Buriani Jumbe, kazi ya miaka 40 imetosha
MZEE wa Dodo hatuko naye tena. Mtumishi amefariki dunia na kuacha simanzi kwa ndugu, jamaa na marafiki.
Ni mwanamuziki nguli wa muziki wa dansi, Hussein Seleman Jumbe ambaye amezikwa juzi Jumanne katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam.
Jumbe mwenye sauti ya gharama alifariki dunia Jumatatu katika Hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Mamia ya wanamuziki, ndugu, marafiki na jamaa walihudhuria mazishi ya mwanamuziki huyo.
Mwaka jana mwishoni mwandishi wa makala haya, alifanya mahojiano na Jumbe ambaye alifunguka mambo mengi.
Hadi Jumbe anafariki dunia, safari yake katika muziki na maisha yake ilitawaliwa na mikasa kibao.
Mikasa ambayo ilimfanya kutunga nyimbo zilizokuwa na visa na matukio ya kweli na nyingi zikiacha simanzi, lakini kibao chake cha mwisho Nipe Kitambaa alichokiacha kikitamba kikibeba ujumbe wa safari yake ya mwisho ikiwamo mwili wake kugombewa sehemu ya kuzikiwa ni kama alijitabiria.
Mikasa ya gwiji huyo aliyekuwa mahiri kwa kutunga nyimbo zenye hisia ilianza mwaka 1999 pale alipozushiwa kifo baada ya kuugua kwa muda mrefu. Akiwa kitandani alisikia vilio vya ndugu sebuleni kwake wakimtaja jina lake kama amefariki dunia.
Jumbe alifafanua kisa hicho baada ya kudai siku hiyo kilitangazwa kifo cha mwanamuziki Mobali Jumbe na vilevile jirani alipokuwa akikaa Temeke kulitokea msiba.
“Watu waliunganisha matukio hayo na kuamini nilikuwa nimefariki dunia,” Jumbe alifafanua.
KUPONA KWA MGANGA
Baada ya kuugua kwa muda mrefu, hatimaye Jumbe alipona kwa mganga wa kienyeji, maeneo ya Duga Maforoni, Tanga.
Kwa mganga huyo, Jumbe alipelekwa na swahiba wake, aliyekuwa mfanyabiashara maarufu, marehemu Mohammed Mpakanjia ‘Meddy’.
“Awali mganga yule mwanamke alikataa kunitibu mpaka nilipopima ukimwi na kuthibitika kuwa sikuwa nao,” alisema Jumbe na kuendelea;
“Alinitoa mbegu za papai katika vifundo vya mguu wangu na baada ya hapo nilipona kabisa.”
Wakati walipokuwa wakirudi Dar es Salaam na swahiba wake walipofika Segera Jumbe ndipo alipopata wazo la kutunga Wimbo wa Nachechemea ambao ulimpa umaarufu mkubwa sana.
“Nilichukua ‘jalbox’ (ganda la sigara) kutoka kwa Mpakanjia, nikamuomba na peni na kuanza kuandika mashairi ya wimbo wa Nachechemea,” alikumbuka Jumbe.
KULALA KWENYE MIHOGO
Kabla ya kujiunga na Sikinde, Jumbe aliwahi kupata mkasa mwingine uliomfanya kulala kwenye shamba la mihogo Chanika, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
“Ilikuwa ni baada ya kuanza kuwaaga wanamuziki wenzangu wa Urafiki Jazz nilipotakiwa na Sikinde.
“Kumbe jambo lile liliwachukiza, nakumbuka mmoja alinikosa ngumi na nikalazimika kukimbia… walinikimbiza nikajificha kwenye shamba la mihogo. Chanika ya kipindi kile sio kama ya sasa, nililala kwenye shamba lile hadi asubuhi,” alisimulia Jumbe aliyewahi pia kufundisha masomo ya lugha.
Hilo halikuwa tukio la kwanza kwa Jumbe mwaka 1986, alijiunga na Juwata Jazz akitokea Mara Jazz na kushiriki kuutengeneza baadhi ya nyimbo lakini hakuwahi kurekodi na bendi hiyo.
“Tukiwa kwenye onyesho pale DDC Kariakoo, niliposhuka stejini nilikikanyaga kiti cha mmoja kati ya wanamuziki wa bendi.
“Mwanamuziki yule alikasirika sana, njia nzima alikuwa akizungumza kuhusu kitendo kile kilivyomkera.”
Jumbe baada ya kukikanyaga kiti kile alikifuta na kitambaa chake lakini mwanamuziki yule mkongwe hakuridhika, akalazimika kumtafutia kiti kingine lakini bado pia hakuridhika.
