Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Pamba Jiji shida iko hapa

PAMBA Pict

Muktasari:

  • Mwenendo huo ni tofauti na ilivyoanza msimu uliopita, ambapo katika mechi zake sita za mwanzo ilikuwa tayari imekusanya pointi tisa, ikishinda mbili, kutoka sare tatu na kupoteza mchezo mmoja. Tofauti hiyo imeanza kuibua wasiwasi kuhusu mwenendo wa timu hiyo ambayo msimu uliopita ilimaliza katika nafasi ya saba.

PAMBA Jiji imeanza vibaya msimu wa 2026/27, ikiwa na mwanzo mgumu baada ya kupoteza mechi zake tano kati ya sita ilizocheza hadi sasa, ikiwa chini ya msimamo wa Ligi Kuu Bara, hali ambayo imeanza kuzua taharuki kubwa ndani na nje ya timu hiyo.

Mwenendo huo ni tofauti na ilivyoanza msimu uliopita, ambapo katika mechi zake sita za mwanzo ilikuwa tayari imekusanya pointi tisa, ikishinda mbili, kutoka sare tatu na kupoteza mchezo mmoja. Tofauti hiyo imeanza kuibua wasiwasi kuhusu mwenendo wa timu hiyo ambayo msimu uliopita ilimaliza katika nafasi ya saba.


PAMBA 01

MABAO 13 KUFUNGWA

Pamba hadi sasa imefunga mabao manne pekee huku ikiruhusu 13, ikiwa timu ya pili kwa kuruhusu mabao mengi baada ya Kagera Sugar ambayo imefungwa mabao 14.

Shida kubwa ya Pamba imeonekana kwenye eneo la ulinzi, kwani imeruhusu bao katika kila mchezo iliyocheza msimu huu. Safu ya ushambuliaji angalau imeonyesha uhai kwa kufunga katika mechi nne, huku ikicheza bila kufunga katika michezo miwili dhidi ya Yanga na JKT Tanzania.

ata hivyo, licha ya kufunga katika mechi nne, bado safu hiyo ina changamoto ya kutumia nafasi ambazo zimekuwa zikitengenezwa. Kushindwa kutumia nafasi hizo kumekuwa moja ya mambo yanayoifanya timu hiyo kushindwa kupata matokeo inayoyahitaji.


MAJERAHA YAWAKALIA

Ukiingia ndani ya kikosi cha Pamba, moja ya sababu kubwa ya mwanzo huo mbaya ni kuanza msimu ikiwa na majeruhi wengi. Baadhi ya wachezaji waliosajiliwa kama tegemeo walipata majeraha wiki chache kabla ya kuanza maandalizi ya msimu mpya.

Pamba ilimsajili kipa Mkenya, Steve Ochieng, aliyekuwa kipa wake namba moja akitokea Ligi Kuu Kenya, lakini baada ya kuanza kazi na timu hiyo alipata jeraha lililomuweka nje kwa muda mrefu. Kipa chaguo la pili, Erick Johola, naye alikumbana na changamoto ya majeraha, ingawa sasa amerejea na kuifanya timu hiyo kuwa na chaguo moja pekee la kipa aliyekuwa akitumika.

Mbali na Ochieng, Pamba pia ilimsajili beki Brian Eshianda ambaye licha ya kuchelewa kujiunga na timu hiyo, baadaye alikumbana na jeraha la muda mrefu. Pia beki wa kulia Abdallah Said ‘Lanso’ alikumbana na changamoto hiyo ya majeraha.


KIPA AUGUA UCHIZI

Baada ya mchezo dhidi ya Yanga ambao Pamba ilipoteza kwa mabao 2-0, kipa wake Onesmo Munishi, ambaye alifanya vizuri katika mchezo huo, alikumbana na hali ya kushtua baada ya kupata tatizo la kuchanganyikiwa akili, hatua ambayo ilizidi kuongeza changamoto katika eneo la makipa wa timu hiyo.


PAMBA 02

WACHEZAJI 22 WAPYA

Pamba ilipoingia msimu mpya ilikuwa na sura mpya kwa kiasi kikubwa baada ya kusajili wachezaji 22 wapya. Mabadiliko hayo yalihitaji muda wa kutosha kuwaunganisha wachezaji hao na wale waliosalia kutoka msimu uliopita.

