Prime
Chilambo anyoosha mambo, Barker afichua siri
Muktasari:
- Chilambo ambaye kwa kawaida hutumika kama beki wa kulia anayepanda kusaidia mashambulizi na kurejea haraka wakati wa ulinzi, katika mchezo huo uliochezwa juzi Jumamosi mkoani Singida, alipewa jukumu la ziada baada ya Simba kubaki na wachezaji 10 kufuatia kadi nyekundu ya Anthony Mligo.
SIMBA imeanza msimu mpya kwa kuonyesha sura tofauti ya kiuchezaji, hasa katika namna wachezaji wake wanavyoweza kubadilika majukumu kulingana na mazingira ya mchezo huku beki wa kulia, Nathaniel Chilambo akiwa mmoja wa walioonyesha uwezo huo katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Singida Black Stars.
Chilambo ambaye kwa kawaida hutumika kama beki wa kulia anayepanda kusaidia mashambulizi na kurejea haraka wakati wa ulinzi, katika mchezo huo uliochezwa juzi Jumamosi mkoani Singida, alipewa jukumu la ziada baada ya Simba kubaki na wachezaji 10 kufuatia kadi nyekundu ya Anthony Mligo.
Badala ya kubaki pembeni muda wote, Chilambo alitakiwa kutumia nafasi yake kwa namna tofauti, akicheza kama beki wa kulia lakini mara nyingi akiingia ndani zaidi ya uwanja na kuongeza idadi ya wachezaji wa Simba katika eneo la kati.
Hivyo, Chilambo alionekana kuwa na majukumu mawili kwa wakati mmoja kuhakikisha upande wa kulia unakuwa salama wakati timu inashambuliwa na kuingia katikati kuongeza nguvu wakati Simba ilipokuwa na mpira.
Ni aina ya jukumu ambalo linahitaji uelewa mkubwa wa mchezo kwa sababu mchezaji anatakiwa kujua wakati wa kubaki pembeni, wakati wa kuingia katikati na wakati wa kurudi haraka kwenye nafasi yake ya awali.
Akizungumzia mabadiliko hayo, Chilambo amesema kwake haikuwa tatizo kwa sababu mpira umebadilika, hivyo amekuwa tayari kuendana na mabadiliko hayo kwa ajili ya kusaidia timu.
"Kwangu haikuwa tatizo hata kidogo kubadilika kwa sababu mwalimu aliona kuna uhitaji wa kufanya hivyo na jambo jema ni kwamba tulipata ushindi, haikuwa mechi nyepesi hata kidogo kutokana na upinzani ambao walionyesha Singida," amesema beki huyo aliyetua Simba msimu huu akitokea Azam.
Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker, amesema mazingira ya mchezo huo hayakuwa rahisi, lakini alifurahishwa na namna vijana wake walivyopambana na kutekeleza mabadiliko ya kiuchezaji yaliyohitajika.
“Ni mazingira magumu kuyaelezea kutokana na kile kinachoendelea, lakini nafurahia namna vijana walivyojitoa, hasa pale ilipobidi kufanya mabadiliko ya kiuchezaji,” amesema Barker.
Barker amesisitiza kwamba, katika mazingira kama hayo, jambo muhimu si mchezaji kucheza nafasi yake ya kawaida pekee, bali ni timu kuwa tayari kubadilika na kila mchezaji kuelewa wajibu wake.
“Unapokuwa pungufu, lazima uwe tayari kubadilika. Wachezaji wanapaswa kuelewa kwamba wakati mwingine unatakiwa kufanya kazi ambayo siyo nafasi yako ya kawaida kwa ajili ya timu,” amesema Barker.
Mchezo dhidi ya Singida ulikuwa wa tatu mfululizo kwa Simba kuonyeshwa kadi nyekundu katika Ligi Kuu Bara msimu huu, baada ya awali kumaliza pungufu dhidi ya Kagera Sugar kwa David Kameta 'Duchu' kuonyeshwa kadi nyekundu na Pamba Jiji ambapo Ibraheem Jabaar alionyeshwa kadi nyekundu.
Licha ya changamoto hiyo, Simba imefanikiwa kupata pointi zote tisa katika michezo yake mitatu ya kwanza ugenini, jambo linaloonyesha uwezo wa timu hiyo kuvumilia mazingira magumu na bado kupata matokeo.
Sasa Simba inarejea Dar es Salaam kwa ajili ya michezo miwili mfululizo ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Coastal Union (Agosti 27) na Geita Gold (Agosti 31), kabla ya kuanza safari ya kimataifa kwenda Malawi kucheza dhidi ya Mighty Wanderers FC katika Ligi ya Mabingwa Afrika.