Sitaki tena Urais – Sehemu ya 09
UTANGULIZI
“Sawa shemeji, usisahau kunisalimia mama watoto”
“Salamu zako zimefika”
Mwanamke huyo alipoondoka Shanga hakukaa sana, alimuaga Maloto na kuondoka.
Siku zikapita. Kampeni zilizojaa ushindani kati ya chama tawala na vyama vya upinzani ziliendelea kurindima katika nci ya Kamisa. Shanga baada ya kufanya kampeni katika jiji la Maloto kwa wiki moja alianza safari za mikoani. Mkoa mmoja baada ya mwingine. Huko kote alilakiwa na umati mkubwa wa watu. Mikutano yake pia ilihudhuriwa na watu wengi ambao walimuahidi kumpa kura katika mikoa yote aliyokwenda.
SASA ENDELEA
Mikutano yake ya kampeni iliendelea kumpa matumaini ya kushinda urais, kwani haukupita muda mrefu vyombo vya habari navyo vilianza kumpa Shanga nafasi ya kwanza ya kushinda urais. Mgombea urais wa chama tawala alipewa nafasi ya pili.
Wakati Shanga akiendelea na kampeni, vyombo vya habari vilianza kumuandama na habari za Shanga zikawa moto kwenye magazeti, redio na televisheni.
Mara kadhaa, vituo mbalimbali vya televisheni nchini humo vilifanya mahojiano na Shanga ikiwa ni mfululizo wa programu za televisheni hizo kuhojiana na wagombea urais.
Shanga alikuwa akijibu kwa ufasaha maswali aliyokuwa akiulizwa na alisisitiza kwamba ataunda baraza dogo la mawaziri, lakini litakalokuwa linafanya kazi usiku na mchana.
Washauri wake walimshauri aandae kabisa baraza lake la mawaziri kwa vile kulikuwa na kila dalili kuwa angeshinda urais. Shanga aliunda baraza la mawaziri, lakini nafasi ya waziri wa mambo ya ndani aliiacha wazi.
Hakupanga kutimiza ahadi ya kumtoa mwanawe yeyote, ila alipanga kutimiza ahadi yake ya kuteua waziri wa mambo ya ndani kutoka katika kundi la Freemasons, na pia kuteua watu wawili kutoka katika kundi hilo kuwa wasaidizi wake wa karibu atakapokuwa Ikulu.
Alikuwa akijiambia baada ya kutimiza ahadi zake hizo mbili na kuiacha ile ya tatu, atakata mawasiliano na watu hao na hivyo atakuwa ameshajiengua na kundi lao.
Muda wa kampeni ukamalizika. Ikawadia siku ya uchaguzi. Siku moja kabla ya uchaguzi huo, Shanga aliitwa na Osaka.
Osaka alimpigia simu Shanga saa moja usiku na kumkumbusha kutokosa mafundisho ya Jumamosi.
“Kesho ni uchaguzi. Unatakiwa kuhakikisha unafika kwenye mafundisho yetu ya leo.”
“Nitafika,” Shanga alimjibu.
Dakika chache kabla ya saa mbili usiku, Shanga aliliingiza gari ndani ya geti la jumba la Freemasons. Aliliegesha gari kwenye eneo la kuegesha magari ambako alikuta magari kadhaa. Aliposhuka kwenye gari, alimuona Osaka amesimama kwenye mlango wa jumba hilo akimsubiri.
Shanga alikwenda kwenye mlango huo na kulakiwa na Osaka.
“Karibu, bwana Shanga.”
“Asante.”
Walipeana mikono, kisha walifuatana kuelekea ndani ya jumba hilo.
Wakati wakitembea kuelekea kwenye ngazi za kushukia chini kwenye ukumbi wa mafundisho, Osaka alimuuliza Shanga.
“Umeionaje mikutano yako ya kampeni uliyoifanya mikoani?”
“Mikutano ilikuwa mizuri. Katika kila mkoa tuliokwenda, tulilakiwa vizuri na mikutano yetu ilijaa watu.”
