Miaka 100 yenye simulizi ya kusisimua San Siro
Muktasari:
- Ni mabeki wenzake, Paolo Maldini aliyefikisha mechi 902 na Franco Baresi aliyefikisha 719, pekee waliocheza mechi nyingi zaidi kwa AC Milan kuliko Costacurta.
MILAN, ITALIA: BAADA ya kucheza mechi yake ya 663 na ya mwisho akiwa na klabu yake pendwa ya AC Milan, Alessandro Costacurta alikuwa na ombi moja la mwisho; kutaka kucheza tena katika uwanja aliouita nyumba yake ya pili, hapo si kwingine bali ni San Siro.
Ni mabeki wenzake, Paolo Maldini aliyefikisha mechi 902 na Franco Baresi aliyefikisha 719, pekee waliocheza mechi nyingi zaidi kwa AC Milan kuliko Costacurta.
Costacurta alishinda mataji 24 katika misimu yake 22 akiwa AC Milan, kuanzia mwaka 1986 hadi 2007, hivyo kujijengea nafasi ya kipekee katika historia ya klabu hiyo.
Mwisho wa uchezaji wake ulipokaribia na wakati wa kuongeza mkataba ulipofika, beki huyo wa kati alikuwa na utaratibu wa kuikabidhi bodi karatasi tupu aliyokuwa ameweka saini yake. Uongozi ungeandika kiasi chochote cha mshahara walichotaka, naye angeendelea kucheza.
“Kwa kweli, sikuwahi kufikiria kwamba fedha ndio jambo muhimu zaidi,” Costacurta anaiambia ESPN.
“Nilikuwa nafurahia kucheza, sikuwa tayari kwa mabadiliko. Nilikuwa tayari nimepata fedha nzuri, na nilichotaka ni kuendelea kuichezea klabu yangu katika San Siro.”
Alipostaafu soka, alitaka kuwashirikisha marafiki zake katika uzoefu huo wa kipekee.
“Nililiomba eneo lote la uwanja liwe langu,” anasema Costacurta.
“Niliwaalika kundi la marafiki ambao hawakuwahi kucheza San Siro, akiwemo mchinjaji wangu na mtu ninayemfahamu kutoka benki. Tulicheza 11 dhidi ya 11; timu moja ikiwa na jezi nyeupe na nyingine jezi nyekundu na nyeusi, bila mashabiki uwanjani.
“Kwao ilikuwa ndoto kutimia, na kwangu pia ilikuwa ndoto kuwaonyesha San Siro.”
Wikiendi iliyopita, San Siro ulitimiza miaka 100 tangu ulipozinduliwa. Sherehe za kumbukumbu zilifanyika Jumamosi Septemba 19, 2026, huku AC Milan ikicheza dhidi ya Lecce, Jumapili Septemba 20, 2026.
Lakini pamoja na historia yake kubwa, siku za uwanja huo zimeanza kuhesabika.
San Siro bado unasimama kwa fahari, ukiwa na nguzo zake maarufu zinazopinda kwa mtindo wa mzunguko na mihimili yake ya rangi nyekundu. Hata hivyo, kabla ya mwisho wa mwaka huu, mwonekano wa uwanja mpya ambao utakuwa makao ya AC Milan na Inter Milan unatarajiwa kuzinduliwa.
Mwaka 2023, ESPN ilichambua changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiukabili uwanja huo. San Siro ulikuwa umeanza kutokidhi mahitaji ya kisasa, huku AC Milan na Inter zikikosa mapato muhimu ya kibiashara ambayo yangeweza kupatikana katika uwanja wa kisasa.
Jambo hilo limezua mjadala mkubwa mjini Milan.
Baadhi wanaamini San Siro unapaswa kuheshimiwa kwa kiwango sawa na alama nyingine maarufu za jiji hilo, kama Duomo, La Scala au mchoro maarufu wa Leonardo da Vinci, The Last Supper.
