Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sitaki tena Urais – Sehemu ya 10

RAIS 10 Pict

UTANGULIZI

Siku moja baada ya kutangazwa kwa mshindi wa urais, Shanga aliapishwa kwenye kiwanja cha taifa kushika wadhifa huo. Kitendo hicho kilifanyika mbele ya halaiki ya wananchi. Baada ya kuapishwa, Shanga alipelekwa Ikulu moja kwa moja.

Siku ileile, Shanga alitangaza baraza lake la mawaziri ambapo alimteua Jacob Niwako kuwa waziri wake wa mambo ya ndani.

Kwa kile alichokieleza kuwa alitaka mawaziri hao waanze kazi mara moja, aliwaapisha mawaziri hao na manaibu waziri asubuhi ya siku iliyofuata na kukabidhiwa wizara zao.

SASA ENDELEA



KATIKA hotuba yake ya kwanza kwa taifa Shanga aliwataka mawaziri hao kuwa askari wapiganaji na wafanye kazi usiku na mchana kulijenga taifa.

Shanga alianza kazi za ikulu kupanga mfumo wa serikali yake aliokuwa anautaka. Kwanza aliwapangua watumishi aliowakuta ikulu, akateua wasaidizi wake wa karibu kutoka katika chama chke. Aliacha maofisa wachache ambao hawakutoka katika chama hicho.


Akiwa katika panga pangua ya ikulu alimpigia simu waziri wake wa mambo ya ndani Jacob Niwako. Niwako alipopokea simu yake Shanga alimuuliza.

“Unaendeleaje na kazi yako?”

“Ninaendelea vizuri”

“Kuna tatizo lolote ulilokutana nalo?”

“Hapana. Sijakutana na tatizo lolote”

“Sawa. Ninataka nipatiwe yale majina mawili ya wasaidizi wangu wa ikulu kutoka kwa Osaka”

“Itabidi niwasiliane na Osaka aweze kunipatia”

“Wasiliana naye leo. Ninayahitaji leo”

“Nitawasiliana naye”

Ilikuwa asubihi Shanga alipompigia simu Niwako. Ilipofika saa sita mchana Niwako alirudisha majibu.

“Nataka nikupatie yale majina”

“Sawa, nipatie”

“Ni Paul Chusama na Benjamin Mutu”

“Wafike ikulu kesho asubuhi pamoja na vyeti vya elimu zao. Watajitambulisha kwa askari na watapelekwa kwa mkurugenzi wa utumishi wa ikulu”

“Sawa mheshimiwa”

Mara tu alipomaliza kuzungumza na Niwako, Shanga alimuita mkurugenzi wa utumishi na kumpa jukumu la kuwapokea na kuwaajiri Paul Chusama na Benjamin Mutu katika safu ya wasaidizi wake.

“Watafika lini” Mkurugenzi huyo alimuuliza Rais Shanga.

“Watafika kesho asubuhi na watafikishwa kwako”

“Sawa mheshimiwa”

Asubuhi ya siku iliyofuata watu hao walifika ikulu na kupelekwa kwa mkurugenzi wa utumishi ambaye aliwahoji na hatimaye kutekeleza agizo la bosi wake la kuwaajiri watu hao.

Baada ya zoezi hilo Paul Chusama na Benjamini Mutu walifikishwa ofisini kwa Rais Shanga. Shanga alipowaona aliwakumbuka mara moja.

Walikuwa ni wale watu wawili ambao siku moja walimfuata katika ofisi za chama chake wakajitambulisha kama wanachama wa chama hicho na kisha walimwambia Shanga kuwa walimuona akiwa pamoja na mtu anayehisiwa kuwa ni freemason katika hoteli ya Pacific.

Shanga alikumbuka watu hao walimuonya juu ya kuwa na uhusiano na watu wa freemason lakini alikuja kuwakuta watu hao ndani ya kundi hilo.

Licha ya kuwakuta ndani ya kundi hilo Shanga hakupata kuwauliza lakini muda ule akiwa nao ofisini kwake aliona alikuwa na nafasi nzuri ya kuwauliza.

