Mauaji ya kutisha - Sehemu ya 13
UTANGULIZI
Majambazi hao wakagundua kuwa walikuwa wamevamiwa na polisi ingawa hawakujua idadi ya polisi hao. Hivyo walitoka vyumbani mwao wakiwa na wanawake zao na kwenda kujificha jikoni.
Walipowaona askari hao wakiingia vyumbani ndipo walipojitokeza na kuwashambulia kwa bunduki walizokuwa wamejichumbia nazo jikoni.
Polisi walioruka ukuta na kuingia uani walikuta nyumba nyingine ndogo iliyojengwa nyuma ya nyumba ile. Polisi hao walishangaa kuona taa zikiwaka kupitia kwenye madirisha hali iliyoonesha kuwa kulikuwa na watu wengine katika nyumba hiyo..”
SASA ENDELEA...
WAKATI risasi zilipoanza kusikika kutoka ndani ya nyumba kubwa, taa zilizimwa katika nyumba iliyokuwa uani na midomo ya bunduki ikapenyezwa kutokea katika madirisha. Polisi hao wakaanza kushambuliwa.
Polisi wawili walipigwa risasi na kufa hapo hapo huku polisi wengine wakiendelea kujibizana kwa risasi na watu waliokuwa ndani ya nyumba hiyo. Polisi walipiga risasi za mfululizo kwenye madirisha na kwenye mlango ambao ulifunguka na kuwa wazi.
Humo ndani Inspekta Amour na wenzake waliokuwa ndani ya vile vyumba walijibizana kwa risasi na majambazi walioanza kuwashambulia. Amour aliyekuwa ameshika bastola alikoswakoswa na risasi mbili za bunduki ambazo zilipiga kwenye mlango, akarudi nyuma kabla ya kutokeza tena kidogo na kushambulia.
Polisi mwenzake aliyekuwa katika chumba kingine alipigwa risasi akafa hapo hapo.
Mapambano yalipamba moto. Risasi zikarindima kutoka pande zote. Amour alifanikiwa kuwaua majambazi wawili hapo hapo. Mwanamke mmoja naye alipigwa risasi na kufa hapo hapo.
Huko uani mbali ya polisi wawili kuuawa kwanza, jambazi mmoja naye aliuawa. Ndani ya nyumba hiyo kulikuwa na majambazi wawili. Baada ya jambazi mmoja kuuawa, mwingine alikamatwa akiwa amejeruhiwa kwa risasi ya kifuani.
Humo ndani jambazi mmoja aliyebaki hai akiwa amejeruhiwa kwa risasi ya tumbo alikamatwa pamoja na wanawake wawili waliosalimika.
Amour alipiga simu makao ya polisi na kuelezea kuhusu tukio hilo. Dakika chache tu baadaye magari matatu ya polisi na polisi kadhaa wakawasili mahali hapo.
Polisi waliouawa pamoja na majambazi walipakiwa kwenye gari na kupelekwa hospitali ya Muhimbili. Katika gari jingine walipakiwa majambazi waliojeruhiwa pamoja na wanawake wawili waliosalimika.
Hakukuwa na polisi wala kachero yeyote aliyejeruhiwa. Polisi wanne wakaachwa kuilinda nyumba hiyo.
Majambazi waliojeruhiwa walikimbizwa hospitali huku jambazi aliyewapeleka polisi hao akilaumiwa kwa kutotoa maelezo sahihi, jambo ambalo lilisababisha polisi wawili kuuawa.
Wale wanawake wawili waliokamatwa walikwenda kuwekwa mahabusi.
Usiku huo huo majambazi hao wakiwa wamelazwa katika chumba cha hospitali wakitibiwa, Inspekta Amour alianza kuwahoji.
Baada ya kubanwa kwa maswali, majambazi hao walikiri kujihusisha na ujambazi katika matukio mbali mbali jijini Dar.
Jambazi mmoja alikiri kuwa walihusika katika ujambazi uliotokea Mikocheni na Sinza uliotoa roho za Martin na James.
