Prime
Athumani China afichua mazito Simba, Yanga
WAKATI mashabiki wengi wa soka nchini wakifurahia burudani kutoka kwa viungo kama Clatous Chama, Feisal Salum, Mudathir Yahya na Yusuph Kagoma, zaidi ya miaka 30 iliyopita Tanzania ilikuwa na mastaa wa hizo kazi.
Alikuwa Athumani China kwa waliobahatika kumuona katika ubora wake, wanamtaja kama kiungo aliyekamilika, alikuwa akitawala mchezo, kupandisha mashambulizi, kukaba, kupiga pasi na kutengeneza nafasi.
Leo, miaka mingi imepita, China anayeishi England, bado hajauacha mpira. Akiwa na umri unaokaribia miaka 60, anasema ukitaka kujua siri ya kwanini bado anacheza, usimwangalie kwenye kumbukumbu za zamani, alitukaribisha Sinza ambako atakuwa huko kwa wiki chache kwa ajili ya mapumziko.
“Unajua niko karibu miaka 60, lakini njoo siku moja pale Sinza Star ndio utajua ni kwa nini. Naweza mpaka sasa kucheza, japo ligi ndogo (England) lakini nacheza. Siri ni jitihada na nidhamu. Nidhamu yangu mimi ni kila kitu kwenye maisha, kwenye mpira na hata watoto wangu lazima wafuate nidhamu. Hicho ndicho kilichonifanya nibakie kuwa juuu,” anasema.
Lakini nyuma ya China huyo tunayemjua uwanjani kuna simulizi ndefu. Ni kijana wa Manzese aliyesaidiwa na marehemu Mohamed Kizele, akaingia Tumaini, akafika Yanga, Taifa Stars, England, Uarabuni na baadaye Simba.
Na safari hiyo, kama anavyosema mwenyewe, haikuwa rahisi.
KIZELE ALINIONA MANZESE
China anapozungumzia mwanzo wa safari yake, jina la hayati Mohamed Kizele haliwezi kukosekana.
“Kweli itakuwa ni dhambi na kutokumshukuru. Kuna kipa mmoja anaitwa Mohamed Kizele, alishafariki. Aliwahi kucheza Yanga B nafikiri akasajiliwa Yanga A lakini msimu huo wakamuacha. Tukawa tunacheza naye huko Tandale, Manzese. Tulikuwa tunacheza ile timu ya National ya Tandale, uwanja wa shule ya msingi Tandale,” anasema.
“Alivyoona ule uchezaji wangu akasema, ‘wewe mbona ni mchezaji mzuri sana!’ Akaniambia twende nikupeleke kuna timu moja inaitwa Tumaini ya Manzese. Ilikuwa timu ya daraja la pili. Akanichukua, akanipeleka Tumaini.”
Hapo ndipo mambo yalipoanza kubadilika.
Anasema: “Tumaini nikacheza sana. Tukacheza msimu mmoja tu. Ile timu ilikuwa na mwenye timu ambaye alikuwa afisa mmoja wa Hoteli ya New Africa na alikuwa mmoja wa viongozi waandamizi wa Yanga. Kwa hiyo yule mzee akaamua kunipeleka Yanga moja kwa moja. Ila kupitia Mohamed Kizele ndio nikaenda Tumaini, Tumaini nikachukuliwa nikapelekwa Yanga B (1987).”
DILI LA KUCHEZA ENGLAND
Baada ya kujijenga Tanzania, China anasema hakuwahi kukaa chini kupanga namna ya kwenda England. Fursa ilimfuata uwanjani.
“Nilikuwa na kiwango kizuri kipindi hicho. Nilikuwa nikikubalika na kila mtu. Akaja Mzungu ambaye alikuwa akifanya shughuli zake za biashara lakini alikuwa akija kuangalia mpira uwanjani. Akavutiwa na uchezaji wangu,” anasema na kuongeza;
“Kisha akanaongea na mimi na kuniuliza kama anaweza kunipeleka England. Hivyo ndivyo nilivyopata nafasi. Sikuwa nimepanga, lakini uwezo wangu ndio ulimfanya mtu aje kuniona na kusema huyu anafaa,” anasema.