Luigi Corbani, aliyekuwa naibu meya wa Milan na rais wa Comitato Si Meazza, aliwahi kuuelezea uwanja huo kwa mtazamo huo mwaka 2023.
Pamoja na mjadala huo, AC Milan na Inter zilitambua hazingeweza kuendelea kutumia San Siro katika hali yake ya sasa.
Zilikuwa na machaguo manne ambao ni kuubomoa na kujenga uwanja mpya katika eneo hilo hilo; kuufanyia ukarabati mkubwa; kujenga uwanja mpya jirani na San Siro na baadaye kuubomoa wa zamani; au kuendelea kuutumia kwa miaka michache huku zikitafuta eneo lingine.
Baada ya mijadala mirefu na taratibu nyingi za kiutawala, zilichagua chaguo la tatu ambalo ni kujenga uwanja mpya jirani na San Siro, kisha kuubomoa uwanja wa zamani.
“Ngazi zake zinazozunguka na minara yake mirefu ni alama ya usanifu wa Milan,” anasema Corbani.
“Kwa nini ubomoe uwanja wa kihistoria ambao bado unafanya kazi vizuri na ambao tiketi zake zimekuwa zikiuzwa zote tangu mwanzo wa msimu?”
Hivyo basi, Uwanja wa San Siro siku zake za kuwa mwenyeji wa mechi kubwa zinaelekea ukingoni.
“San Siro ni miongoni mwa maeneo maarufu zaidi duniani,” anasema Costacurta.
“Nimecheza dhidi ya na pamoja na baadhi ya wachezaji bora kabisa hapo. Watu wanauita Scala del Calcio kwa maana ya Kanisa Kuu la Soka.”
ROHO YA SAN SIRO ITAENDELEA KUISHI
San Siro umekuwa uwanja wa nyumbani wa AC Milan tangu mwaka 1926, wakati Piero Pirelli, aliyekuwa rais wa klabu hiyo na mtoto wa Giovanni Pirelli, mwanzilishi wa kampuni maarufu ya matairi ya Pirelli, alipoujenga.
Mechi ya kwanza ilichezwa Septemba 19, 1926, dhidi ya majirani zao Inter. Inter ilishinda kwa mabao 6-3, ingawa haikuhamia San Siro hadi mwaka 1947.
Sehemu ya kati ya uwanja, yenye minara 11 na ngazi zake maarufu zinazozunguka, iliongezwa mwaka 1955. Uwezo wa uwanja ukaongezeka kutoka watazamaji 35,000 hadi 85,000.
Huo ndio ulikuwa wakati ambao mashabiki wa AC Milan walikusanyika kwa wingi kuitazama Gre-No-Li, safu maarufu ya washambuliaji watatu wa Sweden ambao ni Gunnar Gren, Gunnar Nordahl na Nils Liedholm.
Mwaka 1980, uwanja huo ulipewa jina la Stadio Giuseppe Meazza, kwa heshima ya mshambuliaji huyo aliyecheza mechi 408 akiwa Inter na pia kucheza misimu miwili akiwa AC Milan.
Sehemu ya juu ya uwanja, ikiwa na mihimili yake maarufu ya rangi nyekundu na kuupa mwonekano unaofanana na chombo cha angani, ilijengwa kabla ya Kombe la Dunia la FIFA la mwaka 1990.
“San Siro ni wa kipekee,” anasema kiungo wa zamani wa AC Milan, Demetrio Albertini, aliyekuwa mchezaji wa klabu hiyo kuanzia 1988 hadi 2002.
“Uwanja wenyewe ni wa kipekee, umejaa hisia na kumbukumbu ambazo zitaendelea kubaki nami. Labda viwanja vilivyoniachia alama kubwa zaidi ni Bernabéu na Camp Nou. Vyote ni maarufu kwa namna yake, lakini ni tofauti. Mashabiki nao ni tofauti; wetu wana shauku zaidi na hisia huwa kali zaidi.”
Costacurta anaujua San Siro kwa undani na anafahamu presha ya kucheza ndani ya kuta zake maarufu.
