CHRISTINA MWAGALA; Alivyopenya katikati ya wanaume Ligi Kuu Bara
Muktasari:
- Miongoni mwao ni Christina Mwagala, mwanamke anayesimama kama mfano wa uthubutu na kujituma katika nafasi ya Ofisa Habari kwenye Ligi Kuu Bara.
KATIKA ulimwengu wa soka ambao mara nyingi unaonekana kutawaliwa na wanaume, kuna wanawake wachache wanaothubutu kuvunja mipaka na kuonyesha wanaweza kufanya kazi kubwa sawa na wenzao.
Miongoni mwao ni Christina Mwagala, mwanamke anayesimama kama mfano wa uthubutu na kujituma katika nafasi ya Ofisa Habari kwenye Ligi Kuu Bara.
Kwa sasa, Christina ndiye Ofisa Habari pekee mwanamke anayefanya kazi katika ligi hiyo, jambo linalomfanya kuwa kivutio na msukumo kwa wanawake wengi wanaopenda kuingia katika tasnia ya michezo. Safari yake haikuwa rahisi, lakini kwa juhudi, ujasiri na mapenzi ya dhati kwa mpira wa miguu ameweza kujenga jina lake na kuthibitisha wanawake wana nafasi kubwa katika sekta ya michezo.
ALIVYOANZA
Christina anasema taaluma yake ni uandishi wa habari. Kabla ya kuwa Ofisa Habari, alikuwa akifanya kazi katika vyombo mbalimbali vya habari kama mwandishi wa habari za elimu, huku moyoni akiwa na mapenzi makubwa na michezo, hasa mpira wa miguu.
“Mimi kitaaluma ni mwandishi wa habari. Nilikuwa naandika sana magazetini, hasa upande wa masuala ya elimu, lakini kila nilipopata nafasi ya kwenda viwanjani na wenzangu waliokuwa wanafanya kazi kwenye sekta ya michezo, nilikuwa nikifurahi sana.
“Kwangu sikuwa na ndoto kabisa za kuwa Ofisa Habari wa klabu, kwanza hakukuwa na mwitikio wa wanawake wengi katika nafasi hiyo. Kwa kuwa sikuwa naandika habari za michezo sana, sikuwaza kama nitakuja kufanya kazi kwenye eneo hilo.”
ALIVYOTUA KMC
Anasema alianza kujitolea katika Ofisi ya Meya wa Jiji la Dar es Salaam kwa kipindi cha mwaka mmoja. Baadaye alipata nafasi ya kupewa mkataba na Manispaa ya Kinondoni katika kitengo cha habari.
“Baada ya kutoka Ofisi ya Meya nilipata bahati ya kuonekana na Mkurugenzi wa Kinondoni. Nikaacha kujitolea na kuanza kazi rasmi. Siku moja niliitwa na bosi wangu na kuambiwa sasa natakiwa kwenda kufanya kazi upande wa timu.
“Hapo ndipo nikaingia KMC rasmi, ilikuwa ni mwishoni mwa msimu wa 2017/18 wakati timu zikiwa zinajiandaa kuanza msimu mpya. Sikuwahi kuandika habari za mpira, lakini nilikuwa napenda sana michezo.”
KAZI ILIANZA HIVI
“Kuanza kufanya kazi na wanaume haikuwa rahisi. Nakumbuka siku ya kwanza nilipoanza kazi ugumu ulianza hata kwenye mavazi; nilienda mazoezini nikiwa nimevaa gauni. Nilikuwa nauliza mambo ya kufanya ndipo nikampigia simu Massau Bwire ambaye wakati huo alikuwa Ofisa Habari wa Ruvu Shooting, akanipa ABC za kazi hii.
“Wakati huo kulikuwa na ushindani mkubwa kwa upande wa wasemaji wa klabu, kulikuwa na Jerry Muro na Haji Manara. Nilikuwa nawasikiliza sana na kuwaona mtandaoni kabla sijaingia kwenye kazi hii. Nilipoanza kazi nikajikumbusha maneno na tambo zao na nikagundua inawezekana.”
MECHI YA KWANZA
“Mechi yangu ya kwanza nakumbuka nilienda na gauni langu. Ilikuwa ni KMC dhidi ya Mbeya City, wakati huo tunatumia Uwanja wa Uhuru. Tulishinda mabao manne, kocha akiwa Habibu Kondo.
“Baada ya mechi nilizungumza na wanahabari na nikaanzisha kundi la Whatsapp ili niwe nawapa taarifa. Pia wale waliokuwa na uzoefu walikuwa wakinifuata na kuniambia nilipokosea ili nijirekebishe.
