Chilambo anavyotishia nafasi ya Kapombe, Duchu Simba
Muktasari:
- Chilambo, ambaye alijiunga na Simba dirisha hili, tayari amepata nafasi ya kucheza mechi mbili za Ligi Kuu msimu huu dhidi ya Pamba Jiji na Singida Black Stars akionyesha kiwango kizuri kilichowavutia mashabiki waliomsifia namna alivyoendana haraka na mahitaji ya mfumo wa Simba.
MIONGONI mwa wachezaji waliosajiliwa na Simba msimu huu na kuonyesha mwanga mapema kuliko ilivyotarajiwa ni beki wa kulia, Nathaniel Chilambo aliyetokea Azam FC.
Chilambo, ambaye alijiunga na Simba dirisha hili, tayari amepata nafasi ya kucheza mechi mbili za Ligi Kuu msimu huu dhidi ya Pamba Jiji na Singida Black Stars akionyesha kiwango kizuri kilichowavutia mashabiki waliomsifia namna alivyoendana haraka na mahitaji ya mfumo wa Simba.
Si beki wa pembeni anayekaba, kupanda na kushuka tu, pia aina yake ya uchezaji inampa Kocha Steve Barker chaguo tofauti, hasa Simba inapokuwa na mpira na kutaka kuongeza idadi ya wachezaji katikati ya uwanja.
SILAHA YAKE
Moja ya silaha kubwa ya Chilambo ni uwezo wa kuingia ndani wakati Simba inapokuwa kwenye umiliki wa mpira. Badala ya kubaki pembeni muda wote, anaweza kujisogeza eneo la kiungo na kuwa chaguo la ziada la kupokea pasi.
Hii ndiyo aina ya mabeki wa kisasa maarufu kama 'inverted full-back' na faida ya mchezaji wa aina hii ni anapohama kutoka pembeni kwenda ndani anaunda njia nyingine ya kuanzisha mashambulizi.
Viungo na wachezaji wanaocheza mbele yake wanapata mtu mwingine wa kumpa mpira, huku timu ikiwa na uwezo wa kuzungusha mpira bila kulazimika kila mara kupeleka mashambulizi pembeni.
Katika mfumo ambao Barker anataka wachezaji wake kubadilishana nafasi na kutengeneza machaguo mengi ya pasi, Chilambo anaonekana ameingia kwenye mfumo huo mapema.
CHA TOFAUTI
Dhidi ya Pamba Jiji na Singida Black Stars, Chilambo alionyesha kiwango bora akicheza dakika 180 akichukua nafasi ya Duchu ambaye alipata kadi nyekundu mechi ya kwanza dhidi ya Kagera Sugar, iliyoshinda mabao 2-1.
Baada ya hapo, akapata tena nafasi dhidi ya Singida Black Stars na alikuwa na majukumu mawili zaidi kutoka kucheza beki wa pembeni hadi kiungo mkabaji.
Mechi hizo zilikuwa muhimu kwake kwa sababu zimempa nafasi ya kuanza kujenga uelewano na wachezaji wenzake, kuelewa muda wa kupanda, kubaki na kuingia katikati.
KAZINI KWA DUCHU
Duchu ni beki anayecheza zaidi pembeni, akitumia kasi, nguvu na kupandisha mashambulizi eneo la kulia. Pia akipata nafasi, anaweza kusukuma timu mbele kwa kukimbia pembeni na kusaidia kutoa pasi za mwisho.
Lakini Chilambo anakuja na kitu ambacho kinaweza kumfanya Barker abadilishe namna anavyotumia nafasi hiyo.
Wakati Duchu akiifanya kazi hiyo vizuri pembeni, Chilambo anaweza kuifanya nafasi hiyo iwe sehemu ya kuunganisha pembeni na katikati.
Hiyo ndiyo tofauti kubwa kwa maana nyingine, si lazima Chilambo aichukue nafasi ya Duchu kwa kuwa na kasi zaidi au nguvu zaidi. Anaweza kumlazimisha Barker amchague kutokana na mahitaji ya mchezo.
Simba ikihitaji upana na mashambulizi ya pembeni, Duchu anaweza kuwa na faida. Lakini timu inapohitaji kuongeza mtu katikati na kutawala eneo la kiungo, Chilambo anaweza kuwa chaguo lenye maana zaidi.
BARKER ANA CHAGUO ZAIDI
Kitu kizuri kwa Barker ni ana machaguo mengi kulingana na mahitaji ya timu dhidi ya timu inayokaa nyuma, Chilambo anaweza kuwa muhimu kwa sababu kuingia kwake ndani kunaongeza mchezaji kwenye eneo ambalo mara nyingi huwa na msongamano.
Dhidi ya timu inayoshambulia kwa kasi pembeni, Barker anaweza kuhitaji beki anayebaki karibu zaidi na mstari wa pembeni na mwenye uwezo wa kukabiliana na winga hapo Duchu au Kapombe wanaweza kupata nafasi.
Kwa hiyo, usajili wa Chilambo hauleti ushindani wa nani ni bora kuliko nani tu bali unampa Barker aina tatu tofauti za silaha katika nafasi moja.
MTIHANI WAKE
Hata hivyo, Chilambo bado ana kazi. Kuonekana ameanza kuingia mapema kwenye mfumo hakumaanishi tayari ameshinda nafasi hiyo. Ligi ni ndefu, ratiba ni ngumu na Simba ina mechi za ndani na kimataifa.
Changamoto yake kubwa itakuwa kudumisha kiwango hicho, hasa wakati timu inapopoteza mpira. Kwa sababu anapoingia katikati, nafasi anayoiacha pembeni inaweza kuwa sehemu ambayo mpinzani atajaribu kuitumia kwenye mashambulizi ya kushtukiza.
Anapaswa kujua wakati wa kuingia ndani na wakati wa kubaki pembeni. Anapaswa kujua lini apande na lini asimame. Pia anapaswa kuhakikisha mabadiliko yake ya nafasi hayaiweki Simba kwenye hatari.
TAKWIMU ALIPOTOKA
Takwimu zake za msimu uliopita zinaonyesha hakuwa chaguo la moja kwa moja, kuna mechi alikuwa anaanza na zingine alikuwa benchi kwa Kocha Florent Ibenge kwani alikuwa akishindania namba na nahodha Lusajo Mwaikenda.
Msimu uliopita alicheza mechi 11 za Ligi Kuu kwa dakika 909. Lakini kuanza kupewa nafasi kwenye kikosi kipya unaweza kuwa mwanzo mzuri kwa beki huyo wa zamani wa Ruvu Shooting.
MSIKIE MKWASA
Akizungumzia juu ya kiwango cha Chilambo, Kocha wa zamani wa Taifa Stars, Boniface Mkwasa anasema "Ni mchezaji ambaye kwanza amekuwa na mwendelezo na amebadilika kiuchezaji hivyo nikimwona anaonyesha kiwango chake sishangai.
"Lakini kiasili Chilambo ni kiungo na ndiyo nafasi anayoipendelea zaidi ila nilimbadilisha (wakati yuko Ruvu Shooting) kusogea pembeni kwa sababu niliona anafaa zaidi na unaona namna anavyofanya kwa hiyo sikushangaa alichokifanya."