Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Barker mtegoni Simba!


UPO msemo maarufu wa Kiingereza unaosema; “coaches are hired to be fired,” ambao kwa tafsiri isiyo rasmi ya “kindengereko” ni kwamba “makocha wanaajiriwa ili wafukuzwe.”


Hata hivyo, kwa klabu kongwe nchini za Simba na Yanga, ni kama msemo huo umechukuliwa kwa uzito mkubwa kiasi kwamba si ajabu makocha wanaoingia na kutoka mitaa ya Jangwani na Msimbazi ni wengi kuliko mataji yaliyobebwa ndani ya kipindi husika.

Ndiyo, klabu hizo za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) zimekuwa na bahati ya kuvutia makocha wa kigeni kwa miongo kadhaa sasa, lakini bahati mbaya wengi hawakai kwa muda mrefu.

Makocha mbalimbali wa kigeni wamekuwa wakipokezana kuingia na kutoka ndani ya klabu hizo; wengine wakiletwa kwa mbwembwe kabla ya kutimuliwa kwa fedheha, kama ilivyowahi kuwakuta Tom Saintfiet, Ernie Brandts na Marcio Maximo waliowahi kuinoa Yanga. Miongoni mwa makocha hao wapo waliovuna fedha nyingi; baadhi wakitoka ndani ya Bara la Afrika na wengine kutoka Ulaya na Amerika.

Simba imewahi kupata huduma ya makocha kutoka mabara hayo mawili, na kwa sasa ipo mikononi mwa Steve Barker kutoka Afrika Kusini baada ya kumtimua Dimitar Pantev wa Bulgaria aliyedumu kwa kipindi kisichozidi miezi miwili.

Pantev aliajiriwa Oktoba 3, 2025 akitokea Gaborone United ya Botswana — timu iliyong’olewa na Simba katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huo — na kutimuliwa Desemba 2 mwaka huohuo.

Pantev alimrithi Fadlu Davids kutoka Afrika Kusini na kuingia katika orodha ndefu ya makocha walioingia na kutoka Simba katika kipindi cha miaka 12 iliyopita tangu msimu wa 2014/2015 ilipoachana na Goran Kopunovic wa Serbia hadi sasa ilipo chini ya Barker. Katika kipindi hicho na hata kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita, Simba haijawahi kumpata kocha Mzungu aliyefikia mafanikio ya Dragan Popadic aliyeinoa timu hiyo kwa misimu mitatu kuanzia 1994 hadi 1996.


MAAJABU YA POPADIC

Kocha huyo kutoka Serbia (zamani Yugoslavia) aliipokea Simba kutoka kwa Abdallah ‘King’ Kibadeni na Mhabeshi Etienne Eshente, waliokuwa wameifikisha Simba fainali ya Kombe la CAF 1993 kabla ya kupoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Stella Abidjan. Chini ya Popadic, Simba ilitetemesha soka la Afrika Mashariki na Kati. Timu zilizokutana nayo zilihofia kufanya makosa karibu na eneo la hatari au kuruhusu mipira ya kona.

Popadic aliwafundisha wachezaji wake mbinu za kupiga frii-kiki na kona kwa ustadi mkubwa. Baadhi ya wachezaji waliocheza chini yake ni Mohammed Mwameja, Mwanamtwa Kihwelu, Kasongo Athuman, Mustafa Hoza, Thomas Kipese, Godwin Aswile ‘Scania’, George Masatu na Idd Seleman ‘Nyigu’.

Wengine ni Athuman Abdallah ‘China’, Edward Chumila, Abdul Ramadhani ‘Mashine’, Juma Amir, Bakar Idd, Dua Said, George Lucas ‘Gazza’, Abdallah Mwinyimkuu, Said Mwamba ‘Kizota’, Mchunga Bakar ‘Mandela’, Nteze John na Madaraka Seleman ‘Mzee wa Kiminyio’. Akiwa Msimbazi, aliiongoza Simba kutwaa mataji saba tofauti, yakiwamo mawili ya Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kagame) mwaka 1995 na 1996. Pia alitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mara mbili mfululizo (1994 na 1995), Ligi ya Muungano (1994 na 1995) na Kombe la Nyerere 1995.


