Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Azam balaa zito Misri

El Gouna, Misri. AZAM FC iko wilaya ya El Gouna mkoani Hurghada nchini Misri katika maandalizi ya msimu mpya wa 2022/23. Tutakuwa tukikuletea kila kinachoendelea na leo tukianza na safari ilivyokuwa na siku ya kwanza ya mazoezi.


SAFARI

Azam FC ilisafiri kwa ndege ya shirika la Egyptair. Safari ilianza kwa kuchelewa kwa takribani saa moja kutoka muda wa awali wa saa tatu na nusu asubuhi Julai 22 lakini ikaanza saa nne na nusu asubuhi siku hiyo.

Kikosi cha Azam FC kikiwa na wachezaji 28 kilikuwa kikienda El Gouna, lakini mji huo hauna uwanja mkubwa wa ndege hasa za kimataifa. Kuna kauwanja kadogo kwa ajili ya ndege binafsi, hivyo hutumia uwanja wa mji wa karibu wa Hurghada.

Ndege waliyopanda Azam FC iliiishia Cairo ambapo ilitua saa 10:30 jioni na wakapanda ndege nyingine hadi Hurghada ambako walifika saa mbili usiku. Hapo wakachukua basi la kisasa aina ya Benz hadi Cooks Club Hotel mjini Hurghada.

Hii ni moja ya hoteli nzuri na za kisasa mjini hapa ambazo zimetengenezwa maalumu kwa ajili ya watalii. Kuna watalii wengi wamefikia kwenye hoteli hii kwa ajili ya mapumziko ya majira ya joto.

Kocha mkuu wa Azam FC, Abdihamid Moallin, alibadili utaratibu wa kulala wa wachezaji wake. Kwa kawaida wachezaji hulala wawili wawili na wenyewe walijigawa kulala kama ambavyo hulala kwenye hosteli zao cha Chamazi. Lakini Moallin akapangua utaratibu huo na kuwachanganya ili kubadilisha mazoea.

Anasema amefanya hivyo ili kuimarisha uhusiano baina ya wachezaji kwa sababu wale ambao wamekuwa wakilala pamoja tayari wameshafahamiana vya kutosha na sasa ni zamu ya kufahamiana zaidi na wengine.

Akawachanganya wachezaji wapya na wa zamani. Akawachanganya wanaoongea Kiswahili na wasioongea lugha hiyo hasa wale wageni. Akawachanganya wanaoongea Kiingereza na Kifaransa.

Anasema mchanga-nyiko huu utawafanya wakitoka huku wajihisi ni kitu kimoja na kuimarisha umoja kwenye timu.


SIKU YA KWANZA MAZOEZINI

Azam FC walianza mazoezi siku moja baada ya kufika ambapo saa mbili kamili asubuhi walikuwa wameshafika kwenye uwanja mazoezi wa klabu ya El Gouna ambayo Idris Mbombo alikuwa akiichezea. Kulikuwa na vipindi vitatu vya mazoezi siku hiyo yalianza ya saa mbili asubuhi uwanjani, mchana na usiku uwanjani. Mazoezi ya uwanjani yalihusu umakini na kujenga pumzi. Mazoezi ya mchana yalikuwa kujenga misuli. Mazoezi haya yalishuhudiwa mlinda mlango mpya, Ali Ahamada, akijiunga na wenzake kwa mara ya kwanza.

Ahamada ambaye amekuja moja kwa moja El Gouna akitokea Ufaransa anakoishi alikuja asubuhi ya siku ya kwanza ya mazoezi hivyo kukosa mazoezi ya asubuhi. Halafu kukawa na mazoezi ya usiku ambayo yalihusu zaidi mbinu.


ASUBUHI

Kocha wa makipa, Mhispaniola Dani Cadena alitambulisha mazoezi mengi kwa makipa wake, Ali Ahmed Salula, Wilbol Maseke na Zubery Foba.

Kocha huyo ambaye alishawahi kufanya kazi na Sevilla ya Hispania, ameamua kufanya kazi na Mwalo Ilunga, kama msaidizi wake.

Mwalo ni kijana aliyekulia kwenye akademi ya Azam FC baada ya kuchaguliwa 2011 kutoka timu ya Copa Coca Cola ya mkoani Kigoma.

Huo ndiyo mwaka ambao pia Aishi Manula kutoka timu ya Mkoa wa Morogoro na Hamadi Kadedi kutoka timu ya Mkoa wa Temeke walijiunga na akademi ya Azam sambamba na Farid Mussa, Mudathir Yahya, Gadiel Michael na Sospeter Bajana.

Kocha wa viungo, Mikel Guillen alikuwa bize kujenga pumzi kwa wachezaji wake huku akisaidiana na kocha msaidizi Omary Abdulkarim.


MCHANA

Ali Ahamada akaungana na wenzake kwenye gym ya kisasa iliyopo pembezoni mwa bahari ya Sham. Mikel Guillen alikuwa makini kuhakikisha vyuma vya gym vinashikwa kama inavyostahili.

Ali Ahamada alionekana ni mchezaji aliyekuwa utimamu mkubwa zaidi wa kimwili kwani aliweza kuinua kila chuma mara 10 zaidi ya wenzake.

Bwa’mdogo Twalib Mohamed Noor ambaye amepandishwa kutoka timu ya vijana chini ya miaka 20 ambayo yeye ni nahodha, alionekana kufurahia kila kitu mazoezini.

Akiungana na timu kubwa mara ya kwanza, Twalib ambaye alijiunga na akademi ya Azam FC mwaka 2016 akiwa na miaka 12, amemfurahisha sana kocha mkuu Abdihamid Moallin na kusema anamuona akifika mbali sana katika soka lake.

Kocha huyo amemchukua Twalib peke yake kwenye kambi hii lakini anasema amefurahishwa na wachezaji wengine wawili kutoka timu ya vijana chini ya miaka 20.

Wachezaji hao ni Jamal Jaku na Ashraf Malolo ambao anasema msimu ujao atakuwa akifanya nao mazoezi na kuwapa mechi moja moja kama kuwatia moyo ili wajitume zaidi.


USIKU

Usiku ikawa zaidi zamu ya mbinu na ufundi. Wachezaji wapya kama James Akaminko, Tape Edinho na Kipre Junior walikuwa hawashikiki.

Wachezaji hao wameonyesha uwezo mkubwa sana katika kulisakata kabumbu na kuashiria makubwa msimu ujao.

Kocha wa washambuliaji, Kali Ongala amesema benchi la ufundi litakuwa na wakati mgumu sana msimu ujao kuamua nani wa kucheza na nani wa kusubiri, kutokana na ubora wa kikosi.

Anasema kuna washambuliaji wanne, Prince Dube, Idris Mbombo, Rodgers Kola na Shaaban Idd Chilunda, na wote wameonyesha uwezo mkubwa sana.

Mbaya zaidi kati yao anatakiwa acheze mmoja tu kwa mechi kwa sababu Tape Edinho analazimisha kucheza kama namba 10 na kufuta uwezekano wa kucheza na washambuliaji wawili kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Hii ni siku ya kwanza ya kambi hii ya siku 20. Kadri siku zitakavyozidi kwenda, picha kubwa zaidi inatarajiwa kuonekana.