Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mauaji ya kutisha – Sehemu ya 9

HADITHI 9 Pict

UTANGULIZI

“Sasa hebu tuambie kwa kadiri ulivyofikiria hao watu walijificha kwa wapi wakati marehemu akiwasikia wakiwa nyuma ya nyumba?”

“Kwa kweli sijagundua hadi sasa.”

“Unadhani nani atatueleza wakati wewe ndiye uliyekuwa pamoja na marehemu?”

SASA ENDELEA...



“Ni kweli….”

“Ni kweli nini?”

Mlinzi akanyamaza tena.

“Umemuarifu baba yake?”

“Sina namba yake.”

“Kwa hiyo huko kwa wazazi wake hakuna taarifa yoyote?”

“Hakuna taarifa.”

Hapo hapo Inspekta Amour akatoa simu yake na kumpigia mzee Almasi.

“Mzee Almasi unazungumza na Inspekta Amour hapa.” Amour alimwambia mtu huyo baada ya kupokea simu yake.

“Ndiyo inspekta. Kuna habari  gani?”

“Kuna tukio  limetokea hapa kwa mwanao James”

“Tukio  gani?”

“Hebu fika kwanza.”

“Ni tukio la heri ama la shari?”

“Hatupendi kukueleza kilichotokea. Tunaomba ufike wewe mwenyewe.”

“James mwenyewe yuko wapi?”

“James ndiye aliyefikwa na matatizo mzee, hutaweza kuzungumza naye. Wewe njoo tu.”

Almasi aliguna kabla ya kusema.

“Sawa, nakuja.”

Mke wake alikuwa ameshaamka.

“Ninaitwa nyumbani kwa James. Nimeambiwa kuna matatizo  yaliyotokea,” akamwambia mke wake.

“Matatizo gani tena?”

“Hawakuniambia.”

“Ni  nani aliyekupigia simu?’

“Ni Inspekta wa Polisi, yule alliyekuwa akishughulikia uchunguzi wa mauaji ya Martin.”

“Yaani polisi wameshafika hapo nyumbani kwake?”

“Inaonekana ni tukio kubwa. Hawakutaka kuniambia kwa sababu wameona watanitia wasiwasi.”

“Hebu mpigie James mwenyewe umuulize.”

Almasi akachukua simu yake na kumpigia James. Simu ya James iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa. Inspekta Amour na wenzake waliisikia ikiita chumbani kwa James.

“Simu haipokelewi.” Almasi akamwambia mke wake.

“Sasa nenda ukajue kumetokea nini.”

Zilimchukua Almasi kama dakika ishirini hivi kuwa barabarani. Kwa vile barabara zilikuwa karibu tupu, aliliendesha gari kwa mwendo wa kasi huku akionesha wazi kujaa wasiwasi.

Alipofika  nyumbani kwa James alilikuta geti likiwa wazi akaingiza gari. Alilisimamisha nyuma ya magari mawili ya polisi akalizima  na kushuka haraka.

Inspekta Amour ndiye aliyekwenda kumlaki kando ya gari..

“Shikamoo mzee?”

“Marahaba. Mmenitia wasiwasi sana. Kuna nini?”

“Hebu njoo hapa.”

Amour alisogea mahali ambapo mwili wa James ulichinjwa. Mahali hapo palisambaa damu iliyoganda.

Almasi alipoiona ile damu alishituka.

“Pametokea nini, mbona kuna damu?” Almasi akauliza kwa mshituko.

“Kuna mauaji yametokea.” Amour alimjibu.

“Mauaji ya nani?”

“Mauaji ya mwanao James.”

“James ameuawa?”

“Ameuawa…” Amour alimwambia na kuendelea kumueleza mkasa mzima ulivyotokea kama alivyoelezwa huko kituo cha polisi.

Maelezo hayo yakamshitua Almasi.

“Umeniambia inaaminika kuwa watu waliomuua James ndio wale wale waliomuua Martin?”

