Sitaki tena Urais – Sehemu ya 24
ILIKOISHIA
“Sawa.”
Wakati anapigiwa simu kachero William alikuwa amekaaa baa akizungumza na msichana mmoja aliyekuwa akifanya kazi hapo.
“Nimeitwa. Nitakuja ukuona usiku, sawa?’ William alimwambia msichana huyo huku akinyanyuka kwenye kiti.
“Sawa,” Msichana alimjibu huku akimtazama kachero huyo alivyokuwa anaondoa.
SASA ENDELEA
Nje ya baa hiyo, William alijipakia kwenye gari lake na kuondoka. Dakika chache baadaye akawa amewasili ofisini kwa bosi wake.
“Nimepata taarifa kuwa mwana wa Rais wa Kamisa anayesoma hapa nchini ametekwa nyara na watu wasiofahamika,” Kamishna alianza kumweleza kachero huyo kuhusiana na mkasa huo.
“Kijana huyo anaitwa nani?”
“Anaitwa Otis Max Shanga.”
“Endelea.”
“Chanzo cha taarifa hii ni kwamba leo majira ya saa kumi na nusu, Otis akiwa hapa Canada, alimpigia simu baba yake na kumfahamisha kuwa alikuwa ametekwa nyara na watu wasiojulikana. Hata hivyo, kabla hajamweleza kwa kirefu, mawasiliano yalikatika na simu ya Otis haikuweza kupatikana tena.
“Baada ya taarifa hizo kuletwa nchini kwetu, imefahamika kuwa Otis hajaonekana chuoni kwa siku mbili na hajulikani mahali alipo. Sasa ninakuagiza uende katika kampuni ya Vodafone, ambayo ndiyo inayomiliki namba aliyotumia Otis.”
Mkurugenzi alimpa William kikaratasi kilichokuwa na namba ya Otis.
“Waulize namba hiyo iliwasiliana na namba zipi jana na leo. Pia, mnamo saa kumi na nusu jioni ya leo, hiyo namba ilipotumika, mwenye simu alikuwa katika eneo gani? Nadhani umenisikiliza vizuri?”
“Ndiyo, afande.”
“Sasa unaweza kwenda.”
William alipoondoka ofisini kwa Mkurugenzi wa Upelelezi, aliona kuwa alikuwa amepewa kazi ndogo sana. Aliamini kuwa Otis angefahamika alipo baada ya dakika chache tu.
William alifika kwenye ofisi za kampuni ya Vodafone. Kwa vile haukuwa muda wa kazi, alizuiwa na walinzi kuingia ndani. Hata hivyo, baada ya kujitambulisha na kueleza kuwa ilikuwa muhimu awaone wahusika wa kampuni hiyo muda huo, aliruhusiwa kuingia. Afisa wa kwanza aliyekutana naye na kumweleza tatizo lake alimwomba ampatie namba aliyokuwa akitumia Otis.
Afisa huyo alipoiona namba hiyo alimwambia William akae kwenye kiti.
“Subiri kwa dakika moja tu, nitakupa jibu.”
“Nitashukuru,” William alimwambia huku akiketi.
Afisa huyo wa kampuni ya Vodafone alizunguka kwenye meza yake, akaketi na kuielekea kompyuta iliyokuwa juu ya meza.
Baada ya kubonyeza vitufe vya kompyuta kwa sekunde kadhaa, alimwambia William:
“Kwa saa arobaini na nane zilizopita, namba hii imetumika mara moja tu. Ilitumika leo saa kumi na dakika ishirini. Ilikuwa hewani kwa sekunde kumi na tano kabla ya simu kuzimwa. Namba iliyopigiwa ilikuwa ya nje ya nchi.”
Afisa huyo alimtajia William namba ya Rais Shanga na kuendelea:
“Mnara wetu wa kwanza uliopokea mawimbi ya simu yake saa kumi na dakika ishirini ni mnara namba 105 uliopo eneo la Market. Hii inaonesha kuwa alipopiga simu alikuwa katika eneo hilo.”
“Tunaweza kumfuatilia na kujua yuko mahali gani au katika nyumba gani?” William akamuuliza afisa huyo wa Vodafone.
