CAF wakae chini kuangalia upya sheria ya usajili CHAN
Muktasari:
- Jephte Kitambala wa DR Congo, amesaini kuitumikia Azam FC lakini utambulisho haujafanyika hadi sasa kwa sababu ya kuiogopa sheria hii.
MOHAMED Bajaber wa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, amekosa sifa za kucheza fainali za CHAN mwaka huu kwa sababu amesaini kuitumikia Simba, timu ya nje ya nchi yake.
Jephte Kitambala wa DR Congo, amesaini kuitumikia Azam FC lakini utambulisho haujafanyika hadi sasa kwa sababu ya kuiogopa sheria hii.
Bajaber na Kitambala ni baadhi ya wachezaji wanaoumizwa na sheria tangu mashindano haya yalipoanza, mwaka 2009.
Desemba 2019, Emmanuel Okwi alirejea katika klabu yake ya utotoni ya SC Villa akitokea klabu ya Ittihad Alexandria ya Misri.
Hicho kilikuwa kipindi cha kuelekea CHAN ya 2020 na Uganda ilifuzu kushiriki, wakataka wamtumie lakini CAF wakawazuia wakisema mchezaji huyo hana vigezo.
Na hii ni kutokana na ibara ya 38.2 ya sheria ya 16 inayozungumzia vigezo vya wachezaji wa CHAN.
Sheria hiyo inasema hivi...
Ni wachezaji wenye mikataba ya kudumu tu waliosajiliwa katika timu za ndani ya nchi zao zilizo chini ya vyama vyao vya kitaifa vya soka ndio wanaoruhusiwa.
-Utaona hapo sheria inasema wachezaji wanaoruhusiwa ni wale wenye mikataba ya kudumu na klabu za nchini mwao.
Unaweza ukaelewa kwamba endapo mchezaji amesaini kwenye timu ya nchi nyingine maana yake haruhusiwi.
Lakini nadhani sheria hii inabidi iende mbali zaidi na kufafanua baadhi ya mambo kama muda wa mkataba kabla ya kuanza mashindano.
Vipi kama kuna wachezaji ambao mikataba yao mipya na timu za nje ya nchi zao itaanza Septemba Mosi?
Fainali ya CHAN ni Agosti 30, kwanini mchezaji wa aina hii asiruhusiwe?
Kanuni inasema wachezaji wanaoruhusiwa ni wale wenye mikataba ya kudumu tu.
Maana yake mchezaji aliyepo kwa mkopo haruhusiwi.
Yaani kwa mfano mchezaji wa Kitanzania amesainiwa na klabu ya Afrika Kusini kwa mkataba wa miaka mitano.
Halafu akatolewa kwa mkopo katika klabu ya Tanzania, huyo hatoruhusiwa kucheza CHAN.
Klabu ya Al Hilal ya Sudan ilimtaka kwa mkopo kipa wa Azam FC, Mohamed Mustafa.
Kwanza walitaka achukue nafasi ya kipa wao, Issa Fofana, ambaye ameomba kuondoka.
Pili walitaka acheze CHAN akiwa na Sudan.
Lakini sheria ya mkopo ingewabana kwa takwa lao la pili.
Unaona sheria inavyobana? Yawezekana walioitunga waliogopa ‘transfer doping’ yaani udanganyifu wa usajili (sio neno rasmi).
Yawezekana walihisi nchi zikiona CHAN inakuja, zingehamasisha klabu zao kuwaomba kwa mikopo wachezaji wao bora walioko nje.
Lakini hii haina mantiki hata kidogo. Ni klabu gani itakubali kumtoa kwa mkopo mchezaji wake arudi nchini kwao kwa ajili ya kushiriki CHAN, mashindano ya mwezi mmoja?
CAF wanatakiwa kukaa chini na kuiangalia upya sheria hii ili kupunguza mitafaruku.
Kwa kuwa Bajaber au Kitambala walicheza Ligi za kwao hadi msimu ulipoisha na misimu ya nchi wanayoenda haijaanza...walipaswa wasomeke kama wachezaji wa ndani.
Ni kama ambavyo Okwi alisomeka mchezaji wa nje ilhali alishasaini na klabu ya ndani...akaendelea kusomeka kwa mkataba wake wa nyuma....na hawa iwe hivyo...mikataba ya nyuma ndio ingesomeka kwao hadi msimu mpya uanze wakiwa na timu zao mpya.
Sheria ya usajili wa wachezaji wa CHAN inaumiza.
Mchezaji hata kama amesaini na timu ya nje ya nchi yake, aendelee kusomeka kama mchezaji wa ndani hadi msimu mpya utakapoanza.
Ingekuwa hivyo, Bajaber angekuwepo kuisaidia nchi yake ya Kenya.
Kitambala angekuwa ameshatangazwa na klabu yake mpya ya Azam FC.
Lakini tatizo ni sheria!