Sitaki tena Urais – Sehemu ya 08
UTANGULIZI
Shanga alisita kidogo akawaza kabla ya kumjibu.
“Kuanza kampeni saa nane, tutatakiwa tuanze matayarisho tangu asubuhi.
“Ndiyo, itabidi muanze matayarisho asubuhi na hili jambo tulikubaliana kabla. Au umesahau?”
“Ninakumbuka. Ratiba yetu ilikuwa ni kuanza mkutano wetu saa kumi jionu lakini haidhuru tutabadili ratiba kesho asubuhi”
“Sawa”
“Na kuhusu mafunzo ya jioni kwa kesho sitaweza kufika kutokana na huo mkutano. Sitakuwa na muda saa kumi, isipokuwa nitahudhuria mafundisho ya usiku.”
SASA ENDELEA
“NI sawa, hakuna tatizo”
“Natumaini tumeelewana vizuri”
“Basi wewe rudi ukapumzike. Tulitaka kukukumbusha tu” Osaka akamwambia Shanga huku akimpa mkono wa kuagana.
“Asante”
Shanga akashuka kwenye gari na kuiacha Benz ikiondoka.
Siku iliyofuata Shanga aliagiza matayarisho ya mkutano wake yaanze asubuhi kwa vile alitaka kuanza mkutano saa nane mchana. Matangazo yakatolewa kuwa mkutano huo ungeanza saa nane mchana.
Kutoka saa mbili asubuhi wafuasi wa chama hicho walianza kushughulika hadi saa nane mchana, mkutano ukawa tayari.
Shanga aliwasili kwenye mkutano huo akiwaamefuatana na mke wake.
Mkutano huo wa pili wa chama hicho ulihudhuriwa na watu wengi japokuwa ulifanyika katika muda ambao haukutarajiwa.
Meneja wa Shanga alimnadi mgombea huyo wa urais kwa dakika kadhaa. Alimueleza kuwa ni mtu safi mwenye uwezo na aliyefaa kuwa rais wa Kamisa.
Shanga mwenyewe alipokaribishwa kwenye jukwaa aliendelea kumwaga sera za chama hicho na kueleza nini atafanya akiwa rais.
Mkutano huo ulimalizika saa kumi jioni. Shanga na mke wake wakarudi nyumbani.
**************
Maloto Shanga alikuwa kaka yake Max Shanga. Alikuwa akiishi katika eneo lilikuwa kando ya jiji hilo. Maloto alikuwa mstaafu wa jeshi la ulinzi aliyeishia kuwa mganga wa kienyeji.
Alistaafishwa jeshi baada ya taarifa zake kuonesha kuwa alikuwa na matatizo ambayo yalikuwa yanakosa ufumbuzi wa kisayansi.
Ilidaiwa kuwa Maloto akiwa mwanajeshi alikuwa akipandisha mashetani akidai kuwa hakuwa akitaka tena kazi ya jeshi na kwamba alitaka kuwa mganga wa kienyeji, kazi ambayo ilikuwa ikifanywa na marehemu bibi yake.
Mara kadhaa Maloto alitoroka katika kambi ya jeshi na kupatikana kando ya mto mmoja maarufu akiwa amejenga kibanda cha miti akiishi mahali hapo.
Matatizo ya Maloto yalipozidi alistaafishwa kwa vile alishakaribia umri wa kustaafu.
Lakini badala ya kwenda kuishi nyumbani kwake aliwaacha wanawe na kwenda kukaa katika kibanda alichkijenga kando yam to.
Aliishi hapo kwa miaka miwili. Kila mtu aliyemuona alihisi Maloto alikuwa amepatwa na wazimu. Baada ya miaka miwili Malot alirudi nyumbani kwake akiwa na mikoba ya uganga na gunia zima la miti shamba.
Ndipo alipoanza harakati za kutibu watu waliokuwa na magonjwa sugu yaliyoshindikana, watu waliokuwa na mapepo na waliodaiwa kurogwa.
Baada ya miaka michache tu sifa ya Maloto ikaenea katika sehemu kubwa ya jiji hilo na kuanza kupata umaarufu.
Siku ile ambayo Max Shanga alifanya mkutano wake wa pili wa kampeni, Maloto alimpigia simu Shanga. Ilikuwa saa kumi na moja jioni Shanga alipopokea simu ya Maloto.
“Habari ya siku kaka?” Shanga alimsalimia kaka yake.
“Tunashukuru tunaendelea vizuri. Naona kimya kimezidi ndugu yangu!”
“Ni kweli kaka, ni kwa sababu ya hii mikutano yetu ya kampeni. Nimebanwa sana”
“Mmeanza lii mikutan yenu?”
“Tulianza jana”
“Jana nilikuona kwenye TV usiku”
“Ndiyo hivyo, tunaendelea na leo”
“Una maana hivi sasa uko kwenye mkutano?”
“Hapana. Leo nimeshaanza mkutano saa nane mchana. Nimesharudi nyumbani”
“Sasa hebu jaribu kufika nyumbani kwangu hii leo tuangalie jinsi tutakavyoweza kusaidiana katika suala hilo”
“Ungependa nifike leo?”
“Ukifika leo ni bora zaidi”
“Sawa. Nitafika”
“Basi ninakusubiri”
“Kaka Maloto ametaka niende kwake” Shanga alimwambia mke wake mara tu alipomaliza kuzungumza na Maloto.
“”Ana habari gani?”
“Sijajua, ameniambia niende tuangalie jinsi tutakavyosaidiana katika hili suala”
“Suala gani?”
“Nafikiri anakusudia suala la huu uchaguzi”
“Mtasaidianaje?”