China alipelekwa Walsall FC, klabu yenye historia ndefu England ambako alicheza katika kipindi ambacho ilikuwa ikishiriki daraja la pili.
“Timu yangu ilikuwa ya kihistoria. Kama ulivyosema imeanzishwa muda mrefu sana. Kipindi nachezea ilikuwa Division Two kabla mfumo wao haujabadilika. Kwa hiyo ilikuwa timu ya maana na inayotambulika rasmi kule England,” anasema.
Lakini alipofika huko ndipo aligundua kuwa kucheza mpira England na kuishi England ni vitu viwili tofauti.
ENGLAND ALITESWA NA UPWEKE
“Nilicheza miaka miwili pale. Lakini hiyo nayo ni hadithi ndefu, mpaka nimeitungia kitabu. Kuna vitu nilivikosea, hasa hali ya maisha. Hilo ndilo ambalo napenda sana nichangie au nisaidie kwenye hilo,”
“Hali ya maisha ya England ni ngumu sana kwa Mtanzania. Ndio maana hakuna Mtanzania yeyote mpaka sasa ambaye unaweza kusema ametoka hapa anaenda kucheza mpira kule. Lazima uwe umepita sehemu nyingine, uzoe mazingira, baridi. Kuna mazingira magumu sana ambayo kwa Watanzania hatuwezi kuyapitia kirahisi.”
Na changamoto haikuwa uwanjani pekee. “Upweke, vyakula, maisha... na hela nilikuwa napata ndogo. Wakati huo nilikuwa nalipwa pauni 600 kwa wiki. Unaona pauni 600, lakini ikikatwa nyumba, gari, madeni, bills na kila kitu, unabaki na pauni 150 tu kwa wiki,” anasema.
Anaongeza; “Unaweza kuona ni hela nyingi, lakini ni hela ndogo sana. Bado hujavaa nguo, hujanunua nguo za baridi, hujala. Mwisho unabaki pauni 70, 60. Sasa ukilinganisha na huku Tanzania wakati huo, tunapata laki kadhaa hapa, tunapata hela za viingilio kila Jumamosi, halafu wafadhili pembeni wanakupa laki tatu, laki nne. Unauliza, kwa nini nipate shida kule?”
Ndipo akaanza kuona tatizo ambalo hadi leo anasisitiza Tanzania lazima ilitatue.
“Akili yangu haikuwa imejengwa mapema. Ndio maana akademi zinasaidia. Ukienda kule unatakiwa ujengwe kisaikolojia na kimweili,” anasema.
VIPAJI VIPO, TATIZO NI HILI
China anasema tatizo la Tanzania si kukosa wachezaji wenye vipaji.
“Talenti tunazo. Lakini tunakosa vitu vingi vya kimsingi vya uchezaji wa mpira wa viwango vya kule. Hatuna nidhamu, hatuna ile bidii iliyopitiliza. Kule wana bidii ambayo imepitiliza,” anasema na kuongeza;
“Unaona hata hapa ukitembea kwenye viwanja watoto wanavyocheza, unaona kabisa tuko mbali. Hata ukiangalia ligi inavyochezwa, unaona viwango vyetu viko mbali.”
Anasema tofauti hiyo anaiona hata leo anapokuwa uwanjani. “Mimi mpaka leo nacheza mpira. Nacheza kila siku, Jumatatu, Jumanne, Jumatano. Utaniona nafanya mazoezi dakika 20, 30, 40. Watoto wamekaa chini, wanaangalia, wanasubiri kipindi cha mpira tu,”
“Mpira uko hivyo unataka fitnesi na agiliti hasa mpira wa Ulaya. Huwezi kwenda kule kwa kipaji tu,” anasema.
