Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chama lako linatokaje wikiendi EPL!

WIKIENDI Pict

Muktasari:

  • Achana na mechi hizo, lakini katika EPL mechi moja ilivurumishwa usiku wa kuamkia leo, ambapo Ipswich Town ilikuwa Nottingham Forest, huku mechi nne zikitarajiwa kupigwa leo na zingine tano kesho. Twende pamoja!

LONDON, ENGLAND: WAKATI Manchester City inaongoza Ligi Kuu England (EPL), kipute kilirejea jana usiku baada ya mshikemshike wa michuano ya klabu za Ulaya ulioanza kupigwa Jumanne wiki hii hadi juzi, ambapo timu kibao zilikuwa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa, Europa na Conference League.

Achana na mechi hizo, lakini katika EPL mechi moja ilivurumishwa usiku wa kuamkia leo, ambapo Ipswich Town ilikuwa Nottingham Forest, huku mechi nne zikitarajiwa kupigwa leo na zingine tano kesho. Twende pamoja!


LEO, JUMAMOSI

Aston Villa itakuwa timu inayofuata kujaribu kusimamisha mwenendo mzuri wa Manchester City, ambayo imeanza msimu kwa ushindi katika mechi zote saba. City inaweza kuwa timu ya nane katika historia kushinda mechi nane za mwanzo za msimu katika ligi hiyo, ikifuata nyayo za Everton 1894/95, Sheffield United 1903/04, Tottenham 1960/61, Man United 1985/86, Liverpool 1990/91, Chelsea 2005/06 na Liverpool 2019/20.

Kwa uwezekano wa asilimia 43.2, City ndiyo timu inayopewa nafasi kubwa zaidi ya kupata ushindi ugenini katika mechi za wikiendi hii. Hata hivyo, City, ambayo iliichapa AEK Athens mabao 5-1 katika Ligi ya Mabingwa Ulaya katikati ya wiki, imepoteza mechi mbili zilizopita za ligi dhidi ya Villa. Mara ya mwisho kupoteza mechi tatu mfululizo dhidi ya Villa ilikuwa kati ya Agosti 1962 na Septemba 1966.

Kwa upande mwingine Villa ambayo ina uwezekano wa asilimia 31.7 wa kushinda, haijapoteza katika mechi tatu zilizopita za nyumbani dhidi ya timu zilizokuwa kileleni mwa msimamo wa ligi kabla ya kukutana nayo. Imeshinda mara mbili na kutoka sare moja. Pia, imekuwa katika kiwango kizuri, ikishinda mechi mbili kati ya tatu zilizopita za ligi na kutoka sare moja.

WIKI 01

Gemu nyingine ni ile ya Arsenal dhidi ya Everton, ambapo Arsenal itakuwa ikisubiri kuona kama Man City itateleza ili ipate nafasi ya kupunguza pengo la pointi. Hivyo, itakuwa na lengo la kupata pointi zote tatu dhidi ya Everton. Arsenal inapewa asilimia 69.6 kushinda, ikiwa ndiyo timu inayopigiwa hesabu kubwa zaidi ya kuibuka na ushindi wikiendi hii ikisukumwa na kutopoteza katika mechi saba zilizopita za ligi dhidi ya Everton, ikishinda tano na kutoka sare mbili.

Pia, imeshinda mechi 11 kati ya 12 zilizopita za Ligi Kuu England, huku kipigo kimoja tu kikiwa kimekatiza mfululizo huo. Katika mechi hizo, imeshinda michezo yote sita iliyocheza nyumbani kwenye Uwanja wa Emirates.

Rekodi yake ya ulinzi nayo inaendelea kuvutia. Hakuna timu iliyofungwa mabao machache kuliko Arsenal, ambayo imeruhusu mabao matano pekee. Pia, imekabiliwa na mashuti 21 yaliyolenga lango, huku ikiwa na rekodi ya mabao yanayotarajiwa 5.6, takwimu bora zaidi kuliko timu nyingine yoyote. Kwa upande wa Everton haijashinda katika mechi zake nane zilizopita za ligi ikiwa ugenini, ikipata sare tano na kupoteza tatu.

Mechi zake zote tatu za ugenini msimu huu zimeisha kwa sare, ikipewa asilimia 17.1 kupata sare na 13.3. Hata hivyo, rekodi yake dhidi ya Arsenal ugenini ni mbaya. Everton imeshinda mara moja katika mechi 30 zilizopita za ligi ilizocheza ugenini dhidi ya Arsenal, sare tano na kupoteza 24.

