Cheki utabiri chama lako EPL linavyoanza
Muktasari:
- Mabingwa Arsenal watataka kuanza vizuri katika harakati za kutetea ubingwa huku Liverpool, Chelsea na Manchester United wakitarajia kuungana nao pamoja na Manchester City katika kuwania nafasi za juu.
LONDON, ENGLAND: LIGI Kuu England (EPL), inaanza leo usiku. lakini Supercomputer ya Opta imetoa utabiri wake wa mechi za kwanza za msimu wa 2026/27, huku timu zote zikianza msimu mpya bila matokeo ya nyuma kubeba uzito.
Mabingwa Arsenal watataka kuanza vizuri katika harakati za kutetea ubingwa huku Liverpool, Chelsea na Manchester United wakitarajia kuungana nao pamoja na Manchester City katika kuwania nafasi za juu.
Kwa upande mwingine, Coventry City, Hull City na Ipswich Town zitalenga kudhihirisha mapema huku zikijaribu kuepuka kurejea Championship msimu mmoja tu baada ya kupanda daraja. Mechi za raundi ya kwanza zilianza kupigwa leo, Ijumaa, kesho Jumamosi, keshokutwa Jumapili na keshokutwa Jumatatu. Huu hapa ni utabiri wa supercomputer ya Opta kwa mechi hizo.
ARSENAL VS COVENTRY CITY
Achana na matokeo ya mechi ya jana, kwa asilimia 80.4, Arsenal ndiyo timu iliyokuwa inatajwa kuwa na nafasi kubwa zaidi ya kushinda.
Hilo siyo jambo la kushangaza kutokana na Arsenal kushinda mechi yake ya kwanza katika kila msimu kati ya minne iliyopita ya ligi hiyo.
The Gunners pia wameshinda mechi zote tatu za kwanza za ligi walizocheza wakiwa mabingwa watetezi, huku ushindi mara mbili ukiwa dhidi ya timu zilizopanda daraja.
Kocha Mikel Arteta pia alikuwa anawinda ushindi wake wa 150 wa ligi hiyo akiwa Arsenal na alikuwa hajafungwa katika mechi tano zilizopita dhidi ya timu inayofundishwa na Frank Lampard katika mashindano yote, tangu alipofungwa katika pambano lao la kwanza.
HULL CITY VS MAN UNITED
Mechi za kesho, Jumamosi zitaanza kwa Hull City, timu iliyopanda daraja kuikaribisha Manchester United kwenye Uwanja wa MKM.
Hull ina nafasi ndogo ya kuanza msimu ikivuna pointi tatu ikiwa imeshinda asilimia 12.9, ikilinganishwa na 68.1 za Manchester United. Hivyo, United ndiyo inayopewa nafasi kubwa kushinda ugenini.
Ikumbukwe Hull haijawahi kuifunga United katika mechi zake 10 za ligi hiyo dhidi yao, ikiwa na sare mbili na kufungwa nane. United, ambayo sasa iko chini ya Michael Carrick haijawahi kupoteza katika ligi hiyo inapocheza na timu iliyopanda daraja katika mechi yake ya kwanza ya msimu.
Rekodi yake ni ushindi mara tisa na sare tatu. Carrick ameshinda mechi nne kati ya sita alizokutana na Hull kama kocha katika mashindano yote, huku United ikiwa imeshinda mechi ya kwanza ya msimu wa Ligi Kuu England mara 22, rekodi bora kuliko timu nyingine yoyote.
EVERTON VS PALACE
Katika mechi za saa 11:00 jioni, Pierre Sage atataka kuanza vizuri Crystal Palace ugenini dhidi ya Everton.
Palace imekuwa na makocha 16 tofauti kusimamia mechi za ligi hiyo wakiwemo makocha wa muda, lakini ni wawili tu kati yao walishinda mechi zao za kwanza. Wengine walipata sare nne na kupoteza 10.
Palace imeshinda mchezo mmoja kati ya 23 iliyokutana na Everton katika ligi hiyo ikiwa na sare 10 na kupoteza 12. Ushindi huo ulikuwa wa mabao 3-1 nyumbani Desemba 2021.
Ushindi wa mwisho ugenini dhidi ya Everton ulikuwa 2014/15. Everton imepoteza mechi yake ya kwanza katika kila msimu kati ya minne iliyopita, lakini utabiri unaonyesha inatarajia kuvunja mfululizo huo, ikiwa na asilimia 45.7 ya ushindi dhidi ya 28.4 za Palace. Kuna pia asilimia 25.9 ya uwezekano wa mchezo kumalizika sare.
IPSWICH TOWN VS SUNDERLAND
Timu zote zilizopanda daraja zitataka kuiga mafanikio ya Sunderland msimu uliopita kutokana na kazi nzuri iliyoifanya, ambapo Ipswich Town itaikaribisha Sunderland, huku kocha Gary O’Neill akipewa nafasi kubwa ya kuanza utawala wake kwa ushindi. Ipswich inapewa asilimia 45.5 ya ushindi. Timu hiyo iliifunga Sunderland mara mbili 2023/24 zilipokutana Championship, lakini haijawahi kuishinda mara tatu mfululizo.