“Kama nawakumbuka,” Shanga aliwambia watu hao na kuongeza.

“Siku moja mliwahi kufika ofisini kwangu katika chama chetu na mlinionya kuhusu kuwa pamoja na watu wa freemasons”

“Ni kweli unatukumbuka” Chusama alimkubalia Shanga.

“Ni kwanini mlinionya wakati na nyinyi mlikuwa wanachama?”

“Tulitumwa na Osaka kuja kukupima. Tulitaka kujua ungetoa majibu gani?” Chusama akamjibu.

“Na nilitoa majibu gani?”

“Kusema kweli ulitoa majibu ya kuridhisha na tulikwenda kumueleza Osaka”

“Sasa ni kwanini mlitaka kunipima?’

“Ni kutaka kujua mawazo yako na imani yako kwa wakati ule kuhusiana na freemasons”

“Nimewaelewa. Sasa mtaanza kazi hapa ikulu kama wasidizi wangu wa karibu. Ningependa tushirikiane katika kufanikisha jukumu la ujenzi wa taifa letu,” Shanga aliwambia maofisa hao.

“Sawa mheshimiwa,”  Chusama alimuitikia.

“Na pia ninataka kuwasisitiza kitu kimoja. Mambo yetu ya kule ni ya kule kule nay a hapa ni ya hapa hapa. Tusichanganye vitu hivi viwili”

“Tunaelewa mheshimiwa,” Mutu alimwambia Shanga.

“Baada ya hayo machache ninawakaribisha ikulu. Karibuni sana. Mnaweza kufika ofisini kwangu wakati wowote kama kuna jambo muhimu. Kwa sasa mnaweza kwenda kuendelea na majukumu yenu”

“Asante sana,” wote walimshukuru Shanga na kutoka.

Katika kipindi cha majuma mawili Shanga alikwa na kazi kubwa ya kupanga serikali yake. Baada ya kuteua mawaziri, kuwaapisha na kuwapa majukumu alipanga mfumo wa ikulu kwa kadiri alivyotaka yeye. Baada ya kukamilisha utumishi wa ikulu alianza kuteua maofisa wengine wa serikali yake ambao huteuliwa na rais kama vile wakuu wa majeshi, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya na wengineo.

Shanga alibadili kila kitu alichokikuta ndani ya serikali. Nafasi nyingi alizitoa kwa maofisa waliotoka katika chama chake na akahakikisha kwamba uongozi wa serikali ni wa chama kilichomuweka katika madaraka.

Kuingia kwake ikulu na kutekeleza ahadi mbili kati ya tatu alizoziahidi kwa freemasons, kulikwa ndio mwisho wake katika kundi hilo. Alikata mawasilaano na Osaka na akawa kama aliyekwishajitoa kabisa.

Kina Osaka walikuwa wakisubiri kuona Shanga akitekeleza ahadi ya tatu ya kumtoa mwanawe. Walimpa muda wa kutosha wa kushughulikia serikali yake lakini waliona kimya kilikuwa kinazidi.

Rais Shanga pamoja na kuendelea kuitumia pete aliyopewa aliona hakuwa na wajibu mwingine wowote kwa kundi hilo.

Baada ya kupita miezi mitatu kina Osaka walianza kufanya vikao vya kumjadili Shanga. Vikao hivyo vilihudhuriwa na waziri wa mambo ya ndani Jacob Niwako na maofisa wawili wa ikulu Paul Chusama na Benjamin Mutu.

Kufuatia uamuzi wa vikao hivyo Osaka alimuandikia barua rais Shanga na kumpa Chusama aipeleke kwa rais.

Chusama alimkabidhi rais barua ile mkononi ndani ya ofisi yake. Chusama alitarajia rais angeisoma mbele yake lakini Shanga alipoipokea na kugundua inatoka wapi aliiweka juu ya meza na kumwambia Chusama.