“Baadhi ya wachezaji wanapenda presha hiyo, wengine wanaogopa, lakini mimi nilihisi ilikuwa hisia ya kipekee,” anasema.
“Kuanzia hapo, nilitaka kuichezea AC Milan katika uwanja huo. Ulinipa msukumo. Nilipokuwa na umri wa miaka 13 hadi 19, hilo ndilo nililokuwa nikifikiria siku moja kusimama pale nikiwa nimevaa jezi nyekundu na nyeusi na kumpasia mpira mwenzangu.
“Unaposimama kwenye handaki ukisubiri kuingia uwanjani, tumbo huanza kujaa hisia. Unaihisi presha ndani yako. Kisha unapofunga bao au kufanya jambo vizuri, unasikia kishindo cha mashabiki.
“Nimecheza Wembley, Santiago Bernabéu na Camp Nou, lakini hakuna kinachofanana na kishindo unachokisikia San Siro. Hata baada ya miaka 19 bado nakikumbuka. Ni kitu cha kipekee.”
Albertini, ambaye alicheza mechi 406 akiwa na AC Milan kuanzia 1988 hadi 2002, anaongeza: “Hisia za San Siro hazikuachi hata baada ya kucheza mechi nyingi kiasi gani hapo. Unazihisi pale mashabiki wanapoitikia vibaya baada ya timu kufanya vibaya, pia unahisi nguvu zao zikiongezeka kabla ya mchezo kuanza.
“Sikuwahi kuuzoea uwanja huo, kwa hali yoyote ile. Kila mara nilijaribu kuzitumia hisia hizo kama msukumo wa kufanya vizuri zaidi.”
Albertini pia anakumbuka mchezo wake wa mwisho mwaka 2002, baada ya hapo maelfu ya mashabiki walibaki uwanjani ili kumpa heshima kwa kumpigia makofi.
Hali kama hiyo ilimkuta Costacurta, ambaye mchezo wake wa mwisho ulikuwa wa 663 dhidi ya Udinese, Mei 19, 2007.
“Ilikuwa mara ya kwanza nilipoona kwa kweli namna mashabiki wetu walivyonishukuru. Huenda sikuliona hilo katika kipindi chote cha maisha yangu ya soka hadi wakati huo,” anasema.
“Tulikuwa marafiki, mashabiki na mimi kwa miaka 20. Lakini katika urafiki, wakati mwingine ni vigumu kueleza kila kitu. Katika mechi ile tuliweza kufanya hivyo.
“Nilipoondoka uwanjani kwa mara ya mwisho, kulikuwa na mashabiki 10,000 wakinisubiri. Sikuweza hata kuendesha gari langu kwa sababu watu walikuwa wengi sana. Ilikuwa ishara kubwa sana ya upendo.”
Costacurta pia anakumbuka nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2003 dhidi ya Inter. Mechi hiyo iliisha kwa sare ya 1-1, lakini AC Milan ikaenda fainali kwa kutumia sheria ya mabao ya ugenini.
Miaka miwili baadaye, katika mechi nyingine ya dabi, kipa wa Milan, Dida, alipigwa kichwani na fataki. Tukio hilo lilikumbukwa kupitia picha maarufu ya Rui Costa na Marco Materazzi wakitazama uwanja wa San Siro ukiwa umefunikwa na moshi mwekundu.
“AC Milan tulitaka kila mara kutoa burudani,” anasema Costacurta.
“Tulitaka kuwa timu bora zaidi duniani, lakini pia kucheza soka la kuvutia zaidi. Tulicheza kwa ustaarabu.”
SASA WANATAKA KUSONGA MBELE
Magwiji wa AC Milan wameacha historia ambayo haiwezi kufutwa kwa kubomolewa uwanja. Kumbukumbu zao zitaendelea kuwepo hata katika uwanja mpya.
Hata hivyo, mjadala kuhusu hatma ya San Siro imetawala Milan kwa zaidi ya muongo mmoja.
