Sitaki tena Urais – Sehemu ya 16
ILIKOISHIA
“Sawa, utanifahamisha zaidi”
“Waziri mkuu wangu ameniambia kanali Mbasha anadanganya wananchi!” Shanga aliwambia makamanda aliokuwa nao mara tu baada ya kuzungumza na waziri mkuu.
“Anatumia mbinu ya kuwavunja moyo wanajeshi wetu ili waone kuwa nchi imeshapinduliwa” Kamanda mmoja akamwambia Rais Shanga.
SASA ENDELEA
“Katika vita kuna mbinu nyingi zinazotumika kujipatia ushindi” Kamanda mwingine akasema na kuongeza
“Tunaamini mpaka ikifika asubuhi, uasi huu utakuwa umezimwa kabisa”
Hata hivyo upande mmoja wa akili ya Shanga ulikuwa ukizingatia pia uwezekano wa utawala wake kuangushwa.
Alijiambia asisikilize maelezo ya upande wake tu, ni lazima pia asikilize upande wa pili unasema nini. Alijiambia inawezekana mawaziri wake wanamficha ukweli.
Wazo kwamba utawala wake unaweza kuangushwa na waasi hao lilimfanya afikirie usalama wake na mke wake na mustakabali wa maisha yake.
Aliwaza juu ya mapambano yanayoendelea kiwanja cha ndege ambapo ndio mahali pekee ambapo angeweza kutorokea endapo atathibitisha kuwa kweli Kanali Mbasha amechukua madaraka.
Lakini kama mapambano yatakuwa yanaendelea asingeweza kufika tena kiwanja cha ndege na usalama wake yeye na mke wake utakuwa mashakani.
Kwa mara nyingine akashitushwa na mlio wa simu. Akaipokea simu haraka.
“Mheshimiwa rais waasi wameuachia uwanja wa ndege baada ya kipigo. Hivi sasa uwanja unalindwa na wanajeshi watiifu” Mkuu wa majeshi alimwambia Shanga.
“Una uhakika na unachokisema?”
“Nina uhakika. Nimefika kiwanja cha ndege na nimejionea mwenyewe”
“Bado upo kiwanja cha ndege?”
“Bado nipo”
“Hali ikoje?”
“Kwa sasa hali ni shwari. Hakuna tena mapigano ila kumetokea uharibifu wa vitu kidogo lakini ndege zte ziko salama”
“Kuna waasi wowote waliokamatwa?”
“Ndio wapo lakini wengi wao wameuawa”
“Na una taarifa gani kwa upande wa ikulu?”
“Ndiyo ninajaribu kuwasiliana na mkuu wa kikosi kinachoongoza mapambano katika eneo hilo ili anipe taarifa ya huko”
“Ukipata taarifa utanifahamisha”
“Sawa mheshimiwa”
Shanga akakata simu.
“Wanajeshi wameshaukomboa uwanja wa ndege!” Shanga alimwambia mke wake uso wake ukionesha matumaini.
“Wameshaukomboa uwanja wa ndege?” Joyce akamuuliza kwa sauti iliyopata nguvu.
“Wameshaukomboa. Waasi wengi wamekamatwa na wengine kuuawa. Hivi sasa uwanja unalindwa na wanajeshi wetu”
“Na vipi hali ya ikulu?”
“Sijapata taarifa ya ikulu lakini nadhani itakuwa ni hivyo hivyo”
“kama watakuwa wamewazidi nguvu waasi, ni jambo la kushukuriwa sana”
Simu ya Rais Shanga ikaita tena. Shanga akaipokea. Sasa alikuwa waziri mkuu.
“Taarifa nilizozipata sasa hivi zinasema kuwa wanajeshi wameukomboa uwanja wa ndege!”
“Nimeshapata taarifa hiyo. Nataka taarifa ya ikulu”
“Nimeambiwa kwamba ikulu mapambano bado yanaendelea.”
Baada ya waziri mkuu, waziri wa ulinzi naye alipiga simu na kumueleza rais hayo hayo.
