Chirwa: Mzambia anayepambana kuirudisha Kagera Ligi Kuu
Muktasari:
- Baada ya kuichezea Yanga kuanzia Julai 1, 2016, ila aliachana nayo Julai 17, 2018, kisha kujiunga na Nogoom FC ya Misri, kabla ya kurejea tena hapa nchini na kujiunga na Azam FC, Novemba 8, 2018, huku akiichezea pia, Hobro IK kutoka Denmark.
MSHAMBULIAJI wa Kagera Sugar, Mzambia Obrey Chirwa, sio jina geni kwa mashabiki na wadau wa soka hapa nchini, kutokana na wasifu wake, tangu nyota huyo alipojiunga na Yanga mara ya kwanza, Julai 1, 2016, akitokea FC Platinum ya Zimbabwe.
Baada ya kuichezea Yanga kuanzia Julai 1, 2016, ila aliachana nayo Julai 17, 2018, kisha kujiunga na Nogoom FC ya Misri, kabla ya kurejea tena hapa nchini na kujiunga na Azam FC, Novemba 8, 2018, huku akiichezea pia, Hobro IK kutoka Denmark.
Licha ya kuchezea timu mbalimbali hapa nchini, ila mshambuliaji huyo kwa sasa anaichezea Kagera Sugar, inayoshiriki Ligi ya Championship msimu huu, huku akionyesha kiwango bora cha kukipambania kikosi hicho kurejea tena Ligi Kuu msimu ujao.
KINARA WA MABAO
Chirwa amekuwa na mwenendo mzuri wa kufunga, ambapo mshambuliaji huyo ndiye anayeongoza akiwa na mabao 14, akifuatiwa na Adam Uledi aliyekuwa Transit Camp, anayeichezea kwa sasa KMC FC na Ramadhan Hashim wa B19 FC waliofunga 11, kila mmoja.
Kiwango hicho kizuri kwa Uledi, kiliwafanya mabosi wa KMC FC kumsajili mshambuliaji huyo katika dirisha dogo la Januari 2026, ili kuongezea nguvu eneo hilo la ushambuliaji, huku nyota wa Mbeya Kwanza, Boniface Mwanjonde, akifunga mabao 10.
Abrahaman Mussa aliyeanza msimu huu wa Ligi ya Championship akiwa na Gunners FC ya Dodoma, kisha dirisha dogo la Januari 2026, akajiunga na maafande wa Transit Camp na Samson Albert anayeichezea KenGold, kila mmoja wao amefunga mabao tisa.
Nyota wengine ni Joseph Ambokege na Seif Adam wanaoichezea Mbeya Kwanza na Emmanuel Mpuka wa Polisi Tanzania ambao kila mmoja amefunga mabao manane, wakifuatiwa na Hassan Mwaterema (Kagera Sugar) na Maulid Shaban wa Geita Gold wenye saba.
REKODI YA HAT-TRICK
Mshambuliaji huyo, anashikilia rekodi ya mchezaji wa kwanza wa Ligi ya Championship msimu wa 2025-2026 kufunga mabao matatu (hat-trick), wakati kikosi hicho cha Kagera Sugar kilipoifunga Hausung FC ya Njombe mabao 3-1, Desemba 2, 2025.
Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Kaitaba Bukoba, mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga, Azam, Namungo, Ihefu ambayo kwa sasa ni Singida Black Stars na KenGold, alifunga mabao hayo, ambapo amefikisha 14, akiwa ndiye anayeongoza.
Mwingine aliyefunga hat-trick ni Boniface Mwanjonde wa Mbeya Kwanza katika ushindi wa kikosi hicho wa mabao 5-0, dhidi ya B19 FC, Desemba 17, 2025, ambapo mshambuliaji huyo amerejea tena baada ya uhamisho wake kwenda Fountain Gate kukwama.
