Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mauaji ya kutisha - Sehemu ya 24

MAUAJI 24 Pict

UTANGULIZI

“Jukumu lilikuwa mikononi mwako. Itabidi utupe maelezo ya kina ni kwanini Benjamin ameuawa”

“Niwape maelezo gani tena?”

“Huna budi kuisaidia polisi. Utakuwa mikononi mwetu hadi uchunguzi wetu utakapokamilika”

“Lakini hii si haki jamani!”

“Haki ni ipi?”

Inspekta Amour akaingilia kati.

SASA ENDELEA


“Usituzuie kufanya kazi yetu!  Lazima uwekwe  ndani!”

Mlinzi huyo alikokotwa na kuwekwa ndani.

Almasi alifika makao ya polisi baada ya mazishi ya Benjamin ambayo yalifanyika siku ya pili yake.

Alipofika alikutana na Inspekta Amour ambaye alimuita kachero mwenzake ofisini.

Makachero hao wakaanza kumhoji Almasi.

“Almasi hebu tueleze ukweli, unahisi ni kwanini  watoto wako wanauawa?” Aliyenza kumuuliza alikuwa Amour.

Swali hilo likamshangaza Almasi.

“Unaniuliza ni kwanini watoto  wangu wanauawa?”

“Ndiyo. Inawezekanahujui sababu lakini  kuna vitu unavihisi, ndio tunataka utuambie”

“Nyinyi mlishindwa kugundua?”

“Ndiyo tuko  katika upelelezi” Kachero aliyekuwa na Inspekta Amour  akamwambia.

Almasi alinyamza kidogo. Akaonekana kama alikuwa akifikiria kitu kabla ya kusema.

“Mimi ninahisi ni hujuma tu. Watu  wanaona kama vile nimepata neema  ya watoto  na mali, basi wanataka nifilisike. Nisiwe na mali wala  watoto”

“Unashuku watu hao ni kama kina nani?” Amour akamuuliza huku akimtazama kwa makini.

“Siwezi kuwajua isipokuwa  ninahisi tu kama vile mlivyotaka kupata hisia zangu”

“Umesema watu wanaona umepata neema ya mali na watoto, hebu tuambie una mali ya kiasi gani?”

“Nina nyumba, nina kiwanda kile cha maji safi na  nina vitega uchumi vingine vidogo dogo”

“Watu wengi wana mali zaidi ya hiyo, kwanini wauaji hao wakuandame wewe peke yako. Una sababu yoyote unayoweza kitueleza?”

“Wameamua tu, pengine ni watu wanaonifahamu”

“Huna biashara nyingine zaidi ya hizo ulizotutajia?” Kachero aliyekuwa na Amour akamuuliza.

Almasi akatikisa kichwa”

“Sina  biashara nyingine”

“Hebu tueleze jinsi ulivyochuma mali yako?”

“Inahusianaje na kuuawa watoto wangu?”

“Inaweza kuhusiana. Tueleze tu, sisi tunajua”

“Sijui  nianzie wapi?”

“Pa kuanzia ni pale ulipoanza kupata mali”

“Kabla ya kupata mali nilikuwa mfanyabiashara wa madini”

“Hebu tueleze ulikuwa na mtaji wa kiasi gani wakati huo?” Amour akamuuliza.

“Sikuwa na mtaji wowote. Nilikuwa mtu wa kati. Akitokea mtu ana madini na anatafuta mteja, mimi nilikuwa nawajua wateja wa madini. Hapo ninakuwa nimepata dili”

“Hizo pesa ulizopata zilikutosha ununue kiwanda?”  Amour akaendelea kumuuliza.

“Nlinunua kiwanda baada ya kuwa nimeshatajirika”

“Tueleze jinsi utajiri huo ulivyoupata”

Baada ya kuwa mlanguzi wa madini kwa miaka kadha, hatimaye nilikwenda Marerani mwenyewe. Huko ndiko nilikofanikiwa”

“Ilikuwa ni lini?”

“Kama miaka kumi hivi iliyopita”

“Kuna wenzako wowote uliokuwa ukishirikiana nao?”

