Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sitaki tena Urais – Sehemu ya 04

RAIS 04 Pict

UTANGULIZI

Kulikuwa na mlango mwingine wa kuingilia ndani. Osaka aliufuata mlango huo akaufungua. Shanga alikuwa ameshanyanyuka na kumfuata. Lisha na Bosco walibaki pale pale kwenye sofa.

SASA ENDELEA


SHANGA alimfuata Osaka ndani ya chumba hicho. Walitokea katika ukumbi mrefu uliokuwa na milango sita ya vyumba, mitatu kila upande.

Huku akitembea kwa hatua ndefu na madhubuti Osaka alimuongoza Shanga kuelekea mlango wa tatu wa upande wa kushoto. Alibonyeza tarakimu kwenye kifaa kilichokuwa pembeni mwa mlango. Mlango ukafunguka.

Osaka akamtazama Shanga.

“Karibu ndani,”  alimwambia.

Shanga aliingia kabla ya Osaka. Alisimama kando ya mlango na kukitazama chumba walichoingia. Kilikuwa chumba cha ofisi. Kilikuwa na meza moja, kiti kimja nyuma ya meza na viti viwili mbele ya meza. Juu ya meza kulikuwa na simu na majalada kadhaa. Upande wa kushoto wa meza kulikuwa na kabati na upande wa kulia kulikuwa na ukuta wa kioo cheusi.

Osaka alikwenda kuketi kwenye kiti kilichokuwa nyuma ya meza.

“Karibu kiti,” alimkaribisha Shanga kwenye kiti.

Wakati Shanga anaketi Osaka aliinua mkono wa simu na kubonyeza tarakimu kadhaa kabla ya kusema.

“Mkuu, mgeni wetu yuko tayari kuzungumza na wewe.”

Alisikiliza kidogo kisha akaurudisha mkono wa simu. Ghafla ule ukuta wa kioo ulitoa mwanga wa rangi ya bluu halafu ukaunda taswira ya kivuli cha mtu aliyekuwa ameketi kwenye kiti huku mguu mmoja ameuweka juu ya mwingine. Alikuwa na mwili mnene, kichwa kikubwa chenye nywele ndefu na uso mpana.

Mkono wake mmoja uliinuka  ukaonesha alama za vidole za freemaso. Osaka naye alionesha alama kama hizo. Wakati huo Shanga alikuwa akikitazama kivuli na huku akimtazama Osaka.

“Karibu sana mgeni wetu” Sauti nzito ilisikika ikitokea kwenye kioo hicho.

“Asante sana,” Shanga alijibu huku akionesha wazi kupata hofu. Hakuweza kujua iwapo mtu yule alikuwa nyuma ya kioo akimulikwa na mwanga wa taa au alikuwa sehemu nyingine ambako kivuli chake kilikuwa kinachukuliwa na kamera.

“Bwana  Shanga utakuwa rais wetu wa jamhuri hii bila wasiwasi wowote. Tutakuwa bega kwa bega na wewe hadi unaingia ikulu,” Sauti nzito iliendelea kumwambia kutoka kwenye kioo.

“Hakikisha wakati wote wa kampeni unavaa suti nyeusi na ni lazima uvae kitu chochote cha rangi nyekundu kama vile kiatu tai au soksi.

“Anza mikutano yako siku ya jumanne au jumamosi. Katika siku hizo mikutano yako ianze saa nane au saa mbili asubuhi. Natumaini umenielewa

“Nimekuelewa,” Shanga alijibu na kuuliza.

“Katika siku nyingine mbali ya jumatano na jumamosi, naweza kuanza mikutano wakati wowote?”

“Katika siku nyingine unaweza kuanza mikutano wakati wowote lakini siku zako za bahati ni hizo mbili. Utaanza kampeni katika moja ya siku hizo na utafunga kampeni katika moja ya siku hizo. Kadhalika utaapishwa katika moja ya siku hizo na utaingia ikulu katika moja ya siku hizo”

“Kwa upande wa mavazi umesema nivae suti nyeusi na kitu chochote cha rangi nyekundu, je mavazi hayo nitayatumia kwenye mikutano tu au katika kipindi chote cha kampeni?” Shanga akauliza.

