Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chasambi na Balua wamenipiga mtama mchana kweupe

HISIA Pict

Muktasari:

  • Kwa Chasambi niliona namna amavyokokota mpira kwa ustadi. Kwa Balua nilipenda pia jambo hilo, lakini pia mashuti yake na namna anavyoweza kukata mipira yake katika faulo na kona.

NILIJIGAMBA sana mwanzoni mwa msimu kwamba huenda Ladaki Chasambi na Edwin Balua wangekuwa moto katika safu ya ushambuliaji ya Simba. Kumbe nilikuwa najidanganya tu. Napenda wachezaji wazawa wanapofanikiwa katika timu zetu. Nilikuwa najidanganya tu.

Kwa Chasambi niliona namna amavyokokota mpira kwa ustadi. Kwa Balua nilipenda pia jambo hilo, lakini pia mashuti yake na namna anavyoweza kukata mipira yake katika faulo na kona. Kabla sijawaona nilikuwa nasimuliwa na waandishi wenzangu namna vijana hao mmoja kutoka Prisons mwingine kutoka Mtibwa Sugar walivyokuwa bora.

Zaidi ni namna ambavyo usajili wao ulitingisha. Unakumbuka dau ambalo Simba waliweka katika akaunti ya Chasambi kwa ajili ya nguvu za kuwashinda watani wao Yanga ambao ilidaiwa pia kuwa na wao walikuwa wanamtaka staa huyu wa Mtibwa Sugar. Hata kwa Balua hadithi ilikuwa hii kwamba Yanga walikuwa wanamtaka, lakini Simba wakapanda ndege kwa haraka kumalizana naye Mbeya.

Ukisikia simulizi hizi ulikuwa unapata picha kwamba Simba walikuwa wamenasa mawe mawili ya madini kama ambayo Mzee Laizer aliyanasa kule Arusha. Hata hivyo, kwa sasa yanaonekana sio madini tena na muda wowote ule wanaweza kutolewa kwa mkopo kwenda kwingineko. Hakuna ambaye atashangaa kama Simba wakichukua hatua hiyo.

HIS 01

Niliamini wangefuata nyayo za Clement Mzize aliyepasua katika kundi la washambuliaji wazuri wageni pale Yanga kisha akawa tegemeo klabuni. Katika mpira wetu hizi timu kubwa maeneo ya ulinzi na kiungo wazawa wamepambana kupata nafasi. Kule mbele baada ya kuondoka kwa John Bocco inaonekana Clement Mzize amerithi makali hayo japo kwa ujumla wake hajafukia mambo ambayo Bocco amefanya.

Hawa vijana wangu Chasambi na Balua kwa namna nilivyowaona mwanzoni mwa msimu niliamini wana kitu. Kitu ambacho kingelisaidia taifa katika siku za usoni. Kadri siku zilivyokwenda mbele ndivyo walivyoanza kupotea taratibu uwanjani. Walichoniangusha zaidi ni kwamba walishindwa kupata nafasi za kudumu katika Simba hii ambayo awali ilionekana kama inasuasua katika eneo la ushambuliaji.

Ndiyo, Leonel Ateba hajaeleweka mpaka leo miongoni mwa washambuliaji wa Simba. Joshua Mutale amekuja kueleweka mwishoni zaidi. Kama Chasambi alishindwa kuipora nafasi ya Mutale wakati ule atawezaje kuipora leo? Kibu Dennis hajawa na msimu mzuri, lakini bado Fadlu Davis anaona bora ampange Kibu kuliko Balua au Chasambi. Nini kimewatokea vijana hawa?

HIS 02

Mbona Mzize alipambana katika nyakati ngumu ambapo kulikuwepo na Fiston Mayele na Kennedy Musonda waliokuwa wanatisha katika safu ya ushambuliaji ya Yanga? Ni kitu cha kujiuliza. Je kocha ana matatizo au wao wana matatizo? Watu wangu wa ndani wa Simba wananiambia vijana wetu ndio tatizo. Mmoja kati ya hao amewahi kufeli mara nne vipimo vya pombe vinavyoandaliwa ghafla na kocha Fadlu. Aibu iliyoje.

Na katika hali halisi. Hawa makocha kama Fadlu sio makocha wa kubabaisha. Wamekuja nchini kwa ajili ya kutetea ajira zao. Wanawezaje kumuweka nje mchezaji mzuri bila sababu za msingi? Hili linatokea wakati Simba ikiwa imekabiliwa na mechi nyingi msimu huu kwa sababu imefika mbali katika michuano ya kimataifa.

