Mauaji ya kutisha – Sehemu ya 7
UTANGULIZI
“Umeshajitokeza kwa wazazi wake?” Mama Almasi akauliza.
“Nimeanza kumleta huku kwetu kwanza atambulike kisha atanifikisha kwao.”
“Basi ufanye hivyo haraka ili tuweze kuendelea na taratibu nyingine.”
“Umenipa maelezo ya busara mama yangu. Kitu cha msinngi ninachokitaka kwenu mnieleze je mmemkubali mchumba wangu?”
SASA ENDELEA...
“Sijui baba yako lakini mimi nimemkubali.”
“Baba unasemaje?”
“Sipendi kusengenya katika hilo, umeniuliza mbele yake na nitakujibu mbele yake. Jibu langu ni kuwa kama nyinyi wenyewe mmekubaliana kuwa mke na mume, mimi siingilii hapo. Mimi ninachosema ni kuwa ninawaombea Mungu.”
Nyuso za james na Grace zikachanua tabasamu wakati Almasi na mke wake waliangua kicheko cha furaha.
Siku ya pili yake, James akafikishwa kwa wazazi wa Grace. Huko nako walipata baraka kutoka kwa wazazi wa Grace.
Siku chache baadaye James akamvisha Grace pete ya uchumba. Taratibu zikaendelea kufanyika hadi ikafikia hatua ya ndoa.
Zilikuwa zimebaki siku saba tu James akamilishe mpango wake wakuoana na Grace. Kulikuwa na kitu kingine kilitokea.
Siku hiyo James alikuwa na Grace hadi saa tatu usiku alipomrudisha nyumbani kwao Oysterbay. Grace aliyekuwa amekaa katika siti ya mbele kando ya James alifungua mlango wa gari kisha akamtazama James.
“Baby ninashuka.”
“Shuka kwa amani baby wangu.”
Grace alishuka kwenye gari kisha akazunguka upande wa dereva akaupleka uso wake kwenye uso wa Jamea kisha akambusu.
“Mmwaaa…!”
James naye akambusu.
“Mmwaaa…!”
“Bye bye…”
“Bye…”
Grace akageuka na kuelekea kwenye geti la nyumbani kwao. Akabisha kwenye geti huku akiita.
“Eliza! Eliza….njoo unifungulie.”
Sekunde chache baadaye geti lilifunguliwa. Grace akageuza uso na kumtazama James aliyekuwa akisubiri Grace afunguliwe geti. James akaliondoa gari.
Aliendesha kwa taratibu huku akijisifu kimoyomoyo kumchagua Grace kuwa mwenza wake wa maisha. Alijiambia hakika hakufanya kosa kumchagua msichana huyo mrembo ambaye tangu alipoanza kusuhubiana naye alimgundua alikuwa msichana mwenye sifa zote ambazo mwanaume anazihitaji kwa mke wake.
Si tu alikuwa na ushauri wa busara, alikuwa na hekima, mjanja na mwenye upeo wa kutosha wa kuyaelewa maisha.
Aliiwazia harusi yake ambayo ingefanyika baada ya wiki moja. Akajiambia kutokana na maandalizi yake itakuwa harusi itakayofana sana.
Walikuwa wametenga kiasi cha shilingi milioni tisini kwa ajili ya harusi hiyo ya kitajiri japokuwa mke wake alitoka katika familia ya kawaida.
James alipofika nyumbani kwake aliliingiza gari kwenye geti akaliegesha kwenye banda na kushuka.
Dakika chache baadaye alikuwa bafuni akioga. Alipomaliza alitoka bafuni. Aliona hakuwa na jingine lolote la kufanya zaidi ya kupanda kitandani na kulala kwani alihitajika kuamka asubuhi na mapema kwenda kazini kwa ajili ya kushughulikia mishahara ya wafanyakazi wa kampuni yao. Kilikuwa ni kipindi cha mwisho wa mwezi.
Alipojitupa tu kitandani, usingizi ukampitia.