Aliwambia polisi kuwa matukio hayo waliyafanya wao wakitumia dawa za kichawi wanazopewa na mganga mmoja wa kienyeji aliyekuwa Bagamoyo.
Asubuhi kulipokucha Amour na makachero wenzake walikwenda katika nyumba iliyokutwa majambazi hao kufanya upekuzi. Walikuta jumla ya shilingi milioni ishirini zikiwa kwenye makabati na dola za Kimarekani zenye thamani ya shilingi milioni nane.
Pia walikuta kisanduku cha shaba kilichokuwa na mapambo ya dhahabu ya wanawake. Amour alifikiria kwamba huenda dhahabu hizo ndizo zilizoibiwa nyumbani kwa James baada ya mwenyewe kuuawa.
Kutokana na maelezo ambayo Amour aliyapata kutoka kwa Almasi, masanduku yaliyoibiwa nyumbani kwa James yalikuwa na mapambo ya dhahabu pamoja na vitu vinginne vya harusi.
Baada ya kukamata pesa hizo pamoja na mapambo ya dhahabu, Amour na wenzake walirudi makao ya polisi kabla ya kutoka tena kuelekea Bagamoyo kwa mganga aliyetajwa na majambazi waliokamatwa.
Walipofika katika mji huo wa kale, makachero hao walifanikiwa kuigundua nyumba ya mganga huyo ambaye alikamatwa na kufikishwa hospitali ya Muhimbili.
Walikuta jambazi mmoja miongoni mwa wale waliokamatwa ameshakufa. Jambazi aliyebaki akamtambua yule mganga.
Baada ya mganga huyo kutambuliwa alifikishwa makao ya polisi ambako alitakiwa aeleze ni kwanini amekuwa akiwafanyia dawa majambazi wakati akijua kuwa watakwenda kuiba na kuua watu.
“Nimekuwa nikiwadanganya tu. Mimi sina dawa yoyote ya ujambazi.” Mganga akajitetea.
“Kwa hiyo unakiri kwamba umekuwa ukiwafanyia kweli lakini ulikuwa unawadanganya?” Amour akamuuliza.
“Ndiyo.”
“Na ni kwanini unafanya hivyo?’
“Nafanya hivyo ili kujipatia riziki lakini dawa ninazowapa hazisaidii chochote.”
“Unasema kwamba dawa unazowapa hazisaidii chochote, mbona wanafanikiwa kupora pesa za watu na kuua watu?”
“Ni wao wenyewe, sio dawa zangu.”
“Wewe si ndio unawapa moyo kutokana na dawa unazowapa?”
“Hapana.”
“Mzee unaonekana mtu wa maana, kumbe bure kabisa. Unawashawishi vijana kufanya ujambazi!”
“Sijashawishi kijana yeyote, wanakuja wenyewe.”
“Wale majambazi wamekiri kuhusika na matukio ya ujambazi wa watu wawili ambapo katika tukio la kwanza walimchinja mtu na kupora fedha. Katika tukio la pili walichinja mtu tena na kuiba masanduku. Lakini baada ya matukio hayo walitoweka kimiujiza. Unawapa uchawi gani?”
Mganga alipoulizwa swali hilo alitikisa kichwa.
“Siwapi uchawi wowote.”
“Kwanini wanapofanya uhalifu wao wanatoweka mbele ya macho ya watu?”
Mganga akabetua mabega yake. “Sijui.”
Amour alitaka kumtandika kibao lakini alimuheshimu kwa kuona alikuwa mtu mzima.
“Usijaribu kutuficha kitu. Tueleze ni kitu gani unawapa?” akamuuliza kwa ukali.
“Mimi nafikiri kuna mganga mwingine anayewapa dawa za uchawi. Mimi sina dawa za uchawi.”
“Wamekutaja wewe. Hawakutaja mtu mwingine.”
“Mimi siwappi dawa za uchawi. Kusema ukweli mimi nawadanganya tu nipate riziki yangu.”
“Unasema unawadanganya wakati wao wanafanya uhalifu na wanafanikiwa. Unajua mnatusumbua sana nyinyi!”
Mganga akanyamaza kimya.
