Sitaki tena Urais – Sehemu ya 27
ILIKOISHIA
Shanga alishuku kuwa huenda freemaso wanafanya kampeni maalum ya kuta kumuangusha baada ya jaribio lao la kutaka kumuangusha kushindikana.
Kutokana na wasiwasi wa kushindwa katika mchakato wa kumtafuta mgombea urais ndani ya chama chake, Shanga aliondoka kitandani na kuitafuta ile pete ya freemaso ambayo aliacha kuivaa mara tu alipopata urais.
Alikuwa ameiweka ndani ya kabati lake. Lakini alipolifungua na kuiangalia, hakuiona. Aliitafuta sana lakini hakufanikiwa kuiona. Mwisho akawa anajiambia, sijui imerudi kwa wenyewe au imepotea…?
SASA ENDELEA
Aliporidhika kuwa pete ile haikuwemo ndani ya kabati lake, alirudi kitandani akiwa na wazo moja tu kwamba pete hiyo ilikuwa imerudi kwa wenyewe.
Suala la pete hiyo sasa alikuwa amelipa umuhimu kuliko wakati wowote, akiamini kuwa ilikuwa imechangia katika mafanikio yake.
Wakati anajilaza kitandani, alijiambia kuwa ni lazima afanye jambo lolote kuhakikisha anamuondoa Niwako ndani ya chama chake.
Sasa aliona kuwa chama chake kilifanya kosa kutomfukuza Niwako tangu mapema.
Asubuhi kulipokucha, Shanga alipata wazo la kuwasiliana na kaka yake, Maloto Shanga, ambaye alikuwa mganga wa kienyeji.
Alimpigia simu na kumtaka afike nyumbani kwake kabla ya saa mbili asubuhi. Shanga alitoa taarifa kwa walinzi wake kuwa Maloto aruhusiwe kuingia.
Maloto alifika nyumbani kwa Rais Shanga saa mbili juu ya alama. Alipoingia ndani, Shanga alimkaribisha na kunywa naye chai ya asubuhi.
Wakati wanakunywa chai, ndipo Shanga alipomweleza Maloto kuhusu Jacob Niwako aliyetumwa na Freemason kuwania urais.
“Si mko chama kimoja, kwa nini asikuachie?” Maloto alimuuliza Rais Shanga.
“Katiba yetu inaruhusu mwanachama yeyote anayetaka kuteuliwa kugombea urais kufanya hivyo.”
“Wasiwasi wako ni nini?”
“Yule mtu ni Freemason, si unajua wale watu hutumia nguvu za giza?”
“Sasa nimeelewa kwa nini umepata wasiwasi.”
“Wasiwasi wangu ni huo, wanaweza kunichafua.”
“Sasa ulitaka nikusaidieje?”
“Tumuondoe.”
“Tumuondoe kivipi?” Maloto alicheka kabla ya kuuliza tena.
“Tumuondoe uhai?”
“Hapana. Mimi sitaki hivyo. Tumuondoe tu ndani ya chama.”
“Inawezekana.”
“Nilitaka niwashawishi wajumbe wa mkutano wa chama chetu kuwa Niwako hatufai kwa sababu ni Freemason na niliwahi kumweka kizuizini.”
Lakini wakati akisema hivyo, akilini mwake Shanga aliona jambo hilo lisingewezekana, kwani hata yeye Shanga alikuwa Freemason. Alijiambia Niwako angeweza kumuumbua mbele ya wajumbe wa chama chake kwa kumtolea siri.
“Nafikiri hilo halihitaji msaada wangu,” Maloto alimwambia Shanga.
“Kwani wewe huwezi kumuondoa ndani ya chama, yaani ajitoe mwenyewe?”
“Ninaweza.”
“Kama unaweza, nifanyie hiyo kazi ili nirahisishe mambo. Utahitaji kiasi gani?”
“Nitakwambia nitakapokamilisha hiyo kazi.”
“Lakini ni kazi inayohitajika kwa haraka, kwani kuanzia kesho tunaanza mchakato wa kuteua mgombea.”
“Nitaifanya leo.”
“Nitakushukuru sana.”
