Mauaji ya kutisha – Sehemu ya 12
UTANGULIZI
“Huu uchunguzi ni mgumu kidogo kwa sababu haya mauaji yametokea katika mtindo tofauti. Isitoshe wauaji ni watu wanaoshitukizia na kutoweka ghafla. Ninahitaji muda wa kutosha kuweza kuwagundua na kuwanasa watu hawa.”
“Unadhani nikupe muda gani ambao utakutosha kukamilisha uchunguzi wako?”
Amour alifikiri kidogo kisha akasema.
“Nipe angalau wiki mbili.”
SASA ENDELEA...
“Sawa ninakupa wiki mbili. Kumbuka kwamba huo uchnguzi unasubiriwa na wakubwa. Kitendo cha wewe kufanikiwa kuwapata au kutowapata wauaji hao kitakujenga wewe au kukubomoa.”
“Sawa afande. Nimekuelewa.”
Wakati Amour anatoka ofisini kwa mkurugenzi wa upelelezi, simu yake ya mkononi ikaita.
Aliipokea simu huku akishuka ngazi.
“Hello…!”
“Afande unaongea na Sajenti Isaya wa kituo cha kati. Nipo katika hospitali ya Mwananyamala. Kuna jambazi amepigwa risasi na amekamatwa.Anatibiwa hapa. Tunataka uje umuone.”
“Ana nini?”
“Wakati tunamhoji ametoa maelezo ya kuhusika na wale majambazi wanaotafutwa ambao walifanya mauaji Mikocheni na Sinza.”
“Ninakuja…ninakuja…”
Amour aliirudisha simu mfukoni akashuka ngazi haraka haraka na kutoka nje ya jengo hilo la makao ya polisi.
Alijipakia kwenye gari lake akaliwasha na kuondoka. Dakika kadhaa baadaye alilisimamisha gari hilo katika eneo la kuegesha la hospitali ya Mwananyamala ambako alikuta gari la polisi likiwa nje.
Alishuka kwenye gari na kuingia katika jengo hilo huku akipishana na watu mbalimbali wakiwemo wauguzi waliokuwa wakitoka na kuingia.
Kwa msaada wa muuguzi mmoja Amour alipelekwa katika chumba ambacho kulikuwa na jambazi aliyekuwa akitibiwa. Katika chumba hicho Amour alikuta polisi wanne na makachero wawili. Alimkuta pia jambazi aliyekuwa amelazwa kwenye kitanda baada ya kutolewa risasi aliyopigwa mguuni.
Sajenti Isaya aliyekuwa mmoja wa wale makachero alimwambia Amour kuwa jambazi aliyekuwa na maelezo kuhusu watu watatu waliokuwa wanatafutwa kwa mauaji ya Martin na James, alikuwa ndiye yule aliyelazwa.
Amour aliambiwa kwamba jambazi huyo alipigwa risasi wakati yeye na wenzake wawili waliouawa walipokuwa wakijaribu kupora gari la mtu mmoja mwenye asili ya kiasia katika maeneo ya Mbezi.
“Katika kumhoji maswali amesema anawafahamu majambazi watatu waliohusika na na mauaji yaliyotokea Mikocheni na Sinza. Kama sikosei yaliwahusu wanandugu Martin na James.” Sajenti Isaya alimwambia Amour.
“Ni habari ambayo ninaihitaji sana.” Amour alisema kisha akakisogelea kitanda alicholazwa jambazi huyo.
“Unaitwa nani?” Akamuuliza.
“Naitwa Simon Puto.” jambazi huyo alimjibu huku akikunja uso kuonnesha kuwa alikuwa akisikia maumivu ya risasi.
“Hebu nieleze jinsi unavyowafahamu wale wauaji wa Mikocheni na Sinza.”
“Si wale jamaa ambao wanavaa nguo nyeupe na nyeusi?”
“Ndio hao hao.”
“Wale nawafahamu sana. Wale wanafanya ujambazi kwa kutumia nguvu za kiza.”
“Ndiyo.”
“Wanafuata masharti ya mganga.”
“Tunaweza kuwapataje?”
