Sitaki tena Urais – Sehemu ya 15
Muktasari:
- “Mheshimiwa rais upo salama?” ilikuwa sauti ya waziri wa ulinzi iliyokuwa imejaa taharuki.
- “Nipo salama. Nimearifiwa kuwa kuna uasi wa wanajeshi, wewe una taarifa gani?’
HAPO hapo mawasiliano yakakatika. Kitendo hicho kilizidi kumchanganya Shanga. Aliurudisha mkono wa simu na kumuamsha mke wake. Kabla ya Joyce kuamka sawasawa simu ikaita tena. Shanga akaipokea haraka.
“Mheshimiwa rais upo salama?” ilikuwa sauti ya waziri wa ulinzi iliyokuwa imejaa taharuki.
“Nipo salama. Nimearifiwa kuwa kuna uasi wa wanajeshi, wewe una taarifa gani?’
“Na mimi nilitaka kukujulisha hilo”
“Ni askari gani walioasi?”
“Nimeambiwa ni wa kikosi cha kumi hadi cha kumi na tano”
“Wanataka nini?’
“Bila shaka wanataka kupindua nchi!”
“Wewe kama waziri wa ulinzi umechukua hatua gani hadi sasa kuzima uasi huo?”
”Nimepata taarifa za uasi huo dakika chache tu zilizopita lakini nimeshaagiza askari watiifu watawanywe kukabiliana na waasi hao ikiwemo kulinda sehemu nyeti za nchi”
“Hadi sasa hali ikoje?”
“Usalama bado ni tete. Kumekuwa kukisikika milio ya risasi katikati ya jiji na kuna kikosi kimekuja kulinda ikulu”
“Mkuu wa majeshi alinipigia simu lakini mawasiliano yalikatika ghafla”
“Ninawasiliana naye na nitakufahamisha kinachoendelea”.
“Sawa”
Shanga alipourudisha mkono wa simu alimueleza mke wake kuwa kumekuwepo na uasi wa baadhi ya wanajeshi lakini kabla ya kumaliza kumueleza waziri wake mkuu alimpigia simu.
“Mheshimiwa askari walioasi wameteka kituo cha redio na televisheni ya taifa na wameanza kutoa matangazo kuwa nchi imepinduliwa.”
Papo hapo Shanga na mke wake walianza kusikia milio ya risasi na mizinga, wakajua kuwa waasi hao walikuwa wakielekea ikulu.
“Risasi na mizinga vinasikika karibu na ikulu” Shanga alimwambia waziri mkuu kwenye simu.
“Tutahakikisha usalama wak mheshimiwa rais, subiri…”
Waziri akakata simu.
Sasa Shanga na mke wake alikuwa wameshapata na kiwewe. Waliona walikuwa na usalama mdogo sana.
Waliondoka kwenye kitanda na kuvaa nguo haraka haraka lakini risasi na mizingi vilizidi kuwatia hofu.
Wakati wanamaliza kuvaa simu iliita tena. Shanga akaipokea haraka.
“Mheshimiwa nimetuma askari waje kukuhamisha kwa muda kwa sababu za kiusalama” ilikuwa sauti ya mkuu wa majeshi.
“Risasi na mizinga vinazidi kusikika huku!” Shanga alimwambia mkuu wa majeshi huku akiizuia sauti yake isitoe kitetemeshi.
“Kuna mapigano karibu na ikulu. Askari watiifu wanakabiliana na waasi waliokuwa wanakuja ikulu wakiwa na mizinga”
“Lakini uwezekano wa kuwashinda upo?”
“Uwezo huo upo wa kutosha. Utasubiri kwa dakika chache gari za jeshi zitafika nyumbani kwako”
Baada ya dakika tano hivi magari mawili ya jeshi yaliyokuwa yamejaa askari pamoja na vifaru viwili vilisimama mbele ya nyumba ya rais.
Rais Shanga na mke wake walipakiwa kwenye gari la jeshi na kupelekwa mahali wasikokujua.
Walipotakiwa kuteremka kutoka kwenye gari la jeshi ndipo walipogundua kuwa walipelekwa katika moja ya kambi za jeshi iliyokuwa na ulinzi mkali.
*************
Uasi nchini humo ulianza saa sita usiku. Wanajeshi wa kikosi cha kumi hadi kumi na tano pamoja na maafisa wao walitoka kwenye makambi wakiwa na silaha vikiwem bunduki, vifaru na mizinga.
Mpaka mkuu wa majeshi anapata taarifa, wanajeshi hao walikuwa wameshashika sehemu nyeti za nchi hiyo na sasa walikuwa wanapigania kuiteka ikulu. Baadhi ya maeneo waliyoyashika ilikuwa kituo cha redio na televisheni ya taifa, kiwanja cha ndege na bandari.
Ilimbidi mkuu wa kituo kuwasiliana na makamanda wa jeshi hilo waliokuwa katika maeneo ambayo hayakuwa na uasi ili kwenda kuzima uasi huo.
Askari hao watiifu walipoingia katika jiji la Maloto walikabiliana na upinzani mkali wa waasi hao. Mpaka Rais Shanga na mke wake wanahamishiwa katika kambi ya jeshi kwa usalama wao mapambano yalikuwa yamepamba moto katika jiji hilo. Waasi hao kwa kutumia redio na televisheni ya taifa walikuwa wakiwataka askari wenzao kuwaunga mkono kuuondoa utawala wa Rais Shanga.
