Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sitaki tena Urais – Sehemu ya 28

ILIKOISHIA

Maloto alikutwa nyuma ya nyumba yake akiwa mzima kabisa. Tukio hilo lilimshangaza kila mtu.

Maafisa usalama walifika katika eneo hilo na kuona jinsi nyumba ya Maloto ilivyoteketea.

Kama saa tisa usiku Maloto aliunganishwa kwa simu na kuzungumza  na Rais Shanga.

Maloto akamueleza rais hali iliyotokea. Rais akampa pole nyingi.

Na saa kumi na moja alfajiri Rais Shanga alifika katika eneo hilo. Alikutana na Maloto na waliongea kwa fararagha kwa karibu saa nzima.

SASA ENDELEA


Ilifahamika kuwa kitendo cha Maloto kujaribu kumvuta Jacob Niwako kwenye maji ndicho kilichozusha kizaazaa.

Ilionekana wazi kuwa pete ya Jacob ndiyo iliyosababisha maafa.

Shanga aliamini kuwa Jacob mwenyewe alikuwa anafahamu kilichotokea. Kama alifahamu, ilikuwa aibu kubwa kwa Shanga!

Mchakato wa kumpata mgombea urais wa chama cha Rais Shanga ukaanza. Shanga alihudhuria mkutano huo akiwa amenywea.

Alinywea baada ya kugundua kuwa asingepata tena urais kwani Niwako ndiye angetekelezwa kugombea urais huo badala yake.

Katika mkutano huo, Shanga, ambaye alikuwa anaomba ateuliwe tena kugombea urais kupitia chama hicho, alitakiwa awaeleze wajumbe kwa nini alitaka ateuliwe tena kugombea kiti hicho.

Shanga alisimama na kueleza kuwa alikuwa na sababu za msingi za kuomba kuteuliwa tena kugombea urais katika kipindi kingine cha miaka mitano.

“Mafanikio yaliyokwishapatikana chini ya uongozi wangu ndiyo yanayonipa shauku ya kuomba kuteuliwa tena kugombea urais,” Shanga alisema na kuongeza.

“Nimeitoa nchi yetu katika lindi la umasikini na kuiweka mahali ambapo kila mwananchi sasa anafaidi matunda ya uhuru wa nchi yetu.

“Nataka niyaendeleze mafanikio haya kwani maendeleo hayana mwisho katika uhai wa taifa,” akaeleza Rais Shanga.

Aliwataka wajumbe wamteue yeye na si mtu mwingine kwa vile yeye ni mpambanaji asiyekata tamaa na mwenye uchu wa maendeleo.

“Mkichagua mwingine anaweza kuvurunda. Nawaomba wajumbe mnielewe,” akamaliza.

Mpinzani wake wa kiti hicho, Jacob Niwako, naye alitakiwa kujieleza kwa nini achaguliwe yeye.

Shanga alipomuona Niwako akisimama, moyo wake ulififia. Akahisi kama vile pete ya Jacob ilikuwa imeshavuta hisia za wajumbe wote na kwamba wangemkubali kwa kauli moja awe mgombea urais wa chama hicho.

Lakini, kwa jinsi iliyowashangaza watu wote, Niwako aliposimama alisema:

“Nimesimama hapa si kwa nia ya kujinadi kwenu, bali kwa nia ya kutangaza kuwa nimejitoa kugombea kuteuliwa nafasi ya kuwania urais.”

Niwako alipomaliza kusema hivyo, aliketi.

Rais Shanga hakuamini masikio yake. Akamuuliza katibu wa chama hicho aliyekuwa ameketi karibu yake.

“Amesema nini?”

“Amesema amejitoa kugombea kuteuliwa nafasi ya urais,” katibu huyo akamjibu.

“Kwanini?”

“Hakueleza sababu.”

Shanga akashangaa. “Imekuwaje amejitoa mwenyewe?” akajiuliza bila kupata jibu.

Hata hivyo, alipiga makofi ya kumpongeza. Katibu wa chama hicho na wajumbe wengine pia walipiga makofi. Hapo hapo, katibu huyo alisimama na kumsifu Jacob Niwako.

