Mauaji ya kutisha – Sehemu ya 11
Muktasari:
- “Tukio lile la kaka Martin na lile la juzi yana tofauti. Majambazi walimuua kaka na kumpora mamilioni ya pesa. Lakini kaka John ameuawa na kilichoibiwa hakijulikani!” Akasema Alex.
“Tukio lile la kaka Martin na lile la juzi yana tofauti. Majambazi walimuua kaka na kumpora mamilioni ya pesa. Lakini kaka John ameuawa na kilichoibiwa hakijulikani!” Akasema Alex.
“Si wamepora masanduku yake.” Benjamin akamjibu.
“Sidhani kama wale majambazi walikuja nyumbani kwa kaka kufuata yale masanduku.”
“Kwanini hudhani wakati ndio waliyoyaiba baada ya kumuua?” Alex akamuuliza..
SASA ENDELEA...
“HIVI katika masanduku yale kulikuwa na vitu vyenye thamani kubwa kiasi cha majambazi hao kutoa roho ya mtu?”
“Majambazi hawathamini uhai wa mtu. Wanaweza kukutoa roho kwa kitu kidogo tu.”
“Lakini mkumbuke kwamba majambazi hao ndio wale wale waliomuua marehemu Martin?” Almasi akawakumbusha.
“Sasa baba swali ambalo ninataka kukuuliza, hivi walikuwa wanajua kwamba James waliyemuua alikuwa mdogo wake Martin ambaye walimuua kwamza?” Benjamin akauliza.
“Sina hakika lakini nadhani walikuwa wanajua na ndio sababu nikawauliza kwanza, ni kwanini majabazi hao wameniandama mimi?”
“Labda baba tujadili jinsi ya kujilinda na watu hao kwa mara nyingine.” John akasema.
“Labda tuongeze ulinzi. Nyumba zetu ziwe na walinzi wawili badala ya mmoja na sisi wenyewe tutembee na walinzi,” akasema Almasi.
“Kuongeza walinzi wa nyumbbani inawezekana lakini kuwa na walinzi tunaotembea nao itatugharimu sana,” Alex akasema.
“Kwani baba polisi wanafanya kazi gani. Mimi ninachofahamu kazi ya polisi ni kulinda usalama wa raia na mali zao!” Benjamin alisema na kuwatazama wenzake kwa zamu.
“Ni kweli lakini polisi hawawezi kumlinda kila mtu na mali yake. Jukumu la kwanza la ulinzi ni lako mwenyewe. Polisi anakuwa msaada tu,” Almasi aliwaambia.
“Sasa baba katika hali kama hiyo tutajilinda vipi?”
“Hili sasa limekuwa ni tatizo kwetu. Inabidi tuombe Mungu atuepushe na balaa hili. Suala hili tutalijadili baadaye. Kwa sasa nilichokuwa ninataka kuwambia ni kwamba kaka yenu ambaye ndiye aliyekuwa mhasibu wangu ameshafariki. Sasa tutafanyaje?’
“Itabidi uajiri mhasibu mwingine,” John akamjibu.
“Na inabidi niajiri mhasibu mwingine kwa sababu miongoni mwenu hakuna aliyesomea uhasibu. Si ndiyo?”
“Ndiyo baba. Kwa mfano kama mimi ningesomea uhasibu ningechukua nafasi yake,” John akasema.
“Ni kweli. Na sitaki kuuacha uongozi wa kiwanda changu bila ya nyinyi. Kwa maana hiyo John sasa utakuwa meneja. Meneja aliyepo nitamhamishia katika kiwanda changu cha uchapaji. Wewe utamsimamia mhasibu ambaye nitamuajiri. Mnaonaje mawazo yangu?”
Almasi akawatazama wanawe kwa zamu.
“Nyinyi wengine hamjatoa mchango wenu,” akawambia.
“Hivyo ulivyoamua baba ni sawa. Kaka awe meneja. Hatuwezi kuweka meneja na mhasibu wake tukawaacha wafanye watakavo wao,” Benjamin akasema.
“John unasemaje?”
“Baba ninaukubali huo uteuzi. Nitakuwa meneja wakati utakapoajiri mhasibu mwingine.”
