Mauaji ya kutisha – Sehemu ya 6
UTANGULIZI
“Niliwaona na niliona kila kitu kilichotokea. Wakati huo mimi nilikuwa hapa hapa kwenye kioski change.”
“Mbona kuna watu wanasema sijui eti mmoja wa hao watu shingo yake ilikuwa imechinjwa?”
“Sasa pale ndio sikuelewa wale watu walikuja na miujiza gani. Kweli shingo ya mmojawao ilikuwa imechinjwa na huyo jamaa ndiye aliyetoa panga na kumchinja Yule mhasibu wa kiwanda cha maji safi.”
SASA ENDELEA...
“Halafu inesemekana baada ya kumchinja walipora mkoba wake wa pesa na kukimbia?”
“Ndiyo, walimpora mkoba wa pesa. Inadaiwa jamaa alikuwa anatoka benki. Wakachukua pesa zote.”
“Walikimbilia wapi?”
“Kwa kweli hakuna aliyewaona. Hawa majambazi siku hizi wanatumia haya mambo ya nguvu za giza. Hata yale mavazi waliyokuwa wamevaa yalikuwa hayaeleweki. Yaani baada ya kupora ule mkoba walitoweka pale pale.”
“Unadhani kwamba kuna nguvu za kiza zilizotumika?”
“Lazima. Wale si majambazi wa kawaida. Lakini kitu kilichoshangaza watu ni kwamba kabla ya kumchinja, yule jamaa aliyevaa nguo nyeusi alimwambia yule jamaa. “Baba yako amekuweka kama dhamana na wewe umeshindwa kutimiza masharti ya dhamana.”
Amour akagutuka.
“Alimwambia baba yake alimuweka dhamna wapi?”
“Hakumwambia alimuweka dhamana wapi ila alimwambia umeshindwa kutimiza masharti ya dhamana. Ndio akamchinja.”
“Sasa huyo marehemu alipoambiwa hivyo hakuuliza ni dhamana gani?”
“Nilimsikia akimuuliza. Yule jambazi akamjibu muda wako umekwisha.”
“Ulitwa polisi kutoa maelezo?”
“Baada ya lile tukio nilifunga kioski changu. Polisi waliita watu wengine.”
“Wewe ungeweza kuwa shahidi mzuri kwa sababu ulisikia walichokuwa wanazungumza.”
Kijana huyo akang’aka.
“Hata kama nilisikia, siwezi kuwa shahidi. Ushahidi mara nyingi unaponza halafu unajikuta unapoteza muda mwingi wa kazi ukiwa polisi kama vile wewe ndiye uliyeshitakiwa.”
“Hizo si fikira nzuri. Polisi hawawezi kufanya kitu peke yao bila ushiriikiano na wananchi na wananchi ndiyo nyinyi. Huwezi kusema kwamba utapoteza muda wako kama kweli wewe ni mzalendo wa nchi hii. Ni lazima tushirikiane na polisi kutokomeza ujambazi na uhalifu mwingine.”
“Ni kweli mzee nimekuelewa. Watakapokuja kuniuliza nitawapa ushirikiano.”
Amour alikuwa ameshamaliza kunywa soda yake, akamrudishia chupa kijana huyo na kumlipa pesa zake.
“Asante kijana. Huenda nitahitaji kukuona wakati mwiingine wowote.” Amour alimwambia bila kujitambulisha alikuwa nani.
Kijana naye alimkubalia bila kutambua Amour alikusudia nini na alikuwa nani.
Amour alirudi kwenye gari lake akajipakia na kuonndoka.
**********
Nyumbani kwa Almasi kulikuwa na kikao. Mara tu baada ya maziko. Almasi aliwaita sebuleni wanawe wanne waliobaki ili kuwapa wasia.
Alikuwepo james, John, Alex na Benjamin. James alikuwa mtoto wa pili wa Almasi akifuatiwa John. Baada ya John alizaliwa Alex akamalizia Benjamin.
Katika maisha yake Almasi hakubahatika kupata mtoto wa kike.
