcroatia amekuwa na wakati mzuri tangu alipojiunga na Manchester City chini ya kocha Pep Guardiola, akifanya vyema tangu aliponaswa kutoka RB Leipzig kwenye dirisha la majira ya kiangazi 2023. Saini ya Gvardiol haikupatikana kwa pesa ndogo, Man City ilijikamua kwelikweli kupata huduma ya mkali huyo, mwenye uwezo wa kucheza nafasi nyingi kwenye safu ya ulinzi, ilipolipa Pauni 80 milioni.


9. Antony (Man United, 2022) – Pauni 85 milioni

Manchester United ilimfukuzia winga wa Kibrazili, Antony kwa muda mrefu kabla ya kupata saini yake, ilipomchukua kutoka Ajax kwa ada ya Pauni 80.75 milioni za awali na nyongeza ya Pauni 4.25 milioni.

Hata hivyo, baada ya kutua Old Trafford, mambo ya Antony hayakuwa kwenye viwango bora, tangu alipokuwa chini ya kocha Erik ten Hag hadi hapo alipokuja Ruben Amorim, ambaye aliamua kumtoa kwa mkopo kwenye dirisha la Januari mwaka huu kwenda Real Betis.

MKWA 02

8. Mykhailo Mudryk (Chelsea, 2023) – Pauni 88.5 milioni

Mudryk dau lililotangulia kulipwa wakati anatua Chelsea ni Pauni 62 milioni na pia kulikuwa na nyongeza ya Pauni 26.5 milioni, ambayo klabu yake ya Shakhtar Donetsk ililipwa ili mkali huyo akikipige huko Stamford Bridge.

Winga huyo baada ya kutua Chelsea, alifunga mabao matano na kuasisti sita katika mechi zaidi ya 50 alizocheza kwenye Ligi Kuu England kabla ya kukutana na adhabu ya kufungiwa soka kutokana na kufeli vipimo vya matumizi ya dawa za kusisimua misuli.


7. Paul Pogba (Man United, 2016) – Pauni 89 milioni

Usajili wa Pogba kutua Old Trafford kwenye dirisha la majira ya kiangazi mwaka 2016 bado linatajwa kama moja ya uhamisho wa mchezaji maarufu zaidi kuwahi kutokea kwenye historia ya Ligi Kuu England.

Kwa wakati huo, staa huyo wa Ufaransa alikuwa anarudi tena Old Trafford, ambako aliondoka miaka minne nyuma kwenda Juventus.

Lakini, Man United ilimrudisha kwenye kikosi mchezaji wake wa zamani kwa kumlipia pesa nyingi sana, Pauni 89 milioni, ambayo kwa wakati huo ulikuwa inashikilia rekodi ya uhamisho huko Uingereza.

MKWA 03

6. Romelu Lukaku (Chelsea, 2021) – Pauni 97.5 milioni

Straika Romelu Lukaku alirejea Chelsea kwa pesa nyingi sana wakati wa dirisha la majira ya kiangazi 2021, baada ya miaka miwili ya kuonyesha kiwango bora huko Inter Milan.

Lakini, staa huyo wa Ubelgiji aliporudi Stamford Bridge mambo yake hayakwenda vizuri, akajikuta akitolewa kwa mkopo wa msimu mzima kurudi Inter Milan.

Chelsea ilimsajili straika huyo kwa ada ya Pauni 97.5 milioni na kumfanya kushikilia rekodi ya uhamisho wa England kwa kipindi hicho, huku ada zake zote zilizohusika katika usajili wa Lukaku, zikifikia Pauni 290 milioni.


5. Jack Grealish (Man City, 2021) – Pauni 100 milioni

Jack Grealish alijiunga na Manchester City baada ya kuonyesha kiwango bora sana huko Aston Villa kiasi cha kumfanya kocha Pep Guardiola kuruhusu itumike pesa nyingi kunasa saini yake mwaka 2021.

Man City ilitoa pesa nyingi baada ya kumuona mchezaji huyo kwenye rada za mahasimu wao, Manchester United, ambao pia walikuwa wakihitaji huduma yake.

Grealish alichagua kwenda kujiunga na Man City, huku Pauni 100 milioni ikitolewa kumnasa na kuweka rekodi ya uhamisho kwenye Ligi Kuu England kwa wakati huo.

MKWA 04

4. Declan Rice (Arsenal, 2023) – Pauni 105 milioni

Declan Rice alihama kutoka West Ham United kwenda kujiunga na Arsenal mwaka 2023 na hakutaka kujichelewesha kuliweka jina lake kwenye orodha ya wachezaji muhimu huko Emirates.

Katika msimu wa 2024/25, Rice alifunga mara mbili kwa mipira matata ya friikiki katika ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Real Madrid kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na hivyo kulifanya jina lake kuwa maarufu zaidi kwa mashabiki wa Arsenal.

Na hata saini yake haikuwa ya pesa ndogo, Arsenal ililazimika kuvunja rekodi ya uhamisho Uingereza, ilipolipa Pauni 105 milioni.


3. Enzo Fernandez (Chelsea, 2023) – Pauni 107milioni

Baada ya sakata refu la usajili wake kwenye dirisha la Januari 2023, Chelsea ilifikia makubaliano ya kulipa Pauni 107 milioni ambayo Benfica ilipanga kuwa ndiyo bei halisi ya kiungo huyo wa Kiargentina, Enzo Fernandez.

Na tangu alipotua Stamford Bridge staa huyo alionyesha kiwango bora, wakati huko Benfica alicheza kwa miezi sita tu baada ya kunaswa akitokea River Plate kwa ada ya Pauni 15 milioni.

Enzo alicheza kwa kiwango bora sana kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022, alipoiwezesha Argentina kubeba ubingwa huko Qatar, ambapo alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora Kijana wa fainali hizo.

MKWA 05

2. Moises Caicedo (Chelsea, 2023) – Pauni 115 milioni

Kiungo mkabaji, Moises Caicedo alisababisha vita kali baina ya Chelsea na Liverpool zilipokuwa zikipambana kunasa saini yake kwenye dirisha la uhamisho wa majira ya kiuangazi 2023 na The Blues ilifanikiwa kuibuka na ushindi.

Brighton ilinufaika na ushindani huo wa Liverpool na Chelsea na kufanikiwa kumuuza staa wao kwa pesa nyingi sana, Pauni 115 milioni na kuvunja rekodi ya uhamisho Uingereza.

Chelsea ilianza kulipa Pauni 100 milioni, kisha ililazimika kuongeza Pauni 15 milioni ili kufikia Pauni 115 milioni kutokana na kiwango bora cha mkali huyo wa Ecuador. Kwenye kikosi cha Chelsea, Caicedo ameunda pacha matata kwelikweli kwenye safu ya kiungo na Enzo Fernandez.


1. Florian Wirtz (Liverpool, 2025) – Pauni 116.5 milioni

Kiungo wa kimataifa wa Ujerumani, Florian Wirtz hajawahi kucheza mechi yoyote kwenye soka la England hadi hapo alipofanywa kuwa mwanasoka ghali zaidi kwenye historia ya uhamisho ya Uingereza aliponaswa na Liverpool kwa ada ya Pauni 116.5 milioni kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.

Liverpool ilifanya usajili wa Wirtz kuonyesha jeuri ya pesa kabla ya kumchukua straika wa Eintracht Frankfurt, Hugo Ekitike kwa ada ya Pauni 79 milioni. Kwenye kikosi cha Liverpool, Wirtz amekabidhiwa jezi Namba 27, ambayo mashabiki wake watamwona akiivaa kwenye mechi za Ligi Kuu England msimu ujao.