Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sitaki tena Urais – Sehemu ya 17

RAISI Pict

ILIKOISHIA

“Hapa pia mapigano yalikuwa makubwa. Askari wengi wa waaasi waliuawa hapa” Mkuu wa majeshi alimwambia rais Shanga.

“Nimeona una askari wengi waliouawa na magari yanawaka moto”

“Hata hivyo eneo la ikulu yenyewe lilikuwa shwari ingawa kulikuwa na vifaru na magari ya mizinga na vikosi vya wanajeshi.

“Mheshimiwa tunatua sasa”

“Ndiyo tutue…”

SASA ENDELEA


Wakati huo helikopta ilikuwa ndani ya eneo la Ikulu ya Maloto. Ilitua taratibu kwenye kiwanja kilichokuwa ndani ya eneo hilo.

Baada ya helikopta kutua na Rais Shanga pamoja na mke wake kushuka, mkuu wa majeshi na makamanda wake walimsindikiza Shanga ofisini kwake.

Ikulu ilikuwa tupu. Hakukuwa na mtumishi yeyote wala mlinzi yeyote zaidi ya wanajeshi.

“Inaelekea hawakufika kabisa hapa Ikulu,” Rais Shanga alisema wakati wakielekea katika moja ya majengo ya Ikulu kulikokuwa na ofisi ya rais.

“Hawakuwahi kufika. Askari wetu waliwahi kuwazuia wakati wanakuja kuiteka Ikulu.”

“Mmefanya vyema sana kuwahi kuwazuia. Kama mapigano yangetokea ndani ya Ikulu, tungepata hasara kubwa kwani nyaraka nyingi muhimu zingepotea.”

“Tulilijua hilo. Ndiyo sababu nilitaka askari wetu wafike Ikulu kwanza kabla ya kwenda mahali pengine.”

Rais Shanga aliingia ofisini kwake akiwa amefuatana na mke wake, mkuu wa majeshi na makamanda wawili.

Rais aliinua mkono wa simu na kumpigia katibu wake ambaye hakuwa na habari kuwa uasi ulikuwa umezimwa.

“Njoo Ikulu haraka,” Rais akamwambia.

Baada ya kumpigia katibu huyo, alimpigia waziri mkuu wake.

“Nilikuwa nataka kukupigia, mheshimiwa Rais, kukujulisha kuwa wanajeshi wetu shupavu wamezima uasi uliotokea,” waziri mkuu akawahi kumwambia Rais Shanga.

“Sasa kwa nini umechelewa kunijulisha?”

“Nilikuwa nawasiliana na waziri wa ulinzi kwanza ili...”

“Wewe na waziri wa ulinzi ninawataka mfike Ikulu,” Shanga akamkatiza.

“Mheshimiwa Rais, ngoja kwanza tuhakikishe usalama wa Ikulu.”

“Uhakikishe kwa nani? Mimi niko Ikulu.”

“Alah! Kumbe upo Ikulu! Sasa ngoja nimuarifu waziri wa ulinzi.”

“Waarifu na mawaziri wote wafike hapa kabla ya saa nne asubuhi hii.”

“Nitawaarifu, mheshimiwa Rais.”

Afisa aliyefika kwanza Ikulu alikuwa katibu wa rais. Wakati huo mkuu wa majeshi alikuwa ameshaondoka pamoja na makamanda wake. Kilichobaki ni kikosi maalumu cha jeshi kilichopewa jukumu la kulinda Ikulu.

Baada ya katibu wa rais kufika, alitakiwa kufanya mawasiliano na mkurugenzi wa usalama pamoja na maafisa wengine wa Ikulu. Baada ya muda wa saa moja hivi, Ikulu ilirudi katika hali yake ya kawaida. Watumishi wote wa Ikulu walifika na kuendelea na kazi zao.

Kama waziri mkuu alivyoagizwa, mawaziri wa serikali ya Shanga walianza kufika kabla ya saa nne. Ilipofika saa nne kamili, mawaziri wote walikuwa wameshafika Ikulu.

Rais Shanga akawaeleza mawaziri hao kuhusu jaribio la uasi lililotokea nchini humo na kudumu kwa saa kadhaa.

