Mauaji ya kutisha – Sehemu ya 8
UTANGULIZI
Aliendelea kujiambia kuwa atawaeleza polisi kuwa baada ya kuznguka nyumba na kutowaona watu hao alikuja kumkuta bosi wake ameshachinjwa na pia aliwaona watu watatu waliokuwa wameshika masanduku wakimalizia kutoka kwenye geti.
Mlinzi huyo alijiambia kama polisi hao watamuuliza iwapo aliwafuatilia majambazi hao, atawambia kuwa aliwafuatilia lakini hakuwaona.
SASA ENDELEA...
Aliporidhika na maelezo aliyoyapanga ndipo alipotoa simu yake na kuwapigia polisi.
Nusu saa tu baadaye gari la polisi likasimama nje ya nyumba ya James. Polisi sita waliokuwa na bunduki walishuka kwenye gari ambapo mlinzi huyo aliyekuwa akiwasubiri aliwakaribisha ndani.
“Wewe ndiye mlinzi uliyetupigia simu?” Polisi mmoja aliyeonekana kuwa na cheo cha usajenti alimuuliza mlinzi huyo.
“Ndiye mimi.” Mlinzi huyo akamjibu.
“Hii ndiyo nyumba iliyoingiliwa na majambazi?”
“Ndiyo hii.”
“Wewe ulikuwa wapi wakati majambazi hao wanaingia?”
Mlinzi huyo akaeleza kama alivyokuwa amepanga.
“Hebu tuoneshe huo mwili wa marehemu aliyechinjwa.”
Mlinzi huyo akawapeleka polisi hao mahali ulipokuwa mwili wa James.
“Wamemchinja namna hii!” Polisi mmoja akamaka.
“Wameiba nini na nini?” Polisi mwingine akauliza.
“Waliiba masanduku.”
“Masanduku ya nini?”
“Sijajua ni masanduku ya nini lakini yalikuwa humu ndani”
“Hebu twende ukatuoneshe humo ndani.”
Mlinzi huyo akawaingiza polisi hao ndani ya nyumba hiyo. Waliingia hadi chumbani mwa James.
“Huyu mtu hana mke?” Mmoja wa polisi hao akamuuliza mlinzi.
“Hana mke.”
“Humu ndani wanaishi watu wangapi?”
“Alikuwa akiishi pake yake.”
“Alikuwa akiishi peke yake jumba lote hili?”
“Ndiyo, alikuwa akiishi peke yake.”
“Hebu tutoke huku nje.”
Wakatoka tena nje ya ile nyumba.
“Umesema bosi wako aliamka na kukwambia uzunguke nyuma ya nyumba baada ya kusikia sauti za watu, ni upande upi? Hebu tuoneshe.”
“Ni huku.”
Mlinzi huyo aliwapeleka polisi hao upande wa nyuma wa ile nyumba.
“Sasa wakati narudi tena ndio nikakuta wameshamchinja.” Mlinzi aliwambia.
“Unajua maelezo yako hayaeleweki lakini utakwenda kutueleza vizuri kituo cha polisi. Ngoja kwanza tushughulikie huu mwili wa marehemu.”
Polisi hao walipiga simu ambapo gari la hospitali lilifika na kuuchukua mwili wa James ambao ulipelekwa moja kwa moja hospitali ya Muhimbili kwa uchunguzi.
Nyumba ya James ikafungwa na polisi ambapo mlinzi huyo alichukuliwa kituo cha polisi.
“Sasa hebu tueleze vizuri nini kilitokea?” Mmoja wa polisi wa kituo hicho aliyekuwa na kalamu na karatasi alimuuliza mlinzi huyo aliyekuwa amekaribiswa kwenye kiti.
Mlinzi alieleza kama alivyokuwa amepanga.
“Hao walinzi hawakuvunja geti?”
“Hawakuvunja.”
“Waliingiaje mle ndani?”
“Nafikiri waliruka ukuta.”
“Wewe uliwasikia?”
“Kusema kweli mimi sikuwasikia lakini marehemu aliwasikia, akatoka na kuniambia amesikia sauti za watu nyuma ya nyumba.”