“Alex unakubaliana na hayo?”
“Ninakubaliana baba. Ni mawazo mazuri.”
“Sawa.”
“Sasa kuanzia kesho ninamhamisha meneja wetu kwenye kiwanda cha uchapaji. John utachukua nafasi yake. Kesho hiyo hiyo nitatoa tangazo la ajira.”
“Sawa.” John akamkubalia.
Mambo yalikwenda kama yalivopangwa. Siku iliyofuata Almasi alimpa uhamisho meneja wa kiwanda chake cha maji safi kwenda katika kiwanda kingine cha uchapaji ambacho pia kilikuwa kinamiliiwa na Almasi.
John akaanza kazi ya umeneja katika kiwanda hicho. Siku hiyo hiyo Almasi alipeleka tangazo la nafasi ya kazi ya uhasibu, tangazo ambalo lilitoka katika vyombo vya habari siku ya tatu yake.
Baada ya tangazo hilo kutoka, Almasi alipokea mamia ya barua ya waomba kazi. Almasi na wanawe walizichambua barua hizo na kukubaliana na waombaji watatu ambao waliwaita.
Katika usaili, muombaji mmoja ndiye aliyefanikiwa kupata kazi ya uhasibu. Akapata ajira katika kiwanda cha Almasi.
Juma moja baada ya maziko ya James, Almasi alikwenda kwa mkuu wa jeshi la polisi kumlalamikia.
“Kilichonileta hapa ni kulalamika juu ya matukio ambayo yamekuwa yakinitokea mimi na familia yangu. Tunaambiwa kwamba jukumu la polisi ni kulinda usalama wa raia na mali zao lakini kwangu mimi inaonekana sivyo. Wanangu wawili wameshauawa na kiasi kikubwa cha pesa kimeibiwa. Sijapata msaada wowote wa polisi.” Almasi alimwambia mkuu wa jeshi la polisi.
“Ninalifahamu tatizo lako. Kwanza ninakupa pole kutokana na tatizo hilo. Ni kweli kwamba jukumu la polisi ni kulinda usalama wa raia na mali zao lakini bado polisi ni binaadamu na tuko wachache kuliko ilivyohitajika. Tunahitaji sana msaada wa raia wema. Nataka kwanza ulielewe hilo.”
Almasi alinyamza kimya lakini macho yake yaliyokuwa yakimtazama mkuu huyo wa polisi yalikuwa na mengi.
“Kingine ambacho nataka kukueleza ni kwamba bado polisi wanaendelea na uchunguzi kuhusu matukio yale ya ujambazi yaliyokutokea. Uchunguzi unaweza kuchukua muda mrefu lakini unakuwa na matokeo.”
“Ninafahamu lakini ninauliza, je polisi itanilindaje mimi dhidi ya matukio mengine kama yale?’ Almasi akauliza.
“Polisi haiwezi kumlinda kila mtu. Watu ni wengi kuliko polisi. Siku hizi kuna sheria ya kuajiri walinzi. Kama una wasiwasi unaweza kuajiri walinzi wako binafasi.”
“Ninao walinzi nyumbani, viwandani kwangu lakini bado hali inatia wasiwasi.”
“Nataka kukudokeza tu kwamba tumeanzisha operesheni kabambe ya kutokomeza ujambazi katika jiji hili. Kama tutafanikiwa na ninaamini kuwa tutafanikiwa, hali ya Dar es Salaam itakuwa ni salama kabisa.”
“Hiyo operesheni itaanza lini?”
“Imeshaanza na taarifa mbalimbali za majambazi utazisikia.”
“Sawa. Mimi nawaombea Mungu mfanikiwe ili jiji letu liwe na usalama wa kutosha.”
Baada ya Almasi kuondoka kwa mkuu wa jeshi la polisi, mkuu huyo alimpigia simu mkurugenzi wa upelelezi.
“Nini kinaendelea ofisini kwako?” Akamuuliza.
Mkurugenzi wa upeleleiz hakuwa na jibu la moja kwa moja.
“Kuna kazi tu za kawaida afande.”
“Uchunguzi wa matukio ya ujammbazi yaliyotokea kwa Bwana Almasi na wanawe umefikia wapi?”
