Prime
BADO WAMO: Ronaldo na wazee wenzake aliocheza nao hawataki kung’atuka
Muktasari:
- Kwenye umri kama wake, miaka 40, wachezaji wengi wameshatundika daruga, lakini Ronaldo amehakikisha bado anaendelea kuwasha moto na wala haonyeshi dalili yoyote ya kufikiria kung’atuka.
RIYADH, SAUDI ARABIA: SUPASTAA Cristiano Ronaldo yupo kwenye msimu wake wa 22 wa soka la kulipwa na mambo yake ndio kwanza yanaanza huko Saudi Pro League, akiwasha moto kisawasawa kufukuzia rekodi mbalimbali na mataji ya maana akiwa na kikosi cha Al-Nassr.
Kwenye umri kama wake, miaka 40, wachezaji wengi wameshatundika daruga, lakini Ronaldo amehakikisha bado anaendelea kuwasha moto na wala haonyeshi dalili yoyote ya kufikiria kung’atuka.
Soka limebadilika sana tangu kulipoibuka mambo mengi tofauti mchezoni miaka ya 2000, hivyo hakuna wachezaji wengi wenye umri unaolingana au kukaribiana na wa Ronaldo waliokuwa wakicheza pamoja huko nyuma wanaoendelea kukipiga hadi sasa.
Kwa kuzingatia hilo, hii hapa orodha ya mastaa saba waliocheza pamoja na Ronaldo ambao umri wao unakaribiana na bado wanakomaa kwenye soka.
Luka Modric
Mshindi huyo wa Ballon d’Or 2018 kwa sasa umri wake ni miaka 39 na bado amekuwa sehemu muhimu ya kikosi cha Real Madrid chini ya kocha Carlo Ancelotti.
Pacha wake wa zamani kwenye kiungo ya Real Madrid, Toni Kroos alishastaafu akiwa na umri wa miaka 34, wakati gwiji wa La Liga, Xavi alistaafu akiwa na umri wa miaka 39 – lakini kwa supastaa huyo wa Croatia amecheza mechi 31 msimu huu.
Mkataba wake unafika tamati mwishoni mwa msimu huu na hakuna uhakika ni wapi atakwenda kucheza msimu ujao.
Bila shaka, ofa za kutoka Saudi Arabia zinaweza kutua mezani kwake kwa sababu mchezaji mwenyewe haonekani kuwa na mpango wa kutundika daruga kwa sasa. Ameshacheza mechi 835 na 568 kati ya hizo amecheza kikosini Real Madrid.
Karim Benzema
Straika Karim Benzema na Ronaldo walifanikiwa kuunda pacha matata sana kwenye fowadi ya Real Madrid walipokuwa wakicheza pamoja, ambapo CR7 alisifu ubora wa mchezaji mwenzake, ambaye hakuwa mbinafsi ndani ya uwanja, alimpa mipira na pasi za maana ili yeye kung’ara kwenye kufunga mabao.
Baada ya Ronaldo kuondoka Madrid, Benzema alichukua jukumu la kuiongoza timu hiyo na kwenda kunyakua taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya ambalo lilimfanya fowadi huyo Mfaransa kushinda tuzo ya Ballon d’Or.
Benzema naye alishaondoka Los Blancos na kwenda kukipiga kwenye Saudi Pro League kama ilivyo kwa Ronaldo, ambaye alisaini Al-Ittihad na umri wake wa sasa ni miaka 37, amefunga mabao 15 katika mechi 17 msimu huu. Hana mpango wa kustaafu.
Martin Caceres
Ronaldo na Caceres walicheza pamoja Juventus kwa kipindi kifupi, huku mkali huyo wa kimataifa wa Uruguay, bado anatamba uwanjani akiwa na umri wa miaka 37.
Lakini, ripoti zinafichua kwamba kwenye dirisha la Januari, Caceres aliachana na LA Galaxy ya Marekani na sasa ni mchezaji huru.