Wamefika fainali za Shirikisho. Wako eneo la kileleni la msimamo wa ligi. Lakini pia wamefika nusu fainali za FA yetu. Na hata Fadlu alipopumzisha mastaa kibao katika pambano la nusu fainali dhidi ya Singida Black Stars bado hatukuweza kuwaona vijana wetu wakianza. Na sasa ni wazi kwamba hawa vijana wamenipiga mtama hadharani. Mchana kweupe. Wamefifisha ndoto zangu.

HIS 03

Kuna ile dhana kwamba wachezaji hawa labda wanashindwa kwa sababu ya presha ya kucheza katika timu kubwa. Sidhani kama ni hilo. Siku hizi tuna kundi kubwa la vijana ambao hawamezwi na presha yoyote na wala hawaendekezi presha. Basi tu vijana wetu hawa wameshindwa kuwa na mwendelezo wa ubora (consistency).

Chasambi aliwahi kufunga huko mwanzo. Balua aliwahi kufunga kwa faulo maridadi huko mwanzo na kisha akafunga bao zuri katika pambano dhidi ya Al Ahly Tripoli ya Libya hapa katika Uwanja wa Mkapa. Ulikuwa msingi mzuri wa kujiamini baina yao. Inaelezwa kwamba mchezaji akipata nyakati chache tu nzuri anaweza kuimarika vilivyo na kupata uwezo mkubwa wa kujiamini.

Inachoonekana ni kwamba kila baada ya hapo walishindwa kurudia uwezo wao mazoezini na kumshawishi Fadlu awapange. Hakuna siri kubwa zaidi ya kufanya vyema mazoezini. Wakati mwingine kama unafanya vyema mazoezini unawafanya hata wachezaji wenzako wamlazimishe kocha akupange katika mechi. Imetokea mara nyingi.

HIS 04

Mbona Yusuf Kagoma katika msimu wake wa kwanza Msimbazi anacheza kama vile amekuwa katika timu kwa miaka lukuki? Anafanya anachokiweza bila hofu kwamba amevaa jezi ya moja kati ya timu mbili kubwa zaidi nchini na ambazo zina mashabiki wengi kila zinapoingia uwanjani. Chasambi na Balua matatizo ni yao wenyewe.

Nipo Afrika Kusini katika michuano ya Cosafa. Kuna vijana kibao ambao hawana majina wapo hapa. Kama Chasambi na Balua wangefanya vizuri inamaanisha kwamba wangekuwa hapa kama mastaa wakubwa dhidi ya vijana wengi ambao wapo hapa achilia mbali Fei Toto na Simon Msuva ambao tunajua ukubwa wao.

Hii ina maana gani nyingine? Nawakumbusha tu wale wapigadebe ambao wanataka idadi ya wachezaji wa kigeni ipungue katika klabu zetu. Nawakumbusha tu haya mafanikio ambayo tunayashangilia kwa timu zetu katika mechi za kimataifa yanaletwa zaidi na wachezaji wa kigeni. Bila wachezaji wa kigeni sidhani hata kama tungekuwa tunaingia katika makundi achilia mbali kufika robo fainali.

HIS 05

Kinachonishtua zaidi ni kwamba ungesikiliza sifa za kina Chasambi wakati wanakwenda Simba hauoni kama kuna wachezaji wengine wazawa wanaoweza kushika nafasi zao pindi wao wakitolewa kwa mkopo. Ninawatazama wachezaji wawili ambao naweza kuwashikia dhamana ingawa na wao sijui mambo yatakuwa vipi kama wakienda timu kubwa.

Navutiwa na Often Chikola wa Tabora United. Namna anavyotumia mguu wa kushoto huku akicheza winga ya kulia. Sijui kwanini haitwi katika timu ya taifa, lakini hapo hapo nitashangaa kama jina lake halitawekwa katika orodha ya wazawa ambao wanatakiwa na timu kubwa. Hata hivyo, sina uhakika kama hatakuwa Edwin Balua mwingine.

Mwingine ni Idd Kipagwile wa Dodoma Jiji. Huyu aliwahi kucheza Azam. Ana kasi na anajua mpira. Na yeye nikisikia anatakiwa na Yanga au Simba sitashangaa sana. Hata nikisikia Azam wanamtaka tena sitashangaa ingawa sina uhakika kuwa na yeye hatakuwa Chasambi mwingine. Ebu tusubiri. Wakati utatuambia.