“Ametumia katiba ya chama chetu kuamua kugombea kuteuliwa na baadaye yeye mwenyewe kuamua kujitoa. Tunampongeza kwa uamuzi huo.”

Shanga alishusha pumzi ndefu, lakini dukuduku la kwa nini Niwako alikuwa amejitoa liliendelea kufukuta ndani ya moyo wake.

Baada ya Niwako kujitoa, Shanga hakuwa na mpinzani tena wa kiti hicho. Wajumbe wakampitisha Shanga kwa kauli moja kuwa mgombea urais. Ilikuwa hatua iliyomfurahisha Shanga.

Mkutano ulipomalizika, wajumbe walikwenda kumpongeza Shanga kwa kuteuliwa kwake kuwa mgombea urais wa chama chao.

Shanga alishangaa alipomuona Niwako akimfuata kumpongeza.

“Nakupongeza, mheshimiwa Rais, kwa kuteuliwa tena kugombea urais katika kipindi kingine,” Niwako alimwambia Rais Shanga wakiwa wameshikana mikono.

“Asante sana, Bwana Niwako. Na wewe nakupongeza kwa kujitoa kwako kugombea nafasi hii.”

“Nilijitoa baada ya kuridhika kuwa wewe ndiye unayestahili kutuongoza tena.”

“Nakushukuru sana kwa uamuzi huo.”

Haukupita muda mrefu, kipindi cha kampeni kikaanza. Shanga aliamua kumteua Jacob Niwako kuwa meneja wake wa kampeni. Aliamua kwa makusudi kumteua Niwako ili kukata mzizi wa upinzani ndani ya chama chake na kwa vyama vingine vilivyokuwa vinashiriki katika uchaguzi huo. Shanga alihisi kuwa huenda Freemason walimtaka Niwako ajitoe kugombea kuteuliwa nafasi ya urais kwa sababu walipanga kukiimarisha chama kingine cha upinzani ili kitwae nchi.

Alipata shaka kuwa kulikuwa na mgombea mmoja kutoka vyama vya upinzani ambaye waliamua kumuunga mkono kama walivyomuunga mkono yeye katika uchaguzi uliopita.

Hivyo, kitendo chake cha kumteua Niwako kuwa meneja wake wa kampeni kingeweza kuua upinzani ambao ungeweza kuwepo dhidi yake.

Niwako alikubali kushirikiana na Shanga bila masharti yoyote na walizunguka nchi nzima kufanya kampeni za chama hicho.

Shanga na Niwako walikuwa wanakaa pamoja wakijadiliana na kushauriana kama vile hawakuwahi kutofautiana siku za nyuma, ambapo Shanga alimfukuza Niwako kazi ya uwaziri na pia alimuweka kizuizini pamoja na viongozi wengine wa Freemason.

Shanga aliamini kuwa mawazo ya binadamu hubadilika kila siku na hivyo alichukulia kuwa huenda Niwako alikuwa ameshabadilisha mawazo yake na kuamua kushirikiana naye.

Kipindi cha kampeni kikamalizika, ikafuatia siku ya uchaguzi. Uchaguzi huo ulifanyika kwa amani huku Niwako akimpa Shanga matumaini ya ushindi.

Shanga alikabiliwa na kipindi kigumu sana cha kusubiri matokeo. Alikuwa haamini kuwa angeshinda katika uchaguzi huo licha ya kumtumia Niwako kuwa meneja wake wakati wa kampeni.

Siku ile matokeo ya kura za urais yalipokuwa yakitangazwa, Shanga alikuwa nyumbani kwake. Alikuwa ameketi kimya na mke wake kando ya redio, wakisikiliza idadi ya kura za wagombea urais zilipokuwa zikitajwa.

Yeye na mke wake hawakuamini waliposikia hitimisho la matokeo ya kura, ambapo Shanga aliibuka tena kidedea kwa kuwashinda wagombea wenzake kwa idadi kubwa ya kura.

Shanga alitangazwa tena kuwa Rais wa Jamhuri ya Kamisa katika kipindi kingine cha miaka mitano. Shanga na mke wake wakatazamana kwa furaha, kisha wakanyanyuka na kukumbatiana.

“Nakupongeza, mume wangu, kwa kuchaguliwa kuwa rais wa nchi yetu kwa miaka mitano mingine,” Joyce alimwambia mume wake.