“Kwa sasa amezima simu, hivyo ni vigumu kufuatilia mawimbi yake.”
“Hata hivyo, ninashukuru sana kwa msaada wako.”
Market Street ulikuwa mtaa uliopo katika eneo lililokuwa kando ya jiji hilo. Mtaa huo ulipewa jina hilo kwa sababu ulikuwa umejaa biashara za mikononi kama za wamachinga. Ni eneo wanaloishi watu wa kipato cha chini, lenye nyumba za kizamani na idadi kubwa ya wahamiaji kutoka Asia na Afrika.
Kachero William alitumia dakika kadhaa kuendesha gari katika mtaa huo, akijaribu kuchunguza mahali na Otis alikuwepo na kupiga simu.
William alifika katika eneo hilo mara tu baada ya kutoka katika ofisi za kampuni ya Vodafone iliyokuwa inamiliki mtandao huo.
Katika jiji hilo haikuwa rahisi kukutana na mwendawazimu, awe mwanamke au mwanaume. Lakini katika eneo hilo William alikutana na watu kadhaa wenye matatizo ya akili, waliokuwa na mavazi machafu na wakizungumza peke yao.
Mbali na kuwepo kwa nyumba za kizamani, eneo hilo pia lilikuwa na vibanda vilivyotengenezwa kwa mabati au maboksi, ambavyo vilikaliwa na familia za mume, mke na watoto.
William aligundua kuwa isingekuwa rahisi kujua mahali alipokuwa Otis Shanga, aliyedaiwa kutekwa nyara na watu wasiofahamika, licha ya kufahamika kuwa alipiga simu akiwa katika eneo hilo.
Baada ya kufika eneo lililokuwa na ule mnara wa Vodafone, William aligeuza gari na kurudi. Alirudi ofisini kwa bosi wake na kumweleza alichofahamishwa na afisa wa kampuni ya Vodafone.
“Ulifika katika eneo hilo kufanya uchunguzi?” Mkurugenzi wa Upelelezi alimuuliza William.
“Ndiyo, nimefika. Kwa kweli nimeona si rahisi kugundua huyo kijana atakuwa mahali gani na, kama ametekwa, yuko katika nyumba gani. Inabidi ufanyike uchunguzi wa kina.”
“Mazingira uliyoyakuta yamekuonesha nini?”
“Yamenionesha kwamba, kama kijana huyo alipiga simu akiwa mahali pale, basi kuna uwezekano mkubwa kuwa alipelekwa huko na watu bila hiari yake.”
“Kwa hiyo madai ya kutekwa nyara yanaweza kuwa ya kweli?”
“Inawezekana kuwa ametekwa na amefichwa kule.”
Ilikuwa saa moja asubuhi wakati Waziri wa Mambo ya Nje wa Kamisa alipopokea simu kutoka kwa balozi wa nchi hiyo aliyekuwa Canada.
“Uchunguzi wa polisi umeonesha kwamba kuna uwezekano kuwa Otis Shanga ametekwa nyara,” balozi alimwambia Waziri wa Mambo ya Nje.
“Sasa nimwambieje Rais?”
“Mweleze ukweli kuwa mwanawe ametekwa nyara kwa mujibu wa polisi wa Canada.”
“Sasa polisi wamechukua hatua gani?”
“Polisi wamenieleza kuwa wanaendelea na upelelezi. Suala hilo hivi sasa liko kwa Mkurugenzi wa Upelelezi.”
“Usalama wa huyo kijana hadi sasa utakuwa ni kitendawili.”
“Kwa suala la usalama wake, hatuna majibu kwa sasa, lakini polisi wanaendelea kushughulika ili kujua ni kina nani waliomteka na yuko wapi.”
“Taarifa hii haitamfurahisha Rais.”
“Ninajua kuwa ni taarifa ambayo Rais hataifurahia, lakini hatuna budi kumweleza ukweli.”
“Sawa, nitawasiliana na Rais sasa hivi.”
“Na mimi ndiyo ninarejea nyumbani.”
“Huku kwetu ni asubuhi, ndiyo ninajiandaa kutoka.”
Alipomaliza kuzungumza na balozi, Waziri wa Mambo ya Nje alimpigia simu Rais Shanga na kumjulisha kuhusu taarifa aliyoipata kutoka Canada.