MSIMU UNAOTESA

Ingawa Simba imekuwa ikitumia mamilioni ya fedha kuajiri makocha wa kigeni, haijawahi kunufaika nao kama ilivyokuwa kwa Popadic. Baada ya kuondoka Simba, Popadic alienda Uganda na kuinoa Express FC, akiiongoza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu 1996 na Kombe la Uganda 1997.

Amefundisha pia Angola, Ghana, Libya, Qatar, Hungary na Oman, kisha kurejea Tanzania kuinoa African Lyon na Singida United — japokuwa hakufikia mafanikio aliyopata Msimbazi. Baadhi ya makocha wa kigeni waliopita Simba bila kufikia rekodi ya Popadic ni Nzoysaba Tauzany (Burundi), James Siang’a (Kenya), Trott Moloto (Afrika Kusini), Patrick Phiri (Zambia), Neider dos Santos (Brazil), Milovan Cirkovic (Serbia), Krasimir Balakov, Moses Basena (Uganda), Patrick Liewig (Ufaransa), Zdravko Logarusic (Croatia), Goran Kopunovic (Serbia) na Dylan Kerr (Uingereza).


MIAKA 10 ILIYOPITA

Tangu msimu wa 2014/2015 hadi 2024/2025, Simba imeajiri na kutema makocha 18; kati yao 15 ni wageni na watatu wazawa walioshikilia timu kwa muda. Katika kipindi hicho, klabu imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara nne na Kombe la Shirikisho mara tatu kupitia Joseph Omog, Pierre Lechantre, Patrick Aussems, Sven Vandenbroeck na Didier Gomes. Pia imetwaa Ngao ya Jamii mara tano ile ya mwisho ikiwa chini ya Mbrazili Roberto Oliviera ‘Robertinho’ 2023.


BARKER ATATOBOA?

Barker, aliyeajiriwa Desemba 19 mwaka jana, ana kibarua cha kuvunja “mzimu” wa Popadic kudumu muda mrefu na kuipa Simba mataji. Kwa sasa ana jukumu la kurejesha mataji ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho yanayoshikiliwa na Yanga kwa misimu minne mfululizo, pamoja na Kombe la Muungano. Tayari alishindwa kubeba Kombe la Mapinduzi 2026 baada ya kutolewa nusu fainali.

Iwapo atashindwa na mabosi wa Msimbazi wakamvumilia, basi atapata nafasi ya kupigania Ngao ya Jamii 2026. Hata hivyo, historia inaonyesha makocha wengi waliotamani kudumu waliishia njiani. Lakini kama Barker ataendeleza kasi aliyoanza nayo, hasa baada ya kuingiza mashine mpya kupitia dirisha dogo la usajili, na akapewa muda, anaweza kuleta neema Msimbazi kutokana na rekodi alizonazo — ingawa hakuna mwenye uhakika kama ataipiku rekodi ya Popadic.


MAKOCHA TANGU 2015-2025

1) 2015-2016: Dylan Kerr (England)

2) 2016: Jackson Mayanja (Uganda)

3) 2016-2017: Joseph Omog (Cameroon)

4) 2017: Masoud Djuma (Burundi)

5) 2018: Pierre Lechantre (Ufaransa)

6) 2018-2019: Patrick Aussems (Ubelgiji)

7) 2019-2021: Sven Vandenbroeck (Ubelgiji)

8) 2021: Didier Gomes (Ufaransa)

9) 2021-2022: Pablo Franco (Hispania)

10) 2022: Zoran Maki (Serbia)

11) 2022-2023: Juma Mgunda

12) 2023: Roberto Oliveira 'Robertinho' (Brazili)

13) 2023: Daniel Cadena (Hispania)

14) 2023-2024: Abdelhak Benchikha (Algeria)

15) 2024: Juma Mgunda

16) 2024-2025: Fadlu Davids (Afrika Kusini)

17) 2025: Hemed Morocco

18) 2025: Dimitar Pantev (Bulgaria)

19) 2025- Steve Barker (Afrika Kusini)