“Kwa mujibu wa maelezo tuliyoyapata kutoka kwa mlinzi wa mwanao, tunaamini kwamba wauaji ni watu walewale, walikuja kwa namna ile ile na kwa mavazi yale yale.”

“Mmojawapo shingo yake ilikuwa kama iliyochinjwa kwani kichwa chake kilikuwa kinaning’inia.” Mlinzi akaeleza bila kuulizwa.

“Sasa hao watu ni kina nani. Polisi hamjanieleza kitu. Mnaona sasa wanaendelea kuua wanangu? Sababu yake ni nini?”

“Wameiba masanduku matatu.” Mlinzi aliendelea kutoa maelezo.

“Masanduku ya nini?”

“Labda wewe ndiye utakayetueleza kama unafahamu yalikuwa masanduku ya nini?” Amour akamwambia Almasi.

“Hebu tuingie ndani.”

Wakaingia ndani.

“Tumeambiwa na mlinzi kwamba humu ndani hamkuwa na mtu mwingine aliyekuwa anaishi ni kweli?”  Amour  akamuuliza Almasi.

“James alikuwa akiishi peke yake lakini alikuwa katika maandalizi ya kuoa wiki ijayo.” Almasi alimjibu. Waliingia katika  chumba cha James. Almasi akakikagua kisha akamtazama mlinzi.

“Umesema umeona wakitoka  na masanduku matatu?”

“Ndiyo. Walitoka na masanduku matatu.”

“Nafikiri yalikuwa na vitu ambavyo James alivinunua kwa ajili ya harusi yake.”

“Kama vitu gani?” Amour akamuuliza.

“Sina  hakika lakini nafikiri ni dhahabu za mke wake pamoja  na nguo na vitu  vingine.”

“Vinaweza kuwa na thamani gani?’

Almasi akabetua mabega yake.

“Siwezi kujua kwa sababu alikwenda kuvinunua mwenyewe lakini vitakuwa ni vitu vya pesa nyingi.”

“Tuseme hao majambazi walikuwa wanavihitaji vitu hivyo?” Amour akauliza kama aliyekuwa anajiuliza mwenyewe.

Badala ya kujibu Almasi alitikisa kichwa kusikitika kisha alisema.

“Kwa kweli nimepata pigo kubwa. James ndiye niliyekuwa nikimtegemea baada ya kuuawa Martin, masikini na yeye ameshanitoka!”

Alitoa kitambaa akajifuta machozi huku akijisemea.

“Sijui nitamueleza nini mama yake?”

“Ninakuhakikishia mzee Almasi kuwa tutawatafuta na tutawakamata.” Amour akamwambia huku akimshika bega.

“Ni lazima mniambie ni kwanini hawa watu wameniamdama?” Almasi alisema kwa hamaki. Sasa macho yake yakiwa mekundu.

“Ni majambazi tu. Jambazi anaweza kumuandama mtu yeyote tu. Lakini kama nilivyokwambia tutawakamata.”

Almasi alijifuta tena machozi kwa kitambaa. Alipokirudisha mfukoni Amour alimwambia.

“Hebu fungua kabati tuoine kama kuna chochote kilichoibiwa.”

Funguo ya kabati ilikuwa kwenye kitasa cha kabati. Almasi alipeleka mkono wake akalifungua kabati hilo.

Kila mtu alikodoa macho ndani ya kabati hilo kuona kilichokuwemo. Kulikuwa na safu za nguo zilizopangwa upande wa kulia na wa kushoto yakiwemo mashati, fulana na suruali.

Almasi alifungua vishubaka vilivyokuwa ndani ya kabati na kutoa burungutu la noti nyekundu.

“Kuna pesa,” akasema na kuziweka kwenye kitanda. Baada ya kuzihesabu alisema.

“Ni shilingi milioni tano.”

“Tuseme hawa majambazi hawakuziona pesa hizi?” Mkuu wa kituo akauliza.

“Nadhani hata hili kabati hawakulifungua. Kama wangelifungua tungelikuta wazi.” Amour alimwambia.