“Ni dalili ya kukubalika. Na hata hapa Maloto, gumzo kubwa limekuwa ni kuhusu wewe kuwa rais.”
“Kweli kabisa.”
“Unatakiwa uandae kabisa baraza lako la mawaziri.”
“Nimeshaliandaa, sijajua tu waziri wa mambo ya ndani atakuwa nani.”
“Tutakupa jina lake.”
Walifika kwenye ngazi na kuanza kushuka chini.
“Ni nani?”
“Utamfahamu.”
“Nitamfahamu hii leo?”
“Ndiyo. Tumeshateua jina lake.”
“Hebu nitajie.”
“Hapana, hiyo si kazi yangu.”
Walitokea kwenye ukumbi uliokuwa katika ghorofa ya chini, wakayaacha yale mazungumzo. Ukumbi huo ulikuwa umejaa watu kama inavyokuwa siku za Jumanne na Jumamosi usiku.
Shanga na Osaka walikwenda kukaa kwenye viti vya mbele. Dakika chache baada ya mafundisho kumalizika, sauti kutoka kwenye kioo kilichounda taswira ya kivuli cha mtu ilimwita Shanga.
Shanga alinyanyuka na kwenda karibu na meza. Osaka, aliyeonekana kama mpambe wa Shanga, naye alinyanyuka na kumfuata.
“Muda wa kampeni umekwisha na kesho ni uchaguzi. Je, unayakumbuka makubaliano yetu?” Sauti iliendelea kumuuliza Shanga.
“Makubaliano yetu ninayakumbuka.”
“Kama unakumbuka, tutajie tulikubaliana nini na nini?”
“Tulikubaliana kuwa kama nitashinda urais, nitateua waziri wa mambo ya ndani kutoka hapa.”
“Na nini kingine?”
“Pia nitenge nafasi mbili za wasaidizi wangu wa Ikulu kutoka hapa.”
“Na nini kingine?”
Shanga alisita. Alishajua kingine kilikuwa kitu gani.
“Na nini kingine?” Sauti ilimuuliza tena kutoka kwenye kioo.
“Kingine ni kumtoa mtoto wangu.”
“Sawa sawa. Je, unatuhakikishia kwamba utatimiza ahadi zako mara tu utakapoapishwa kuwa rais?”
“Nitatimiza.”
“Sawa. Sasa nataka kukupa jina la atakayekuwa waziri wa mambo ya ndani.”
“Sawa, nipatie.”
Baada ya kimya kifupi, sauti ilisema.
“Ni Jacob Niwako.”
Shanga akafurahi.
“Namfahamu sana, ni mfadhili wetu mkuu.”
“Jacob, njoo mbele usalimiane na Shanga.”
Jacob aliyekuwa ameketi katika viti vya katikati alinyanyuka na kwenda mbele kusalimiana na Shanga. Watu wote waliokuwepo wakapiga makofi.
“Niwako, tumekuteua wewe uwe waziri wa mambo ya ndani na tunalikabidhi jina lako kwa Shanga atakayekuwa bosi wako,” ilikuwa sauti iliyotoka kwenye kioo kilichokuwa mbele ya meza.
“Nashukuru sana,” Niwako alisema huku akitabasamu.
“Wewe ni mwanachama hai wa chama chetu na umetoa mchango mkubwa katika kukiimarisha chama chetu. Nitakapokuwa rais wa nchi hii, kukuteua wewe kuwa waziri wa mambo ya ndani ni haki kabisa,” Shanga alimwambia Niwako huku akimpigapiga begani.
“Hakuna shaka kuwa utakuwa rais wetu,” Niwako alimwambia Shanga.
“Na hakuna shaka kuwa wewe utakuwa waziri wa mambo ya ndani.”
Watu wakapiga makofi kushangilia.
Mawakala wa vyama vitatu vilivyokuwa vinashiriki katika uchaguzi huo walianza kufika katika vituo vya upigaji kura walivyopangiwa tangu saa kumi na moja alfajiri.
