Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mauaji ya kutisha – Sehemu ya 3

MAUAJI 3 Pict

UTANGULIZI

Almasi mwenyewe ndiye aliyetoa jina hilo kumpa mjuu wake. Alipofahamishwa kuwa mkwe wake alikuwa amejifungua alikwenda hospitalini alikokuwa amelazwa Hilda.

Pamoja na mambo mengine, alimpa  pole na  hongera mkwe wake. Akakishika kichanga kilichozaliwa na kukiambia.

“Wewe ni Almasi”

Tangu hapo mtoto huyo akaanza kuitwa Almasi wakijua kuwa babu yake alikuwa ameshampa jina hilo..

Kuzaliwa kwa Almasi kulimfurahisha Martin na kumpa  hisia kwamba alikuwa ametoka katika kundi la utoto na kuingia katika kundi la utu uzima kwani si muuda mrefu atakuwa akitwa  baba..

SASA ENDELEA...



ALIPOINGIA katika eneo la Mikocheni kilipokuwa kiwanda cha baba yake cha kuzalisha maji safi, Martin aliona watu wa ajabu waliokuwa wamesimama katikati ya barabara mbele yake

Walikuwa watu watatu waliovaa mavazi kama kanzu. Wa kwanza alivaa kanzu nyeupe, wa pili alivaa kanzu nyeusi na wa tatu alivaa kanzu nyeupe, wakiwa miguu peku peku.

Yule aliyekuwa katikati ambaye alivaa kanzu nyeusi, kichwa chake kilikuwa kikining’inia kikiwa na ishara ya kuchinjwa kwenye koo huku michirizi ya damu iliyoganda ikionekana. Kwenye mkono wake wa kulia alikuwa ameshika upanga uliokuwa unang’aa.

Martin alishituka na kusimamisha gari. Wakati anafungua mlango wa gari ili atoke, wale watu walishamfikia kwenye mlango.

Yule mtu ambaye kichwa chake kilikuwa kikining’inia alimuuliza Martin.

“Wewe ni mtoto wa Alamsi?”

“Ndiyo.”  Martin alijibu kwa kiwewe.

“Baba yako alikuweka kama dhamana na wewe umeshindwa kutimiza masharti ya dhamana!”

“Masharti yapi?”

“Muda wako umekwisha, huwezi kupata jibu.”

Hapo hapo ule upanga ukapita kwenye koo la Martin na kulichinja!

Martin hakuwahi hata kupiga kelele. Ule mshituko wa kuchinjwa ulimfanya akurupuke na kutoka mbio huku shingo yake ikining’inia baada ya kuchinjwa. Ilifanana na ya yule aliyemchinja.

Martin hakuweza kupiga hata hatua tano akaanguka chini akiwa amekufa.

Yule mtu aliyemchinja alitia mkono kwenye gari na kuuchukua ule mkoba wa pesa akapotea na wale wenzake.

                                                            **********

Ndani ya ofisi ya Idara ya Upelelezi wa Makosa ya jinai, Makao Makuu ya polisi jijini Dar, Inspekta Amour alikuwa amekiacha kiti na kusimama kando ya dirisha akitazama nje ya ofisi.

Anapokuwa amekabiliwa na maamuzi mazito, mara nyingi alipenda kusimama kuliko kukaa.

Siku ile ilikuwa ni moja ya siku ambazo aliiona kazi yake kuwa ngumu. Tangu kulipokucha alishapokea kesi  nzito zaidi ya sita ambazo zilihitaji uchunguzi wake.

Kulikuwa na mauaji ya watu watatu yaliyotokea Kigamboni ambayo  licha ya silaha iliyotumika katika mauaji kupatikana, muuaji alifanikiwa kutoweka.

Ilidaiwa kuwa yalikuwa mauaji ya kulipa kisasi lakini kilichowashitua zaidi polisi ni bunduki ya kijeshi  ambayo ilikutwa katika  eneo la tukio ikiwa na upungufu  wa risasi tatu ambazo polisi waliamini ndizo zilizotumika katika mauaji hayo.

