Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

'Panenka' ya Panenka ilivyomgeuza Diaz kituko AFCON 2025

Muktasari:

  • Wenyeji wanacheza fainali yao ya kwanza baada ya miaka 22 na wanatafuta Kombe lao la kwanza katika miaka 50.

NI fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 huko Morocco kwenye dimba la Mwanamfalme Moulay Abdellah jijini Rabbat, kati ya wenyeji, Morocco dhidi ya Senegal.

Wenyeji wanacheza fainali yao ya kwanza baada ya miaka 22 na wanatafuta Kombe lao la kwanza katika miaka 50.

Wameusubiri sana wakati huu na sasa wako tayari. Wamepitia mengi katika kipindi chote, lakini zaidi wamepitia mengi kwenye mashindano haya.

Lawama nyingi zinatupwa kwao wanapendelewa, wananunua ushindi na mambo mengine kama hayo.

Mechi inaenda hadi dakika ya 90+2, Ismaila Sarr wa Senegal anafunga bao, lakini mwamuzi analikataa kwa sababu alishapuliza filimbi ya madhambi kabla kutokana na tukio lililowahusisha Achirah Hakimi wa Morocco na Abdoulaye Seck wa Senegal.

Kunatokea mivutano na hatimaye mpira unaanza tena na dakika chache baadaye Morocco wanashambulia na mwamuzi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Jean Jackies Ndala anaamua ni penalti kwa faida ya wenyeji baada ya Elhadji Malick Diouf wa Senegal kumshika Brahimi Diaz wa Morocco.

Hata hivyo, Senegal wanagoma na kuamua kutoka nje ya uwanja, huku Sadio Mane anakuwa mtu wa mwisho na wakati anataka kutoka anakutana na kocha wa zamani wa Senegal, Cloud Leroy.

Mfaransa huyu ni mmoja wa makocha wanaoheshimika sana Afrika.

Ujerumani kuna mchezaji anaitwa Leroy Sane, mtoto wa mchezaji wa zamani wa Senegal Souleiman Sane ambaye alipewa jina hilo (Leroy) kwa heshima ya Cloud, ambaye alimfundisha baba yake.

Basi mkongwe huyo anamsimamisha Mane na kumshauri maneno ya busara wasitoke, watakuwa wameuiabisha mpira na hivyo, nyota hao wanashauriana warudi uwanjani kuendelea na mchezo.

Senegal wanarudi na penalti inapigwa na Youssef En-Nesyri na angepiga na kupata angefikisha mabao sita ya AFCON na kuifikia rekodi ya taifa lao inayoshikiliwa na Ahmed Faras na alimaliza akiwa na matano.

Hata hivyo, anabadili mawazo na kumpa mpira Brahim Diaz, nyota wa Real Madrid mwenye mabao matano, yote kayafunga katika mashindano haya na hadi sasa ndiye mfungaji bora.

En-Nesyri ana mabao matano lakini alifunga kwenye AFCON mbalimbali.

Diaz anachukua mpira na kushusha pumzi kidogo apige penalti hiyo muhimu kwa Morocco na akifunga siyo tu ataifikia rekodi ya taifa, bali pia atakonga kiu cha miaka 50 ya taifa lake kubeba Kombe hili. Anarudi nyuma na kukusanya nguvu, anakwenda kuukabili mpira kwa kasi...mbele yake yupo Edouard Mendy, kipa bora wa dunia 2021 na anapiga shuti kali....hapana, ni shuti mtoto na Mendy anadaka bila shida na mechi inaisha hapo hapo na kuingia dakika 30 za ziada.


ALICHOPIMIWA MVUMBUZI

Penalti aliyopiga Diaz inaitwa Panenka, ilivumbuliwa na mtu aliyeitwa Antonin Panenka, raia wa Czechoslovakia katika mechi ya fainali ya Mataifa ya Ulaya (Euro Cup) mwaka 1976 kati ya taifa lake na mabingwa dunia, Ujerumani Magharibi na kama tu kwa Brahimi, Panenka naye mbele yake alikuwa kipa aliyechopesha kwa mpira wake, Sepp Maier. Hii haikuwa tu mechi ya mpira, bali itikadi pia.

Ulikuwa wakati wa kilele cha vita baridi iliyoigawanya dunia katika pande kuu mbili hasimu, Magharibi chini ya Marekani na Mashariki chini ya Urusi.

Ujerumani Magharibi ilikuwa kambi ya Magharibi ambayo itikadi zao ni ubepari na Czechoslovakia ilikuwa kambi ya Mashariki ambayo itikadi yao ni Ukomunisti.

Mshindi wa mechi hii, sio tu kashinda mpira bali kashinda vita vya kiitikadi.

Mechi ikamalizika kwa sare ya 2-2 baada ya dakika 120 na ikatakiwa kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti.

Czechoslovakia wakafunga penalti zao nne za kwanza huku Ujerumani Magharibi wakikosa moja baada ya nyota wao Uli Hones kupaisha penalti yake, ndipo Antonin Panenka alipoenda kupiga penati ya tano, akifunga wamebeba Kombe naye anakuwa shujaa wa taifa.

Akauchukua mpira, akauweka kwenye kiduara, akarudi nyuma...kisha akaja kwa kasi kama anapiga shuti kali, lakini akaugusa kidogo tu na kumtesa vibaya kipa...mpira ulee unaingia wavuni taratibu sana. Dunia ikashuhudia penalti ambayo haikuwahi kuonekana kabla.

Kuanzia hapo aina hiyo ya penalti zikapewa jina la mpigaji wake wa kwanza, Panenka.


ALICHOPIMIWA DIAZ

Panenka alifunga penalti yake na kuwa shujaa...na hadi penalti hizo kupewa jina lake...lakini umewaza nini kingemkuta endapo angekosa.

Nchi yake ya Czechoslovakia chini ya utawala wa kiongozi wa chuma, Gustáv Husák, aliyeweka sheria kali za kikomunisti, isingemwelewa kabisa endapo angekosa penalti kwa upigaji ule.

Angeonekana katumika na mabepari kuuhujumu ukomunisti na adhabu ingeweza kuwa hata kifo.

Hakuna dhambi mbaya kwa wakomunisti na kutumika na mabepari.

Lakini Panenka aliweka pembeni yote haya na kujaribu kitu kipya...cha hatari.

Lakini hiyo haipo kwa Diaz, akakosa penalti yake na maisha yakaendelea kama kawaida.

Katika dakika 30 za ziada, Senegal ikafunga bao kwa shuti kali sana, kupitia Pape Gueye na kutwaa ubingwa na Diaz aliyekuwa shujaa wa Morocco wakati wote wa mashindano haya, anageuka kituko kwa shuti moja tu.

Hivyo ndivyo mpira unavyoweza kumfanya mtu. Panenka aligeuka shujaa, Diaz kageuka kituko...hata hivyo mwishowe mpira umeshinda.