Akawaeleza kuwa uasi huo uliongozwa na afisa wa jeshi, Kanali Mbasha, ambaye alisikika kwenye redio akitangaza kuwa ameupindua utawala wa Shanga na kutwaa madaraka.

“Lakini baada ya jaribio lake kuzimwa na wanajeshi watiifu, ametoroka na hivi sasa anasakwa ili akamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya kisheria,” Rais Shanga aliendelea kueleza.

Akaongeza, “Kinachonisikitisha ni kuwa upuuzi wa mwanajeshi mmoja huyu mwenye uroho wa madaraka umegharimu roho za watu wengi na kusababisha hasara kubwa kwa taifa, pamoja na kuwatia hofu wananchi bila sababu za msingi.”

“Ninachotaka kuwaarifu ni kwamba jaribio hilo limezimwa na hivi sasa nchi ni shwari. Ninawataka muendelee na majukumu yenu bila hofu yoyote. Kama kutakuwa na mengine, nitawaeleza,” Rais akamaliza.

Kanali Robert Mbasha, aliyeongoza uasi nchini Kamisa, alikuwa amepanga kuingia Ikulu saa moja asubuhi baada ya askari waliokuwa wakimtii kumpa uhakika kuwa ifikapo saa moja asubuhi wangekuwa wameshaiteka Ikulu.

Baada ya kurekodi kanda ya kujinadi kuwa ameupindua utawala wa Shanga na kanda hizo kusikika kwenye redio, Mbasha alikuwa ndani ya gari maalumu lililofuatana na askari wake waliokuwa wakielekea Ikulu.

Ilikuwa ni baada ya kipigo kikali walichokipata kutoka kwa wanajeshi watiifu ndipo waasi hao waliposambaratika na Mbasha kutoroka kwa gari la kiraia.

Gari hilo lilitelekezwa na dereva aliyekimbia mapambano. Mbasha alijipakia pamoja na wanajeshi wawili aliowatumia kama walinzi wake.

Waliondoka katika eneo hilo la Ikulu na kurudi katikati ya jiji. Meja Denis Lazaro alimuona Kanali Mbasha wakati anakimbia. Meja Lazaro naye akachukua gari lililotelekezwa, akawapakia wanajeshi wawili na kuanza kuiandama gari aliyotoroka nayo Kanali Mbasha.

Mbasha hakutambua kuwa alikuwa akifuatiliwa mpaka alipoingia mjini. Aliona gari lililokuwa nyuma yake likimfuata kila alipoelekea.

Kwa vile magari yote mawili yalikuwa yakienda kwa mwendo kasi, Kanali Mbasha alijaribu kukatiza kwenye mitaa ili kulikwepa gari hilo. Lakini kila alipokata, gari hilo lilikuwa nyuma yake.

Akaanza kupata wasiwasi. Hakujua ni kina nani waliokuwa wakimfuatilia, lakini alishuku huenda walikuwa maafisa wa Usalama wa Taifa waliotaka kumkamata.

Hakutaka kwenda huko alikokusudia kwenda. Akaona ni bora alitege gari hilo la nyuma na kisha alilipue!

Wakati huo, Meja Lazaro alikuwa ameshawasiliana na mkuu wake kupitia redio ya mawasiliano na kuomba msaada wa helikopta ya kumfuatilia Kanali Mbasha ili aweze kukamatwa.

Wakati Mbasha anamaliza tu kuzungumza kwenye redio yake ya mawasiliano, alishitukia risasi za SMG zikivunja kioo cha mbele cha gari alilokuwa akiendesha. Risasi moja ilimpata mwanajeshi aliyekuwa ameketi kando yake na kumuua papo hapo.

Mbasha aliyumbisha gari ili kukwepa risasi zilizokuwa zikiwamiminikia kutoka katika gari lililokuwa mbele yao. Risasi hizo zilitoboa tairi za mbele za gari hilo na, kwa vile lilikuwa katika mwendo kasi, likapinduka kichwa chini, miguu juu!

Meja Lazaro na askari mwenzake walitoka kwenye gari hilo kupitia dirishani na kumuacha maiti ya mwenzao ndani ya gari. Walijificha nyuma ya gari hilo. Meja alichomoa bastola yake ya kijeshi na mwenzake akashika bunduki yake, kisha wakaanza kujibu mashambulizi.