“Ndiyo ninakwenda kumsikiliza, labda anataka kunipa dawa niwazidi wagombea wenzangu”
Joyce akacheka.
“Shemeji anafurahisha kweli kweli. Nenda ukamsikilize”
Dakika chache kabla ya saa kumi na mbili kamili Shanga alilisimamisha gari alilokuwa akilitumia mke wake mbele ya nyumba ya Maloto katika mtaa mtulivu, nje kidogo ya jiji hilo.
Shanga alilazimika kutumia gari la mke wake ili asitambulike kwa vile alikuwa anakwenda kwa mganga aliyekuwa maarufu.
Aliona kama angefika hapo na gari lake ambalo lilikuwa limepambwa kwa picha zake za kampeni, wananchi wangeshuku kuwa alikuwa amekwenda kwa mganga kutengeza dawa ili ashinde urais.
Shuku hiyo ingemuharibia katika kampeni zake hasa itakapowafikia itawafikia wapinzani wake.
Aliamini kwamba wapinzani wake wangeitumia taarifa ya kuonekana kwake kwa mganga, kumchafulia jina kwamba alikuwa mtu mshirikina asiyejiamini.
Alipolisimamisha gari alishuka na kwenda kubisha mlango wa nyumba hiyo ambayo ingawa ilikuwa ya mganga wa kienyeji ilikuwa nzuri na ya kupendeza.
Wakati wa jioni nyumba hiyo ilionekana kuwa tulivu lakini wakati wa mchana inakuwa na pilikapilika nyingi za wateja wanaofika kwa mganga huyo kupata huduma mbalimbali.
Baada ya Shanga kubisha mlango, mlango huo ulifunguliwa na Maloto mwenyewe.
“Oh Max! Karibu ndani” Malto alimkaribisha Shanga huku akimpisha kwenye mlango.
Shanga aliingia ndani akatokea kwenye sebule pana iliyopambwa vizuri. Maloto akafunga mlango.
“Karibu ukae kwenye sofa”
Shanga likaa kwenye sofa na Maloto alikwenda kukaa karibu yake.
“Habari za nyumbani kwako?”
“Nzuri sana, sijui wewe”
“Hapa hatujambo, tumepoteana kwa muda”
“Ni kweli tulikuwa na maandalizi ya kampeni na sasa tumeanza mikutano ya kampeni. Muda wangu umekuwa mdogo sana”
“Samahani Shanga inabidi nikuulize, tangu umekuja nimepata mshituko kidogo na hata majini yangu yalinywea yalipokuona. Una kitu gani?”
Shanga akashituka.
“Sijakuelewa. Nina kitu gani kivipi?”
“Naona kama una kitu kikali kwenye mwili wako!”
“Kitu…?”
“Hebu nyoosha viganja vyako”
Shanga alinyoosha viganja vyake vya mikono. Ile pete alikuwa ameivaa.
Maloto alipoiona alishituka.
“Hii pete umeipata wapi?”
Shanga akanywea na kutabasamu.
“Kwanini kaka unaniuiza hivyo?”
“Hii pete ina nguvu sana. Si pete ya kawaida. Tangu umeingia nimeona nguvu yake”
“Mbona ni pete ya kawaida tu”
“Hapana, niambie ukweli”
“Nilipewa na rafiki yangu mmoja”
“Kwa ajili gani?”
Shanga alisita kujibu.
“Alikupa kwa ajili gani?” Maloto alirudia kumuuliza.
“Aliniambia ni pete ya ushindi” Shanga akamjibu.
“Ni pete ya ushindi kweli nakutabiria kuwa utashinda urais”
“Unaniambia kweli kaka?”
“Kweli kabisa. Nilikuita ili tuangalie jinsi nitakavyokusaidia katika uchaguzi huu. Lakini naona hutahitaji msaada tena”
Shanga hakusema lolote. Alibaki kumtazama Maloto huku akitingisha kichwa kidogo dogo.
“Unaweza kunitajia aliyekupa hiyo pete?”
“Ni mwanachama mmja wa chama chetu ambaye ni rafiki yangu”
“Natumaini ni mtaalamu”
“Sina hakika”
Maloto aliiangalia tena ile pete sasa akiwa ameushika mkono wa Shanga kisha akamwambia.
“Hapo utakapokuwa rais kuna kitu nitakueleza kuhusu pete hii”
“Nieleze sasa hivi kaka”
“Hapana. Kwa sasa nenda ukaendelee na kampeni zako”
Mke wa Maloto akatokea pale kwenye sebule.
“Shemeji umekuja saa ngapi?”
“Nimekuja punde tu. Habari yako?”
“Mie mzima shemeji. Unamuonaje mke mwenzangu?”
“Hajambo”
“Mnaendeleaje na mikutano yenu ya kampeni?”
“Tunaendelea vizuri”
“Sawa shemeji, mimi niko jikoni ninapika”
“Vizuri shemeji. Nikimaliza mazungumzo na kaka nitaondoka”
“Si usubiri chakula shemeji”
“Asante shemeji. Nitakujakula siku nyingine”
“Sawa shemeji, usisahau kunisalimia mama watoto”
“Salamu zako zimefika”
Mwanamke huyo alipoondoka Shanga hakukaa sana, alimuaga Maloto na kuondoka.
Siku zikapita. Kampeni zilizojaa ushindani kati ya chama tawala na vyama vya upinzani ziliendelea kurindima katika nci ya Kamisa.
Shanga baada ya kufanya kampeni katika jiji la Maloto kwa wiki moja alianza safari za mikoani. Mkoa mmoja baada ya mwingine.
Huko kote alilakiwa na umati mkubwa wa watu. Mikutano yake pia ilihudhuriwa na watu wengi ambao walimuahidi kumpa kura katika mikoa yote aliyokwenda.