Prime
Adhabu za Saa 72, kituko kingine Ligi Kuu Bara
NILISHAANDIKA sana kuhusu uamuzi unaofanywa na watu wanaoangalia picha za marudio za video na kutoa hukumu iliyotakiwa ifanywe na mwamuzi wa kati, lakini inaonekana hawa jamaa, maarufu kama Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi, wameweka pamba masikioni.
Hawa wanaelekea hatua ambayo wataweza kufuta mabao yaliyokubaliwa na refa na kuhesabu mabao yaliyokataliwa na refa, iwapo hakutatokea jitihada za kukomesha tabia hiyo inayozidi kukua ya kufanya uamuzi wa mechi badala ya yule anayepewa dhamana kisheria.
Wakati tunaunda Kamati ya Mashindano, ambayo sasa ndio inayoitwa ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi au Kamati ya Saa 72, tuliweka mwongozo bayana kabisa wa jinsi kamati hiyo itakavyokuwa inafanya kazi.
Kamati inatakiwa ishughulikie yale maamuzi yaliyofanywa na refa tu na si kuanzisha uamuzi wake (kamati). Yaani kama refa alipuliza filimbi na kumuonyesha mchezaji kadi nyekundu ya moja kwa moja, basi kamati itakapokutana itaidhinisha kadi hiyo ili iingie katika rekodi rasmi za Ligi na kutoa adhabu ya ziada kwa kuwa kosa lilistahili kadi nyekundu ya moja kwa moja.
Na makosa hayo ndio kama yale ya mchezo wa hatari, kupiga au kupigana na mengine yanayovuka mstari wa makosa ya kawaida ya kimchezo.
Lakini kutokana na teknolojia, kamati sasa inaweza kufanya uamuzi pale ambapo mwamuzi hakuona tukio wakati mchezo ukiwa umesimama. Kwa mfano, refa akipuliza filimbi ya kusimamisha mchezo, halafu mchezaji mmoja akamvizia mwenzake na kumpiga ngumi bila refa kuona na mchezo ukaendelea kama kawaida. Kamati itakapokutana itaangalia marudio ya video ya tukio hilo na kumuadhibu mchezaji huyo kulingana na kanuni.
Hata ubadilishe kanuni vipi, hakuna sheria itakayoweza kuruhusu watu waliokaa mezani kuamua tukio ambalo refa hakuliona wakati hajapuliza filimbi ya kusimamisha mchezo. Hii ni kote duniani.
Kwa hiyo, kitendo cha kamati hiyo kuamua eti kumfungia beki wa Yanga, Ibrahim Bacca kwa tukio ambalo refa hakuliona na hakupuliza filimbi kusimamisha mchezo, ni kituko cha karne na kinaonyesha ni kwa kiasi gani hatuelewi utamaduni wa mchezo wa soka, sheria na kanuni zake.
Na kama tunaelewa basi uamuzi kama huo unafanywa kwa makusudi kwa lengo ama la kumkomoa mchezaji ama kuikomoa timu yake. Na hii ni aibu kwa soka la Tanzania.
Ni kweli Bacca alimgonga mguu mchezaji wa Mbeya City, Ame Ibrahim ili asiufikie mpira kabla ya yeye mwenyewe kuupiga. Ni kweli kwamba kitendo chake kilistahili hata kadi nyekundu kama refa angekiona, lakini si kamati inayotakiwa imuadhibu kwa tukio ambalo halikupuliziwa filimbi na refa.
Kazi ya kamati ilikuwa ni kuangalia kwanza tukio lenyewe, lakini pili ni sehemu ambayo mwamuzi wa kati alikuwepo ili kujua kama aliliona na akalifumbia macho, au hakuliona au hakuwa sehemu sahihi kulingana na kasi ya mchezo. Wenzetu wanatumia hadi teknolojia ya V.A.R kufanya uamuzi sahihi hivyo mwamuzi kutolipata tukio hilo vizuri, inaweza kuwa ni kutokana na kasi ya mchezo na hata ujanja wa mchezaji kufanya kitendo kwa kasi ili asionekane.