“Ni lazima tutakufungulia kesi tu. Wewe na wao nyote ni majambazi tu.”
Mganga aliinamisha kichwa chake kisha akasema kwa sauti ndogo. “Mimi sidhani kama mahakama inaamini uchawi.”
“Eti nini…!” Amour akamuuliza akiwa ameukunja uso wake kisha akaongeza.
“Unajifanya wewe unajua zaidi sheria kuliko sisi? Wewe huoni kama unawachochea kwa kuwapa moyo wafanye uhalifu kutokana na dawa zako. Sasa hata kama mahakama haiamini uchawi tutakupeleka kwa sababu unalo kosa la kujibu.”
Mganga akaamua kubaki kimya. Baada ya kumuhoji mganga huyo Amour alitaka apelekewe mmoja wa wale wanawake waliokamatwa na majambazi hao.
Mwanamke aliyepelekwa kwake alijitaja kwa jina la Regina. “Una umri gani?” Amour akamuuliza.
“Miaka ishirini na minane?”
“Bwana wako ni nani katika wale majambazi watatu?”
“Ni Jex.”
Jex alikuwa ni mmoja wa majambazi waliolazwa hospitali.
“Na wewe ni jambazi?”
“Hapana. Mimi si jambazi na nilikuwa sijui kama yeye ni jambazi.”
“Mlianza lini uhusiano wenu?”
“Kama wiki moja iliyopita.”
“Mlikutana wapi?”
“Baa. Alikuja kunywa akanikuta pale akaniambia amenipenda.”
“Huo ni uongo mtupu unaoueleza hapa! Hili kundi la majambazi umekuwa nalo kwa muda mrefu. Ninachotaka uniambie umeshashiriki katika matukio mangapi ya uhalifu hapa Dar?”
“Mimi ninakueleza ukweli jamani. Sijakuwa na hawa watu kwa muda mrefu. Nimemjua yule bwana juzi juzi tu.”
Amour alimtazama mwanamke huyo kwa utulivu kisha akamuamuru.
“Kaa pale chini.”
Mwanamke huyo alikwenda kukaa chini mahali alipooneshwa. Amour akaagiza apelekwe mwanamke mwingine.
Huyu wa pili ambaye alimwambia Amour anaitwa Mage alikiri kila kitu.
“Mwanaume wako ni nani?’
“Ni Jackson Lambunya”
Lambunya alikuwa mmoja wa majambazi waliouawa.
“Ni mmoja wa wale waliouawa?’
“Ndiyo”
“Uliishi na yule mtu kwa miaka mingapi?”
“Miaka miwili.”
“Na wewe ulikuwa ukishiriki katika vitendo vya ujambazi?’
“Alikuwa akienda peke yake.”
“Katika siku za hivi karibuni waliwahi kufanya matukio mangapi ya ujambazi?”
“Mimi sijui. Ninawaona wakitoka tu na kurudi.”
“Hujawahi kwenda nao hata siku moja?”
“Sijawahi ila nilikuwa nikimkataza lakini alikuwa hasikii.”
“Tumeambiwa kuwa walikuwa wanakwenda kwa waganga. Wewe unalijua hilo?’
“Ndiyo ninajua.”
“Uliwahi kwenda nao?’
“Ndiyo.”
“Wapi?”
“Bagamoyo.”
“Walikuwa wanakwenda kwa huyo mganga kufanya nini?”
“Yule mganga alikuwa anawapa dawa ili wanapofanya ujambazi wasikamatwe na polisi.”
“Alikuwa anawapa na dawa gani nyingine?’
“Ni hizo hizo tu za kufanikisha ujambazi wao.”
“Huyo mganga unamfahamu vizuri?”
“Ndiyo namfahamu.”
“Ukimuona unaweza kumtambua?”
“Ndiyo naweza kumtambua.”
“Sawa. Hebu mtazame yule mtu aliyekaa pale chini.”
Amour alimuonesha yule mganga kisha akamuuliza.
“Unamjua yule?”
Mwanamke huyo baada ya kumtazama mganga huyo alisema.
“Ndiyo namjua.”