Hata hivyo, Ipswich imepoteza mechi yake ya kwanza katika kila msimu kati ya minne iliyopita ya ligi hiyo. Sunderland inayopewa asilimia 27.6 ya kushinda, imeshinda mechi yake ya kwanza ya ligi katika misimu miwili iliyopita. Hii ndiyo mechi inayotajwa kuwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kumalizika kwa sare, ikiwa na asilimia 26.9.
NOTTINGHAM VS LEEDS UNITED
Oliver Glasner ni kocha mwingine mpya anayetarajiwa kuanza kwa ushindi wakati Nottingham Forest itakapowakaribisha Leeds United.
Makocha sita wa mwisho wa kudumu wa Forest walipoteza mechi zao za kwanza za ligi wakiwa madarakani. Hata hivyo, Glasner ameshinda mechi yake ya kwanza ya ligi akiwa kocha katika klabu nne kati ya tano alizowahi kufundisha, huku akipoteza moja.
Opta inatarajia ataanza safari yake City Ground kwa pointi tatu. Forest ina nafasi ya asilimia 43.1 ya kushinda dhidi ya Leeds yenye asilimia 30.9. Leeds ilimaliza msimu uliopita kwa nguvu baada ya kuepuka kushuka daraja, na imepoteza mechi yake ya kwanza katika misimu miwili tu kati ya 18 iliyopita ya ligi hiyo.
Msimu wa 2025/26 ulikuwa wa kukatisha tamaa kwa Forest iliyopunguza pointi zake kwa 21 ikilinganishwa na uliotangulia kutoka 65 hadi 44. Hata hivyo, ni timu nne pekee zilizokusanya pointi nyingi kuliko Forest katika mechi 10 za mwisho za ligi msimu uliopita, ambapo Forest ilipata pointi 17.
BRENTFORD VS SPURS
Mechi ya kwanza, kesho Jumamosi jioni itakuwa Brentford dhidi ya Tottenham Hotspur, ambayo imetumia fedha nyingi katika usajili na itataka kuepuka tena kujiingiza katika vita vya kushuka daraja.
Spurs imemuunga mkono kocha Roberto De Zerbi katika soko la usajili, lakini Brentford inaonekana kuwa na nafasi ndogo zaidi ya kushinda, ikiwa na asilimia 40.9, huku Spurs ikiwa na 34.2.
Hata hivyo, Spurs ni moja ya timu mbili pekee, pamoja na Chelsea, ambazo zimecheza zaidi ya mara moja Uwanja wa Brentford Community katika ligi hiyo bila kupoteza.
Kila moja imecheza mara tano bila kufungwa. Mechi nne kati ya tano ambazo Spurs imecheza uwanjani hapo ziliisha kwa sare, huku ushindi pekee ukiwa Februari 2025.
Brentford imeanza msimu wa ligi kwa ushindi mara tatu katika misimu 14 iliyopita, ikiwa na sare sita na kufungwa mara tano.
Kuanzia mwanzoni mwa Machi hadi mwisho wa msimu wa 2025/26, Burnley pekee ndiyo iliyoshinda mechi chache za ligi hiyo kuliko Brentford, ambayo ilishinda moja, sare saba na kupoteza mbili. Hivyo, Spurs inaweza kuingia katika mchezo huo ikiwa na matumaini.
ASTON VILLA VS BRIGHTON
Aston Villa imepitia mabadiliko makubwa ikiwa imewauza wachezaji nyota kama Youri Tielemans na Morgan Rogers. Ezri Konsa naye anajiunga na Arsenal.
Brighton, kwa upande mwingine haijafanya shughuli kubwa katika dirisha la usajili, ingawa Carlos Baleba anaonekana kuwa njiani kujiunga na Manchester United.
Brighton inapewa nafasi kubwa Jumapili, ikiwa na asilimia 44.2 dhidi ya Villa yenye 31.4. Uwezekano wa sare ni asilimia 24.5. Hata hivyo, Villa haijapoteza katika mechi zote nne za ligi hiyo dhidi ya Fabian Hurzeler, ikiwa imeshinda tatu na kutoka sare moja.
Tangu ifungwe 3-1 na Chelsea katika mechi ya kwanza msimu wa 2020/21, Brighton haijapoteza mechi yake ya kwanza katika misimu mitano ya Ligi Kuu England ikiwa imeshinda minne na sare moja.
Mustakabali wa straika Ollie Watkins bado haujawa wazi, lakini ana rekodi nzuri dhidi ya Brighton.
Hakuna timu nyingine ambayo Watkins amehusika katika mabao mengi ya ligi hiyo kama Brighton ikiwa ni 11, akifunga tisa na asisti mbili. Mabao hayo yote yamepatikana katika mechi zake tisa za mwisho dhidi yao.