Wakati akiwa usingizini alisikia kama kuna sauti za watu zilizomuita jina lake na kumuamsha. Akafumbua macho na kuwasha taa. Ndani ya nyumba ile alikuwa akikaa peke yake. Zaidi yake alikuwa ni mlinzi wa nyumba yake ambaye hukaa kwenye geti.
Akajiuliza ni sauti za kina nani alizozisikia zikimuita. Aliuhisi moyo wake ukianza kupata hofu. Akashuka kitandani na kwenda kufungua kabati akaingiza mkono na kutoa bastola yake ambayo wakati wote ilikuwa na risasi ndani.
Akafungua mlango wa chumbani na kutoka ukumbini. Akiwa ukumbini alisikia kama hatua za watu waliokuwa wakitembea nyuma ya nyumba yake. Alikwenda sebuleni akapenua pazia na kumchungulia mlinzi wake, akamuona amekaa barazani macho yake yakitazama kwenye geti.
James akafungua mlango na kutoka uani.
“Vipi umelala?” Akamuuliza mlinzi huyo aliyeshituka kumuona Jemes amefungua mlango.
“Niko macho. Kuna shida gani?”
“Nimesikia kama hatua za watu nyuma ya nyumba, hebu zunguka uangalie.”
Mlinzi akainuka haraka. Aliishika sime yake vizuri kisha akapiga hatua kuelekea kwenye kona moja ya jumba hilo la kifahari. Wakati mlinzi anapotea katika kona hiyo ya nyumba, watu watatu wa ajabu wakatokea katika kona nyingine.
Jinsi James alivyoshituka kuwaona watu hao, ile bastola aliyokuwa ameshika ilimponyoka ikaanguka chini.
Mara moja aliwaona watu hao watatu wameshamfikia mahali alipokuwa amesimama.
Miongoni mwa watu hao watatu, aliyekuwa amesimama katikati ya wenzake alikuwa amevaa mavazi meusi. Wenzake walivaa mavazi meupe.
Yule wa katikati shingo yake ilikuwa imechinjwa. Na kichwa chake kilikuwa kikining’inia kama vile kilitaka kuanguka.
Mtu huyo ndiye aliyemsemesha James.
“Wewe ni mtoto wa Almasi?”
“Ndiye mimi” James alimjibu huku akitetemeka.
“Baba yako alikuweka kama dhamana lakini umeshindwa kutiimiza masharti ya dhamana yako!”
“Dhamana gani, sijawekwa kama dhamana mahali popote!”
“Una hakika?”
“Kwani nyinyi ni akina nani?”
“Muda umekwenda sana, huwezi kupata jibu kwa sasa.”
Mtu huyo akatoa panga na kulishika vyema. James akakurupuka. Alikumbuka hata kaka yake aliyefariki dunia aliulizwa hivyo hivyo na watu waliomuua.
Licha ya kukurupuka alijikuta akiishia mikononi mwa wale watu wawili waliovaa mavazi meupe.
Yule mtu aliyetoa upanga akamchinja James kama kuku. James alikoroma kama mbuzi aliyekuwa anachinjwa. Sekunde chache tu baadaye mwili wake ulianguka chini.
Mlinzi aliyekuwa akiizunguka ile nyumba alishazisikia zile sauti, akawa anarudi mbio ili kujua walikuwa ni kina nani waliokuwa wakizungumza na bosi wake. Alipofika aliwakuta watu hao wakimalizikia kutoka kwenye geti wakiwa wameshika masanduku huku mwili wa James uliochinjwa ukiwa chini.
Mlinzi huyo alishituka hasa alipouona mwili wa bosi wake umelala chini ukiwa umechinjwa. Alichokiwaza ni kuwa watu aliowaona wakimalizia kutoka walikuwa majambazi ambao waliingia humo ndani wakamchinja bosi wake aliyekuwa ametoka hapo nje kisha wakaingia chumbani mwake na kuiba masanduku alioyaona wakitoka nayo.
Lakini yale mavazi ya watu hao yalimsababishia mshangao mwingine. Hakuwahi kuona majambazi waliokuwa wamevaa mavazi ya aina ile.