Gari alilokuwa akiendesha Mbasha lilikuwa limesimama mita chache mbele yao. Mbasha na askari wenzake walikuwa wakilitazama gari alilokuwa akiendesha Meja Lazaro wakati linapinduka baada ya wao kulishambulia kwa risasi.

Risasi walizofyatua Meja Lazaro na mwenzake ziliweza kutoboa tairi za nyuma za gari walilokuwamo Mbasha na wenzake. Gari hilo halikuweza kuendeshwa tena.

Walitoka ndani ya gari hilo na kutafuta gari jingine, lakini ghafla waliona helikopta ya jeshi juu yao.

“Hatuwezi kufika mbali. Helikopta inatufuata,” Mbasha aliwaambia wenzake.

Wakaingia katika mfereji uliokuwa kando ya barabara.

“Tukimbie kwa kuinama, twende mbele. Kule tutatokomea kwenye vichochoro,” Kanali Mbasha aliendelea kuwaambia wenzake.

Helikopta iliwafuata na kuruka chini kabisa.

“Tusiende mbele tena. Tusimame hapa hapa tuone kama itatua chini!” Mbasha alisema.

Wanajeshi hao walisimama hapo hapo na kuiona helikopta ikiwasogelea juu ya mfereji.

“Wanataka kutusonga watukamate. Fyatua risasi kwenye tenki la mafuta!” Kanali Mbasha alisema huku akiwa ameishikilia bastola yake ya kijeshi.

Wenzake walikuwa wameshika SMG. Wakazielekeza kwenye tumbo la helikopta iliyokuwa meta chache tu juu yao na kufyatua risasi kadhaa mahali lilipokuwa tenki la mafuta. Tenki likapasuka na helikopta ikalipuka!

“Sasa tukimbie!” Mbasha aliwaambia wenzake wakati helikopta hiyo ikiwaka moto.

Wakakimbia wakiwa kwenye mfereji. Helikopta ilianguka chini.

Wakati Shanga anaingia Ikulu, Mbasha alikuwa ameshalipua helikopta na kutokomea.

Yeye na wenzake waliibuka katika eneo moja lililokuwa kando ya jiji. Walifika kwa gari walilolipora kutoka kwa raia mmoja.

Mbasha alikuwa amemhamishia mke wake katika nyumba moja iliyokuwa katika eneo hilo wakati akiandaa mpango wa kuipindua serikali.

Alisimamisha gari mbele ya nyumba hiyo, akashuka pamoja na wenzake wawili. Kwa vile alikuwa ameshampigia simu mke wake kabla ya kufika hapo, walikuta geti limeshafunguliwa.

Aliyefungua geti alikuwa mke wake.

“Mke wangu, hali ni mbaya. Mpango wetu haukufanikiwa,” Mbasha alimwambia mke wake huku akifunga geti. Akaongeza:

“Tunahitaji kubadili hizi sare za jeshi na kuondoka haraka.”

“Nimeona kwenye TV. Kwani imekuwaje?”

“Kumekuwa na usaliti. Wenzangu wamekuwa ndumilakuwili, wamenisaliti. Sasa ni lazima tukimbie.”

Mbasha aliingia ndani. Wenzake walimfuata. Humo ndani aliingia chumbani. Baada ya muda kidogo alitoka akiwa amebadili nguo. Alivaa kiraia, suti nyeusi, pama jeusi na miwani myeusi.

Alikuwa ameshika suruali mbili na mashati mawili. Akawarushia wenzake waliokuwa wakimsubiri sebuleni.

“Ingieni kwenye chumba kile pale mvae hizo nguo tuondoke.”

Wakati wanajeshi hao wameingia katika chumba hicho, Mbasha alimtazama mke wake aliyekuwa mbele yake.

“Sisi tukiondoka, na wewe utaondoka urudi kijijini kwa muda,” akamwambia.

“Kwani nyinyi mtaelekea wapi?”

Kabla ya Mbasha kujibu, geti lilibishwa.

“Kuna mtu anabisha geti,” Mbasha akasema. “Hebu nenda kamsikilize.”

Mke wake alitoka na kwenda kwenye geti, akalifungua.

Maafisa wa usalama wapatao kumi wakaingia wakiwa na bastola mikononi.

“Yuko wapi Kanali Mbasha?” mmoja wao akamuuliza.