Rais Shanga alikuwa tayari ameshafika ofisini. Alipopata taarifa hiyo, naye alimpigia simu mke wake.
Mke wake alisikitika sana. Alikuwa amejiinamia kwenye sofa, akiwaza kwa majonzi. Alimkumbuka mwanawe wa kwanza aliyekufa kwa ajali ya gari, ambaye mwili wake haukupatikana. Na sasa maisha ya mwanawe wa pili yalikuwa yameingia matatizoni.
Akajiuliza ni mkosi gani uliowaandama watoto wake.
Licha ya kupata taarifa kuwa polisi nchini Canada walikuwa wakiendelea na upelelezi wa kumtafuta Otis, Joyce alikuwa na wazo moja tu kwamba Otis naye atauawa kama alivyouawa mwenzake.
Siku hiyo Joyce alipanga kutokwenda popote ili abaki nyumbani kusikilizia taarifa za mtoto wake. Kila wakati alijaribu kupiga namba ya Otis bila mafanikio.
Wakati ikikaribia kuwa saa sita mchana, Shanga alipokea simu ya mkononi ya moja kwa moja. Namba ya simu aliyopokea ilikuwa ya nje, iliyofanana na ya Otis.
“Hallo, Rais Shanga hapa!” Shanga alisema alipoipokea simu hiyo.
“Ndiyo, tunajua ni wewe,” sauti nzito ya mtu mzima ikasikika kutoka upande wa pili wa simu. Ilikuwa sauti ya mtu ambaye hakuzungumza kwa haraka, kama mtu aliyetoka usingizini.
“Umepata taarifa za mwanao?”
“Za kuhusu nini?”
“Kutekwa nyara.”
“Ndiyo, nimezipata. Wewe ni nani?”
“Sisi ni watu wa Freemason, ndiyo tunaoshughulika na Otis.”
Rais Shanga akashituka.
“Mnashughulika naye vipi?”
“Yuko mikononi mwetu.”
“Yaani nyinyi ndiyo mmemteka?”
“Ndiyo, lakini yuko salama.”
“Kwanini mmemteka mwanangu?”
Badala ya kusikia jibu, Shanga alisikia sauti ya kicheko cha polepole kikitokea kwa mbali. Kisha aliisikia tena ile sauti ikimuuliza:
“Umeshtuka sana?”
Mbali na kushitushwa na taarifa kwamba watu hao ndiyo waliomteka mwanawe, ile sauti iliyokuwa ikizungumza polepole na kwa kutojali, kana kwamba ilikuwa ikizungumza na mtoto mdogo, ilimkera Rais Shanga. Ilimkera zaidi baada ya mtu huyo kuangua kicheko wakati yeye alikuwa ametaharuki.
“Kwanini mmewaandama watoto wangu?” Shanga akauliza kwa sauti ya kuhamaki.
“Tunataka uwaachie wenzetu saba uliowaweka kizuizini nchini mwako!”
“Nimewaweka kizuizini kwa sababu wanajihusisha na uvunjaji wa sheria.”
“Mtu anayevunja sheria anapelekwa mahakamani, si kuwekwa kizuizini!”
“Mahakamani... wapi?”
“Mahakamani. Kwanini hukuwapeleka mahakamani?”
“Ndivyo nilivyoamua mimi.”
“Sasa tunakupa saa ishirini na nne uwapeleke mahakamani au uwaachie huru!”
“Nitaamua mimi hatima yao.”
“Na sisi ndiyo tutakaoamua hatima ya mwanao!”
“Mnajua kwamba taarifa za Otis ziko polisi na polisi wanawatafuta watu waliomteka?”
“Polisi hawawezi kutukamata.”
“Kwanini?”
“Hawana taarifa kuwa Otis tunaye.”
“Sasa si mmeshanieleza?”
“Hatua yoyote utakayochukua utakuwa unamdhuru mtoto wako. Unatakiwa uamue ama uwapeleke mahakamani wenzetu saba au uwaachie huru. Vinginevyo, itakuwa vigumu kwako kuijua hatima ya mwanao!”
Hapo hapo simu ikakatwa.