Walipomaliza mazungumzo yao, waliagana. Rais Shanga alimsindikiza Maloto hadi kwenye gari lake. Maloto akajipakia na kuondoka.
Aliporudi nyumbani kwake, aliketi kwenye sofa na kuanza kutafakari.
Mke wake alimfuata na kumuuliza:
“Shemeji anasemaje?”
“Ana matatizo yake, anahitaji msaada wangu.”
“Matatizo yapi?”
Maloto akamweleza.
“Mimi nilifikiri marais hawatumii uganga.”
“Amezidiwa. Anajua urais unaweza kumtoka. Mwenzake ni Freemason.”
“Sasa utamsaidiaje?”
“Walimu wangu watanieleza.”
“Basi ngoja nikuache uendelee kufikiria.”
“Sawa.”
Mke wake alipoondoka, Maloto alisikia sauti ya mmoja wa majini yake ikimwambia akilini mwake:
“Nenda ukachukue maji ya bahari, ndoo moja, halafu uiweke katika sehemu yangu.”
Hapo hapo Maloto alinyanyuka na kumwita mtumishi wake.
“Chukua gari, nenda baharini unichotee ndoo moja ya maji ya bahari uniletee hapa,” Maloto alimwambia mtumishi huyo na kumpa funguo za gari.
Mtumishi aliondoka na gari. Baada ya saa moja alirudi. Alimpa Maloto ndoo moja ya maji ya bahari. Maloto aliichukua na kwenda kuiweka katika chumba chake cha uganga.
Wakati anaiweka chini, aliisikia ile sauti ikimwambia tena akilini mwake:
“Utatia vipande vitatu vya vitambaa ndani ya ndoo, chekundu, cheupe na cheusi. Viwe na urefu wa robo mita.”
Maloto akauliza kwa sauti ya kusikika:
“Hivyo vitambaa nivitie sasa hivi?”
Ile sauti ikamjibu akilini mwake:
“Ndiyo, vitie sasa hivi kama vipo.”
Humo ndani alikuwa na vitambaa vya rangi mbalimbali. Alichana vipande vitatu kama alivyoagizwa, akavizamisha ndani ya ile ndoo.
“Ikifika saa sita usiku utachoma ubani, kisha utachinja beberu mwekundu juu ya ndoo. Utaacha damu iingie ndani ya ndoo. Kichwa cha beberu utakitia ndani ya ndoo. Umenielewa?” Sauti iliendelea kumweleza akilini mwake.
“Nimekuelewa, lakini sijui tunafanya nini?”
“Tunamvuta Jacob Niwako ndani ya ndoo ili tuweze kumbadili kama alivyotaka rais.”
“Kwa hiyo tukifanya hivyo, Jacob atakuja kwenye maji?”
“Atakuja na tutamfanya tunavyotaka.”
“Sawa.”
Maloto alikwenda kwenye zizi la mbuzi wake na kumtazama beberu mwekundu. Akaona kulikuwa na mabeberu watatu, mmoja wao akiwa mwekundu. Akajiambia kuwa ikifika saa sita usiku atamchinja yule beberu mwekundu kama alivyoagizwa.
Ilipofika saa sita usiku, Maloto alimuamsha mke wake na kumuagiza akamchukue beberu mwekundu kutoka zizini.
“Mlete kwenye chumba cha uganga.”
Yeye mwenyewe alikwenda kuchukua kisu kikali. Beberu alipoletwa, yeye na mke wake walimshika na kumchinja juu ya ndoo. Damu yake ilichanganyika na maji ya bahari yaliyokuwa ndani ya ndoo. Maloto akakitia kichwa cha mbuzi ndani ya maji.
“Sasa kawashe makaa ya moto uniletee hapa,” Maloto akamwambia mke wake, ambaye alitoka kwenda jikoni.
Baada ya muda kidogo, mwanamke huyo alirudi akiwa na chetezo cha udongo kilichokuwa na makaa ya moto.
“Kiweke karibu na hiyo ndoo,” Maloto alimwambia mke wake.
Mwanamke huyo aliweka chetezo hicho karibu na ile ndoo. Maloto akatia aina fulani ya ubani kwenye makaa ya moto na mara moja moshi mwingi ukaanza kufuka.