“Wamekodisha nyumba nzima Buguruni, wanaishi na mabibi zao.”
“Tutawapataje?”
“Wanapatikana, hawana ujanja. Mimi nitawaelekeza nyumba wanayoishi.”
“Una uhakika kwamba tutawapata?”
“Hii leo nilikuwa nao.”
“Ulikuwa nao mkipanga kitu gani?”
“Ni kawaida tunakutana kubadilishana mawazo.”
“Tutakuomba kwa daktari utupeleke hapo wanapoishi.”
“Mimi naona mwende wenyewe. Nikiwaelekeza nyumba hamtapotea.”
“Hapana. Tutakwenda na wewe.”
“Sasa niwambie kitu, kwa muda huu hamuwezi kupata mtu. Lakini saa kumi alfajiri nina uhakika kuwa mtaweza kuwakamata.”
“Sawa. Hebu tuambie wako wangapi katika hiyo nyumba?”
“Wanaishi watu watatu na mabibi zao.”
“Na ndio hao hao tunaowatafuta?”
“Ndio hao hao.”
“Wana silaha za aina gani?”
“Sijui.”
Amour akakunja uso.
“Usilete utani kwenye kazi!”
“Nasema kweli kuwa sijui wana silaha gani.”
Amour akawageukia wale polisi.
“Huyu awekwe chini ya ulinzi mkali sana hadi hiyo saa kumi alfajiri tutakapokuja kumchukua atupeleke huko Buguruni.”
“Atawekwa chini ya ulinzi mkali, hakuna tatizo afande. Naamini umepata maelezo ya kutosha.”
“Kama maelezo yake yatakuwa na ukweli atakuwa ametusaidia sana.”
Lile jambazi likajifanya linacheka.
“Afande usiwe na wasiwasi, hao jamaa utawakamata tu. Mbali na hao, mbona kuna wengi tu ninawafahamu.”
“Tuanze na hao kwanza.”
“Sawa afande, usijali.”
Amour aliwaaga wale polisi na kutoka. Akiwa nje ya hospitali alijipakia kwenye gari lake na kuondoka
Huku akiendesha gari hilo kwa mwendo wa taratibu, Amour alianza kupata faraja ya moyo. Tatizo lililokuwa likisumbua akili yake sasa lilikuwa likielekea kupata ufumbuzi.
Alijiambia kama atafanikiwa kuwakamata majambazi hao atakuwa amejiondolea lawama kwa Mkurugenzi wa Upelelezi.
Alikumbuka maneno aliyoambiwa kwamba kufanikiwa au kutofanikiwa kuwapata majambazi hao ndiko kutakako mjenga au kumbomoa.
“Kama nitafanikiwa kuwakamata, tukio hilo litakuwa limenijenga.” Alijiambia kimoyo moyo.
Sasa aliamini ile dhana yake kwamba wauaji hao hutumia nguvu za kiza kama alivyoambiwa na jambazi aliyekamatwa.
Kitendo cha kuvaa nguo za ajabu ajabu huku mmoja wao akionekana kama amechinjwa na kitendo cha kutoweka ghafla mbele ya macho ya watu, vinaashiria kuwa majambazi hao hutumia nguvu za kiza, akajiambia.
Kesho asubuhi nitakwenda kwa mkurugenzi wa upelelezi nikiwa na taarifa ya kupendeza, aliendelea kujiambia.
Majira ya saa tisa na nusu usiku magari mawili ya polisi yalisimama mbele ya lango la kuingiilia katika hospitali ya Mwananyamala.
Katika gari la kwanza ambalo lilikuwa likitumiwa na polisi kulikuwa na polisi sita waliokuwa na bunduki kila mmoja. Ndani ya gari la pili ambalo lilikuwa la idara ya upelelezi kulikuwa na makachero sita akiwemo Inspekta Amour. Kila mmoja alikuwa na bastola yake ndani ya koti. Hakukuwa na askari yeyote aliyeshuka zaidi ya Inspekta Amour. Aliingia ndani ya hospitali hiyo na baada ya muda mfupi alitoka akiwa na jambazi aliyekuwa akitibiwa mguu uliokuwa umepigwa risasi na polisi.