“Ni vizuri uyatumie katika kipindi chote cha kampeni”

“Sawa”

“Sasa jaza fomu huku mimi nikishuhudia”

Osaka akachomoa fomu moja kwenye jalada na kumsogezea Shanga pamoja na kalamu.

“Isome halafu uijaze”

Shanga aliichukua fomu hiyo na kuisma. Miongoni mwa maswali yaliyotakiwa kujazwa ni majina matatu ya anayeomba uanachama. Jinsia yake. Umri wake na anuani yake.

Mengine ni kazi yake. Kama ameshaoa au kuolewa. Na kama ameshaoa au kuolewa jina la mke wake au mume wake. Kadhalika muomba uanachama alitakiwa kujaza kama alikuwa na watoto, idadi yao, jinsia zao na majina yao.

Taarifa zingine zilizotakiwa kujazwa kwenye fomu hiyo ni pamoja na kutaja mahali ambapo muhusika anaishi, majina manne ya majirani zake na majina manne ya marafiki zake wa karibu.

Shanga baada ya kuisoma fomu hiyo alihisi kupatwa na wasiwasi lakini hakuweza kujua wasiwasi huo ulitokana na nini. Akainua kichwa chake na kumtazama Osaka.

“Naweza kwenda kuijazia nyumbani na kesho nikairudisha?” alimuuliza.

“Hapana, fomu hiyo inajazwa hapa hapa. Hairuhusiwi kutoka nje!” Osaka alimwambia akiwa amemkazia macho.

“Hakuna tatizo lolote kujaza hapa hapa. Hizi ndio taratibu zetu. Ondoa wasiwasi na kuwa na amani” Sauti iliyotoka kwenye kivli cha mtu kilichokuwa kwenye kioo ilimwambia.

Shanga akachukua kalamu na kuanza kujaza kipengele kimoja baada ya kingine.

Kwenye kipengele kilichohusu watoto aliozaa aliandika alikuwa na mtoto mmoja mwanamke. Aliyekuwa anaitwa Tina. Ukweli ni kwamba alikuwa na watoto watatu, wawili wanawake waliokuwa na majina ya Tina na Ida na mmoja mwanaume aliyeitwa William. Wote hao walikuwa wakisoma nje ya nchi.

Mahali hapo aliamua kuficha ukweli.

Alipomaliza kujaza fomu hiyo aliweka sahihi kisha akamrudishia Osaka. Osaka aliipokea akaisoma na kisha kuiwekea sahihi kabla ya kuiweka kwenye faili.

“SIsi hatutoi jibu kwa mtu kukubaliwa uanachama. Unapojaza fomu yetu na ukaipokea, maana yake tayari wewe ni mwanachama wetu,” Osaka alimwambia Shanga.

“Sawa”

“Sasa kuna hatua moja muhimu iliyobaki ili uanachama wako ukamilike. Hebu njoo hapa”

Osaka alinyanyuka kwenye kiti na kwenda kwenye ukuta karibu na kabati. Mahali hapo palikuwa na lenzi iliyotokeza kwenye ukuta.

“Simama mbele ya hii lenzi,” Osaka akamwambia Shanga aliyekuwa amesimama nyuma yake.

Wakati Shanga anasimama mbele ya lenzi hiyo alisikia sauti iliyotokeza mahali hapo hapo ikimwambia.

“Inua kichwa chako kidogo”

Shanga akainua kichwa chake kidogo.

“Sasa tayari,” Sauti ilimwambia tena.

“Unaweza kuondoka” Osaka akamwambia Shanga.

Shanga alipogeuka hakukiona tena kile kivuli cha mtu kilichokuwa kwenye kioo ingawa kioo hicho kiliendelea kutoa mwanga.

“Sasa tutakwenda sehemu nyingine ya kukutambulisha kwa wanachama.wenzako,” Osaka akamwambia Shanga kabla ya kutoka naye. Hawakutumia tena njia ile waliyokwendea. Walipotoka kwenye chumba hicho walitumia mlango mwingine uliowafikisha kwenye ngazi. Walishuka chini ambako waliendelea kushuka kwenye ngazi ya chini kwa chini.