“Wewe ukafanya nini?”
“Nikazunguka nyuma ya nyumba.”
“Ukaona nini?”
“Sikuona kitu.”
“Sasa hawa majambazi walitokea wapi na walimchinja vipi bosi wako?’
“Sijui. Wakati mimi natokeza upande wapili wa nyumba nikamuona bosi wangu amelala chini akiwa tayari ameshachinjwa. Niliwaona pia watu watatu waliokuwa wamebeba masanduku wakitoka kwenye geti.”
“Hao watu uliwafuatilia?”
“Niliwafuatilia lakini nilipotoka kwenye geti sikuwaona.”
“Hebu tueleze wakoje hao watu?”
“Wawili walikuwa wamevaa mavazi meupe, mmoja mavazi meusi.”
Mlinzi huyo akawaelezea watu hao kwa jinsi alivyowaona. Polisi huyo alipotajiwa yale mavazi waliyokuwa wameyavaa na kusikia maelezo kwamba shingo ya aliyekuwa amevaa mavazi meusi ilikuwa kama imechinjwa na kwamba kichwa cha mtu huyo kilikuwa kinaningi’inia, polisi huyo alishituka. Kumbukumbu za mauaji ya Martin zikaanza kumjia.
Japokuwa mauaji ya Martin yalishughulikiwa katika kituo kingine cha polisi, taarifa zake zilisambaa katika vituo vyote vya polisi jijini Dar.
“Mbona watu hao ni kama wale waliodaiwa kumuua Martin?” polisi huyo akajiuliza moyoni mwake kisha akamwambia yule mlinzi.
“Kulikuwa na mauaji yaliyotokea huko Mikocheni hivi karibuni. Watu wanaodaiwa kufanya mauaji hayo ni kama hao uliowaona!”
“Unazungumzia mauaji ya Martin”
“Ndiyo Martin”
“Huyu jamaa aliyeuawa leo ni mdogo wake baba mmoja, mama mmoja!”
Yule polisi alishituka akawatazama polisi wenzake waliokuwa wamesimama kwa pembeni.
“Si mnamkumbuka yule jamaa aliyeuawa Mikocheni juzi juzi tu?” Akawauliza.
“Si yule jamaa aliyechinjwa na majambazi waliopora mkoba wake uliokuwa na pesa!” Polisi mmoja akamwambia.
“Ndiye huyo huyo. Sasa huyu mlinzi anasema yule jamaa na huyu aliyeuwa leo ni ndugu. Na wauaji wanaonekana kama ni wale wale!”
Suala hilo likazua taharuki zaidi.
“Inabidi tuwafahamishe wakubwa wetu usiku huu.” Yule aliyekuwa akiandikisha maelezo ya mlinzi akawambia wenzake.
Mkuu wa kituo alikuwa hayuko, akaitwa kwa radio coll. Alipofika kituoni hapo alielezwa kuhusu tukio hilo. Mkuu huyo wa kituo akaanza kumhoji yule mlinzi. Alipothibitisha kuwa wauaji wa James walikuwa ni wale wale waliomuu Martin na kwamba Martin na James walikuwa ndugu, akapiga simu makao makuu ya polisi.
Katika muda wa saa moja, makachero watatu akiwemo Inspekta Amour walikuwa wameshaamshwa usingizini. Walifika makao ya polisi na kuchukua gari iliyowapeleka katika kituo hicho.
Baada ya kupata maelezo kuhusu tukio lililotokea, Inspekta Amour alimhoji mlinzi huyo.
“Kama wewe ndiye mlinzi wa nyumba ya marehemu, hao watu waliingia vipi na kuweza kumchinja marehemu na kuiba na kisha wakaweza kuondoka wakati wewe ukiwepo?”
“Naona ilikuwa kama miujiza hivi….” Ilikuwa ndiyo sentensi aliyoanzia mlinzi huyo kabla ya kutoa maelezo ambayo alishayatoa kwa polisi alipohojiwa kwa mara ya kwanza.