Uwanja huo bila shaka ni sehemu muhimu ya historia na utamaduni wa Milan, lakini kulikuwa pia na hoja ya kibiashara: San Siro ulikuwa umezeeka, huku AC Milan na Inter Milan zikikosa fursa muhimu za kuongeza mapato kupitia huduma za kisasa za kibiashara na maeneo maalumu kwa kampuni.
Klabu hizo zilikuwa zikiviangalia kwa hamu viwanja vya kisasa kama cha Tottenham. RedBird, wamiliki wa AC Milan, walitambua kwamba Rossoneri walihitaji uwanja mpya. Majirani zao Inter nao walikuwa na mtazamo huo.
Msumari wa mwisho kwenye hatma ya San Siro uliingia Septemba 2024, wakati UEFA ilipoiondoa Milan kwenye orodha ya wenyeji wa fainali ya Ligi ya Mabingwa ya mwaka 2027. San Siro katika hali yake ya sasa pia haukuwa kwenye mpango wa kuwa mwenyeji wa Euro 2032.
AC Milan na Inter zilinunua ardhi hiyo kutoka kwa halmashauri ya jiji, Novemba 2025 kwa euro milioni 197, hatua iliyowaondolea kikwazo kimoja muhimu cha kiutawala.
Ujenzi wa uwanja mpya wa Milan, unaosimamiwa na kampuni za Foster + Partners na MANICA, unatarajiwa kuanza mwaka 2028. Lengo ni AC Milan na Inter Milan kuanza kuutumia mwaka 2031.
Uwanja wa zamani utavunjwa hatua kwa hatua, tofali baada ya tofali na mnara baada ya mnara. Hatimaye utabaki kuwa sehemu ya kumbukumbu, yenye vivuli na mwangwi wa historia, badala ya kuwa uwanja wenye shamrashamra, kelele na msisimko unaoonekana kila wikiendi.
Msanii maarufu wa muziki wa rock, Bruce Springsteen, amefanya maonyesho San Siro mara kadhaa katika kipindi cha zaidi ya miaka 30 na mwaka 2019 alisema angehuzunika kuuona ukibomolewa.
Springsteen ameimba San Siro zaidi ya mara tano tangu mwaka 1985. Aliliambia gazeti la Corriere della Sera mwaka 2019: “Kuubomoa San Siro? Itakuwa jambo baya sana. Kila jengo lina roho yake, maisha yake ya kiroho. Na maadamu bado yana uhakika huo, napenda kucheza katika majengo hayo. Majengo mapya hayana roho hiyo.”
Albertini ana mtazamo tofauti. Anasema: “Nimecheza katika viwanja vingi ambavyo baadaye vilijengwa upya karibu viwanja vyote nilivyochezea vimefanyiwa mabadiliko lakini kinachobaki, bila kujali mabadiliko hayo, ni roho ya uwanja,” anasema.
“Na roho ya San Siro itaendelea kuishi katika uwanja mpya.”
Unaweza kumwelewa Costacurta kuwa na mtazamo tofauti na Springsteen. Licha ya kutumia sehemu kubwa ya maisha yake San Siro na hata kuishi karibu na uwanja huo, anaamini kwamba wakati mwingine ni lazima uchukue uamuzi mgumu kwa ajili ya maendeleo na usalama wa muda mrefu.
“Sikiliza, nilidhani nilikuwa nimepata upendo wa maisha yangu, nikamuoa, lakini tuliachana baada ya mwaka mmoja,” anasema Costacurta.
“Mwezi mmoja baada ya talaka, nilikutana na mwanamke mwingine na sasa nimeishi naye kwa miaka 32. Huo ni mfano mzuri.
“Nimefungamana sana na San Siro, lakini ninaamini klabu inahitaji kitu kipya na cha kisasa. Lazima usonge mbele. Huenda nimekuwa katika uwanja huo zaidi ya mara 500.
“Nimecheza mechi za AC Milan, mechi za kirafiki na pia mechi za timu ya taifa. Lakini ninaelewa kwa nini klabu inahitaji kusonga mbele.”