Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sitaki tena Urais – Sehemu ya 25

Muktasari:

  • “Hatua yoyote utakayochukua utakuwa unamdhuru mtoto wako. Unatakiwa uamue ama uwapeleke mahakamani wenzetu saba au uwaachie huru. Vinginevyo, itakuwa vigumu kwako kuijua hatima ya mwanao!”

ILIKOISHIA

...“Mnajua kwamba taarifa za Otis ziko polisi na polisi wanawatafuta watu waliomteka?”

“Polisi hawawezi kutukamata.”

“Kwanini?”

“Hawana taarifa kuwa Otis tunaye.”

“Sasa si mmeshanieleza?”

“Hatua yoyote utakayochukua utakuwa unamdhuru mtoto wako. Unatakiwa uamue ama uwapeleke mahakamani wenzetu saba au uwaachie huru. Vinginevyo, itakuwa vigumu kwako kuijua hatima ya mwanao!”

Hapo hapo simu ikakatwa..

SASA ENDELEA


SHANGA alibaki na kizungumkuti. Alitambua kuwa urais wake ulikuwa umetiwa majaribuni kutokana na kosa lake la kujiunga na kundi la freemaso. Sasa alitambua kuwa alifanya kosa kushawishika na kukubali ujiunga na kundi hilo kwa imani ya kupata urais.

Alijiambia urais wake umekuwa kama usio na maana kutokana na kuandamwa na misukosuko tangu alipoamua kujitoa katika kundi la freemasons.

Alikuwa akidhni uwa kufunga shughuli zao na kuwaweka ndani viongozi wao, atakuwa amelimaliza tatizo hilo na kumbe ameliongeza.

Sasa afanye nini? Akajiuliza. Awaachie viongozi hao saba ili umnusuru mwanawe au aendelee uwaweka kizuizini na kisha atoe taarifa za kundi hilo kuhusika kumteka mwanawe kwa polisi wa Canada.

Alipowaza hivyo Shanga aliyakumbuka maneno ya mtu aliyempigia simu dakika chache zilizopita.

“Hatua yoyote utakayochukua utakuwa unamdhuru mtoto wako. Unatakiwa uamue ama uwapeleke mahakamani wenzetu saba au uwaachie huru, vinginevyo itakuwa vigumu kwako kuijua hatima ya mwanao….”

Shanga alijiambia hatua yoyote atakayochukua zaidi ya kuwaachia watuhumiwa hao au kuwafikisha mahakamani, inaweza kuwa na madhara kwa mwanawe.

Mwanagu anaweza kuuawa kama alivyouawa kaka yake! Alijiambia.

Kuwafikisha mahakamani viongozi hao saba lilikuwa wazo la msingi lakini Shanga alisita kufanya hivyo.

Alisita kwa sababu aliona endapo atawafungulia kesi watu hao, watamfichua mahakamani kwamba na yeye alikuwa mwenzao. Jambo hilo linaweza kumuumbua na kumdhalilisha ama rais wa nchi.

Shanga hakutaka ushauri kwa mtu yeyote kuhusu suala hilo na hakutaka amueleze yeyote. Akajiambia atatoa uamuzi yeye mwenyewe.

Baada ya kuwaza kwa dakika kadhaa aliona kuwa ilikuwa ni lazima achukue hatua itakayosalimisha maisha ya mwanawe. Akainua simu na kumuita Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa.

Mkurugenzi huyo alipofika ofisini kwake, Shanga alikuwa ameshasaini kibali cha kuwaachia huru viongozi saba wa freemasons aliokuwa amewaweka kizuizini.

“Ninaagiza viongozi saba wa freemaso walioko kizuizini waachiwe. Kibali cha kuwatoa hiki hapa”

Shanga alimpa mkurugenzi huyo kibali hicho.

“Nataka uhakikishe kuwa watu hao wanaachiwa leo hii”

Mkuu wa gereza la Maloto alipoonyeshwa kibali kilichokuwa na sahihi ya rais Shanga cha kumtaka awaachie huru viongozi saba wa freemaso waliokuwa wamewekwa kizuizini katika gereza hilo, alitekeleza agizo hilo.

