Touré: tulieni mabao yanakuja
Muktasari:
- Touré alitua Jangwani akitokea Al-Jabalain FC ya Saudi Arabia, ambako msimu uliopita alikuwa katika kiwango bora, akifunga mabao 19 na kutoa asisti tano katika mechi 34.
MSHAMBULIAJI wa Yanga, Cheikh Ibrahima Touré amesema hana presha licha ya kutofunga kwa ki-wango anachotarajia tangu alipowasili Tanzania, akisisitiza anaamini muda wake wa kufunga utafika na ataanza kuifungia timu yake mabao mengi.
Touré alitua Jangwani akitokea Al-Jabalain FC ya Saudi Arabia, ambako msimu uliopita alikuwa katika kiwango bora, akifunga mabao 19 na kutoa asisti tano katika mechi 34.
Touré alisema tofauti kubwa aliyoiona kati ya Ligi Kuu Tanzania na Ligi ya Saudi Arabia ipo katika upande wa nguvu za mwili na Tanzania kuna ushindani mkubwa wa kimwili. Hata hivyo, alisema Yanga ina kikosi imara na anaamini kina uwezo wa kufanya vizuri zaidi katika ligi hiyo.
“Nadhani ligi hii ina nguvu zaidi kimwili. Tuna timu imara na naamini tunaweza kufanya vizuri zaidi. Lab-da ligi ya Saudi Arabia ina mambo yake ambayo ni tofauti, lakini hapa tunaweza kufanya vizuri,” ames-ema Touré.
Mchezaji huyo raia wa Senegal, kabla ya kujiunga na Yanga, aliwahi kucheza katika klabu mbalimbali na kuonyesha kiwango cha hali ya juu uwanjani, hata hivyo hadi sasa bado hajaonyesha makali yake akiwa na Yanga baada ya kufunga bao moja pekee kwenye michezo mitano ya timu yake.
Akizungumzia hali yake ya sasa, Touré alisema anaamini mabao yake yatakuja na bao la kwanza linawe-za kuwa mwanzo wa kufunga zaidi.
“Sijisikii vibaya kwa sababu najua magoli yatakuja. Nasubiri wakati wangu na najua nikifunga, magoli mengi yatafuata. Nimetulia kiakili na ninaamini kila kitu kitakuwa vizuri, Inshaallah,” alisema.
Kuhusu mechi ya Kariakoo Derby, Touré alisema amevutiwa na mazingira ya mchezo huo kutokana na uwepo mkubwa wa mashabiki na hamasa inayozunguka pambano hilo.
Alisema anatamani kufunga katika mchezo huo mkubwa dhidi ya Simba ili kuendelea kuwa na hali ya kujiamini.