Kwenye wakati wake, Caceres alicheza kwenye timu za maana kwelikweli ikiwamo Barcelona, Juve, Sevilla, Lazio, Southampton na Fiorentina.
Mchezaji huyo alifanikiwa kunyakua Kombe la MLS mwaka 2024, lakini alicheza na Ronaldo kwenye mechi tatu tu huko Italia kikosini Juventus.
Sergio Ramos
Moja ya beki wa kati bora kabisa kwenye kizazi chake. Ramos alikuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Real Madrid kilichopata mafanikio makubwa uwanjani ambapo uwanjani alitamba akiwa na supastaa Ronaldo kwenye mechi kibao.
Ramos, mwenye umri wa miaka 38, aliondoka Real Madrid kwenda Paris Saint-Germain na kucheza huko kwa miaka michache kabla ya kurudi kwenye klabu yake ya zamani ya Sevilla msimu uliopita.
Hata hivyo, tangu alipoondoka kwenye timu hiyo, Ramos amekuwa mchezaji huru, anatafuta timu kwa sasa, hataki kutundika daruga.
Ripoti za karibuni iliripotiwa kwamba anaelekea huko Mexico kujiunga na Monterrey, ambako anaweza kwenda kusaini mkataba wa mwaka mmoja au zaidi na tayari ameshatangazwa kuwa mchezaji wa Rayados akikabidhiwa jezi namba 93.
Ramos alicheza mechi 671 kwenye kikosi cha Real Madrid na kufunga mabao 101.
Keylor Navas
Navas hakuwa anapewa hadhi yake anayostahili wakati alipokuwa kwenye kiwango bora cha soka lake, ambapo alikuwa kipa wa kiwango cha juu kabisa, ambaye alikuwa kwenye goli la Real Madrid iliyonyakua taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa misimu mitatu mfululizo kuanzia msimu wa 2015-2017.
Alidaka mechi 162 kwenye kikosi cha Madrid kabla ya kuhamia PSG na baadaye alikwenda kwa mkopo Nottingham Forest, 2023. Aliachana jumla na klabu hiyo ya Ufaransa mwaka 2024 na alikuwa mchezaji huru kwa siku kadhaa kabla ya kwenda kujiunga na timu ya Argentina ya Newell’s Old Boys, ambako hadi sasa amecheza mechi moja. Mkataba wake utakwisha Desemba 2026 na kipindi hicho atakuwa amefikisha umri wa miaka 40.
Jose Fonte
Mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi waliopo kwenye orodha hii, ambapo beki huyo wa kati, umri wake ni miaka 41.
Staa huyo wa zamani Southampton bado anacheza na yupo fiti.
Fonte alicheza pamoja na Ronaldo kwenye timu ya taifa ya Ureno na walinyakua taji la Euro 2016 pamoja, huku sehemu kubwa ya soka lake la klabu alicheza kwenye timu za Southampton, Lille na Crystal Palace.
Baada ya miaka mitano Lille iliyokomea 2023, alikwenda Ureno kujiunga na klabu ya Braga kabla ya kwenda kujiunga na Casa Pia ya Primeira Liga, ambako ana mkataba hadi mwisho wa msimu.
Javier Hernandez
Straika wa zamani, mkali huyo wa Mexico umri wake wa sasa ni miaka 36 na bado anakipiga huko kwenye nchi yao akiitumikia klabu yake ya zamani ya Guadalajara.
Hernandez maarufu kama Chicharito alicheza na Ronaldo kwenye kikosi hicho cha Real Madrid alipokwenda kwa mkopo katika msimu wa 2014-15, alipocheza mechi 33 akifunga mabao tisa na asisti tisa.
Kipindi chake kilichofanya Chicharito afamike zaidi ni wakati alipokuwa Manchester United, ambapo alicheza kwa misimu mitano.
Baada ya hapo alikwenda kukipiga Bayer Leverkusen, West Ham United, Sevilla na Los Angeles Galaxy kabla ya kurudi kwao Mexico mwaka 2024 na amenyakua mataji makubwa sita katika maisha yake ya soka.