Polisi aliyekuwa akimlinda jambazi huyo alikuwa akiwafuata kwa nyuma na bunduki yake.
Jambazi huyo alipakiwa kwenye gari hilo la idara ya upelelezi ambalo lilitangulia kuondoka likafuatia gari la polisi.
Msafara huo ulienda hadi Buguruni. Ilikuwa ni katika mtaa mmoja wa Buguruni Malapa ndipo magari hayo yaliposimama mbele ya nyumba moja ambayo jambazi aliyepakiwa kutoka hospitali ya Mwananyamala aliwaeleza makachero hao kuwa nyumba hiyo ndiyo iliyokuwa ikiishi majambazi watatu waliokuwa wanatafutwa.
“Una uhakika kwamba hivi sasa wamo ndani?” Amour akamuuliza jambazi aliyekuwa amepakiwa.
“Watakuwa wamo. Wanaishi katika nyumba hii.” Jamabzi hilo likajibu.
“Umesema wako watu wangapi?”
“Wako watatu pamoja na mabibi zao.”
“Jumla kutakuwa na watu sita au siyo?”
“Watakuwa sita.”
“Wana silaha gani?”
“Watakuwa na bunduki.”
“Bunduki ngapi?”
“Hapo siwezi kujua.”
“Majambazi wa siku hizi hutumia pia mabomu.”
“Sidhani kama wao watakuwa na mabomu.”
“Sasa tuambie ramani ya nyumba hii kwa ndani ikoje?’
“Hii nyumba ni kubwa lakini ina vyumba vinne tu na sebule moja. Ukiingia unatokea kwenye sebule. Upande wa kushoto wa sebule kuna chumba kimoja. Anaishi mtu mmoja. Ukiivuka sebule kuna vyumba viwili, pia viko mkono wa kushoto.”
Makachero hao pamoja na polisi walishuka kwenye magari wakawa wanajipanga na kujadiliana. Jambazi aliachwa kwenye gari akilindwa na polisi mmoja.
Baada ya majadiliano yaliyochukua kama robo saa hivi, nyumba hiyo ilizingirwa na makachero pamoja polisi. Polisi wanne waliruka ukuta na kutumbukia ndani ambako waliizunguka nyumba kwa upande wa ndani.
Mlango wa mbele wa nyumba hiyo ulivunjwa kwa risasi mbili. Polisi watatu na makachero wawili akiwemo Inspekta Amour wakaingia ndani haraka haraka wakiwa na silaha zao mkononi.
Wote walikimbilia kwenye milango ya vyumba vitatu vilivyokuwa upande wa kushoto kama walivyoelekezwa na jambazi waliyekwenda naye kuwaonesha nyumba hiyo.
Walipoijaribu ile milango waliona inafunguka. Wakaifungua kwa kushitukizia huku bastola na bunduki zikitangulia.
Pamoja na kutegemea kuwakuta majambazi hao vyumbani humo, vyumba hivyo havikuwa na watu ingawa taa zilikuwa zinawaka.
Wamekwenda wapi? Polisi na makachero hao wakajiuliza.
Kumbe wale polisi walipokuwa wameruka ukuta na kuingia uani walionekana na majambazi hao waliokuwa wakiwachungulia kwenye madirisha.
Majambazi hao wakagundua kuwa walikuwa wamevamiwa na polisi ingawa hawakujua idadi ya polisi hao. Hivyo walitoka vyumbani mwao wakiwa na wanawake zao na kwenda kujificha jikoni.
Walipowaona askari hao wakiingia vyumbani ndipo walipojitokeza na kuwashambulia kwa bunduki walizokuwa wamejichumbia nazo jikoni.
Polisi walioruka ukuta na kuingia uani walikuta nyumba nyingine ndogo iliyojengwa nyuma ya nyumba ile. Polisi hao walishangaa kuona taa zikiwaka kupitia kwenye madirisha hali iliyoonesha kuwa kulikuwa na watu wengine katika nyumba hiyo.
Itaendelea kesho...