“Kwa hiyo walitaka yale masanduku, mlikuwa na nini cha zaidi?” Mkuu wa kituo akaendelea kuuliza.

“Ni mapema mno kujua kila kitu lakini naamini uchunguzi utabainisha kila kitu.” Amour alimwambia.

Almasi alizitia zile pesa mfukoni mwake.

“Sijisikii vyema mpaka niuone mwili wa mwanangu,” akasema.

“Tunaweza kwenda hospitali kuuangalia.” Amour alimwambia.

“Nataka kwenda kuuona ili nijiridhishe kuwa mwanangu ameuawa.”

“Sawa.”

Dakika chache baadaye Inspekta Amour na makachero wenzake walikuwa wamefuatana na gari la Almasi kuelekea hospitali ya Muhimbili.

Mlinzi wa nyumba ya James alikuwa amerudishwa kituo cha polisi na nyumba ya James ilikuwa inalindwa na polisi.

Walipofika hospitali ya Muhimbili, Almasi alioneshwa mwili wa james uliokuwa umewekwa mochwari. Wakati anautazama Almasi alisali akaweka alama ya msalaba kwenye mabega na paji la uso wake kisha alianza kulia kimya kimya.

Inspekta Amour na makachero wenzake walifanya kazi  ya ziada kumyamazisha. Hapo hapo simu ya Almasi ikaita mfukoni mwake.

Alipoitoa mfukoni aligundua kuwa aliyekuwa akimpigia alikuwa mke wake.

“Mbona kimya. Umeshafika huko nyumbani kwa James?” Mke wake akamuuliza.

“Nimeshafika, hivi sasa niko hospitali.”

“Kumetokea nini?”

“Ni matatizo matupu. Nitakuja kukueleza nyumbani.”

“Lakini mwanangu yuko salama. Mbona sauti yako imekuwa nzito?”

“Mke wangu nitakuja kukueleza huko huko. Ninakuja sasa hivi.”

Almasi akakata yeye simu.

“Sasa mzee wewe rudi nyumbani, kesho asubuhi ufike makao ya polisi tuonane.” Amour alimwambia Almasi.

Almasi alipoondoka, Amour aliwambia wenzake.

“Huu si ujambazi wa kawaida, ni lazima tutafute kiini cha mauaji haya.”

Wakati anarudi nyumbani, Almasi aliendesha gari huku akiomboleza. Alijiona wazi kuwa hakuwa makini kwenye sukani. Laiti ungekuwa mchana angegonga au angegongwa yeye. Lakini alishukuru usiku huo hakukuwa na magari mengi yaliyokuwa yakipita barabarani.

Alipofika nyumbani kwake alimwambia mke wake.

“Mke wangu naomba ujikaze nikupe taarifa za mwanao James.”

“Niambie tu mume wanngu.”

“James hatuko naye.”

Mke wake akagutuka.

“Unasemaje mume wangu?”

“James ameuawa…amechinjwa kama alivyochinjwa kaka yake Martin!”

“Yesu wangu! Mwanangu amefanya kosa gani?”

“Polisi waliponipigia simu walinificha, hawakuniambia kilichokuwa kimetokea. Wakati unanipigia simu nilikuwa Muhimbili, nimeushuhudia mwenyewe mwili wa James.”

“Ni nani aliyemfanyia hivyo  mwanangu?”

“Ni tukio kama lile lililotokea kwa kaka yake. Inasadikiwa wauaji ni wale wale na walivaa nguo zile zile. Baada ya kumuua waliiba masanduku matatu na kutoweka.”

“Mlinzi wake hakuwepo?”

“Alikuwepo ndiye aliyetoa maelezo lakini malezo yake hayaeleweki.”

“Amesemaje?”

Almasi alimueleza mke wake mkasa mzima uliotokea bila kumficha lolote. Mke wa Almasi aliangua kilio kikali.

Huku majonzi na huzuni vikiwa vimetawala kwenye nyumba ya Almasi, Almasi aliwapigia simu watoto wake wote. Aliwaamsha usingizini na kuwambia wafike nyumbani kwake haraka.