Mchezo mwingine utakuwa kati ya Coventry City dhidi ya Fulham. Itakumbukwa kwamba Kocha Alvaro Arbeloa alipata ushindi baada ya Fulham kuifunga Hull City katika mchezo uliopita, na sasa anakabiliwa na mtihani mwingine dhidi ya Coventry City, timu iliyopanda daraja.

WIKI 02

Fulham inapewa asilimia 29.9 kushinda, huku Coventry ikiwa na 43.4. Hii itakuwa mara ya tatu timu hizo kukutana katika Ligi Kuu England, na ni mara ya kwanza tangu 1967/68. Fulham haijapoteza zilipokutana mara mbili hivi karibuni, ikishinda moja na sare moja. Hata hivyo, Fulham haijashinda katika mechi nane zilizopita za ligi ugenini. Katika mechi hizo, imekuwa ikibadilishana sare na vipigo, ikitoka sare nne na kupoteza  nne.

Kwa asilimia 26.7, mchezo huu ni miongoni mwa mechi inayotarajiwa zaidi kuisha kwa sare wikiendi hii. Coventry imepoteza mechi tano kati ya saba za ligi msimu huu, ikishinda mbili. Ni mara ya kwanza tangu 1996/97 kupoteza mechi tano katika hatua hii ya msimu. Katika msimu huo, ilinusurika kushuka daraja siku ya mwisho.

Leo pia kuna mchezo kati ya Tottenham Hotspur dhidi ya Chelsea ambapo Spurs itataka kujenga juu ya ushindi wake wa Jumatatu dhidi ya Coventry itakapokutana na matajiri wa London ambao hawakuruhusu bao msimu huu walipoifunga Everton wiki iliyopita.

Chelsea inapewa asilimia 53.6 kushinda, ikiwa imeshinda mechi sita zilizopita za ligi dhidi ya Tottenham ukiwa ni mfululizo wake mrefu zaidi wa ushindi dhidi ya wapinzani hao, sawa na ilivyofanya kati ya Januari 2000 na Machi 2002. Chelsea pia imepoteza mchezo mmoja kati ya 16  nyumbani katika ligi dhidi ya timu nyingine za London. Kwa upande mwingine, Spurs imepoteza mechi sita zilizopita za ligi dhidi ya timu za London. Haijawahi kupoteza mechi saba mfululizo za aina hiyo.

WIKI 03

Tangu kuanza kwa msimu uliopita, Spurs imeshinda mechi mbili za ligi mfululizo mara mbili pekee na inapewa asilimia 22.6 ya kushinda dhidi ya Chelsea na 23.8 kutoka sare. Hata hivyo, rekodi yake katika Uwanja wa Stamford Bridge ni mbaya.

Spurs imeshinda mara moja katika safari 36 zilizopita za ligi uwanjani hapo, ikipata sare 11 na kupoteza 24. Ushindi huo ulikuwa wa mabao 3-1 msimu wa 2017/18 chini ya kocha Mauricio Pochettino. Tangu wakati huo, imekusanya pointi mbili pekee katika safari nane, baada ya kutoka sare mbili na kupoteza sita.


KESHO, JUMAPILI

Miongoni mwa mechi za mapema itakuwa kati ya Crystal Palace dhidi ya Newcastle United ambazo zitakuwa zinasaka kurejea kwenye ushindi zitakapokutana katika Uwanja wa Selhurst Park. Palace ilichapwa mabao 5-0 na wapinzani wake wa karibu, Brighton, wikiendi iliyopita.

Licha ya kipigo hicho, Palace inapewa nafasi kubwa zaidi ya kushinda mchezo huu, ikiwa na uwezekano wa asilimia 40.5 ikilinganishwa na 32.8 za Newcastle. Palace inataka kushinda mechi mbili mfululizo za ligi dhidi ya Newcastle kwa mara ya kwanza tangu ilipofanya hivyo katika mechi tatu kati ya Agosti 1971 na Septemba 1972.

Newcastle nayo imeshinda mara moja katika safari 11 zilizopita za ligi dhidi ya Palace katika Uwanja wa Selhurst Park, huku ikitoka sare sita na kupoteza nne. Palace haijafanya vizuri sana nyumbani hivi karibuni, lakini inalenga kushinda mechi mbili mfululizo za ligi kwa mara ya kwanza tangu Aprili 2025, iliposhinda tatu mfululizo.

Changamoto nyingine kwa Newcastle ni rekodi mbaya ya ugenini ikipoteza mara mbili zilizopita katika ligi kwa mabao 4-1 na Leeds United na Coventry mtawalia. Mara ya mwisho Newcastle kupoteza mechi nyingi zaidi mfululizo ugenini kwa tofauti ya mabao matatu au zaidi ilikuwa kati ya Januari na Machi 2008 ilipopoteza nne za aina hiyo.