NIKAONDOKA ENGLAND, URABUNI
Baada ya miaka miwili, China aliamua kuondoka England na kwenda Uarabuni ambako aliona angeweza kupata maisha mazuri zaidi.
“Uarabuni wakawa wananishawishi na hela. Nikawa napata hela nyingi kuliko nilizokuwa napata England. Mimi nilikuwa na familia, matatizo na nilikuwa natakiwa kusaidia familia,” anasema fundi huyo.
China anaongeza kwa kusema; “Nimerudi nyumbani hata likizo zile kutoka England siwezi kuisaidia familia yangu. Nikasema, ‘Huku England nafanya nini? Nimepoteza miaka miwili halafu sina kitu cha maana?’ nilikuwa napata hela ya kawaida, lakini haikutosheleza.”
Lakini Uarabuni nako hakukuwa na mwisho alioutarajia. “Nilipata mkataba mzuri, lakini mkataba wa Waarabu wakati huo ulikuwa wa mtu na mtu. Yaani kuna tajiri unaingia naye mkataba, sio kama timu. Yeye ndio anakulipa.”
Anaendelea; “Yule mtu akapata ajali, akafa. Ile timu ikawa haina tena mtu ambaye anaweza kunilipa hela tuliyokubaliana. Ikabidi mkataba ule niukate nirudi huku.” Na aliporudi Tanzania, mlango mwingine ukafunguka ambapo alijiunga na Simba.
SIMBA ILIKUWA ‘MEZA YA MAZUNGUMZO’
“Niliporudi huku ndio nikajiunga Simba. Wakati huo nimetoka Yanga. Simba wakaniaprochi tukakaa mezani tukazungumza wakanipa mkataba mzuri wa hela. Nikaenda kucheza kwa sababu mpira ndio maisha yangu,” anasema.
Lakini safari yake Simba iliishia katika mazingira ambayo hadi leo anayakumbuka.
“Simba walinifukuza kwa sababu kulikuwa na mambo ya imani za kishirikina. Kulikuwa na mechi na Yanga. Wanacheza, wanataka unawe maji, maji yananuka, sijui wametoa maji ya maiti, sijui nini. Mimi nikasema mimi vitu hivyo sifanyi, namwamini Mungu,” anasema na kuongeza;
“Siku hizo hizi timu zilikuwa na matatizo sana. Wakasema labda unataka kutusaliti. Mtu akazua hayo maneno, nikasimamishwa. Mimi nikakasirika, nikaachana nao. Kwa hiyo stori yangu na Simba iliishia hapo, iliishia vibaya.”
YANGA SIKUNUFAIKA
China anasema licha ya umaarufu alioupata Yanga, maisha yake hayakubadilika.
“Kiukweli Yanga mimi sikunufaika katika maisha yangu ya mpira. Nilicheza kwa umaarufu, lakini sina nilichogeni sana kwenye maisha. Yaani kusema unaweza ukawa umejenga, umefanya nini, kwa sababu walikuwa wanakuchukulia huyu ni mtoto wetu. Tumemkuza wenyewe kutoka timu B,” anasema.
Anaongeza: “Watu wanasajiliwa wanapata hela, nyinyi hampati. Kwa hiyo wakati nakuja Simba, angalau tukakaa mezani tukazungumza, wakanipa mkataba mzuri.”
Hata hivyo, China hana ubaya na timu hizo mbili.
“Nimeinjoi zote. Ni timu za ushindani, zinashindana, zina mashabiki wazuri, wanazipenda timu zao. Kwa hiyo kwa timu zote mimi nimeinjoi na niko fair. Niko timu zote mbili,” anasema.
GABON, MECHI SIWEZI KUSAHAU
Katika maisha yake yote ya soka, China anasema kuna mchezo mmoja ambao bado upo kichwani.