“Nilikuwa nao”

“Wako wapi?”

“Tumechangukana. Nilisikia mmoja yuko Nairobi. Mwingine yupo hapo Kibaha”

“Mlipotezana lini?’

“Miaka mingi sana”

“Na hao wenzako ni matajiri?”

“Inawezekana ni matajiri lakini si kama  mimi”

“Kwanini, wakati mlikuwa pamoja?”

“Tulikuwa pamoja lakini mimi  ndiye niliyekuwa bosi wao”

“Hata huyo aliyeko Kibaha hamuwasiliani?”

“Hatuwasiliani”

“Kwanini?”

“Yule tulifarakana kule kule Marerani”

“Kwanini mlifarakana?”

“Hatukuwa tukielewana. Ni mtu mwenye tamaa sana. Kila unachompa  kwake kinakuwa kidogo”

“Ulivyosikia anafanya nini hapo Kibaha?’

“Nilisikia ana gesti na ana mradi wa ufugaji kuku”

Amour aliwaza kidogo kisha akamuuliza.

“Nilisikia hii kazi ya madini si kazi ya kuiingia kikichwa kichwa. Unaweza kudhulumiwa au kudhulumu. Kwako wewe ilikuwaje?”

“Ilikuwa safi tu”

“Hamkudhulumiana na wenzako?”

“Hapana”

“Sasa kwanini huyo mwenzakohamuwasiliani wakati mpo karibu tu?”

“Ni kwa sababu ya roho yake mbaya”

“Anaitwa nani?”

“Mosha”

“Mosha nani?”

“Nilikuwa namfahamu kwa jina hilo tu”

“Gesti yake inaitwaje?”

“Inaitwa hivyo hivyo Mosha Guest House”

Amour akaitazama saa yake.

“Tuna maswali mengi ya kukuhoji lakini naona muda hauturuhusu. Kwa leo tuishie hapa. Tutakuhitaji tena hapo kesho”

“Sawa”

Almasi alipoondoka, Amour alimwambia kachero aliyekuwa naye.

“Meja Elias twende Kibaha”

“Kwa ajili gani?”

“Tumfuate  huyo  jamaa tuliyelezwa..”

“Nani, Mosha?”

“Kuna kitu tunaweza kukipata kutoka kwake. Almasi anashuku tu kuwa kuna watu wanaomfanyia hujuma lakini huenda huyo Mosha akawa mmojawapo”

“Kutokana na maelezo yake inaonekana watu hawa hawako sawa”

“Mimi nina mashaka kwamba huyu Almasi alimdhulumu huyo mwenzake ndio maana wamefarakana na inavyoonesha wana uadui. Inawezekana kabisa kuwa ndiye anayemhujumu”

“Ni wazo zuri. Twende”

Dakika chache baadaye Inspekta Amour na Meja Elias wakawa kwenye gari la polisi wakielekea Kibaha.

“Huyo Mosha anaweza kuwa anatuma watu kumuulia mwenzake watoto wake” Amour alimwambia Elias wakati gari hilo la polisi likielekea Kibaha.

“Unajua  unanikumbusha kitu. Yule aliyeshuhudia wakati Benjamin anauawa alituambia alimsikia huyo muuaji akimwambia marehemu kuwa baba yako alikuweka dhamna lakini umeshindwa kutimiza masharti ya dhamana. Huoni kuwa hapo pana kitu?”

“Kitu kipo, ndio maana nikakwambia twende Kibaha. Tukimpata huyo Mosha tutajua mengi”

“Hatukumuuliza Almasi huyo Mosha anaishi eneo gani?”

“Ametuambia ana gesti inayoitwa kwa jina lake. Tutaulizia hiyo gesti. Tukiipata na yeye mwenyewe tutakuwa tumempata”

Saa chache baadaye Inspekta Amour na kachero Elias wakawa kwenye gari wakielekea Kibaha.

“Tulikosea tangu mwanzo kutomchunguza huyu Almasi” Amour alimwambia mwenzake wakati gari hilo likiwa kwenye mwendo.

