Sitaki tena Urais – Sehemu ya 30
ILIKOISHIA
Usingizi ukaniruka kidogo kutokana na mawazo. Nilimuwaza sana usiku ule. Kikubwa kilichonifanya nimuwaze sana ni ukweli kwamba katika maisha yangu sikuwahi kusuhubiana na msichana jamali na mtembo kama alivyo Zena.
Pia nilijiambia kama Zena atakuwa binti wa tajiri, anaweza kunisaidia kimaisha. Kama alivyoniambia mwenyewe tutakapokutana tutasaidiana.
Nikapata ushawishi wa kwenda Dar ili nionane naye na kama wanavyosema vijana wa kileo tuyajenge.
SASA ENDELEA
Nikajiambia kwamba, kwa kuwa mwenyewe ameniruhusu nilale kwake, maana yake ni kwamba msichana huyo ana uwezo na tayari amenikubali kimapenzi.
Asubuhi ya siku iliyofuata ilikuwa Ijumaa. Nikaenda zangu kazini nikiwa na furaha tele. Nilikuwa ninaimba na kupiga miondoko ovyo. Wafanyakazi wenzangu waligundua kwamba nilikuwa tofauti siku ile.
Mmoja wao akaniambia:
“Karim, inaelekea leo una furaha sana.”
“Kwanini?” Nikamuuliza.
“Uko tofauti na siku nyingine. Umechangamka sana,” akanijibu.
“Mbona niko kawaida tu?”
“Hapana. Tunaona leo una miondoko mingi na unaimba nyimbo za mapenzi kama vile umeoa.”
Nikacheka kidogo. “Kawaida tu. Nyie mnataka siku zote ziwe sawa. Haziwezi kuwa sawa. Kuna siku mtu anaweza kuwa na furaha na kuna siku anajikuta akiwa na huzuni...”
“Lakini kunakuwa na sababu.”
“Sababu kama ipi, kwa mfano?”
“Umeoa, umepata pesa nyingi usizozitarajia na sababu nyingine kama hizo.”
Nikawaza kwamba ile sababu ya kuoa inaweza kulingana kidogo na hali yangu, ingawa mimi sikuwa nimeoa bali nilikuwa nimepata mtu ambaye ningeweza kuja kumuoa, tena mtu tajiri ambaye angeweza kunipaisha.
“Hamuwezi kujua, labda mwenzenu nimepata bingo...”
Wafanyakazi wenzangu wakacheka. Na mimi nikacheka sana.
Jioni nilipotoka kazini, nikapitia kwenye ofisi ya kampuni moja ya mabasi kuulizia usafiri wa siku iliyofuata kwenda Dar. Usafiri wa kutoka Morogoro kwenda Dar upo siku zote na wakati wote. Lakini ule hamu ya kukutana na Zena ulinifanya niende kuulizia safari hiyo siku moja kabla.
Nilipopata uhakika wa usafiri, siku iliyofuata nikaenda kazini kwangu. Kwa kawaida, siku za Jumamosi tunafanya kazi hadi saa nane mchana, ambapo nilipanga kusafiri kwenda Dar. Kwa bahati mbaya, siku ile tukapata kazi ya dharura iliyohitaji kukamilishwa siku hiyo hiyo. Badala ya kutoka kazini saa nane, tulitoka saa kumi na moja jioni.
Lakini sikuvunja safari yangu. Nilirudi nyumbani, nikaoga na kubadili nguo. Nikatia nguo yangu ya akiba kwenye begi la mgongoni kisha nikatoka.
Nilipata gari iliyokuwa inaondoka saa kumi na mbili jioni kwenda Dar. Tukaanza safari. Tulifika Dar saa tatu usiku. Baada ya kushuka kwenye gari, nikampigia simu Zena. Zena alipopokea simu, nikamwambia:
“Nimeshafika Dar.”
“Mbona umechelewa sana?” Akaniuliza.
“Nilichelewa kuondoka Moro.”
“Nilidhani hutakuja. Baada ya kuona kimya, niliondoka nyumbani.”
Nikashituka kidogo.
“Umeondoka, umekwenda wapi?”
“Niko hapa hapa Dar, lakini niko mbali kidogo.”
“Kwa hiyo?”
“Tafuta usafiri wa kukuleta Tegeta. Ukifika utanipigia simu.”