“Wanangu tuko katika kipindi cha huzuni sana. Tumempoteza kaka yenu katika tukio ambalo nyote mnalijua vizuri na sijisikii kulirudia tena.” Almasi aliwambia wanawe.
Vijana hao walimkubalia kwa pamoja.
“Nyinyi mliobaki nawaomba muendelee kushikamana mdumishe upendo na kuheshimiana. Kila linapotokea tukio ambalo linatukusanya pamoja ni lazima niwape nasaha zangu kwa sababu mimi ni baba yenu. Tukio lililotokea ni kubwa na limetuhuzunisha sana. Nawaomba wanangu muwe na mioyo ya subira na mumuombee kaka yenu apumzike pema peponi.”
“Amin.” Sauti za vijana hao zikasikika kwa pamoja.
“Martin alikuwa mhasibu wa kapuni yangu. Amefanya kazi vizuri sana na kwa uaminifu. Ni wazi kwamba kifo chake kimeacha pengo si tu kwenye familia yetu bali pia katika uongozi wa kampuni. Kwa hiyo leo ninawajibika kuteua mhasibu mwingine miongoni mwenu kushika nafasi ya marehemu Martin.” Almasi aliendelea kuwambia.
Kisha ghafla akamtazama James.
“James ni wa pili kuzaliwa na ndiye kaka wa nyinyi nyote mlioko hapa. Yeye ndiye niliyempendekeza ashike nafasi ya Martin. Kwa vile James alisoma chuo kimoja na Martin ninaamini kuwa ataimudu vizuri kazi yake au mnasemaje?”
“Ni sawa Baba.” Ilikuwa sauti ya John.
“Hiyo nafasi ni lazima aishike kaka yetu ambaye ni James,” akasema Alex.
“Mimi pia ninaunga mkono uteuzi huo,” akamalizia Benjamin.
“Hakuna mwenye kinyongo?” Almasi akawauliza wote kwa pamoja.
“Hakuna.” Wote walijibu hivyo.
“Nimefurahi kusikia kuwa nyote mmependa James ashike nafasi ya marehemu kaka yenu. Sasa kuna kitu kimoja nataka kukuuliza James.” Almasi alimwambia james huku akimtazama.
“Unatuhakikishia hapa mimi na ndugu zako kwamba utamudu majukumu yako na utafanya kazi kwa uaminifu kama alivyokuwa kaka yako?”
“Ninawahakikishia wewe baba yangu na ndugu zangu kwamba nitamudu majukumu yangu na nitafanya kazi kwa uaminifu kama alivyokuwa kaka yetu na lengo kubwa ni kuleta tija na ufanisi kwenye kampuni yetu. Najua hivi sasa tuko katika ushindani mkubwa wa kibiashara kwani kampuni za maji safi ziko nyingi.”
“Umezungumza vizuri James na umenipa moyo. Asante sana. Sasa kuna kitu kingine ambacho nataka muwe macho nacho nyinyi wote. Ujambazi umekuwa mwingi sana hasa katika jiji la Dar. Nawaomba muwe makini sana. Na kwa upande wako James badala ya kwenda benki kuchukua pesa taslimu utakuwa unatumia hundi. Mishahara ya wafanyakazi utaiingiza benki, kila mtu kwenye akaunti yake. Umenielewa?”
“Nimekuelewa baba.”
******
Ilikuwa imepita miezi sita. James alikua ndiye mhasibu wa kampuni ya maji safi ya baba yake. Tangu alipokabidhiwa wadhifa huo alikuwa amefanya kazi vizuri sana na kuiletea mafanikio makubwa kapuni hiyo.
Alipata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa baba yake na kwa ndugu zake na pia kwa wafanyakazi wa kampuni hiyo jambo ambalo lilimuongezea moyo wa kuipenda kazi yake.
Utaratibu ulikuwa ni kama ule waliopanga na baba yake pamoja na ndugu zake. Ule mtindo wa awali wa kuchukua pesa nyingi kutoka benki kwa ajili ya kugawa mishahara ya wafanyakazi uliachhwa. Wafanyakazi walikuwa wakiwekewa mishahara kwenye akaunti zao.
