Sitaki tena Urais – Sehemu ya 26
ILIKOISHIA
Mbele ya waziri wa mambo ya nje Shanga alitoa simu yake ya mkononi na kumpigia Otis. Aliposikia simu inaita alifarijika sana.
“Hello Otis! Hujambo mwanangu?” Shanga alisema mara tu simu ilipopokelewa.
“Sijambo baba. Msiwe na wasiwasi” Sauti ya Otis ikasikika wenye simu.
“Ulikuwa wapi?”
“Nipo chuoni lakini hii leo nimeambiwa eti nilikupigia simu na kukwambia uwa nimetekwa nyara!”
“Ndiyo ulinipigia ukanieleza kuwa umetekwa nyara”
“Sikumbuki ingawa simu yangu inaonesha nilikupigia kweli”
SASA ENDELEA
“Uliniambia kuwa umetekwa nyara!”
“Sijatekwa. Sina kumbukumbu kuwa nilitekwa. Nashangaa sana kuambiwa hivyo.”
“Afya yako ikoje?”
“Afya yangu ni nzuri tu.”
“Na hivi sasa uko wapi?”
Ndiyo nimetoka polisi kuhojiwa.”
“Hao polisi wamesemaje?”
“Wameniambia wataendelea na uchunguzi wao.”
“Sawa. Sasa uende ukapumzike.”
Rais Shanga alipoagana na mwanawe, alimpigia simu mke wake na kumjulisha kuwa Otis ameachiwa.
“Oh, ameachiwa! Amesema alikuwa wapi?”
“Hajui alipokuwa, anasema alikuwa amelala!”
“Au walimpiga sindano ya usingizi?”
“Haijajulikana, lakini mwenyewe anakanusha kuwa alitekwa.”
“Anakanusha!”
“Anakanusha, anasema hana kumbukumbu kuwa alitekwa.”
“Sasa alikuwa wapi?”
“Anasema alikuwa amelala.”
“Alikuwa amelala wapi?”
“Alikutwa amelala chumbani mwake.”
“Alifikaje hapo chumbani?”
“Haijajulikana.”
“Lakini ni yeye mwenyewe aliyekupigia simu na kukuambia kuwa ametekwa!”
“Nimemuuliza. Anasema kuwa hakumbuki kama alinipigia simu.”
“Baba Otis! Huyo mtoto kweli ana akili timamu au ameshaharibiwa?”
“Hilo suala liko mikononi mwa polisi. Kama kutakuwa na lolote, watatuambia. Uchunguzi unaendelea.”
Joyce alisita kidogo kabla ya kusema:
“Hebu kata, nimpigie.”
“Mpigie umsikilize,” Rais Shanga alimwambia na kukata simu.
Joyce akampigia simu Otis. Alibonyeza vitufe vya simu kwa pupa, kisha akaiweka simu sikioni kusikiliza. Simu iliita na punde tu ikapokelewa.
“Hello, mama!” Sauti ya Otis ikasikika kwenye simu.
“Ndiyo, mwanangu, hujambo?”
“Sijambo, mama. Habari za huko?”
“Huku ni wema. Tumesikia umepata matatizo.”
“Sasa, mama, mimi sielewi. Polisi wamenihoji, wanataka kujua nilikuwa wapi, kwani kuna madai kuwa nilitekwa nyara. Lakini mimi sifahamu kitu.”
“Wewe si ulimpigia simu baba yako, ukamwambia kuwa umetekwa nyara?”
“Inaonekana nilimpigia simu, lakini sikumbuki nilimpigia wakati gani na nilimweleza nini.”
“Kwani tangu jana ulikuwa wapi?”
“Niko chuoni tu.”
“Mbona inasemekana hujaonekana hapo chuoni kwa siku mbili?”
“Sasa sielewi sijaonekana wapi, kwa sababu mimi sijakwenda mahali popote na sikuona watu wowote walioniteka kama ninavyoelezwa.”
“Inawezekana umepoteza kumbukumbu. Ni lazima ufanyiwe uchunguzi wa akili yako. Sisi tunaamini kuwa ulikuwa umetekwa. Sasa hatujui hao waliokuteka wamekufanya nini hadi kumbukumbu zako zimepotea.”
