Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kizazi kipya cha wasemaji wa timu kinavyokimbiza

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ni kwamba, kila timu inayoshiriki Ligi Kuu Bara ni lazima iwe na ofisa habari ambaye kitaaluma anapaswa kuwa mwandishi wa habari kulingana na sheria za nchi, na kwa maana hiyo mtu huyo ndiye anayekuwa msemaji wa klabu.

KUMEIBUKA kizazi flani hivi kinaupiga mwingi kwenye eneo la kuzisemea timu za Ligi Kuu Bara, wakiibuka na ladha ya tofauti kabisa tofauti na zamani ilivyokuwa.

Kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ni kwamba, kila timu inayoshiriki Ligi Kuu Bara ni lazima iwe na ofisa habari ambaye kitaaluma anapaswa kuwa mwandishi wa habari kulingana na sheria za nchi, na kwa maana hiyo mtu huyo ndiye anayekuwa msemaji wa klabu.

Licha ya utaratibu huo kuwapo na kusisitizwa zaidi miaka ya karibuni, baadhi ya klabu ziliwahi kuwa na wasemaji kwa miaka mingi, hususan Yanga, Simba, Azam na Mtibwa Sugar, ingawa katika miaka ya sasa kuna kizazi flani kinachotesa kuzisemea timu wanazofanyia kazi.

Awali, kulikuwa na wasemaji wenye majina makubwa ambao walitamba sana kwa kazi zao katika eneo hilo wakiwemo Jerry Murro ambaye alikuwa ofisa habari wa Yanga wakati huo upande wa pili wa watani zao, Simba, alikuwapo Haji  Manara.

Nyakati hizo kulikuwa hakupoi kwani wawili hao wakiwa kwenye klabu hizo kubwa mbili, huku kule Azam alikuwapo Jaffary Idd ambaye hakuwa na makeke kama wawili hao, lakini alikuwa akienda nao sawa kwenye kuisemea klabu yake.

Kizazi hicho kilipita na kabla ya kupita ilionekana kama ni vigumu kupatikana wasemaji wengine ambao wangekuja kuwazima wakongwe hao, lakini mambo yamegeuka na wakaibuka watu ambao wamezima flani mbwembwe za  wakubwa waliowatangulia na hawa hapa chini ni baadhi ya wanaokimbiza kwa sasa.


ALLY KAMWE (YANGA)

Ally Kamwe ni kijana mwenye mwili mdogo, lakini kinywa chake kina maneno yanayowasisimua mashabiki wa soka nchini hususan wale wa Yanga.

Kamwe aliingia Yanga akisimamia upande wa habari, lakini kipindi hicho msemaji alikuwa Manara.  Lakini, hivi sasa kijana huyo amefanikiwa kuikamata vyema hadhira ya mashabiki wa Jangwani, kwani kila anapozungumza ni kama ameikamata klabu mkononi akifanikiwa kuwashawishi mashabiki vilivyo.

Kwa sasa Manara hayupo tena kwenye majukumu ya usemaji, lakini huwezi kuliona pengo lake kutokana na mambo anayofanya Kamwe.

Unakumbuka ule mkwara aliokuwa akiutema wakati wa lile sakata la "hatuchezi" mwaka jana, aliposema "atoke mwanaume aikate Yanga pointi". Kauli ile ilibamba sana na sasa anasumbua na kile kipande chake cha "jasusi".

Kamwe ameonyesha uwezo mkubwa kuibeba Yanga katika kuisemea, ingawa haina maana kwamba amefunika kipaji cha Manara, lakini amekuja kivyake na kujitofautisha na mkongwe huyo huku kukionekana hakuna pengo kwenye idara hiyo ndani ya mabingwa hao wa soka nchini.


AHMED ALLY (SIMBA)

Upande wa Simba baada ya Manara kuondoka nako kulionekana kama kungekuwa na ugumu au maisha ya Wekundu  wa Msimbazi yangekuwa magumu katika uwasilishwaji na upokeaji wa taarifa zinazohusu klabu hiyo. Lakini, katikati ya sintofahamu ya Manara kuacha kazi na kutimkia Yanga akaibuka Ahmed Ally aliyetokea kwenye utangazaji palepale alipotoka Kamwe kwenye Kituo cha Azam Media.

"Wanasimbaaaa....", hiyo ilikuwa moja ya vichombezo alivyoibuka navyo na kuanza kuwakosha mashabiki wa kandanda. Hapo ndipo Ahmed alitoka kirahisi, kisha akaja na mikato mingi ikiwamo ile ya "Simba tumesajili straika refu kuliko goli, akiruka tu anaweka waaa". Kauli hizo za msemaji huyo zilivuma sana na kuibeba timu yake.

Nyingine kali inayokumbukwa kwake ni ile akili ya uhamasasishaji akitumia kipaza sauti kilichopewa jina la "kispika" ambapo Simba licha ya nyakati flani kupitia kipindi kigumu cha ubora uwanjani, lakini hajawahi kukata tamaa. Amebaki kwenye mstari na hutumia ubunifu wake kuwarudisha mashabiki wa klabu hiyo uwanjani kutokana na hamasa anazozifanya zinazoendana na kauli mbinu bunifu na uwasilishaji wake maridhawa.

Nyakati ambazo chama hilo liliyumba kwa ubora hakuna mtu aliyewapunguzia presha mashabiki kama Ahmed ambapo pia alipokuwa akikutana na Kamwe kwenye matukio ya pamoja kuna utani wao flani umekuwa ukiwaacha   mashabiki wa pande zote na vicheko.