“Kuna maneno ya soka ambayo mwanzoni sikuweza kuyatamka vizuri, lakini watu walinisaidia sana. Mwishowe nikajikuta nimekaa sawa. Wakati huo kulikuwa na msemaji mwingine anaitwa Jamila Mutabazi, lakini baada ya JKT Tanzania kushuka daraja alipotea na nikabaki peke yangu hadi leo.”
TUKIO LA KUHUZUNISHA
Christina anasema katika maisha yake ya kazi, hakuna wakati mgumu kwa msemaji kama kipindi ambacho timu inafanya vibaya.
“Msimu ambao tulikaribia kushuka daraja ulikuwa mgumu sana kwangu kwa sababu nilikuwa bado mgeni kwenye kazi hii. Hata nilipokwenda Tabora United nilikutana na hali kama hiyo. Inafika mahali unajisikia vibaya sana kama kiongozi wa timu.”
ALIVYOTUA TABORA
“Baada ya mkataba wangu na KMC kuisha hawakuonyesha nia ya kuendelea na mimi, hivyo nafasi yangu akapewa Khalid Chukuchuku.
“Sikujisikia vibaya kwa sababu ni kawaida katika kazi hizi, mtu anatoka na mwingine anaingia. Hilo halikunipa shida, badala yake lilinipa ujasiri zaidi kwa sababu niliamini sitaweza kupotea.
“Baada ya hapo nikaenda FA upande wa habari katika Chama cha Soka Mkoa wa Pwani kwa miezi miwili, ndipo uongozi wa Tabora United uliponitafuta na kuanza kazi Januari. Kwa sasa timu imenunuliwa na TRA.”
BATA LA TRA
Christina anasema kuna tofauti kubwa kati ya kufanya kazi katika klabu binafsi na taasisi ya serikali kama TRA.
“Ni kweli huduma zimebadilika sana. TRA ni taasisi kubwa ya serikali, hivyo mambo mengi yameboreshwa kuanzia namna timu inavyoishi hadi mazingira ya kazi. Namshukuru Mungu kwa kweli kuna vitu vingi vimebadilika.”
WANAWAKE WANAVYOVUTIWA NAYE
Anasema wanawake wengi wanavutiwa na kazi yake lakini wanaogopa kufanya kazi katika mazingira yenye wanaume wengi.
“Wengi wanatamani lakini wanadhani kazi hii ni uhuni. Wananiuliza sana nawezaje kufanya kazi na wachezaji, wengine wanafikiri nakaa nao na kulala nao, lakini si kweli.
“Mimi nakutana nao kwenye mazoezi na kwenye shughuli za timu tu. Mara nyingi wachezaji wananiita Mama, Dada au Madam, na si vingine. Hawajawahi kunitongoza kama watu wengi wanavyodhani.”
FAMILIA NA KAZI
Anasema imekuwa rahisi kwake kuifanya kazi hiyo huku akitunza familia yake.
“Hii ni kazi ninayoipenda, kwa hiyo hainichoshi kabisa. Hata mtu niliye naye anaelewa kwa sababu amenikuta nikiifanya kazi hii. Anaiheshimu kwa sababu anajua sina tabia zisizofaa.”
SIASA KWENYE DAMU
Christina anasema ndoto yake kubwa ni siku moja kuingia kwenye siasa.
“Mbali na kufanya vizuri kwenye kazi yangu ya sasa, natamani siku moja kuwa mwanasiasa mkubwa. Inawezekana kwa sababu kazi ya usemaji inanijenga sana kujiamini na kuzungumza mbele za watu.”
ANAVYOZITESA SIMBA NA YANGA
Anasema amefanya kazi na wasemaji wa klabu kubwa hivyo anawafahamu vizuri, lakini mara nyingi watu hudhani anaiogopa Yanga.
“Ukweli ni kwamba nawatesa Yanga kwa sababu ni timu ambayo niliwahi kuifunga. Simba bado hawajanipa nafasi ya kujigamba sana kwa sababu sijawafunga, lakini msimu huu nimejipanga kuhakikisha ninawafunga.
“Ahmed Ally na Ally Kamwe ni watu wazuri na tunafanya kazi vizuri pamoja. Pia kuna Hussein Masanza na wengine ambao tumekuwa na ushirikiano mzuri. Lakini nikiwafunga lazima niwatambie.”
MAFANIKIO
Christina anasema soka limemfungulia milango mingi ya mafanikio.
“Nimepata mafanikio makubwa kutokana na soka. Siwezi kuyataja yote kwa sababu ni mengi, lakini kwa kifupi nimefungua duka la asali ambalo watu wengi wanapenda na kuiamini kwa sababu wanajua inatoka moja kwa moja Tabora.”