Licha ya polisi kuumiza vichwa kwa kujiuliza muuaji huyo alikuwa nani na watampata wapi, bado walikuwa katika taharuki baada ya kukuta silaha  iliyotumika katika  mauaji ilikuwa ni ya kijeshi tena mali ya jeshi la polisi!

Amour alifika katika eneo la tukio ambapo aliambiwa na mkuu wake amtafute muuaji hadi amtie mikononi.

Wakati huo tayari Amour alikuwa na kesi kadhaa zilizohitaji upepelelezi.

Kama haitoshi nusu saa tu iliyopita alikuwa ameitwa katika tukio jingine la ujambazi uliofanyika katika benki moja ya jijini.  Ingawa hakukuwa  na mtu yeyote aliyeuawa, fedha za benki zilizokuwa zikitoka Benki Kuu zaidi ya shilingi bilioni tatu zilikuwa zimeibiwa.

Matukio hayo ambayo yangehitaji uchunguzi wake, yalikuwa  yakimuumiza kichwa. Baada ya kuwasili ofisini kwake alipekuwa majalada yaliyokuwa mezani kwake kisha akainuka  na kusimama kando ya dirisha.

Alifahamu kuwa uzembe wa walinzi wa benki ambao alikuwa amewatia ndani, ndio uliosababisha kuporwa kwa pesa hizo. Amour alishuku kuwa ujambazi huo ulifanikiwa  kutokana na njama kati ya majambazi hao  na walinzi wa benki.

Wakati akiwaza hayo alishitushwa na muungurumo wa simu iliyokuwa juu ya meza yake. 

Alirudi kwenye meza akauinua mkono wa simu huku akiketi kwenye pembe moja ya meza.

Akauweka mkono wa simu sikioni kisha akasema.

“Inspekta Amour hapa.”

“Amour kuna kazi gani iliyoko  mikononi mwako?” Sauti ya mkurugenzi wa upelelezi ikaunguruma kutoka simu ya upande wa pili.

“Kazi zilizoko mikononi mwangu ni nyingi. Kuna  lile tukio la  mauaji lililotokea Kigamboni na  kuna ule  ujambazi uliofanyika benki.”

“Ziache kazi hizo, nitawapa wapelelezi wengine. Kuna tukio la mauaji ya ajabu limetokea huko Mikocheni. Tafadhali fika hapa  ofisini kwangu sasa hivi.”

Inspekta Amour aliurudisha mkono wa simu kwenye sehemu yake kisha akauchukua ufunguo  wa  gari uliokuwa juu ya meza.

Wakati Amour anatoka ofisini  mwake alishangaa kuona alikuwa akiongezewa kazi wakati tayari akiwa na  kazi zilizomlemea.

Alijiuliza kama hakukuwa na makachero wengine wenye sifa ambao  wangeweza kupewa kazi aliyotakiwa kupewa yeye.

Alipotoka ofisini mwake aliingia kwenye lifti akapaa  hadi horofa ya saba ilikokuwa ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi.  Kama afisa maalum aliruhusiwa kuingia na kuonana na mkurugenzi huyo.

“Kaa kitako tafadhali” Mkurugenzi huyo  alimwambia Amour alipomuona akiingia ofisini kwake.

Licha ya umri wake kukaribia miaka sitini, mkurugenzi huyo alionekana mkakamavu na mwenye wajihi wa kupendeza. Nywele zake zilikuwa nyeupe tupu.

Alikuwa amevaa shati jeupe na suruali nyeupe na  alikuwa amefunga tai.

Amour alikaa kwenye kiti mbele ya meza ya mkurugenzi. Hakumsalimia kwa  sababu walishakutana asubuhi.

“Amour kuna mauaji yametokea Mikocheni sasa hivi” Mkurugenzi alianza kumueleza Amour.

“Nimekuita wewe kwa sababu yanaonekana ni mauaji ya kutisha kidogo na si ya kawaida kutokea”

“Ni watu wangapi waliouawa?”

“Ni mtu mmoja. Watu  wanaodaiwa kuua ni  watatu lakini walioshuhudia tukio hilo wamewaeleza polisi  kuwa hao watu ni wa ajabu.”