Matangazo ya redio yalikuwa bado yakiendesha propaganda kuwa nchi ilikuwa imepinduliwa. Rais Shanga alishuku kuwa tangazo hilo lilirikodiwa katika mkanda na lilikuwa likirudiwa hilo kwa hilo.
Aliamini pengine hakukuwa na muasi yeyote studio na kwamba tangazo hilo lilikuwa likijirudia lenyewe.
Mpaka inafika saa kumi na moja alfajiri matangazo ya kwenye redio yalibadilka. Msemaji ambaye alijitaja kwa jina la Kapteni Constantino alieleza kuwa nchi haikupinduliwa na akawataka wananchi kuwa watulivu.
Hapo Rais Shanga aliwatazama makamanda aliokuwa nao na kutoa tabasamu. Ilikuwa ni mara ya kwanza uso wake kuonesha tabasamu tangu alipopata taarifa ya kutokea kwa uasi. Alitaka kusema kitu lakini tangazo la kwenye redio lilimfanya anyamaze na kusikiliza.
“…kilichotokea ni uasi wa wanajeshi wachache wenye uchu wa madaraka ambao kwa sasa wako mikononi mwa dola” Tangazo hilo la kwenye redio liliendelea.
Huku akisikiliza kwa makini Shanga alikuwa akitingishatingisha kichwa kuonesha kukubaliana na yale yaliyokuwa yanazungumzwa.
“Hivi sasa nchi iko shwari, waasi wote wameshakamatwa na wengi wameuawa baada ya kutishia amani ya nchi” Msemaji ambaye alikuwa ni mwanajeshi aliendelea kueleza.
Akaongeza. “Matangazo yaliyokuwa yakitolewa kuwa nchi imepinduliwa ni propaganda ya waasi kuwadanganya wananchi. Rais wetu bado yupo na ndiye anayeongoza nchi hii”
“Huyu kapteni Mbasha amezungumza maneno makubwa sana yenye ukweli. Nitamuagiza mkuu wa majeshi amuongeze cheo kutokana na ujasiri wake. Nadhani sasa baada ya taarifa hii wananchi watakuwa watulivu” Shanga aliwambia makamanda aliokuwa nao katika kile chumba.
“Tulikwambia mheshimiwa rais, haitafika asubuhi uasi huu utakuwa umezimwa” Kamanda aliyekuwa ameyasema maneno hayo alirudia tena kumueleza rais.
“Kwa hiyo watakuwa wamezima uasi wote?” Shanga alimuuliza kama vile yeye ndiye aliyekuwa akiongoza mapambano dhidi ya uasi huo.
“Tusubiri taarifa kamili lakini ninaimani kuwa uasi wote utakuwa umezimwa
Ilipofika saa moja asubuhi helikopta ya jeshi ilitua ndani ya eneo hilo la kambi ya jeshi.
Kwa vile ilitua bila taarifa askari waliokuwa wakilinda kambi hiyo walikaa tayari na bunduki zao kuona ni kina nani watashuka.
Aliyeshuka alikuwa mkuu wa majeshi na baadhi ya makamanda wa jeshi hilo. Askari wote walimpigia saluti mkuu wa majeshi. Baada ya kupokea saluti zao aliongozwa kuelekea chumba alichokuwamo rais.
Wakati huo Rais Shanga na makamanda aliokuwa nao walikuwa wakiwatazama kupitia kwenye dirisha.
Mkuu wa majeshi alipoingia katika chumba hicho alimpigia saluti mkuu wake wa nchi kisha alimwambia.
“Mheshimiwa rais jeshi letu limezima uasi wote na tumekamata waasi mia moja na wengine wengi wameuawa. Pia wapo wachache waliotoroka akiwemo kiongozi wa waasi hao”
Shanga akampa mkono mkuu huyo wa majeshi.
“Nimefurahi sana kusikia maneno hayo”
“Tumegundua kuwa kanali Mbasha alikuwa akiwarubuni askari waliokuwa chini yake kwa karibu wiki mbili ili waitie nchi katika machafuko na ionekane kuwa umeshindwa kuongoza” Mkuu wa majeshi aliendelea kumueleza rais.