Shanga alishangaa kuona mahali walikokuwa wakielekea kulikuwa na mwanga hafifu. Walifika chini na kutokea katika ukumbi mpana. Upande mmoja wa ukumbi huo ulikuwa umepangwa safu za viti huku kukiwa na watu wachache waliokuwa wameketi wakizungumza.

Mbele ya viti hivyo kuliwekwa meza ndefu iliyotandikwa kitambaa chekundu. Juu ya meza kulikuwa na mitungi mitatu iliyochorwa picha za majoka na uso kama wa mbuzi mwenye pembe za kutisha. Mitungi hiyo ilikuwa ikifuka moshi kama vile ilikuwa na makaa ya moto yaliyotiwa buhuri (vitu ambavyo hufukishwa na waganga wa kienyeji}

Upande wa pili wa meza kulikuwa na ukuta wa kioo kama ule uliokuwa katika chumba cha kwanza. Kioo hicho kilionesha picha ya alama ya freemaso na picha zingine ambazo Shanga hakuweza kuzielewa.

“Twende kule kwa wenzetu,” Osaka alimwambia Shanga.

Wakatembea hadi sehemu iliyokuwa na viti.

“Jamani tuna mwanachama mpya, nataka kuwatambulisha” Osaka akawambia watu hao.

“Ndiyo mkuu,” Sauti ikasikika kutoka kwa watu hao.

“Huyu ni Max Shanga, ni mwanasiasa na ni mgombea urais kupitia chama cha UM” Osaka aliendelea kuwambia.

“Sasa mje mmoja mmoja msalimiane naye”

Mtu mmoja mmoja aliondoka kwenye kiti na kwenda kumpa mkono Shanga. Kila aliyekwenda kwa Shanga alijitambulisha mwenyewe.

Mtu wa tatu kwenda kumpa mkono alikuwa ni yule mfadhili mkuu wa chama cha UM, Jacob Niwako. Pia aliwaona watu ambao alikuwa akiwafahamu lakini hakuwa akijua kama walikuwa freemaso. Baadhi ya watu hao walikuwa ni wanamichezo, wanamiziki na watu wa kada zingine. Hapo ndipo Shanga alipogundua kuwa freemaso ilikuwa jumuia kubwa iliyohusisha watu wa kada mbalimbali.

Baada ya watu wote kumalizika hawakurudi tena kukaa wenye viti. Watu watatu walitokea wakiwa na vyano vilivyokuwa na glasi za vinywaji. Wakawa wanavipitisha kwa kila mtu. Kila mtu alichukua glasi na kugonganishana na mwenzake kabla kunywa. Shanga naye alichukua glasi yake na kuigonganisha na glasi ya Osaka. Aliipeleka midomoni akiwa hajui kilikuwa kinywaji gani.

Hata baada ya kukionja kinywaji hicho hakuweza kutambua kilikuwa kinywaji gani na hakuweza kumuuliza yeyote.

Kilikuwa kinywaji chenye kakasi. Hakikuwa kitamu na pia hakikuwa kichungu lakini kilikuwa baridi kinachoburudisha.

Wakati wanakunywa kila mmoja alionesha dhamiri ya kuongea na Shanga.

Karibu watu wote walimkaribisha Shanga na kumpa matumaini. Wengine walimpongeza kwa uamuzi wake wa kujiunga nao.

Walimwambia kwamba wanahitaji kuwa na rais wa nchi atakayetambua harakati zao.

Osaka akamwambia Shanga kuwa watu hao aliowakuta hapo ndio nguzo za freemaso ncini mwao na hukutana kila siku usiku na kujadili mambo mbalimbali ya kifreemaso.

“Wako wengine wengi tu, unaweza kukutana nao muda mwingine”Osaka aliendelea kumwambia.

“Lakini kuna kitu kimoja, zingatia sana ushirikiano na wenzako. Sisi ni wajenzi huru. Ushirikiano wetu ndio utakaotuwezesha kuijenga dunia hii.”