Nayo Hull City itakuwa wenyeji wa Brentford, ambapo wikiendi iliyopita ilikuwa ya kukatisha tamaa kwa Brentford iliyopata kipigo chake cha kwanza cha ligi msimu huu na kumaliza mchezo ikiwa na wachezaji tisa dhidi ya Liverpool. Lakini, inapewa asilimia 38.1 kushinda leo, huku Hull ikiwa na 35.8. Hiyo itakuwa mara ya kwanza kwa timu hizo kukutana katika EPL.

WIKI 04

Brentford pia itakuwa ikisaka ushindi wake wa kwanza wa ligi huko Yorkshire, baada ya kutoka sare mara nne na kupoteza mchezo mmoja. Kwa Hull haijashinda katika mechi zake tano zilizopita, ikitoka sare tatu na kupoteza mbili, baada ya kuanza msimu kwa ushindi mara mbili mfululizo. Hata hivyo, bado haijapoteza mechi ya ligi nyumbani msimu huu, ikishinda moja na sare mbili.

Kwingine, Liverpool dhidi ya Brighton inayoingia katika wikiendi hii ikiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi, baada ya kushinda mechi nne zilizopita kwa jumla ya mabao 15-0. Pia, imeshinda mbili kati ya tatu zilizopita za ligi dhidi ya Liverpool, huku ikipoteza moja. Licha ya mwenendo huo, Brighton inapewa asilimia 26.8 tu kushinda, leo Jumapili, ukiwa juu kidogo ya uwezekano wa sare wa asilimia 26.4.

Liverpool ndiyo inayopigiwa hesabu kubwa zaidi ya ushindi, ikiwa na asilimia 46.8. Hata hivyo, Liverpool haijashinda katika mechi tano zilizopita za ligi nyumbani, ikitoka sare nne na kupoteza moja.

Ni mara mbili katika historia imewahi kuwa na mfululizo mbaya zaidi wa kutoshinda nyumbani katika ligi hiyo; kwanza ilikuwa mechi saba kati ya Novemba 2002 na Februari 2003, na pili mechi nane kati ya Desemba 2020 na Machi 2021.

Na huko Old Trafford, Manchester United itakutana na Bournemouth; United imekusanya pointi saba pekee katika mechi saba za ligi msimu huu  ikishinda moja, sare nne na kupoteza mbili.

Huo ni mwanzo wake mbaya zaidi wa msimu tangu 1989/90, ilipokusanya pointi saba katika mechi saba za kwanza. Changamoto inaweza kuendelea dhidi ya Bournemouth, ambayo United haijaifunga katika mechi sita zilizopita.

Bournemouth pia haijapoteza katika safari tatu zilizopita za ligi kwenye Uwanja wa Old Trafford, ikishinda mbili na sare moja, lakini pamoja na rekodi hiyo United inapewa nafasi kubwa zaidi ya kushinda kwa asilimia 48.5 dhidi ya 25.7 za Bournemouth, ilhali sare ikiwa ni asilimia 25.8.

Mechi za wikiendi zitafungwa katika Uwanja wa Stadium of Light, ambako Sunderland na Leeds United zitakuwa zikisaka kumaliza mfululizo wa kutopata ushindi. Sunderland imepoteza mechi nne zilizopita za ligi.

Mara ya mwisho ilipata mfululizo mrefu zaidi wa vipigo ilikuwa Desemba 2015. Pamoja na hali hiyo, Sunderland inapewa nafasi ndogo ya kushinda kwa asilimia 38.8 dhidi ya 34.7 za wapinzani wao na 26.5 itakuwa sare.

Sunderland imepata pointi nne katika mechi saba za ligi msimu huu, baada ya kushinda moja, sare moja na kupoteza tano. Hiyo ndiyo idadi ndogo zaidi ya pointi ambazo Sunderland imekusanya katika hatua hii tangu 2016/17 msimu ambao ilishuka daraja.

Kwa upande wa Leeds, imepoteza mara moja katika safari zake nane zilizopita za ligi dhidi ya Sunderland, ikishinda sita na sare moja.

Kipigo hicho kilikuwa cha mabao 2-0 Novemba 2001. Hata hivyo, Leeds haijawahi kushinda mechi ya Ligi Kuu England inayoanza saa 1:30 usiku katika majaribio yake manane, ikiwa imetoka sare tatu na kupoteza tano. Leeds ina sare nyingi zaidi za ligi mwaka huu wa 2026 kuliko timu nyingine yoyote, ikiwa nazo 13, ikiwemo ya mabao 1-1 dhidi ya Man United wikiendi iliyopita.