“Wakati tunarudishwa na gari, bado alikuwa akizungumza tukio lile, nikaona isiwe tabu, ilikuwa usiku sana, nikashuka Ilala sokoni na kulazimika kulala pale hadi asubuhi ndipo nilipopata usafiri wa kurudi nyumbani, Magomeni.”
Mikasa ya Jumbe la ni mingi sana. Hata alipoanza safari yake ya muziki ilikuwa ni mikasa juu ya mikasa.
ALIACHA KAZI KISA MUZIKI
Mwaka 1983, baba yake Mzee Selamani alimtafutia kazi katika kampuni ya vyombo vya plastiki. Jumbe aliiacha kazi hiyo baada ya kupata pesa ya kwenda kusomea muziki na kumkasirisha baba yake.
“Nilinyan’ganywa nguo zote nilizonununuliwa na kulazimika kuvaa vilaka na kandambili zilizofungwa na waya,” alisimulia Jumbe enzi za uhai wake. Baada ya kuona maisha magumu, ndipo alipotoroka na kwenda kujiunga na Tabora Jazz akiwa kama mpiga dramu.
KALENGA AGUNDUA KIPAJI CHAKE
Siku moja Tabora Jazz, ilikuwa ikisafiri kwenda Mpanda kupiga muziki, wakiwa ndani ya treni kwenye behewa la daraja la pili kukaa (sitting) alfajiri, ndipo mwanamuziki Shem Kalenga alipomsikia Jumbe akiimba wimbo wa Marijani Rajabu.
“Tuliporudi Tabora, Kalenga aliniambia kuanzia siku hiyo ningekuwa mwimbaji, nilimwambia siwezi kuimba lakini aliniambia alinisikia nikiimba kwenye treni.”
Tangu hapo Jumbe aliingia kwenye uimbaji na sauti yake kukonga nyoyo za wengi huku tunzi zake zikipagawisha.
Katika safari yake ya muziki, Jumbe amepitia katika bendi za Tabora Jazz, Mara, Jazz, Juwata Jazz na Urafiki Jazz.
Oktoba 10, 1987 Jumbe alijiunga na DDC Mlimani Park na baadaye TOT Plus. Mwaka 1995 alijiunga na Msondo Ngoma na alirudi Sikinde kabla ya kuibukia Mikumi Sound ya Morogoro. Mwaka 2008 alirudi Msondo Ngoma na baadaye kuanzisha Talent Band.
KIPENZI CHAKE
Jumbe alikuwa akivutiwa sana na mwanamuziki, Marijani Rajabu tangu alipokuwa na bendi ya Safari Trippers.
Wakati baba yake alikuwa akimtaka Jumbe asome sana dini hususan kitabu cha Quraan, yeye kila wikiendi alikuwa hakosekani kwenye ukumbi wa Princess ambako Trippers ilikuwa ikitumbuiza.
“Nilikuwa nampenda Marijani na nilifuata nyayo zake katika utunzi na uimbaji,” alifunguka Jumbe.
ALIKUWA MNYAMA SANA
Jumbe alizaliwa Desemba 25, 1963 na alipata elimu yake ya awali Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko na Shule ya Sekondari Kinondoni Muslim.
Enzi za uhai wake, Jumbe alikuwa shabiki wa kulialia wa Simba Sports akiwa amezaliwa na baba akiwa mwenyeji wa Kivindo, Bonde jijini Tanga.
Ameacha mke mmoja, Zakhia Hussein na amebahatika kupata watoto tisa, kati ya watoto wake, wawili Ima (prodyuza) na Shady (drums) ni mashabiki wa kubwa wa Yanga. Watoto wake wengine ni Lillah, Warda, Yassir, Idd, Hashim na Nuru. Jumbe ameondoka, lakini hakiwa hana deni kwa mashabiki wa muziki nchini, kwani kzi aliyoifanya kwa miaka 40 imemheshimisha na kumfanya aache alama kubwa.
Baadhi ya tungo zake ni Epuka No2’, ‘Nuru ya Upendo’, ‘Shamba’, ‘Mtoto wa Mitaani’, ‘Chozi la Kejeli’, ‘Nachechemea’ na ‘Isaya Mrithi Wangu’, Kiapo mbali na nyimbo kibao akiwa na kundi lake la Talent Band lililofyatua wimbo uliotabiri mwisho wake uitwao ‘Nipo Kitambaa’ ambao unaendelea kutamba kwa sasa.
Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake sehemu salama, amin.