Yeye mwenyewe pamoja na maofisa wawili wa chini yake walisimamia zoezi la kuwaachia viongozi hao mbele ya maafisa usalama wa taifa.

Lakini viongozi hao walipoambiwa wameachiwa na rais waligoma kutoka jela

“Hatutaki kuachiwa, tunataka tufikishwe mahakamani” Osaka alimwambia mkuu wa gereza hilo huku maafisa usalama.wakisikilza.

“Rais mwenyewe ndio ameamua kuwaachia” Mkuu wa gereza akawambia.

“Lisiwe tatizo kati yako na sisi. Mwambieni rais kuwa hatutaki kuachiwa tutaendelea kubaki kizuizini mpaka atakapotufikisha mahakamani”

“Hamuwezi kubaki humu ndani kwa amri yenu. Mwenye mamlaka ya kuwaweka kizuizini ni rais peke yake na kama ameamua kuwaachia, nyinyi hamuwezi kuendelea kujiweka kizuizini wenyewe. Inabidi muondoke tu”

“Hatuwezi kuondoka. Vinginevyo rais aje hapa tumueleze wenyewe”

“Rais hawezi kufika hapakwa ajili yenu”

“Na sisi hatutaondoka”

“Nyinyi ni watu wa ajabu sana”

Baada ya juhudi za kuwatoa watu hao kushindikana, mmoja wa maafisa usalama waliofika hapo alimwambia mkuu wa gereza.

“Nitakwenda kumueleza rais wanachokitaka”

Dakika chache baadaye mkurugenzi wa usalama wa taifa aliomba kuonana na rais, rais alipomruhusu aliingia ofisini kwake na kumwambia.

“Wale watu wamekataa kuachiwa”

“Unasema nini?” Rais Shanga alimuuliza kwa kugutuka.

Mkurugenzi wa usalama alimueleza kilichojiri katika gereza la Maloto. Rais Shanga alivyoyasikia yale maelezo alijihisi kama yumo ndani ya mtego ambao utamnasa mwanawe Otis. Kwanini hawataki kuachiwa? Wanataka mwanangu auawe? Alijiuliza.

“Wasiniletee upuuzi wao. Mimi nimeamua kuwaachia huru, ni lazima waondoke. Hawawezi kulazimisha niwapeleke mahakamani. Ninayo mamlaka ya kisheria ya kumuweka mtu kizuizini bila kumfikisha mahakamani”

“Basi wamegoma kabisa!”

“Kama wamegoma watolewe kwa nguvu. Hatuwezi kuwabembeleza. Wasitarajie kuwa tuna chakula cha bure cha kuwapa kila siku”

“Sasa nitapeleka maafisa wakawatoe kwa nguvu”

“Ndiyo. Wachukue polisi wakawapakie watu hao kwenye gari wakawapeleke kwenye jumba lao”

“Pia mheshimiwa rais, hukueleza kama wataruhusiwa kuendelea na shughuli zao ama la”

Hapo rais Shanga alinyamaza kimya na kuwaza. Alionekana kama mtu aliyepatwa na fadhaa. Baada ya kimya kifupi alisema.

“Na waendelee tu. Serikali haitawaingilia tena”

“Vizuri mheshimiwa. Vijana watarudi tena kutekeleza agizo lako”

Maafisa usalama waliotumwa safari hii walikwenda kwa kamanda wa polisi wa jiji la Maloto na kumueleza kuwa walihitaji msaada wa askari.

“Ninahitaji mnieleze tatizo lenu” Kamanda wa polisi akawambia.

“Kuna viongozi saba wa freemaso waliowekwa kizuizini kwa amri ya rais, hii leo rais ameamua kuwaachia. La ajabu ni kwamba watu hao wamegoma kuachiwa” Afisa usalama mmoja alimueleza kamanda huyo.

“Kwanini wamegoma kuachiwa?”

“Wanataka wafikishwe mahakamani au waendelee kubaki kizuizini”

“Sasa mmeamua kuchukua hatua gani?”