MAN CITY VS BOURNEMOUTH
Enzi za Manchester City baada ya Pep Guardiola zilianza kwa kipigo cha aibu cha mabao 3-0 dhidi ya Arsenal katika Ngao ya Jamii Jumapili iliyopita. City pia imemuuza kiungo wake nyota Rodri, huku ikikabiliwa na mtihani mwingine dhidi ya Bournemouth nyumbani.
Mechi hiyo haitakuwa rahisi kwa kocha Enzo Maresca. Hata hivyo bado inatabiriwa kwamba City itashinda, ikiwa na nafasi ya asilimia 63.3, huku Bournemouth ikiwa na 16.9 pekee.
Makocha wanne wa mwisho wa City, wakiwemo makocha wa muda, wote walishinda mechi zao za kwanza za ligi.
Kocha wa mwisho kupoteza mechi yake ya kwanza alikuwa Mark Hughes, Agosti 2008, alipochapwa 4-2 na Aston Villa.
Bournemouth haikupoteza hata mchezo mmoja kati ya 18 ya mwisho 2025/26 chini ya Andoni Iraola, ikiwa na ushindi mara nane na sare 10.
Huo ndiyo mfululizo mrefu zaidi wa kutopoteza kwa sasa katika ligi. Bournemouth pia iliongoza ligi msimu uliopita kwa mashambulizi ya moja kwa moja, ikiwa nayo 83, na hakuna timu iliyofunga mabao mengi kutokana na mashambulizi hayo kuliko wao yakiwa ni sita.
Straika Antoine Semenyo atakutana na klabu yake ya zamani. Alifunga bao kwa Bournemouth katika mechi yao ya kwanza katika kila misimu miwili iliyopita ya Ligi Kuu.
NEWCASTLE UNITED VS LIVERPOOL
Mechi kubwa ya kwanza itakuwa Newcastle United dhidi ya Liverpool, huku timu zote zikiwa chini ya makocha wapya. Kuondoka kwa Eddie Howe katikati ya maandalizi ya msimu lilikuwa jambo la kushangaza kwa Newcastle, ambayo sasa iko chini ya kocha Matthias Jaissle.
Liverpool, kwa upande mwingine ilimtimua Arne Slot mwishoni mwa msimu uliopita na kumteua Iraola, aliyefanya kazi nzuri akiwa Bournemouth.
Msimu uliopita kipindi kama hiki kulikuwa na drama kubwa kati ya Newcastle na Liverpool kutokana na sakata la Alexander Isak. Mechi kama hii msimu uliopita iliishia Liverpool kushinda 3-2.
Jumla ya mabao 198 yamefungwa katika mechi za Ligi Kuu kati ya Newcastle na Liverpool. Mabao mawili zaidi katika mchezo huu yataufanya kuwa wa tatu katika historia ya ligi hiyo kufikisha 200, baada ya Liverpool dhidi ya Tottenham (211) na Arsenal dhidi ya Tottenham (200).
Newcastle haijashinda katika mechi 19 zilizopita za ligi hiyo dhidi ya Liverpool, ikiwa na sare tano na kufungwa 14. Hata hivyo, mfumo wa utabiri unaona mchezo huo kuwa mgumu kutabiri, ingawa unaipa Newcastle nafasi ndogo ya ushindi kwa asilimia 39.9 dhidi ya Liverpool 33.5. Uwezekano wa sare ni asilimia 26.6.
FULHAM VS CHELSEA
Mechi ya kwanza itafungwa kwa Dabi ya London Magharibi kati ya Fulham na Chelsea kwenye Uwanja wa Craven Cottage, ambapo makocha wawili waliokuwa Real Madrid msimu uliopita watakutana.
Alvaro Arbeloa alichukua nafasi ya Xabi Alonso Santiago Bernabeu mwezi Januari, ingawa naye hakudumu muda mrefu kama kocha wa Los Blancos.
Watakuwa makocha wa 10 na 11 kuchukua timu Ligi Kuu England kwa mara ya kwanza wikendi hii. Hii ndiyo idadi kubwa zaidi ya makocha wapya kwenye mechi ya kwanza katika msimu mmoja katika historia ya ligi hiyo ukiondoa msimu wa 1992/93. Alonso ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kushinda, huku Chelsea ikiwa na ushindi wa asilimia 48.8 kabla ya mechi, wakati Fulham 26.7.
Chelsea haijashinda mechi yake ya kwanza ya msimu wa Ligi Kuu England katika misimu mitatu iliyopita, ikiwa na sare mbili na kupoteza moja.
Mara ya mwisho kutoshinda mechi ya kwanza kwa misimu minne mfululizo ilikuwa kati ya 1995/96 na 1998/99.
Fulham, kwa upande wake, imeshinda mechi yake ya kwanza katika msimu mmoja tu kati ya sita iliyopita ya ligi hiyo ikiwa iliifunga Everton msimu wa 2023/24.