Hofu yangu baada ya uamuzi huo wa Bacca, ambao unatakiwa upingwe kwa nguvu zote, ni kwamba kamati hii inazidi kuvuka mipaka ya sheria, kanuni na utamaduni wa mpira wa miguu bila ya kuwa na teknolojia inayoruhusiwa kuchukua uamuzi kama huo.
Huko tunakoelekea refa na msaidizi wake watashindwa kwenda na kasi ya mpira na hivyo kutoweza kujua kama mpira ulivuka mstari au la kabla haujaokolewa na beki. Kwa vigezo ilivyotumia kufikia uamuzi wa kumuonyesha kadi nyekundu Bacca kutokea mezani, kamati hiyo itaangalia marudio ya video ya tukio hilo na kuamua kuwa bao lilikuwa halali na kumuadhibu refa kwa kutong’amua kuwa mpira ulivuka mstari.
Ndio, hivyo ndivyo walivyofanya kwa Bacca na ndivyo walivyofanya mwaka juzi kwa Khalid Aucho.
Ukishaamua kufanya uamuzi unaopaswa kuchukuliwa na mwamuzi ambaye sheria za mpira wa miguu ndio zinasema uamuzi wake ni wa mwisho, hutashindwa kufuta goli la timu au kuhesabu goli ambalo picha za marudio zinaonyesha mpira ulivuka mstari. Je, huko ndiko tunakotaka kwenda?
Wakati Diego Maradona anafunga bao kwa kutumia mkono na kuiwezesha Argentina kuiondoa England kwa mabao 2-1, hakukuwapo na teknolojia ya mstari wa goli (goal-line technology) wala Refa Msaidizi wa Video (V.A.R), lakini televisheni zilikuwapo na picha za mnato zilikuwapo na zilionyesha dhahiri kuwa gwiji huyo wa zamani aliusukumia mpira wavuni kwa kutumia mkono.
Kwa kutumia teknolojia hiyo ndogo waliyokuwa nayo wakati huu, kama wangekuwa ni hawa wetu wa Kamati ya Saa 72, wangefuta bao hilo na kumuadhibu refa kwa kutoliona. Lakini refa anabakia kuwa mwamuzi wa mwisho na anawajibika kwa uamuzi wake.
Labda ni teknolojia ya mstari wa goli tu ndio ambayo refa hawezi kupingana nayo kwa kuwa hupewa taarifa kwenye saa yake sekunde chache baada ya tukio, lakini V.A.R haitoi uamuzi wa mwisho labda tukio liwe bayana.
Yaani refa hupewa nafasi ya kwenda kuangalia tukio kutoka pande tofauti na ndiye anayefanya uamuzi kuamua kuwa kulikuwa na kuotea, rafu wakati wa kwenda kufunga, rafu ya kuzuia mpira ndani ya penalti au matukio mengine yaliyoorodheshwa kwenye protokali za V.A.R.
Kwa hiyo, hata teknolojia bado inampa mwamuzi, uamuzi wa mwisho wa kuamua tukio kama hilo la kadi nyekundu lakini si watu waliokaa ndani ya chumba cha mkutano. Na sasa hata kadi ya pili ya njano, refa atalazimika kujiridha kwenye picha za marudio za video kwa kuwa zina athari kwa timu.
Pale inapothibitika kuwa refa alifanya uamuzi tofauti na sheria zinavyotaka, yeye ndiye anatakiwa abebeshwe msalaba. Hiyo ndiyo maana halisi ya refa kuwa mwamuzi wa mwisho kwa mujibu wa maoni yake.
Kamati ya Saa 72 isijibebeshe majukumu ya kusimamia sheria 17 na tafsiri zake. Hilo ni jukumu la refa alilopewa kwa mujibu wa sheria za soka na anapoboronga basi aadhibiwe kwa makosa au udhaifu wake. Hatutaki kuona kamati inafikia uamuzi wa kufuta au kuhesabu goli.