“Nimeipokea, asante”

Ilimbidi Chusama amuage rais na kuondoka kwa vile alishaufikisha ujumbe ulikotakiwa.

Mara tu Chusama alipotoka ofisini kwa rais, Shanga aliifungua ile bahasha na kuisoma. Iliandikwa misitari michache iliyosema.

“Tunakukumbusha juu ya ahadi yetu ya tatu, ni muhimu uitekeleze kabla ya wiki hii kumalizika”

Shanga aliirudisha ile barua kwenye bahasha yake na kuitia kwenye mfuko wa ndani wa koti lake. Hakutoa jibu lolote kwa Chusama na chusama hakuthubutu kumuuliza tena.

Ingawa Shanga aliamua kubaki kimya lakini ile barua ilimkera. Aliona kama vile ilikuwa imemvunjia heshima yake. Kadhalika kitendo cha Chusama kuiwakilisha kwake pia kilimkera.

Kwa muda ule yeye alikuwa mkuu wa nchi aliyeheshimiwa na kutegemewa na taifa, ujumbe kama ule haukustahiki kwake hata kidogo.

“Hivi hawa hawatambui kuwa mimi ni mkuu wan chi, wananiandikia barua ya kipuuzi namna hii!” Shanga alijiambia kwa hasira.

Akaendelea kujiambia.

“Kama Chusama ataniletea tena barua ya namna hii nitamuuliza kama anataka kazi au hataki kazi!”

Mwishoni mwa wiki ile Shanga alibaki peke yake nyumbani kwake baada ya mke wake kuwa na ziar ya kikazi katika mkoa mmoja.

Mbali ya ikulu alikuwa akiishi na mke wake katika nyumba maalum ambayo huishi marais wanapokuwa madarakani.

Wakati anatoka bafuni kuoga simu yake ya mkononi aliyokuwa ameiweka kwenye kimeza kilichokuwa mchagoni mwa kitanda iliita.

Alikwenda kando ya kitanda akaiangalia namba ya simu iliyokuwa inaita kabla ya kuichukua simu. Aligundua kuwa aliyekuwa akipiga alikuwa Osaka. Akaipokea.

“Heshima yako mheshimiwa rais,” Osaka alimwambia rais Shanga mara tu Shanga alipopokea simu.

“Asante. Heshima yako na wewe pia”

“Nashukuru. Ninakuarifu kuwa ninataka kuonana na wewe nyumbani kwako muda huu”

“Ruksa,” Shanga alisema bila kuwaza.

“Nitafika baada ya nusu saa”

“Karibu sana”

“Asante”

Shanga akakata simu.

Hata baada ya kuirudisha simu kwenye kimeza cha mchagoni mwa kitanda Shanga hakuwaza lolote. Hakujiuliza ni kwanini Shanga anataka kuja nyumbani kwake na kwanini alimruhusu wakati alishaamua kuachana nao. Hakujiuliza kitu.

Baada ya kuvaa alimpigia simu ofisa usalama aliyekuwa akiratibu ulinzi wa nyumba aliyokuwa akiishi.

“Kuna mgeni wangu wa kifamilia atawasili punde tu, anaitwa Osaka. Aruhusiwe kuingia na gari lake” Shanga alimwambia afisa usalama huyo.

“Nikuelewa mheshimiwa rais.” Shanga akakata simu na kwenda kuketi sebuleni. Dakika chache tu baadaye afisa usalama aliyempigia simu aliingia akiwa amefuatana na Osaka.

“Karibu mgeni wangu”

“Asante” Osaka alimwambia rais Shanga akampa mkono na kumsalimia.

Ofisa usalama alitoka akimuacha Osaka akiketi kwenye sofa.

“Tumepotezana muda mrefu kidogo lakini tunajua ni kwa sababu ya majukumu” Osaka akamwambia rais uso wake ukiwa umepambwa kwa tabasamu.

“Ni kweli. Kama unavyojua ndiyo kwanza nimeanza kushika madaraka. Nilikuwa na kazi kubwa ya kuunda serikali yangu.”