“Mechi ambayo naikumbuka na hata wengi wanaikumbuka labda ilikuwa timu ya Taifa Tanzania na timu ya Taifa ya Gabon. Tulicheza mwaka 1991. Hiyo mechi sijawahi kucheza mechi kama hiyo katika maisha yangu,” anasema na kuongeza:
“Tulicheza kweli. Tulifungwa goli moja tu, lakini tulikuwa tukishinda tunafuzu. Bahati mbaya tukafungwa goli moja tu tukatolewa. Inasikitisha, lakini ndio mechi ambayo siwezi kuisahau.”
“HAKUNA WA KUNIFANANISHA NAYE”
China anapoulizwa mchezaji wa kizazi cha sasa anayemkumbusha yeye, anacheka kwanza kabla ya kutoa jibu.
“Nikisema hakuna, inaweza kuwa dharau au dhambi. Lakini kusema ukweli, katika hii ‘generation’ hakuna. Huoni mtu kama mimi. Wapo wanaokaribia, lakini wanakosa vitu fulani,” anasema.
Anawataja Mudathir Yahya na Yusuph Kagoma. “Mudathir mimi nampenda kwa sababu anafanya kazi kubwa sana ya kukaba. Lakini huwezi kumfananisha na mimi kwa sababu anakosa vile vile utaalamu wa kucheza pasi nyingi, kupiga chenga, kupunguza,” anasema. Kuhusu Kagoma anasema naye anajitahidi lakini ubora wake bado upo chini kitu ambacho anavitiwa kwake ni uwezo wa kukaba kisha anarudi kwa kizazi kilichopita.
“Labda nyuma unaweza kusema Haruna Moshi. Boban alikuwa mchezaji kweli. Kama angejitunza, angejiweka, akaenda mbele zaidi, labda unaweza kusema huyu anaweza kuwa sawa na China,” anasema.
SOKA LIMEPANDA
China anakubali Tanzania imepiga hatua, lakini hataki mafanikio yapimwe kwa maneno pekee.
“Ushindani ni mkubwa na maendeleo yapo. Umesikia nimesema kitu gani pale? Takwimu zinajionyesha. Sisi tunaweza kusema tulikuwa wazuri, lakini takwimu hazitusaidii,” anasema.
“Mpira umepanda. Lakini kuna uwekezaji tofauti na zamani. Zamani hakukuwa na uwekezaji, hakuna uhamasishaji. Wachezaji walikuwa hawalipwi vizuri, hawaishi vizuri. Leo utakuta kila mchezaji ana gari, ana nyumba. Hizo siku za nyuma nyumba ilikuwa kitu adimu sana,” anasema.
Kwa mtazamo wake, biashara imeubadilisha mpira. “Haya mafanikio ni kwa sababu ya uwekezaji. Timu zimewekeza, lakini zaidi makampuni ya biashara yamekuwa mengi yanajitokeza kudhamini timu. Kwa hiyo mpira ni biashara. Umekuwa sekta na unaendeshwa kibiashara.”
AKIWA RAIS WA TFF
China anaamini suluhisho la Tanzania kuingia kwenye ramani ya soka la dunia si kusubiri mchezaji mmoja azaliwe na kipaji kikubwa.
“Nafikiri ni kuzidisha wigo wa vituo. Vituo vya ufundishaji soka. Kwa sababu soka tunayocheza halina msingi, halina uimara, mtu hajui mchezaji wa Kitanzania anatakiwa aweje. Ndio maana nikakuambia mwanzo, itakuwa vigumu kwa mchezaji wa Kitanzania kwenda kucheza mpira nje. Lazima tuwe na mipango ya kimkakati,” anasema kiungo huyo.
Anasema aliwahi kujaribu mpango wa aina hiyo miaka iliyopita. “Niliandaa program na tulikuwa tunafanya program ambayo rais alikubali wakati huo, Rais Kikwete. Mawaziri wakaingia, lakini kwa kutokuwa makini zile program zikavunjwa,” anasema na kuongeza;
“Nilichokuwa nashauri ni kwamba timu moja England ipokee wachezaji watano kila msimu kutoka Tanzania. Wale wachezaji waende kule, wawe kama wako sokoni. Mimi kazi yangu iwe kutumia uzoefu wangu na vile nilivyopotea mimi, nilivyofanya nisifanikiwe, kuwaongoza wale ili wafanikiwe.”