Kadhalika matumizi mengi ya pesa yalikuwa yakifanywa kwa hundi badala ya pesa taslimu.
Miezi mitatu tu baada ya James kuwa katika kiwanda hicho akajikuta ameingia katika penzi na mmoja wa wafanyakazi wa kampuni hiyo aliyeitwa Grace.
Penzi hilo lilianza kuchanua moyoni mwa kila mmoja na kuwa siri yake lakini taratibu likaanza kujitokeza kwa kila mmoja. James ndiye aliyeanza kumuonesha Grace kuwa alikuwa akimpenda.
Siku moja James alichukua namba ya simu ya Grace. Jioni alipokuwa nyumbani kwake akampigia simu Grace na kumuomba akutane naye katika hoteli moja iliyopo Sinza ambako James alikuwa anaishi.
Grace akaukubali mualiko huo bila kupingwa. Wakakutana saa mbili usiku katika moja ya kumbi za hoteli hiyo.
Walikula chakula cha usiku huku wakizungumza hili na lile lakini baada ya chakula hicho, James alibadili mazungumzo na kumueleza Grace lililokuwa moyoni mwake.
Grace naye bila kuonesha hiyana alimueleza wazi James kuwa hata naye alikuwa akiumia.
Hapo ndipo penzi lilipoanza rasmi kati ya James na Grace.
Grace alikuwa msichana wa Kihaya aliyekuwa akiishi Mwenge. Licha ya kuwa na umbo jamali na sura jamili alikuwa mrembo aliyevuta macho ya kila mwanaume.
Penzi la James na Grace lilianza kama ua lililochukua muda kuchanua. Lilianza kama siri yao wawili. Hawakutaka wafahamike kuwa walikuwa wapenzi. Lakini taratibu penzi hilo likaanza kuchanua na kudhihirika. Likawa bayana kwa kila mfanyakazi wa kampuni hiyo. Kila mfanyakazi alifahamu kuwa Grace alikuwa mwandani wa bosi wao.
Kufuatia kufahamika kwa penzi lao, Grace akawa bosi kivuli wa kampuni kwani alijitwalia mamlaka ya kuamrisha wafanyakazi wengine vile anavyotaka yeye na pia kuwashitakia kwa James wale ambao hawakutaka kumtii. Grace akaanza kuogopewa.
Grace alikwenda kazini siku aliyotaka yeye na aliondoka kazini muda aliotaka yeye. Hakukuwa na wa kumuuliza. Habari zikamfikia mzee Almasi.
Kwa kujua kuwa angeitwa na baba yake wakati wowote na kuulizwa kuhusu madai ya kuwa katika penzi na mfanyakazi wake, James alitinga nyumbani kwao akiwa amefuatana na Grace ambapo alimtambulisha Grace kama mchumba wake.
Mzee Almasi na mke wake walishangaa.
“Huyu si Grace?” Almasi akamuuliza. Alikuwa akimfahamu.
“Ndiye yeye.” James alimjibu akitabasamu.
“Uchumba wenu ulianza lini?”
“Hauna muda mrefu.”
“Kwa hiyo mmepanga kuoana?”
“Ndiyo baba.”
“Ni vizuri lakini nataka kujua bado ni mfanyakazi wetu au umeshamuachisha?”
“Bado ni mfanyakazi wetu.”
“Ninakushauri wakati mnaendelea na mipango yenu, umuachishe kazi.”
“Sawa.”
“Mnatarajia ni lini mtavalishana pete ya uchumba?”
“Siku mbili hizi hizi tutafanya hivyo.”
“Umeshajitokeza kwa wazazi wake?” Mama Almasi akauliza.
“Nimeanza kumleta huku kwetu kwanza atambulike kisha atanifikisha kwao.”
“Basi ufanye hivyo haraka ili tuweze kuendelea na taratibu nyingine.”
“Umenipa maelezo ya busara mama yangu. Kitu cha msingi ninachokitaka kwenu mnieleze je mmemkubali mchumba wangu?”