“Sasa nuia unachokitaka. Jacob atakuja sasa hivi,” sauti ikasikika ghafla ndani ya akili ya Maloto.
Wakati Maloto ananuia, maji ya bahari yaliyokuwa ndani ya ndoo yalikuwa yametulia. Vitambaa vitatu vilivyotiwa ndani vilikuwa vimeloa maji na kuzama chini. Juu ya vitambaa hivyo kulikuwa na kichwa cha mbuzi.
“Jacob analetwa sasa…” Sauti ya jini ikamwambia Maloto akilini mwake.
Maloto aliyakaza macho yake kuelekea kwenye ile ndoo, akitarajia kumuona Jacob Niwako kwenye yale maji.
Lakini hakumuona. Alikiona kivuli cha mtu kilichoingia mara moja na kutoka.
“Anakinzana! Lakini endelea tu, nguvu zake zitakwisha,” ilikuwa sauti aliyokuwa akiisikia akilini mwake.
Maloto alimweleza mke wake alivyokuwa akiambiwa. Ghafla waliona pete imetokea ndani ya ndoo. Maloto aliwaza kwamba huenda ilikuwa pete ya Jacob, kwani ilikuwa na alama za Freemason.
“Imekuja pete tupu!” Maloto akamaka peke yake.
Ghafla maji yaliyokuwa ndani ya ndoo yakafurika kama povu na kisha yakalipuka kama petroli! Moto ulisambaa chumba kizima!
Wakati moto huo unalipuka, ulimpiga Maloto kifuani na kumwangusha chini. Mke wake, aliyekuwa karibu yake, aliwahi kunyanyuka na kutoka mbio. Alikimbia hadi uani akiwa amepatwa na kiwewe, kisha akarudi tena na kuchungulia kwenye kile chumba.
Alikikuta kimepamba moto huku mume wake aliyekuwa amelala chini akipiga kelele. Moto huo uliofanana na moto wa petroli ulikuwa ukiwaka hewani na kutoka kwenye mlango.
Mke wa Maloto alikimbilia tena uani. Alijaribu kutia maji kwenye ndoo na kwenda nayo ukumbini ili kuuzima moto huo, lakini akakuta ukumbi wote ulikuwa umeshapamba moto. Vifaa vilivyokuwa sebuleni vilikuwa vikiwaka.
Ndipo alipoiacha ndoo na kukimbia kurudi uani huku akipiga kelele. Alitoka nje kupitia mlango wa nyuma na kuendelea kupiga kelele.
“Jamani, moto! Jamani, moto! Nyumba yetu inaungua! Mzee Maloto anaungua!”
Sauti ya mke wa Maloto iliwaamsha majirani, ambao walijitokeza na kuanza juhudi za kuuzima moto huo kwa kuurushia maji. Juhudi hizo hazikufanikiwa. Nyumba iliendelea kuteketea.
Jirani mmoja aliwahi kupiga simu kwa kikosi cha zimamoto. Wakamwambia kuwa wanakuja.
Ingawa ilichukua nusu saa tu kwa magari mawili ya zimamoto kufika hapo, moto ulikuwa umeshapamba nyumba nzima.
Mke wa Maloto alikuwa akiendelea kupiga kelele kama aliyekuwa amerukwa na akili. Majirani zake walikuwa wamemshikilia ili asiingie ndani kwenda kumtoa mumewe, ambaye bado alikuwa ndani.
Mpaka kikosi cha zimamoto kilipofanikiwa kuuzima moto huo, nyumba ya Maloto ilikuwa imebaki kama gofu na kila kitu kilichokuwemo ndani kilikuwa kimeteketea.
Maloto alikutwa nyuma ya nyumba yake akiwa mzima kabisa. Tukio hilo lilimshangaza kila mtu.
Maafisa usalama walifika katika eneo hilo na kuona jinsi nyumba ya Maloto ilivyoteketea.
Majira ya saa tisa usiku, Maloto aliunganishwa kwa simu na kuzungumza na Rais Shanga. Maloto akamweleza rais hali iliyotokea. Rais akampa pole nyingi.
Saa kumi na moja alfajiri, Rais Shanga alifika katika eneo hilo. Alikutana na Maloto na walizungumza kwa faragha kwa karibu saa nzima.