Mpango wake ulikuwa wa hatua kwa hatua. “Niliwaambia tuanze. Watakwenda timu ndogo, daraja la pili, baadaye daraja la kwanza, baadaye Ligi Kuu England. Hatua kwa hatua. Kwa hiyo tutapata mchezaji wa kumtengeneza sisi wenyewe kama nchi.” Na anasisitiza elimu isiwekwe pembeni.
“Serikali iwalipe ada. Kuna manufaa mawili. Wasipofanikiwa kwenye mpira, watakuwa wamesoma, watakuja kutusaidia kimasomo. Lakini katika wale watano lazima atatokea mmoja au wawili watatoboa. Akifanikiwa, anafungua mlango,” anasema na kuongeza;
“Hela ambayo Serikali itawekeza kwenye masomo na maisha kule inaweza kurudi kwa mchezaji mmoja tu akauzwa. Hizo hela za masomo hazifiki hata karibu na thamani ambayo mchezaji anaweza kuuzwa.”
SAMATTA BUANA
China alipomuona Mbwana Samatta akifika Aston Villa, alihisi fahari kama Mtanzania, lakini pia aliona changamoto ambazo huenda Samatta hakuziona.
“Mimi nilijisikia faraja sana. Nilijisikia faraja, angalau kuna mtu amekuja kutukomboa. Nilikuwa najivunia na yeye pale alipofikia,” anasema.
Lakini ana jambo moja analolijutia. “Nilijua kwamba atafeli. Sio kwamba namtakia afeli, lakini nilijua mazingira. Watu waliomzunguka... hakujaribu kujiongeza akatafuta watu kama sisi. Sisemi kila kitu ni mimi, lakini kuna wachezaji wengi kule kina Makuruzo, kina Hussein Masha na wengine ambao walikuwa maarufu.”
Pamoja na hilo, China anamhesabu Samatta kama mfungua mlango. “Angeweza kukaa na hao watu wakaeleza nini au wamweleze nini kingetokea, afanye nini. Lakini matokeo yake hakufanikiwa, akacheza muda mfupi. Hata hivyo ametufungulia njia, ametukomboa na amejitahidi kwa jitihada zake. Hicho ndio kitu kidogo ninachoweza kusema.”
MPIRA NI MIAKA 10
Mwisho China anatoa ushauri kwa kizazi kipya kuhusu jambo ambalo mara nyingi hujadiliwa pembeni ya uwanja, mahusiano na familia.
“Hatuwezi kusema ndoa au kuwa na rafiki si jambo la kiasili baina ya binadamu. Lakini kipindi cha mpira ni kidogo, angalau miaka 10. Kama mtu ameanza miaka 18, anatakiwa ajibane tu hiyo miaka 10,” anasema.
Anasema mchezaji anapaswa kujua wakati wa kuweka starehe pembeni. “Unaweza kuwa na rafiki, lakini rafiki sio mke. Mke ambaye kila siku mtakutana, mtatenda matendo ya kihusiano ambayo yanakuharibu kabisa kama mchezaji. Huwezi kudumu.”
China anasema maisha yake mwenyewe yalikuwa na nidhamu hiyo. “Mimi nilipokuwa Yanga kila mwaka wanakuja wachezaji wapya. Wale wachezaji msimu mmoja wameondoka. Mimi niko miaka sita, saba, nipo tu kwa sababu nilikuwa na nidhamu na nilijitunza. Sio kama sina rafiki wa kike, ninaye, lakini sikuwa na wa kuishi naye kitanda kimoja kila siku.”
“Tulikuwa tunakutana labda wiki moja, wiki mbili. Kuna wakati zinapita hatujaonana. Lakini ukiwa na partna ambaye mko nyumbani pamoja, lazima iwe tatizo. Nafikiri mnanielewa. Huwezi kudumu,” anasema.