“Rais ameagiza kuwa watolewe kwa nguvu”

“Kwa hiyo mlihitaji askari wa kwenda kuwatoa, au sivyo?”

“Ndiyo hivyo”

“Sawa. Nitawapa askari na mbwa wa kuwatishia endapo wataendelea kufanya ubishi”

“Sawa kabisa. Tutahitaji pia gari la kuwapeleka kule walikokamatwa”

“Sawa?

Kamanda huyo wa polisi aliagiza askari kumi, mbwa wawili na magari mawili yafuatane na maafisa usalama hao hadi katika gereza la Maloto kuwatoa watuhumiwa waliogoma kuachiwa.

Kazi hiyo ikafanyika. Polisi hao na mbwa walifanikiwa kuwatoa viongozi hao wa freemasons kwa nguvu na kuwapakia kwenye gari. Gari la maafisa usalama liliyaongoza magari ya polisi hadi lilipokuwa jumba la freemaso. Viongozi hao saba walishushwa na kuachwa hapo.

Siku ileile wakati jua linakuchwa, waziri wa mambo ya nje wa Kamisa alipigiwa simu na balozi wa Kamisa nchini Canada na kuambiwa kuwa Otis amepatikana.

“Amepatikanaje?”

“Kusema kweli amepatikana katika mazingira ya kutatanisha sana”

“Mazingira yapi?”

“Amekutwa atika chumba anacholala akiwa kwenye usingizi mzito”

“Alifikaje hapo?”

“Haijafahamika, hakuna aliyemuona alipoingia. Alikutwa humo chumbani na wenzake. Alipoulizwa alikuwa wapi, alijibu alikuwa amelala”

“Alikuwa amelala wakati tangu juzi alikuwa hajulikani alipo? Na pia alimpigia simu baba yake na kumjulisha kuwa ametekwa!”

“Amedai kuwa hakuwahi kumpigia simu baba yake na hakuwa ametekwa!”

“Basi yatakuwa mambo ya ajabu!”

“Ni ya ajabu sana. Bado anaendelea kuhojiwa na polisi”

“Sasa anasema alikuwa wapi kwa siku mbili ambazo alikuwa haonekani?”

“Anasema alikuwa yuko hapo chuoni kama kawaida”

“Au hao waliomteka walimwambia asiseme?”

“Anachodai yeye ni kuwa hana kumbukumbu zozote kuwa alikwenda mahali popote au kama alitekwa au alimpigia simu baba yake”

Waziri wa mambo ya nje akashusha pumzi ndefu.

“Basi subiri nimfahamishe rais. Tangu asubuhi amekuwa na wasiwasi sana”

“Sawa, mfahamishe. Polisi wakikamilisha uchunguzi wao watanitumia taarifa”

“Sawa”

Waziri wa mambo ya nje alipomaliza kuzungumza na balozi, alikwenda mwenyewe ikulu uonana na rais.

Baada ya kumueleza rais taarifa aliyoipata kutoka Canada. Rais Shanga hakushangaa sana kwa sababu alijua kuwa aliachiwa baada ya yeye kuwaachia watuhumiwa wa freemasons aliokuwa amewaweka kizuizini.

Pia hakushangaa kuelezwa mazingira aliyokutwa Otis kwani alijua uwa watu hao hutumia nguvu zilizo nje ya uwezo wa binaadamu.

Mbele ya waziri wa mambo ya nje Shanga alitoa simu yake ya mkononi na kumpigia Otis. Aliposikia simu inaita alifarijika sana.

“Hello Otis! Hujambo mwanangu?” Shanga alisema mara tu simu ilipopokelewa.

“Sijambo baba. Msiwe na wasiwasi” Sauti ya Otis ikasikika wenye simu.

“Ulikuwa wapi?”

“Nipo chuoni lakini hii leo nimeambiwa eti nilikupigia simu na kukwambia uwa nimetekwa nyara!”

“Ndiyo ulinipigia ukanieleza kuwa umetekwa nyara”

“Sikumbuki ingawa simu yangu inaonyesha nilikupigia kweli.”