“Polisi wameniambia nitafanyiwa uchunguzi wa akili, lakini mimi najiona niko sawa.”
“Huwezi kujigundua mwenyewe. Acha tusubiri huo uchunguzi ufanyike.”
“Sawa, mama.”
“Sasa unafanya nini?”
“Jichunge sana, mwanangu. Ukitoka masomoni usizurure ovyo.”
“Sawa, mama, nimekusikia.”
Joyce akakata simu.
Huko Canada, polisi walimwita Otis mara kadhaa kumhoji kuhusiana na madai ya kutekwa nyara. Waliamini kwamba kwa kumhoji mara nyingi huenda Otis akaamua kueleza ukweli kuhusu mahali alipokuwa.
Kukanusha kwake madai ya kutekwa nyara kuliwafanya polisi wahisi kwamba Otis alikuwa ametishwa asiseme ukweli kuwa alitekwa au alikuwa amepoteza kumbukumbu.
Hivyo, polisi hao walimpa muda Otis wa kutafakari na kufanya uamuzi mpya.
Hata hivyo, mara zote ambazo Otis aliitwa kuhojiwa, alieleza kuwa hakuwa na kumbukumbu kwamba alitekwa na pia hakuwa na kumbukumbu kwamba alimpigia simu baba yake na kumweleza kuwa alitekwa.
Alipopelekwa katika eneo lililoelezwa kuwa alipiga simu akiwa hapo, Otis alikanusha kufika mahali hapo katika siku za karibuni.
Baada ya juhudi za polisi kugonga mwamba, walimpeleka Otis hospitalini kufanyiwa uchunguzi wa akili yake.
Taarifa ya uchunguzi huo iliwasilishwa kwa mkurugenzi wa upelelezi. Ilieleza kuwa Otis alikuwa na afya njema ya akili na hakuwa na tatizo lolote la kupoteza kumbukumbu.
Baada ya polisi kupata taarifa ya uchunguzi huo, waliamua kuliacha suala hilo. Walimwandikia balozi taarifa ya uchunguzi wao na kueleza kuwa hawakupata ukweli kuhusu madai ya kutekwa kwa Otis kutokana na Otis mwenyewe kukanusha madai hayo.
“Kwa sababu hiyo, tunaamini kuwa Otis alimdanganya baba yake alipompigia simu na kumweleza kuwa alikuwa ametekwa...” ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya polisi iliyowasilishwa katika ofisi za ubalozi wa Kamisa nchini humo.
Taarifa hiyo iliambatanishwa na taarifa ya uchunguzi wa madaktari iliyoonyesha kuwa Otis hakuwa na tatizo lolote la kupoteza kumbukumbu.
Balozi alipoipata taarifa hiyo, aliituma katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Kamisa, ambako ilimfikia Rais Shanga.
Rais Shanga hakushangazwa na chochote kilichokuwamo katika taarifa ya polisi na taarifa ya madaktari, bali alishangazwa na miujiza ya freemasons. Aliamini kwamba freemasons ndio waliomfanya mwanawe apoteze kumbukumbu za tukio la kutekwa.
Kuanzia siku ile ambayo Shanga alipata taarifa za kuachiwa kwa mwanawe, aliwahadhari sana freemasons na kuwaona kama watu hatari kwake. Alifuta usajili wao na hakutaka tena kuingilia shughuli zao.
Aliendelea kuiongoza nchi ya Kamisa hadi kipindi chake cha miaka mitano kilipomalizika. Wakati chama chake kinajiandaa kuingia katika mchakato wa kumpata mgombea urais, wafuasi wa freemasons walifanya mkutano wa faragha ambapo walimteua mfadhili wa chama cha Rais Shanga na aliyewahi kuwa waziri wa mambo ya ndani katika serikali ya Shanga, Jacob Niwako, kuingia katika kinyang’anyiro cha kumtafuta mgombea urais ndani ya chama hicho.
Jacob Niwako alikuwa bado ni mwanachama wa chama cha UM, licha ya kuwa miongoni mwa viongozi wa freemasons waliowekwa kizuizini na Rais Shanga.