“Uchunguzi ule bado unaendelea…”
Mkuu wa jeshi la polisi akamkatiza.
“Najua unaendelea. Nataka kujua umefikia wapi?”
“Sijapata taarifa kutoka kwa mpelelezaji ambaye ni Inspekta Amour.”
“Sasa nataka nipate taarifa yake kabla ya saa sita. Sawa?”
“Sawa afande.”
Mara tu baada ya mkuu wa polisi kukata simu, mkurugenzi wa upelelezi alimpigia Inspekta Amour.
“Inspekta ule uchunguzi wako umefikia wapi?”
“Kuhusu nini?”
“Kuhusu yule kijana aliyechinjwa kule Mikocheni na yule aliyechinjwa juzi nyumbani kwake.”
“Bado ninaendelea na uchunguzi huo.”
“Bado hujawakamata wale waliohusika?’
“Kwa kweli sijawagundua bado.”
“Inaonekana kama hufanyi kazi Inspekta. Matokeo ya uchunguzi huo yanatakiwa na mkuu wa polisi. Utamueleza nini?”
Inspekta akanyamaza kimya.
“Hebu njoo ofisini kwangu sasa hivi. Njoo na hilo jalada la uchunguzi wako.”
“Sawa afande.”
Amour alipouweka mkono wa simu chini alitikisa kichwa chake kusikitika. Alijiuliza atakwenda kumueleza nini bosi wake kuhusiana na uchunguzi huo?
Mpaka wakati huo jalada lenye uchungzui huo halikuwa na taarifa ya kutosheleza. Hakukuwa na watuhumiwa wowote waliokamatwa. Na jalada hilo halikuwa na maelezo yoyote yanayoonesha kama kulikuwa na washukiwa wowote.
Uchunguzi wa kipolisi uliokamilika ni lazima uoneshe kosa linalochunguzwa, uoneshe washukiwa, uoneshe watu waliokamatwa kuhusiana na kosa hilo na pia uoneshe ushahidi.
Hivyo ndivyo vipengele muhimu katika uchungzi wowote ule wa polisi. Jalada la Amour mbali ya kuonesha makosa yanayochunguzwa pamoja na kuwa na maelezo ya mashuhuda, halikuwa na kingine chochote cha maana. Hata kama atalipeleka kwa mkurugenzi wa upelelezi halitasaidia kitu.
Hata hivyo kwa vile alishaagizwa afike kwa mkurugenzi huyo na afike na jalada hilo, Amour hakuwa na kingine zaidi ya kutii amriya mkuu wake. Na hiyo ndiyo nidhamu ya kazi yoyote ya kiaskari, kutii amri za mkubwa wao.
Dakika chache baadaye, Amour alibisha kwenye mlango wa ofisi ya mkurugenzi wa upelelezi kabla ya kuingia ndani.
Mkurugenzi aliyekuwa amesimama kando ya dirisha akitazama mandhari ya nje alirudi kwenye kiti na kumwambia Amour.
“karibu kiti”
Amour alikaa kwenye kiti kilichokuwa mbele ya meza.
“Umeniletea jalada nililokuagiza?”
“Ndiyo afande, hili hapa.”
Amour aliliweka juu ya meza.
Mkurugenzi alilifungua na kulisoma. Alilisoma kwa kuruka ruka mistari ili awahi kulimaliza.
“Naona maelezo ya mashuhuda tu. Uchunguzi wako uko wapi?” Mkurugenzi akamuuliza.
“Kama nilivyokueleza kwenye simu bado ninaendelea na uchunguzi. Uchunguzi wangu ukikamilika nitakuwa na maelezo ya kutosha?”
“Kitu gani kinachelewesha uchunguzi wako?”
“Huu uchunguzi ni mgumu kidogo kwa sababu haya mauaji yametokea katika mtindo tofauti. Isitoshe wauaji ni watu wanaoshitukizia na kutoweka ghafla. Ninahitaji muda wa kutosha kuweza kuwagundua na kuwanasa watu hawa.”
“Unadhani nikupe muda gani ambao utakutosha kukamilisha uchunguzi wako?”
Amour alifikiri kidogo kisha akasema.
“Nipe angalau wiki mbili.”