“Ni kweli. Waswahili wanasema kikulacho kinguoni mwako. Huenda haya matatizo yanatokana na yeye mwenyewe”

“Vile alivyotaja biashara ya madini, nimepata shaka sana. Huenda amedhulumiana na wenzake na wakawekeana visasi. Kwanini yeye awe tajiri wenzake wasiwe matajiri wakati walifanya biashara moja?  Au kwanini atuambie kuwa alikorofishana na Mosha tangu wakiwa machimboni? Lazima patakuwa pana kitu. Tukichunguza  kwa  makini tunaweza kugundua”

“Mimi  nayafikiria sana yale  maneno “Baba yako alikuweka kama dhamana na wewe umeshindwa kutimiza masharti ya dhamana”

“Sasa hapo sipanaonesha pana  jambo. Mwenyewe tulipomuuliza anakanusha”

“Jambo jingine ambalo nimekuwa  nikilifikiria ni kwamba majambazi wanaua kwa lengo la kufanya uporaji, kwanini  watoto wake wanauawa bila hata kupekuliwa mifukoni?  Huoni kama pana kisasi hapa?”

“Ninaamini kabisa kwamba tunaelekea kugundua  kitu”

Walipofika Kibaha hawakusumbuka kuipata  Mosha Guest House. Kwani vibao vilivyowekwa pembezoni mwa barabara  vikionesha gesti hiyo ilipo, viliwangoza hadi mtaa uliokuwa  na  gesti hiyo.

Ilikuwa  ni gesti iliyounganishwa na baa.

“Huyu  atakuwa ni mchaga hasa. Wachaga hupenda kuunganisha baa na gesti” Amour alimwambia Elias  wakati wakiitazama gesti hiyo.

“Ukienda mikoani wachaga ndio wanaomilliki sana biashara ya gesti na baa”

Mara tu baada ya kuigundua gesti hiyo, walikwenda kituo cha polisi na kuonana na mkuu wa polisi wa wilaya hiyo.

“Tulikuwa tunamtafuta mtu anayeitwa Mosha. Tumeambiwa anamiliki gueti house” Amour alimwambia mkuu huyo wa polisi wa wilaya ya Kibaha mara tu walipoingia ofisini mwake.

“Amefanya nini?” Mkuu  huyowa kituo akawauliza.

“Tumeambiwa kwamba alikuwa akishitrikiana na mtu mmoja anayeitwa Almasi, mkazi wa  Dar es Salaam ambaye watoto wake wamekuwa wakiuawa na hivi sasa wamemalizika wote…”

“Nimeshasikia kuhusu mtu huyo. Sasa Mosha anahusikaje?”

“Tukokwenye uchunguzi. Tumegundua kwamba huenda wanaomfanyia hivyo Almasi ni watu aliokuwa akishirikiana nao kwenye biashara yake ya madini ambayo aliwahi kuifanya na ndiyo iliyompa utajiri”

“Mosha aliwahi kushirikina  na mtu huyo kwenye biashara ya madini?”

“Aliwahi kushiriikiana naye na kisha walifarakana. Tunadhani walidhulumiana mali na waliwekeana visasi kwa sababu pamoja na  urafiki wao, hivi sasa wana uhasama”

“Mosha  namfahamu sana, ana gesti yake ambayo pia ni maarufu”

“Gesti yake tumeshaiona. Tunataka kukupa taarifa kuwa tupo hapa kikazi. Kama tutahitaji msaada wako tutakuarifu”

“Sawa. Hakuna tatizo”

“Sasa  acha twende  tukaonane naye”

“Labda niwape askari muwe nao?”

“Tukihitaji  msaada huo tutakuwambia”

“Sawa”

Makachero hao wakatoka. Walikwenda katika gesti ya Mosha wakashuka kwenye gari. Vile ambavyo walivaa kiraia na gari walilotumia lilikuwa na  namba za kiraia, hakukuwa na mtu yeyote aliyewatambua kuwa ni makachero.