Changamoto hiyo imekuwa kubwa zaidi kutokana na timu kuanza msimu bila kupata muda mrefu wa maandalizi ya pamoja, huku baadhi ya wachezaji wapya wakikumbana na majeraha mapema.


WALIONDOKA TATIZO

Baada ya kumaliza msimu uliopita katika nafasi ya saba, Pamba iliondokewa na baadhi ya wachezaji wake muhimu, akiwemo kipa namba moja Yona Amos pamoja na kiungo na nahodha wake James Mwashinga.

Kuondoka kwa wachezaji hao kumeacha pengo ambalo hadi sasa timu hiyo imekuwa ikihangaika kupata watu sahihi wa kuziba nafasi zao na kiwango walichokuwa wakikionyesha.


KIGOGO Pict

MIGOGORO NDANI KWA NDANI

Mbali na changamoto za uwanjani, ndani ya Pamba bado kunaonekana kukosekana umoja mkubwa katika eneo la utawala, huku baadhi ya viongozi wakitajwa kuwa na tofauti zao za chini kwa chini, jambo linaloweza kuathiri umoja unaohitajika katika kuisimamia timu.

Ndani ya Baraza la Madiwani nako kumekuwa na mgawanyiko, ambapo baadhi wanaona uwepo wa timu hiyo unaigharimu Serikali, huku wengine wakipinga hoja hiyo na kuona bado kuna umuhimu wa kuendelea kuipigania timu yao.


HAMDUNI ATAZIBA PENGO LA MTANDA?

Aliyekuwa mlezi mkubwa wa Pamba Jiji, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, ambaye sasa amehamishiwa Simiyu, alikuwa na nguvu kubwa katika kuipigania timu hiyo, hasa kwenye hamasa na mambo mengine yanayohusu maslahi ya wachezaji.

Ingawa Pamba inaendeshwa chini ya Halmashauri, sasa macho yanaelekezwa kwa Mkuu wa Mkoa mpya, CP Salum Hamduni, aliyeingia kuchukua nafasi ya Mtanda, kuona namna atakavyoshughulikia changamoto zinazoikabili timu hiyo.


MSIKI MWENYEKITI

Mwenyekiti wa Pamba Jiji, Anitha Rwezahura, akizungumzia changamoto hizo, alikiri wameanza ligi kwa kasi ya chini, huku akitaja uwepo wa majeruhi wengi ni moja ya sababu iliyowaangusha.

“Huwa sipendi sana kuzungumza, lakini ni kweli kwamba timu yetu haijaanza vizuri msimu huu. Shida kubwa ambayo tumekuwa tukikabiliana nayo ni uwepo wa majeruhi wengi. Kuna wachezaji wengi tuliwasajili, lakini bahati mbaya wakaumia,”alisema Rwezahura.

“Benchi la ufundi linaendelea kupigania hilo, lakini sisi kama uongozi tuna imani kwamba hizi changamoto zitapita, timu itasimama imara na Pamba itarudi kwenye ubora wake.”


PAMB 01

KOCHA BARAZA

Kocha wa timu hiyo, Mkenya Francis Baraza, naye amekiri kiwango cha chini ambacho timu yake imeonyesha, akisema majeraha pamoja na kuondokewa na wachezaji bora ni miongoni mwa mambo yaliyowaangusha.

“Kwanza nianze kwa kupongeza viongozi wangu kwa jitihada ambazo wamekuwa wakizichukua kwenye timu, lakini pili ni kweli tumeanza kwa kiwango cha chini msimu huu. Kubwa ambalo nitaliweka wazi ni suala la majeraha,” alisema Baraza.

“Kuna wachezaji wengi wapya ambao wakati tunawasajili tuliamini wangeweza kutupa kitu kikubwa, lakini walipofika tu wakaumia. Tulisajili kipa kutoka Kenya, alipoanza mazoezi akaumia. Tulileta beki wa kati mzuri ambaye naye ni Mkenya, lakini tulimtoa Ligi ya Zambia, alipofika wiki chache naye akaumia.”

Baraza alisema hali hiyo iliendelea kuwa ngumu baada ya kipa mwingine wa timu hiyo kukumbwa na tatizo la kiafya.

Wakati huo huo, Baraza alisema kurejea kwa baadhi ya wachezaji waliokuwa majeruhi kunawapa matumaini ya kubadilisha hali ya timu baada ya mapumziko haya.