Inspekta Amour alikuwa amemkazia macho mlinzi huyo wakati akieleza. Hata baada ya kutoa maelezo yake ambayo yalizua maswali mengi, Amour aliendelea kumtazama lakini bila kumuuliza chochote.
Yale macho ya Amour yalimfanya yule mlinzi aanze kujishuku mengi. Baada ya kimya cha sekunde kadha ndipo Amour alipomuuliza tena.
“Hao watu watatu waliomchinja marehemu uliwaona vizuri?”
“Niliwaona wakimalizia kutoka?”
“Swali langu nimekuuliza uliwaona vizuri?”
“Sikuwaona vizuri kwa sababu niliwaona wakimalizia kutoka kwenye geti.”
“Walivaa mavazi gani?”
“Wawili walivaa mavazi meupe, mmoja alivaa mavazi meusi?”
“Umesema huyo aliyevaa mavazi meusi alikuwaje?”
“Kichwa chake kilikuwa kinaning’inia na shingo yake ilikuwa imechinjwa.”
Amour akanyamaza tena kwa muda kabla ya kumuuliza.
“Walipotoka kwenye geti wewe ulifanya nini?”
“Niliwafuta lakini nilipotoka tu nje ya geti sikuwaona tena.”
“Umesema waliiba nini?”
“Niliona wakitoka na masanduku.”
“Masanduku mangapi?”
“Masanduku matatu.”
“Waliyachukua wapi?”
“Nafikiri chumbani kwa marehemu.”
“Hivi wakati wote huo, watu hao wakimchinja bosi wako wakaingia ndani na kuiba, wewe ulikuwa unazunguka nyumba tu?”
“Ndiyo. Nilikuwa nyuma ya nyumba baada ya marehemu kuniambia nizunguke nyumba kwa kuwa alisikia sauti za watu.”
“Kuizunguka nyumba ungeweza kutumia dakika tatu au nne, si nyumba ya kawaida tu au ina ukubwa gani?”
“Ni nyumba ya kawaida tu.”
“Sasa hizo dakika tatu au nne za kuizunguka nyumba ndizo zilizowawezesha watu hao kumchinja marehemu, kuingia ndani na kuiba…?”
“Ndiyo maana nikasema lile tukio lilitokea kimiujiza ujiza tu. Hata sijui lilitokeaje?”
“Hebu twende hapo nyumbani tukapaone.”
“Sawa.”
Dakika chache baadaye gari moja la makachero likiwa na makachero watatu kutoka makao ya polisi na gari jingine la polisi wa kituo hicho likiwa na polisi watatu akiwemo mkuu wa kituo hicho pamoja na mlinzi wa nyumbani kwa marehemu James, yalielekea katika eneo la tukio. Walipofika nyumbani kwa marehemu, mlinzi huyo aliwaonesha mahali alipochinjwa james. Pia aliwaingiza ndani na kuwaonesha chumba cha James.
“Huyu kijana hakuwa na mke?” Amour akamuuliza mlinzi.
“Hakuwa na mke lakini alikuwa na mchumba wake ambaye alikuwa akifika naye hapa nyumbani.”
“Hakuna watu wengine wanaoishi humu ndani?”
“Alikuwa anaishi peke yake.”
Walipotoka mle chumbani, Amour alimwambia mlinzi awaoneshe alivyoizunguka nyumba hiyo wakati James alipomwambia alisikia sauti za watu.
Mlinzi alionesha jinsi alivyoizunguka nyumba huku Inspekta Amour na wenzake wakimfuata kwa nyuma. Walipotokeza upande wa pili, Amour alimwambia mlinzi.
“Hatukutumia hata dakika tatu wakati tumetembea kwa taratibu.”
Mlinzi akanyamza kimya.
“Sasa hebu tuambie kwa kadiri ulivyofikiria hao watu walijificha kwa wapi wakati marehemu akiwasikia wakiwa nyuma ya nyumba?”
“Kwa kweli sijagundua hadi sasa.”
“Unadhani nani atatueleza wakati wewe ndiye uliyekuwa pamoja na marehemu?”