Amitabh Bachchan anazeeka na pesa zake
Muktasari:
- Leo tumekusogezea, undani wa utajiri wa msanii huyu, kuanzia mali anazomiliki na bishara alizonazo pamoja na mapato aliyopata kutokana na karibia filamu 200 ambazo ameigiza hadi sasa.
MUMBAI, INDIA: KAMA ilivyo kwa mastaa wakubwa wa michezo waliostaafu lakini wanaendelea kunufaika kifedha kutokana na biashara na vyanzo vingine, ipo hivyo pia kwa msanii maarufu kutoka India, 'babu' Amitabh Bachchan, ambaye licha ya kuwa na umri wa miaka 83, ameendelea kuwa katika orodha ya waigizaji wenye pesa nyingi duniani.
Leo tumekusogezea, undani wa utajiri wa msanii huyu, kuanzia mali anazomiliki na bishara alizonazo pamoja na mapato aliyopata kutokana na karibia filamu 200 ambazo ameigiza hadi sasa.
ANAPIGAJE PESA
Kwa mujibu wa tovuti mbalimbali, Amitabh anakadiriwa kuwa na utajiri wa takribani Dola 410 milioni.
Kiasi kikubwa cha utajiri wake unatokana na mpunga wa maana anaoupata kutokana na kampuni zake binafsi.
Kwanza anamiliki kampuni ya uzalishaji wa filamu ya Amitabh Bachchan Corporation Ltd (ABCL) ambayo ilianzishwa mwaka 1995 na imezalisha filamu na vipindi vya televisheni vingi, kwa mwaka humwingizia zaidi ya Dola 50 milioni.
Pia anamiliki hisa katika kampuni mbalimbali kama JustDial, Stampede Capital na Ziddu.com ambazo zote humpa gawio la takribani Dola 20 milioni kijumla kwa mwaka.
Mbali ya yote, mkongwe huyu alipata pesa za kutosha kutokana na malipo ya kuigiza katika filamu mbalimbali ambazo hadi sasa baadhi zimeendelea kumnufaisha.
Kwa mujibu wa tovuti ya Celebrity Net Worth, Amitabh anapata takribani Dola 5 milioni kwa mwaka kutokana na muvi hizo kwa sasa.
Ameingiza pia mpunga wa kutosha kupitia ubalozi wa kampuni mbalimbali ambayo aliwahi kufanya nayo kazi wakati huo ambazo baadhi ameendelea kuwa balozi wake hadi sasa.
Kampuni hizo ni pamoja na ICICI Bank, Dabur, Kalyan Jewellers, Gujarat Tourism, Luxor Pens, OnePlus na JustDial. Anaingiza wastani wa Dola 10 milioni 10 kwa mwaka kupitia matangazo pekee.
NYUMBA ANAZOMILIKI
Anamiliku majumba kadhaa ya kifahari mjini Mumbai, ya kwanza ipo maeneo ya Juhu, yenye thamani ya zaidi ya Dola 15 milioni.
Pia ana nyumba ya familia iliyopo Pratiksha aliyoijenga mwaka 1980. Ana nyumba Janak na Vatsa ambako watoto ndio wanaishi, pia inadaiwa amejenga mjengo wa kifahari huko Dubai. Kijumla nyumba zake zote zina thamani ya Dola 20 milioni.
MSAADA KWA JAMII
Kupitia Amitabh Bachchan Foundation, nguli huyu amekuwa akichangia misaada mbalimbali ya kijamii.
Aliwalipia madeni ya zaidi ya wakulima 1,000 kutoka vijiji vya Uttar Pradesh na Maharashtra, pia amekuwa balozi wa Kampeni ya Polio-Free India, ambayo ina lengo la kuelimisha jamii juu ya ugonjwa wa Polio.
Ametoa mamilioni kusaidia hospitali, elimu na waathirika wa maafa kama mafuriko na tetemeko la ardhi, pia anashirikiana na shirika la UNICEF katika kampeni za kusaidia watoto kupata elimu.
NDEGE
Ana ndege binafsi inayokadiriwa kuwa na thamani ya Dola 3 milioni, ambayo hutumika kwa safari za kikazi na familia.
NDINGA
Bentley Continental GT -Dola 280,000
Rolls-Royce Phantom VII - Dola 500,000
Lexus LX570 - Dola 120,000
Mercedes-Benz S-Class - Dola 150,000
Range Rover Autobiography - Dola 250,000
Mini Cooper - Dola 45,000
MAISHA YA FAMILIA NA BATA
Amitabh yupo katika ndoa na mwigizaji mwenzake Jaya Bhaduri Bachchan tangu mwaka 1973 na wamebarikiwa watoto wawili Abhishek Bachchan (mwigizaji) na Shweta Bachchan Nanda (mwandishi na mfanyabiashara).
Hapendi maisha ya kujivinjari na muda wake mwingi anautumia kwenye kusoma, kusaidia jamii na kuigiza.