“Ni kwanini kanali Mbasha alitaka ionekane nimeshindwa kuongoza nchi?” Rais Shanga alimuuliza mkuu wa majeshi akionesha kuficha hamaki.
“Kuna uwezekano mkubwa kuwa alikuwa anatumiwa. Tumeanzisha msako wa kumtafuta ili atueleze”
“Ni kweli kwamba walikuwa wameiteka ikulu?”
“Hapana. Walidhibitiwa kabla ya kufika ikulu. Mapigano yalikuwa karibu na ikulu.”
“Nawashukuru sana kwa ujasiri mliouonesha. Nyinyi ni wanajeshi shupavu sana”
“Na kwa sababu hiyo tumeufuata kwa helikopta ili tukurudishe ikulu kwa vile sasa hali ni shwari”
“Sawa”
“Kabla ya kwenda ikulu tutakuzungusha katika maeneo yaliokuwa na mapigano ili ujionee hali halisi”
Rais Shanga na mke wake pamoja na mkuu wa majeshi walitoka nje ya chumba hicho huku wakifuatiwa na makamanda wa jeshi hilo.
Shanga na mke wake walikuwa wa kwanza kupanda kwenye helikopta, wakafuatiwa na mkuu wa majeshi ambaye aliteua makamanda wanne kuingia kwenye helikopta.
Helikopta iliruka na kuzunguka kwenye maeneo ya jiji hilo. Mkuu wa majeshi alimuonesha Rais Shanga sehemu ambazo mapigano yalitokea. Sehemu ya kwanza waliyopita ilikuwa ni kwenye kituo cha redio na televisheni ya taifa. Kulikuwa na maiti kadhaa za askari waliokuwa wamelala chini nje ya kituo hicho na kwenye barabara iliyoelekea hapo.
Wanajeshi walikuwa wakipakia maiti hizo kwenye malori ya jeshi. Majengo ya kituo yalikuwa yametobolewa matundu kwa risasi.
Sehemu ya pili waliyokwenda ilikuwa uwanja wa ndege. Hapo palikuwa na malori mengi ya jeshi pamoja na vifaru. Askari waliokuwa na bunduki walikuwa wametawanyika uwanja mzima.
Kulikuwa na magari mawili nje ya uwanja huo yaliyokuwa yanawaka moto. Wafanyakazi wa kikosi cha zima moto walikuwa wakiendelea kuzima moto huo.
Hapa ndio palitokea mapigano makali na waasi wengi waliuawa” Mkuu wa majeshi alimueleza Rais Shanga ndani ya helikopta.
“Panaonesha”
“Walikuwa wameushika huu uwanja na walishazuia ndege kutua na kuruka. Uwanja waliumiliki wao”
“Kwa hiyo shughuli zote za kiwanja cha ndege zilisimama?”
“Zilisimama kwa muda. Makamanda wangu wangeweza uukomboa uwanja wa ndege mapema sana lakini wangesababisha madhara makubwa na hasara kubwa”
“Kwakweli mlitumia busara sana”
Helikopta sasa ilikuwa ikielekea eneo la ikulu. Karibu barabara yote iliyoelekea ikulu kulikuwa na maiti za wanajeshi zilizozagaa. Kulikuwa na magari kadhaa ya kiraia yaliyokuwa yamelipuliwa na mengine yakiendelea kuwaka moto.
Wanajeshi walikuwa wakishughulika kuondoa maiti barabarani ili barabara hiyo iweze kupitika.
“Hapa pia mapigano yalikuwa makubwa. Askari wengi wa waaasi waliuawa hapa” Mkuu wa majeshi alimwambia rais Shanga.
“Nimeona una askari wengi waliouawa na magari yanawaka moto”
“Hata hivyo eneo la ikulu yenyewe lilikuwa shwari ingawa kulikuwa na vifaru na magari ya mizinga na vikosi vya wanajeshi.
“Mheshimiwa tunatua sasa”
“Ndiyo tutue…”