Mkurugenzi wa upelelezi alimueleza Amour jinsi tukio  hilo la mauaji lilivyotokea kama  lilivyoelezwa  na mashuhuda.

Maelezo ya mkurugenzi huyo kidogo yalimshangaza Inspekta Amour.

“Umeniambia kuwa huyo  mchinjaji na yeye alikuwa amechinjwa?”

“Ni kwa mujibu wa watu walioshuhudia tukio  hilo.  Wamesema kwamba shingo  ya mchinjaji ambaye alikuwa amevaa mavazi meusi, ilikuwa ikining’inia ikionesha ishara ya kuchinjwa.”

“Huyo mtu aliyechinjwa atakuwa na uwezo wa kumfuata mtu na kumchinja na kisha  kutoweka?” Amour aliuliza kwa mshangao.

“Ndiyo maana nimekueleza kuwa mauaji yenyewe si ya kawaida. Kuna kitu kama miujiza ndani yake. Hebu nenda kafanye uchunguzi wako. Kwanza fika  katika eneo la tukio, uliza tukio lilitokeaje na uanze upelelezi mara moja. Nataka uhakikishe hao  wauaji wanakamatwa haraka”

   *************

Amour alifika katika eneo la tukio. Alikuta bado polisi walikuwa katika eneo hilo. Pia kulikuwa na watu waliokusanyika mahali hapo  kuangalia kilichotokea.

Amour aliliegesha gari akashuka na kujipenyeza kwenye kundi la watu ambao  walimpa nafasi  ya kupita hadi akalifiikia gari la Martin.

Mwili wa Martin  ulikuwa  bado  haujaondolewa. Polisi walikuwa wakiupiga picha. Polisi wengine walikuwa wameshika  futi wakipima urefu wa kutoka mwili huo  ulipoanguka na gari  lake lilipokuwa.

Kando ya mlango  wa gari upande wa dereva ambapo palikuwa na michanga, alama za miguu za watu waliomuua Martin zilionekana. Alama hizo  nazo zilipigwa picha

Mzee Almasi, baba  yake Martin alikuwa amesimama nyuma ya polisi aliyekuwa akipiga picha huku ameshika kitambaa cha kujifutia jasho  mkononi.

Alikurupushwa nyumbani kwa simu aliyopigiwa na rafiki yake ambaye alimuarifu kwamba mwanawe alikuwa ameuawa.

“Unasemaje?” Almasi aliuliza kwa hamaki mara tu alipoarifiwa kuhusu tukio  hilo.

“Mwanao Martin amekutwa ameuawa hapa Mikocheni mbali kidogo na kiwanda  chenu cha maji safi.”

“Ameuawa na nani?”

“Haijafahamika bado lakini ungefika kwanza ili ushuhudie mwenyewe.”

Almasi alikumbuka  kwamba  Martin alikuwa amekwenda benki kuchukua pesa za mishahara ya wafanyakazi. Akahisi huenda pesa hizo zilikuwa zimeporwa. Alikata simu aliyokuwa amepigiwa akampigia Martin. Simu ya Martin iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa. Ilipopokelewa sauti ilikuwa  ni ya mtu mwingine.

“Jitambulishe wewe  ni nani?” Sauti hiyo  ambayo ilikuwa ya polisi ikamuuliza.

“Mimi  ni  Almasi, ninampigia  mwanangu Martin.”

“Unazungumza na polisi.  Kuna kijana ambaye ameuawa hapa Mikocheni. Inawezekana ndiye mwanao. Tafadhali hebu fika hapa haraka.”

Hapo ndipo Almasi alipoamini kuwa kulikuwa na tukio hilo. Aliondoka nyumbani bila kumuarifu lolote mke wake. Akajipakia kwenye gari na  kuondoka. Alifika  Mikocheni na kushuhudia mwenyewe kilichokuwa  kimetokea.  Aliliona gari la mwanawe kisha akauona  mwili  wa Martin uliokuwa umechinjwa.

Ingawa alijikaza kiume, aliona machozi yakianza kumtiririka. Alitoa kitambaa kutoka mfukoni mwake akajifuta machozi pamoja  na jasho lililokuwa limetanda usoni kwake.