Walikuwa wameshapatiwa semina ya uwakilishi katika zoezi hilo siku moja kabla ya uchaguzi huo. Wakati wakiwasili katika vituo, kila mmoja alikuwa akitambua jukumu lake.
Zoezi la upigaji kura lilianza saa moja asubuhi, lakini misururu ya wapiga kura ilianza kuonekana tangu saa kumi na mbili asubuhi.
Shanga na mke wake walipiga kura katika kituo kilichokuwa katika mtaa waliokuwa wanaishi. Baada ya hapo, waliondoka kwenda katika ofisi za chama hicho.
Baadhi ya maofisa wa chama hicho walikuwa katika duru la kuzunguka vituo vyote vya kupigia kura kuona jinsi zoezi hilo lilivyokuwa likiendelea.
Wakati ilipotimu saa tano, ndipo Shanga alikumbuka kwamba hakuwa amekunywa chai asubuhi. Yeye na wapambe wake walikwenda kunywa chai katika hoteli moja iliyokuwa katikati ya jiji. Mke wake alikuwa amesharudi nyumbani.
Hata chai hakuinywa kwa utulivu na furaha. Wakati wote alionekana mwenye fadhaa na mwenye wahaka wa kupokea simu alizokuwa akipigiwa mara kwa mara ili kuelezwa jinsi zoezi la upigaji kura lilivyokuwa likiendelea nchi nzima.
Zoezi hilo liliendelea hadi saa kumi jioni. Muda huo ulikuwa wa mwisho uliowekwa na tume ya uchaguzi kwa ajili ya kupiga kura.
Matokeo ya kura za wabunge yalianza kutangazwa saa sita mchana siku iliyofuata. Kura za urais zilikuwa zikiendelea kuhesabiwa. Siku ya tatu yake, saa kumi jioni, ndipo yalipofanyika majumuisho ya kura za urais.
Taifa zima la Kamisa lilikuwa na shauku ya kujua nani atakuwa rais wa Kamisa katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Kila mwananchi alikuwa kando ya redio yake akisikiliza matokeo yaliyokuwa yakitangazwa.
Shanga mwenyewe alikuwa akihaha. Wakati wote alikuwa amezungukwa na wapambe wake wakijadiliana hili na lile.
Ilipofika saa mbili usiku, ilitangazwa kuwa matokeo kamili ya kura za urais yatatangazwa kuanzia saa mbili asubuhi siku inayofuata.
Hakukuwa na kulala kwa upande wa vyama vyote. Mashabiki wa vyama walikesha usiku kucha kando ya ofisi za tume ya uchaguzi. Wagombea urais wote hawakulala usingizi kwa wasiwasi.
Kulipokucha asubuhi, matokeo ya kura za urais yaliendelea kutangazwa na ilipofika saa sita mchana, mwenyekiti wa tume ya uchaguzi alimtangaza mshindi wa urais.
Watu hawakuamini waliposikia Max Shanga akitangazwa kuwa mshindi wa urais. Matokeo ya kura yalionyesha kuwa alikuwa amewazidi wagombea wenzake kwa kura nyingi.
Kutangazwa kwa Shanga kuwa rais wa Kamisa kulisababisha shangwe na hoi hoi nchi nzima.
Siku moja baada ya kutangazwa kwa mshindi wa urais, Shanga aliapishwa kwenye kiwanja cha taifa kushika wadhifa huo. Kitendo hicho kilifanyika mbele ya halaiki ya wananchi. Baada ya kuapishwa, Shanga alipelekwa Ikulu moja kwa moja.
Siku ileile, Shanga alitangaza baraza lake la mawaziri ambapo alimteua Jacob Niwako kuwa waziri wake wa mambo ya ndani.
Kwa kile alichokieleza kuwa alitaka mawaziri hao waanze kazi mara moja, aliwaapisha mawaziri hao na manaibu waziri asubuhi ya siku iliyofuata na kukabidhiwa wizara zao.