“Sawa.”
Daladala Dar ni nyingi kama karanga. Nikafika Tegeta. Niliposhuka kwenye daladala, nikampigia simu Zena.
Zena alipopokea simu, nikamwambia:
“Nimeshafika Tegeta.”
Zena akanielekeza barabara ambayo alitaka niifuate ili niweze kufika nyumbani kwake. Alinielekeza mtaa aliokuwa akiishi, ambao aliniambia haukuwa na nyumba nyingi kwa sababu majengo mengi yalikuwa yakijengwa wakati huo.
Nikafuata maelekezo yake. Kwa vile ilikuwa usiku, nilipata tabu kidogo kuzitambua barabara. Hata hivyo, nikafika mahali alipotaka nifike. Badala ya kukuta nyumba, nilikuta mti mkubwa aina ya mkuyu. Kulikuwa na nyumba kwa mbali.
Nikasimama kando ya ule mti na kumpigia simu.
“Nimeshafika hapa uliponielekeza. Nimekuta mti mkubwa, lakini hakuna nyumba.”
“Nisubiri hapo hapo.”
“Unakuja?”
“Ndiyo, ninakuja.”
“Usichelewe, hapa mahali panatisha na niko peke yangu.”
“Sitachelewa, ninakuja sasa hivi.”
Nikasimama kando ya ule mti nikiwa na begi langu mgongoni. Simu yangu niliitia mfukoni. Mbele ya ule mti kulikuwa na njia ya wapita kwa miguu.
Kulikuwa na watu mmoja mmoja waliokuwa wanapita wakiwa kwenye shughuli zao. Ingawa Zena, ambaye alikuwa ndiye mwenyeji wangu, aliniambia anakuja muda ule, lakini hadi saa tano usiku nilikuwa sijamuona. Sasa sikuona tena watu waliokuwa wanapita pita.
Nikatoa simu yangu na kumpigia.
“Mbona sikuoni?” Nikamuuliza kwa wasiwasi.
“Niko njiani ninakuja, usiondoke.”
“Unajua kwamba hapa mahali panatisha na sasa inakaribia kuwa saa tano na nusu.”
“Niko karibu kufika. Mimi ni mwanamke na niko peke yangu, mbona siogopi? Wewe mwanaume unaogopa nini, mwanaume mzima?”
“Siyo hivyo. Hii sehemu inatisha.”
“Haitapita hata dakika moja utaniona.”
Nikakata simu. Nikaona nisiendelee kusimama pale chini kwa sababu nilikuwa nikionekana kirahisi. Ningeweza kuvamiwa na watu na kunyang’anywa begi langu na simu yangu. Nikaamua kukaa juu ya ule mti. Nikapanda juu ya mti huo na kukaa kwenye tawi. Nilipokuwa hapo, nikajiona niko salama zaidi.
Wakati natupa macho huku na kule nikiwa juu ya mti, macho yangu yakaona dude lililokaa kwenye tawi jingine lililokuwa karibu yangu. Nikatoa simu yangu na kulimulika.
Kumbe lilikuwa joka! Kwa haraka nikazima tochi iliyokuwa kwenye simu. Nikatulia kimya kama sanamu.
Nikajiambia nilifanya ujinga kupanda juu ya ule mti bila kwanza kuangalia kulikuwa na nini. Sasa nilikuwa nimekaa na joka karibu kiasi kwamba nikijitikisa tu lingeweza kunivamia. Laiti ningekuwa mbali nalo, ningeweza kushuka kwenye mti huo taratibu, lakini lilikuwa karibu sana.
Mara nikasikia sauti za vijana wawili kutoka chini ya ule mti. Mmoja alisema:
“Alikuwa amesimama hapa hapa.”
Mwenzake akajibu kwa kuuliza:
“Sasa amekwenda wapi?”
“Naona ameondoka.”
Wakawa wanasogea chini ya ule mti.
“Tulifanya kosa kumuacha, tungemvamia muda ule ule. Tumemuacha, sasa amekwenda zake.”
Nikawaza kwamba vijana hao wakitazama juu tu, wataniona. Lile joka likawa linashuka taratibu. Wakati linatambaa kwenye ule mti, lilikuwa linatoa mlio. Wale vijana wakashituka na kutazama juu. Wakaliona. Acha wakimbie! Joka hilo lilishuka chini kabisa na kuanza kuwafukuza.