Nyota huyo amechangia mabao 14, ya Mbeya Kwanza, msimu huu baada ya kufunga 10 na kuasisti manne, ambapo Januari 2026, alijiunga na Fountain Gate inayoshiriki Ligi Kuu, japo uhamisho wake ulikwama, baada ya kikosi hicho kufungiwa kusajili.
MABAO MAWILI, TIMU MOJA
Moja ya jambo la kuvutia kwa mshambuliaji huyo, katika mabao yake mawili ya Ligi Kuu Bara aliyofunga kwa msimu wa 2024-2025, aliyafunga akizichezea timu mbili tofauti, japo, kiujumla yote aliifunga klabu moja, ambayo ni ya Fountain Gate.
Msimu wa 2024-2025, Chirwa alianza kuichezea Kagera Sugar, ambayo aliifungia bao moja, wakati kikosi hicho kilipochapwa mabao 3-1, dhidi ya Fountain Gate, katika mechi kali na ya kuvutia ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa, Septemba 27, 2024.
Baada ya kuichezea Kagera, dirisha dogo la Januari 2025, nyota huyo alijiunga na KenGold kwa mkopo, ambayo aliifungia pia bao moja, katika ushindi wa kikosi hicho wa mabao 2-0, dhidi ya Fountain Gate, mechi iliyopigwa, Februari 10, 2025.
MBILI ZAMSHUSHA DARAJA
Katika timu alizocheza mshambuliaji huyo kwa msimu wa 2024-2025, kwa maana ya Kagera Sugar na KenGold, zote zimeshuka daraja, zikitoka Ligi Kuu Bara na kushiriki Ligi ya Championship, kutokana na kutokuwa na mwenendo mzuri kwa msimu huo. Kagera iliyodumu katika Ligi Kuu Bara kwa miaka 20, tangu ilipoanza kushiriki 2005, ilishuka daraja msimu wa 2024-2025, baada ya kushinda mechi tano tu, sare minane na kupoteza 17, ikishika nafasi ya 15, kufuatia kukusanya pointi zake 23.
Timu hiyo inayonolewa na aliyekuwa nyota wa Simba, Yanga na timu ya Taifa Stars, Juma Kaseja aliyewahi kuitumikia pia Kagera Sugar akiwa mchezaji na kocha wa makipa, kwa sasa anakipambania kikosi hicho ili kirejee tena katika Ligi Kuu Bara.
Kwa upande wa KenGold baada ya msimu bora wa 2023-2024, ilipotwaa ubingwa wa Championship, mambo yalikuwa tofauti, kwani iliposhiriki Ligi Kuu msimu wa 2024-2025, iliburuza mkiani na pointi 16, ikishinda mechi tatu, sare saba na kupoteza 20.
Kwa msimu wa 2023-2024, KenGold ilitwaa ubingwa wa Championship, ikiibuka kinara na pointi 70, ikiungana na Pamba Jiji ya Mwanza iliyomaliza ya pili na pointi 67, ikirejea tena Ligi Kuu Bara baada ya miaka 21, tangu iliposhuka mwaka 2001.
MFUNGAJI BORA KOMBE LA FA
Miongoni mwa kumbukumbu nzuri kwa Chirwa katika soka la Tanzania, ni kuibuka pia mfungaji bora wa Kombe la Shirikisho la FA, ambapo nyota huyo anakumbukwa msimu wa 2016-2017, alipoibuka kinara, baada ya kufunga mabao matano akiwa na Yanga.
Nyota huyo aliibuka kidedea msimu huo wa 2016-2017, ikiwa ni msimu wa pili tangu michuano hiyo iliporejea tena kuchezwa baada ya kutofanyika kwa miaka 13, mfululizo, tangu mara ya mwisho iliposimama ikifahamika kwa Kombe la FAT mwaka 2002.
Katika msimu wa 2016-2017, Chirwa alifunga mabao hayo matano ya Kombe la FA na kuibuka kinara wa ufungaji bora, ingawa, nyota huyo alikosa ubingwa huo wa michuano hiyo, baada ya kuchukuliwa na watani zao Simba iliyoifunga Mbao FC mabao 2-1.