Dhamira ya wafuasi wa kundi hilo kumteua Niwako kuingia katika kinyang’anyiro hicho ilikuwa ni kumwekea upinzani Rais Shanga ndani ya chama hicho ili asiteuliwe tena kugombea urais.
Wafuasi hao walikuwa na uhakika kuwa Niwako angemshinda Shanga na hivyo kuwa mgombea urais kutoka chama hicho. Pia waliamini kwa asilimia mia moja kuwa Niwako akiwa mgombea urais angeshinda uchaguzi na kuwa rais wa Kamisa. Endapo Niwako angekuwa rais, kwa mara ya kwanza nchi ya Kamisa ingekuwa na rais ambaye ni freemason.
Shanga alipata habari za kiintelijensia zilizomtambulisha kuwa angepata mpinzani ndani ya chama hicho na mpinzani mwenyewe alikuwa Jacob Niwako, ambaye alikuwa ameandaliwa na freemasons kuwa rais wa Kamisa.
Baada ya kupata habari hizo, Shanga, ambaye alitaka kuendelea kuwa rais wa Kamisa kwa kipindi kingine cha miaka mitano, alianza kupata wasiwasi. Aliamini kuwa kama Niwako angeshiriki katika kinyang’anyiro hicho, angeweza kumpa upinzani mkali na pengine kuichukua nafasi yake ya kuteuliwa tena kugombea urais.
Habari hizo zilimkosesha raha na alilieleza dukuduku hilo mke wake.
“Nimepata habari eti Jacob Niwako anataka kuingia katika kinyang’anyiro cha kuteuliwa kugombea urais!”
“Una maana yule aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani?”
“Ndiye huyo huyo.”
“Una wasiwasi kuwa atakupa upinzani ndani ya chama?”
“Anaweza kunipa upinzani. Yule ni freemason. Freemasons hutumia nguvu za giza!”
“Kumbe yule ni freemason?”
“Ndiyo sababu nilimfukuza kazi alipokuwa waziri wa mambo ya ndani. Alikuwa miongoni mwa viongozi wa kundi hilo niliowaweka kizuizini.”
“Kama ni freemason, atakubalika kweli?”
“Wale wanatumia nguvu za giza!”
“Heri wewe unayetumia nguvu za Mungu. Mimi naamini utamshinda.”
“Tulifanya kosa kutomfukuza ndani ya chama.”
“Huna sababu ya kuwa na wasiwasi naye. Mimi naamini hatakubalika.”
“Huwezi kujua mawazo ya watu.”
“Kama watamteua, watakuwa wamevipa vyama vya upinzani nafasi ya kuchukua urais.”
“Na hatuwezi kukubali kushindwa kizembe. Ni lazima tuchukue hatua tangu sasa,” Shanga alimwambia mke wake kwa hasira.
“Mtachukua hatua gani?”
“Itafahamika muda si mrefu.”
Ilikuwa mchana. Usiku ulipoingia, Shanga aliwaza sana. Akiwa amejilaza kitandani, alikumbuka jinsi freemasons walivyomhakikishia kuwa angepata urais na kweli akaupata. Alikumbuka jinsi walivyompa ile pete kimiujiza na kumweleza kuwa ilikuwa pete ya ushindi, na kweli alishinda.
Sasa alijiambia kuwa ushindi huo unaweza kwenda kwa Jacob Niwako. Shanga alishuku kuwa huenda freemasons walikuwa wanafanya kampeni maalumu ya kumwangusha baada ya jaribio lao la kutaka kumwangusha kushindikana.
Kutokana na wasiwasi wa kushindwa katika mchakato wa kumtafuta mgombea urais ndani ya chama chake, Shanga aliondoka kitandani na kuitafuta ile pete ya freemasons ambayo aliacha kuivaa mara tu baada ya kupata urais.
Alikuwa ameiweka ndani ya kabati lake. Lakini alipolifungua na kuiangalia, hakuiona. Aliitafuta sana, lakini hakufanikiwa kuiona. Mwishowe akawa anajiuliza, “Sijui imerudi kwa wenyewe au imepotea...?”