Walikuwa wakieleza kuwa tangu Rais Shanga alipotwaa madaraka ameonesha kutokuwa na uwezo wa kuongoza nchi na inabidi jeshi hilo lichukue madaraka ili kuinusuru nchi ya Kamisa.
Rais Shanga na mke wake walikuwa wamewekwa katika chumba kitulivu wakiwa na baadhi ya makamanda wa jeshi hilo. Shanga alikuwa ameshika redio ndogo akisikiliza kile kilichokuwa kinaelezwa na waasi hao.
Mara kwa mara Shanga alikuwa akitikisa kichwa kusikia kuwa alikuwa ameshindwa kungoza nchi. “Mimi naamini hawa waasi wanatumiwa na watu wasioitakia mema nchi yetu” Shanga aliwambia makamanda waliokuwa wamemzunguka. Akaongeza.
“Watasemaje kuwa nimeshindwa kuongoza nchi wakati katika kipindi kifupi tu cha uongzi wangu nchi imepata mafanikio makubwa”
“Ni kweli mheshimiwa, nchi imepata mafanikio makubwa. Kuna watu wenye uchu wa madaraka wametia mkono kwenye jeshi letu” alisema mmoja wa makamanda hao.
“Kwanini hawasemi nimeshindwa wapi?. Wangesema ili tuwaelewe” Rais aliendelea kusema akionesha wazi kuhamaki. Akamtazama mke wake aliyekuwa amejaa hofu.
“Tulia mke wangu. Hili ni tatizo dogo tu. Ondoa wasiwasi”
“Vita si tatizo dogo kwa sababu linagharimu roho za watu” Joyce alisema.
“Hapana, hivi si vita. Ni uasi wa askari wachache tu na watadhibitiwa muda si mrefu. Uongozi wowote ulio bora hauwezi kukosa misukosuko”
Wakati wote akiwa mafichoni Rais Shanga alikuwa akipokea taarifa mbalimbali kutoka kwa wasaidizi wake na kutoka kwa waziri mkuu na kutoka kwa waziri wa ulinzi na mkuu wa majeshi.
Taarifa hizo zilikuwa zinatofautiana. Taarifa ya mwanzo ya mkuu wa majeshi ilionesha kuwa vikosi vya wanajeshi watiifu vilikuwa vimewazidi nguvu waasi ambao walianza kusambaratika.
Baadaye taarifa ya waziri mkuu ikaeleza kuwa kulikuwa na mapambano makali yaliyokuwa yakiendelea katika eneo la kiwanja cha ndege na eneo la ikulu ambapo walinzi wa ikulu walikuwa wamekimbia. Taarifa ya waziri wa ulinzi ikasema baadhi ya waasi walianza kujisalimisha hali iliyoonyesha kuwa wamezidiwa.
Lakini taarifa iliyotoka kwa wasaidizi wake ilimueleza Shanga kuwa bado walikuwa wakiendelea kutoa upinzani kwa wanajshi watiifu na kwamba waasi hao wanashikilia kiwanja cha ndege na wanakaribia kuishika ikulu.
Taarifa ya wasaidizi wa rais ilithibitishwa na taarifa ya waasi hao iliyosikika katika redio kwamba walikuwa wameishika ikulu. Taarifa hiyo iliendelea kudai kuwa wanajeshi wengi wamejiunga na waasi hao.
Katika kuonyesha kuwa waasi hao walikuwa wamefanikiwa, askari aliyedai kuwa ndiye kiongzi wa waasi hao kanali Mbasha alijitambulisha katika redio na kueleza kuwa yeye ndiye anayeiongoza Kamisa kwa sasa.
Shanga alikuwa ameketi lakini aliposikia taarifa hiyo alihamaki na kusimama ghafla.
“Ana maana serikali yangu haipo!. Kwanini anawadanganya wananchi?” aliuliza huku akiwatazama wale makamanda.
Kabla ya kamanda yeyote kumjibu simu yake iliita tena.
“Mheshimiwa taarifa zinazotolewa redioni si za kweli. Lengo lao ni kuwadanganya wananchi waone kuwa serikali haipo, ukweli ni kuwa serikali bado ipo,” sauti ya waziri mkuu ilisikika kwenye simu.
“Kwanini wanajeshi wanashindwa kuvamia kituo cha redio na kumkamata mtu anayedai kuwa anaongoza nchi hii?” Shanga akauliza.
“Kuna mapigano makali katika njia zote za kuelekea katika kituo cha redio na televisheni. Isitoshe kanali Mbasha anayedai kuwa kiongozi wa waasi hayuko katika kituo hicho bali mkanda wake uliorikodiwa ndio unaosikika”
“Ninaamini waasi waliovamia kituo hicho ni wachache, ninashangaa kuwa mpaka sasa hawajawamaliza kabisa”
“Wanajeshi wetu wanachukua tahadhari ili wasisababishe madhara kwa wananchi kwani kituo hicho kipo katika eneo wanaloishi watu…lakini mbinu zinatumika kuhakikisha wanadhibitiwa wote”
“Waasi hao wamedai pia kuwa wameshaiteka ikulu!”
“Sijapata taarifa ya ikulu. Bado naendelea kupokea taarifa kutoka sehemu mbalimbali”
“Sawa, utanifahamisha zaidi”
“Waziri mkuu wangu ameniambia kanali Mbasha anadanganya wananchi!” Shanga aliwambia makamanda aliokuwa nao mara tu baada ya kuzungumza na waziri mkuu.
“Anatumia mbinu ya kuwavunja moyo wanajeshi wetu ili waone kuwa nchi imeshapinduliwa,” kamanda mmoja akamwambia Rais Shanga.