“Asante, nakushukuru sana, mke wangu. Wewe ndiye uliyenipa moyo wa ushindi wakati wote hadi hii leo ninapotangazwa kuwa mshindi.”

“Ni kwa sababu ya uwezo uliouonesha katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Kila mwananchi alijua kuwa wewe utakuwa rais wa Kamisa.”

“Asante, nashukuru sana.”

Kuanzia muda huo, Shanga alianza kupata salamu za pongezi kutoka kwa watu mbalimbali. Shanga alishangaa kupata simu kutoka kwa Osaka, kiongozi mwandamizi wa Freemason nchini Kamisa, ambaye alimpongeza kwa kuchaguliwa kwake kuwa rais.

Alimwambia, “Nakutakia uongozi wenye mafanikio, baraka tele na wenye amani na uhuru kwa wananchi wako.”

Shanga alimjibu, “Asante sana.”

Baada ya hapo, watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa chama chake, wanasiasa na watumishi wa Ikulu walifika nyumbani kwake kumpongeza.

Usiku wa siku ile haukuwa mzuri kwa Shanga. Mnamo saa nne usiku, Shanga alipokea simu kutoka kwa kiongozi wa Freemason Afrika anayeishi Afrika Kusini, ambaye alimwambia:

“Tunafurahia kuchaguliwa kwako kwa mara nyingine kuwa rais wa Kamisa na tunakukumbusha juu ya ahadi yetu ya awali. Tulikubaliana utakapoanza kipindi kingine cha urais tuchukue mwana mwingine.”

Shanga akashituka.

“Sikubaliani na wazo hilo. Mimi nilishajitoa katika kundi lenu. Mwanangu hawezi kuhusika tena,” Shanga alijibu kwa kutaharuki.

“Huwezi kukataa ahadi uliyoitoa mwenyewe. Hata kama umejitoa, lakini urais bado unao. Sisi tunalazimika kutekeleza ahadi yetu,” sauti ilimwambia kwenye simu kwa utulivu.

“Sikubali mwanangu achukuliwe. Mwanangu hahusiki na nyinyi...!”

“Ni lazima tutamchukua.”

“Sasa nitalazimika kumuwekea ulinzi.”

“Haijalishi.”

“Mimi sitaki maafa mengine. Kama tatizo ni huu urais wangu, mimi najitoa. Sitaki tena urais! Lakini mwanangu apone.”

“Hapo umesema sawa. Acha urais, mwanao apone.”

“Kesho asubuhi nitatangaza kujiuzulu.”

“Tunasubiri tuone.”

“Sawa.”

Simu ya upande wa pili ikakatwa. Kwa haraka, Shanga akampigia Otis, ambaye kwa wakati ule alikuwa katika jiji lile. Lakini simu ya Otis haikupatikana. Shanga akapata hofu na wasiwasi.

Wakati wote mke wake alikuwa akimtazama na kusikiliza alichokuwa akiongea. Yalikuwa ni masuala ya siri yake, lakini kwa vile maji yalikuwa shingoni, Shanga hakujali kuona mke wake alikuwa akimsikiliza.

Baada ya Shanga kumkosa Otis kwenye simu, alijikuta akikabiliwa na swali kutoka kwa mke wake.

“Baba Otis, kwani ni vipi? Mbona nasikia maneno ya ajabu nisiyoyatarajia!”

“Nitakueleza kila kitu. Ingawa nilikuwa nakuficha, sasa itabidi nikueleze,” Shanga alimwambia mke wake, uso wake ukiwa umetaharuki.

Hapo ndipo Shanga alipomweleza mke wake ukweli wote. Alimweleza jinsi alivyoshawishiwa na watu wawili ajiunge na Freemason ili apate urais katika ule uchaguzi wa kwanza.

Pia alimweleza jinsi alivyokubali kujiunga na Freemason na kutoa ahadi ya uongo kuwa atamtoa mwanawe pindi atakapopata urais.

Akamweleza jinsi alivyokuja kuwageuka Freemason na kujitoa katika kundi lao alipopata urais. Akamweleza kuhusu kifo cha mtoto wao wa kwanza ambaye mwili wake haukupatikana.