Punde tu likarudi. Nilikuwa natetemeka kama niliyepatwa na homa ya baridi. Joka hilo likapanda tena juu ya ule mti na kukaa mahali pale pale.
Nikahisi kwamba, kutokana na muda ulivyokuwa umekwenda na matukio yaliyotokea, Zena asingeweza kuja tena na mimi sikuwa na mahali pengine pa kwenda. Nilitaka kutazama saa ili kujua ilikuwa imefika saa ngapi, lakini nilishindwa kwa sababu saa niliyoitumia ilikuwa ya kwenye simu. Nikitoa simu, ningelishtua lile joka. Nikabaki kimya.
Ghafla nikaona lile joka linabadilika kimiujiza. Umbile la joka likaondoka na badala yake likatokea umbile la kibinadamu, tena la msichana. Nilishituka na kumtazama msichana mwenyewe.
“Asalaam alaykum, muungwana,” akanisalimia.
“Wa alaykum salaam,” nikamjibu kwa kitetemeshi cha hofu iliyonipata.
“Pole kwa safari na karibu nyumbani kwangu,” akaniambia huku akitabasamu.
“Asante.”
“Tafadhali ondoa hofu yako, tuzungumze. Mimi ni Zena unayeniona kwenye Facebook.”
“Kweli wewe ni Zena?” Nikamuuliza.
“Ndiyo, ni mimi.”
“Tuliongea kwenye simu muda mchache tu uliopita, ukaniambia unakuja.”
“Ndiyo, nimekuja hivi. Nilikuja muda kidogo uliopita. Nilikuwa ninakulinda.”
Nikaguna kwa mshangao na hofu, lakini niliguna kimoyomoyo. Nikajiuliza, huyu Zena ni kiumbe wa aina gani?
Kwa vyovyote vile, nilijiambia, hakuwa binadamu.
Nikaendelea kujiambia kwamba kama hakuwa binadamu, nitakuwa nimejiingiza mahali pasipostahili.
Lakini kila nilipomtazama uso wake, jinsi alivyoonekana mrembo na mzuri wa kutamanisha, nilishindwa kuuthibitishia moyo wangu kwamba hakuwa binadamu.
Yalinijia maswali kadhaa ambayo nilitaka kumuuliza, lakini kutokana na uoga nilishindwa kumuuliza.
Fikiria ilikuwa karibu saa sita usiku, mahali pale palikuwa kimya, nikiwa mimi na msichana huyo aliyekuwa tayari amenionesha vituko. Ningewezaje kumuuliza maswali ya kuchokonoa undani wake kabla hata hatujazoeana?
“Umeshakula?” Akaniuliza.
“Sijakula bado. Niliposhuka kwenye basi nilikuja hapa moja kwa moja na sijaondoka.”
“Sasa tushuke twende tukatafute chakula.”
Nikainua mikono ili nishike tawi lililokuwa juu yangu niweze kujirusha chini.
“Hilo begi liache hapa hapa, utakuja kulikuta,” akaniambia.
Nikashangaa na kumtazama msichana huyo.
“Liache tu,” akaniambia.
“Halitaibiwa?”
“Haliibiwi. Utakuja kulikuta hapa hapa.”
Kutokana na vituko alivyonionesha, ilibidi nimwamini. Nikalivua begi hilo mgongoni mwangu.
“Niliweke wapi?” Nikamuuliza.
“Lilete...” akaniambia.
Nikampa lile begi. Akalichukua na kulitundika juu ya tawi mojawapo la ule mti.
“Sasa tushuke.”
Mimi niliruka chini. Yeye akashuka kwa kukumbatia ule mti.
Tulipokuwa chini, nikamuuliza:
“Sasa tunakwenda wapi?”
“Kuna hoteli moja inayotoa huduma saa ishirini na nne. Tutakwenda na bodaboda.”
Kwa vile mimi nilikuwa mgeni na mwenyeji alikuwa yeye, sikumuuliza ni hoteli gani.
Tukatembea kwa miguu kuelekea barabarani. Mimi nilikuwa na wasiwasi kwa vile ulikuwa usiku mwingi, lakini mwenzangu hakuwa na wasiwasi hata chembe.