Kwa vile kwenye geti hilo taa ilikuwa inawaka alikiona kichwa cha mmojawao aliyekuwa amevaa mavazi meusi kikining’inia kutokana na kuchinjwa kwenye koo.
Akiwa katika mastaajabu, mlinzi huyo alikwenda kuitazama maiti ya bosi wake ambayo ilikuwa bado ikivuja damu kisha akakimbilia kwenye geti ambalo sasa lilikuwa wazi baada ya watu hao kutoka. Alichungulia nje lakini hakuona mtu yeyote.
Akajiuliza watu hao walitoweka vipi kwani tangu walipotoka katika geti hilo hazikupita hata sekunde kumi na tano. Kwa sekunde hizo alipaswa awaone watu hao wakiendelea kutokomea.
Kama wangekuwa na gari, mlinzi alijiambia, angeusikia muungurumo wa gari hilo wakati linaondoka lakini hakusikia muungurumo wowote.
Mlinzi huyo alisali kimoyo moyo akajifanyia ishara ya msalaba kwenye uso na mabega yake kabla ya kurudi tena mahali ulipolala mwili wa James.
Alichutama na kuutazama kwa makini mwili huo. Kutokana na uchunguzi wa macho yake, mlinzi huyo aligundua kuwa James alikuwa amechinjwa.
Akiwa bado amechutama mahali hapo mlinzi huyo alijiuliza, watu hao waliingia kwa wapi kwani wakati bosi wake anatoka na kumtaka aizunguke nyumba, geti lilikuwa limefungwa kwa ndani.
Alipokuwa nyuma ya nyumba ndipo aliposikia sauti za watu, akarudi mbio na kuwakuta watu hao wakimalizia kutoka wakiwa wamebeba masanduku.
Watu hao waliingiaje humo nadani? Akajiuliza. Akaendelea kujiuliza, wakati bosi wake anatoka na kumwambia amesikia sauti za watu, watu hao walikuwa wapi?
Baada ya kukosa majibu,aliinuka akaingia ndani ya ile nyumba kufanya uchunguzi. Mlango wa chumba cha James ulikuwa umeachwa wazi. Mlinzi huyo alichungulia ndani ya chumba hicho kisha akatoa kichwa chake na kurudi ulipokuwa umelala mwili wa James.
Sijui wameiba nini na nini? Akajisemea peke yake.
Sasa nifanye nini? Akajiuliza.
Akajiambia ni lazima apige simu polisi. Alikuwa ameshatia mkono mfukoni kuitoa simu yake, aliposita.
Alijiuliza polisi hao watakapofika atawaeleza nini?
Alijiambia ni muhimu apange maelezo yake kwa usahihi vinginevyo ni yeye atakayewekwa ndani kutokana na tukio hilo lililohusisha mauaji.
Akaanza kupanga maelezo ya kuwambia poolisi. Alijiambia awambie polisi kuwa majambazi hao waliruka ukuta upande wa nyuma wa nyumba hiyo ambapo bosi wake aliwasikia.
Baada ya bosi wake kuwasikia alitoka na kumuarifu kuwa alisikia sauti za watu nyuma ya nyumba.
Mlinzi huyo aliendelea kupanga maelezo yake kwamba alizunguka nyuma ya nyumba lakini tayari majambazi hao walikuwa wameshajificha sehemu ambapo baada ya yeye kuzunguka nyumba, majambazi hao walijitokeza na kumchinja bosi wake kisha waliingia ndani na kuiba masanduku.
Aliendelea kujiambia kuwa atawaeleza polisi kuwa baada ya kuznguka nyumba na kutowaona watu hao alikuja kumkuta bosi wake ameshachinjwa na pia aliwaona watu watatu waliokuwa wameshika masanduku wakimalizia kutoka kwenye geti.
Mlinzi huyo alijiambia kama polisi hao watamuuliza iwapo aliwafuatilia majambazi hao, atawambia kuwa aliwafuatilia lakini hakuwaona.