ZAKA, IBWE (AZAM)

Kwa Azam FC kuna vichwa viwili vinavyotesa katika kuisemea klabu hiyo, baada ya kuondoka kwa Jaffary Iddi.

Kabla ya Ibwe alikuwa Thabit Zacharia maarufu kwa jina la Zaka Zakazi peke yake ambaye moja ya eneo lake bora ni kujua kupambana na wenzake kwa namba au takwimu.

Zaka ana kumbukumbu nzuri, ambapo amekuwa anasubiri kuona wasemaji wenzake wanapoteleza kisha hushuka na namba au takwimu ambazo huibua raha flani kwa mashabiki wa soka. Pia mejaliwa kuwa na kumbukumbu nzuri za matukio ya nyuma, uwezo ambao wengi wamekuwa wakiukosa.

Kando ya Zaka kuna Hashim Ibwe anayemsaidia mkongwe huyo, ambaye naye ameibukakimtindo na sasa anakimbiza  kwa mistari ya 'vijimaneno vya kishabiki vya kukera'. Hivi karibuni alimbana Ahmed alipohoji "vipi Iriza... basi lenu limeshafika?" Alipojibiwa "bado" akamuongezea kuwa "Azam inaleta chuma kipya na ile Iriza inayotumiwa sasa inakwenda timu ya vijana". Mambo hayo.


HUSSEIN MASSANZA (SINGIDA BLACK STARS)

Singida Black Stars nayo ina kichwa chake. Huyo ni Hussein Massanza ambaye ana vitu vyake hasa linapokuja suala la tambo za ubora wa kikosi walichonacho, na ni hapo ambapo amekuwa 'akizisimanga' timu zingine zikiwamo kubwa za mitaa ya Msimbazi na Jangwani, kwamba wanazigawia wachezaji kwa kuwa wao ni bora na wana mastaa mahiri kutokana na kuwa na maskauti bora wa kusaka vipaji Afrika.

Massanza buana! Amewahi kukaririwa akirusha kijembe kwamba katika hilo la wachezaji wanaweza kugawia timu kubwa na ndogo wachezaji, lakini kamwe wao hawaishiwi watu bora kikosini kwao.



CHRISTINA MWAGALA (TRA UNITED)

Msemaji pekee mwanamke kwenye klabu za Ligi Kuu Bara ni huyu Christina Mwagala ambaye kama utani amekuwa na kijiji chake kwa kuthubutu ‘kuvimba’ mbele ya wasemaji wa hizo klabu kubwa nchini akiziibulia vita ya maneno.

Mwagala alianza kule Pwani kisha akahamia Tabora United ambayo ndio iliyomuongezea ukuaji wa jina lake kabla ya klabu hiyo kuuzwa na sasa kuwa TRA United ambapo kauli yake kubwa inayombeba ni ile pila mapato pila kodi ambayo inaibeba taasisi yake kwenye biashara yao mama ya kukusanya mapato kupitia kodi.


KHALID CHUKUCHUKU (KMC)

KMC ipo mkiani katika msimamo wa Ligi Kuu Bara na hatua hiyo imempunguzia mbwembwe msemaji wa timu hiyo, Khalid Chukuchuku ambaye amejikuta akiwa kimya. Awali, msemaji huyo alikuwa na utani wa burudani na wasemaji wa timu zingine.

Chukuchuku amekuwa akitamba na klabu yao kumiliki uwanja ule wa KMC Complex ambao uliwahi kuzifanya wakati flani Simba na Yanga kupigana vikumbo kuutumia kwa mechi zao, akiziambia "karibuni hapa mjisitiri" hatua ambayo iliwafanya Kamwe na Ahmed kuwa wapole.


WANASHIRIKIANA

Kundi hilo la wasemaji na wengine wana umoja flani hivi wakishirikiana kwenye matukio ya pamoja, ambapo imekuwa rahisi hata kukiwa na mechi za kimataifa zinazohusu timu ya Taifa kuwaona wakiwa pamoja wakiitanguliza nchi mbele huku wakiwa na vichekesho na vijembe mbalimbali.


WASIKIE MASHABIKI

Akizungumzia mbwembwe za wasemaji, Soud Mlingano anasema wamekuwa wakisaidia kufikisha taarifa za klabu kwa kutumia semi, utani na kaulimbiu zinazobamba na kwenda na nyakati, hivyo kuliweka hai soka la Tanzania.

"Mfano ukimsikiliza Ahmed Ally akirusha kijembe cha dabi kwa Ally Kamwe utadhani wao wawili hawasalimiani, lakini ukweli ni kwamba zile ni mbwembwe tu za mambo ya mpira na zaidi ujumbe unakuwa umefika na siku ya mechi sisi mashabiki lazima tuujaze uwanja," anasema Soud.

Mwikamo Ndalahwa anasema kizazi cha sasa cha wasemaji wa klabu hakitofautiani sana na kile cha zamani, japo hawa waliopo wanatumia usasa zaidi kufikisha taarifa ikizingatiwa kwamba vyombo vya habari hususan vya mitandaoni vimekuwa vingi.

"Zamani kulikuwa na Thobias Kifaru, Jerry Muro, Manara na Masu Bwire mambo yalikuwa hayo hayo. Mfano kukiwa na mechi ya Simba na Yanga utawasikia Muro na Manara wanatambiana kama ilivyo Ahmed Ally na mwenzake Ally Kamwe. Nadhani kizazi cha sasa kinabebwa zaidi na wingi wa mitandao na taarifa kufika kwa haraka kwa mashabiki," anasema Ndalahwa.