Mauaji ya kutisha – Sehemu ya 10
UTANGULIZI
“Amesemaje?”
Almasi alimueleza mke wake mkasa mzima uliotokea bila kumficha lolote.
Mke wa Almasi aliangua kilio kikali.
Huku majonzi na huzuni vikiwa vimetawala kwenye nyumba ya Almasi, Almasi aliwapigia simu watoto wake wote. Aliwaamsha usingizini na kuwambia wafike nyumbani kwake haraka.
SASA ENDELEA...
Kwanza alimpigia John. John alipoamka alimwambia kuwa anamuita nyumbani kwake.
Baada ya kumpigia John, alimpigia Alex. Naye akamwambia hivyo hivyo.
Alex akamfahamisha Benjamin aliyekuwa akiishi naye nyumba moja.
Licha ya John na Alex kumuuliza baba yao kulikoni, hakuna yeyote aliyeambiwa kitu gani kilikuwa kimetokea.
Aliyefika kwanza nyumbani kwa Almasi alikuwa John ambaye alikuwa mtoto wa tatu wa Almasi. Yeye alikuwa akiishi peke yake katika nyumba yake iliyokuwa Oysterbay. Alex na Benjamin walikuwa wakiishi katika nyumba moja iliyokuwa Mikocheni.
John alipofika aliikuta ile hali ya huzuni ambayo ilimshitua. Mama yake alikuwa akiendelea kulia huku baba yake akiwa ameshika simu akiwapigia ndugu na jamaa.
“Mama kumetokea nini?” John akauliza kwa mshituko.
Aliacha kumuuliza baba yake aliyekuwa amemuita kwa sababu alikuwa akiongea kwenye simu, akaona amuulize mama yake.
Kwa kutaka kumueleza mwanawe huyo nini kimetokea, mwanamke huyo aliacha kulia.
“Kaka yako James hatuko naye!” Akamwambia na kuongeza.
“Wanangu tunakabiliwa na kipindi kigumu kwa sababu juzi juzi tu kaka yake naye alitutoka.”
Mshangao wa John ulizidi kusomeka kwenye uso wake.
“Hatuko naye kivipi mama?”
“Hayuko duniani, roho yake imedhulumiwa kama ilivyodhulumiwa ya kaka yake.”
John alikuwa amekaa kwenye kochi akainuka na kumfuata mama yake.
Alijikalisha chini yake na kumuuliza.
“Mama sijakuelewa bado. Niambie kaka amefanya nini?”
Almasi alikuwa ameshamaliza kuzungumza kwenye simu akaingilia yale mazungumzo.
“John ameuawa muda mchache tu uliopita, yamemkuta kama yale yaliyomkuta kaka yake.”
“Jamani kaka ameuawa wapi?”
“Ameuawa nyumbani kwake. Walikuja watu watatu kama wale waliomuua Martin wakam….”
Almasi hakuweza kumaliza kauli yake, machozi yakamtiririka. Akaacha kuzungumza na kujifuta machozi.
Wakati huo Alex na Benjamin walikuwa wanaingia. Na wao wakapatwa na mshangao.
“Kaeni chini.” Almasi aliwambia huku akiwaashiria kwa mkono.
“Wanangu tumepata msiba, kaka yenu John ameshatutoka,” akawambia.
Wote wawili walishituka. Hawakukaa tena.
Alex alimfuata baba yake na Benjamin alimfuata mama yake. Kila mmoja akataka kuelezwa nini kimetokea. Wakati huo John alikuwa akilia.
Baada ya kupata maelezo ya kina ya nini kimetokea, vilio vilitawala kwenye nyumba ya Almasi.
Wakati kunakucha asubuhi, watu mbalimbali waliopelekewa taarifa ya mkasa huo wakaanza kuwasili nyumbani kwa Almasi.
***********
Saa tatu asubuhi, Almasi alisimamisha gari katika eneo la kuegesha magari la makao ya polisi. Alilizima moto akashuka na kutembea kuelekea katika mlango wa kuingilia katika jumba hilo.
Kwa vile ofisi ya Amour alikuwa akiifahamu baada ya kuitwa kwa mara ya kwanza alipouawa mwanawe Martin, alipanda lifti hadi horofa ya tatu ilikokuwa ofisi hiyo.
Alipoingia ofisini humo Inspekta Amour aliwambia.
“Karibu mheshimiwa.”
“Asante. Habari ya asubuhi?”
“Tunashukuru kumekucha salama. Pole kwa matatizo na karibu kiti.”
Almasi alikaa kwenye kiti mbele ya meza ya Amour.
“Yule mlinzi wa nyumba ya marehemu mwanao tumemuweka ndani. Kwa hiyo kwa sasa ninakushauri utafute mlinzi mwingine wa kulinda ile nyumba.” Amour alimwambia Almasi.
“Kwanini mmemuweka ndani?”
“Tumemuweka ndani kwa ajili ya uchunguzi wetu. Kama yeye ndiye mlinzi na kuna mtu ameuawa hapo hapo, tutamshuku nani?”
“Si kuna wauaji waliotoweka na masanduku ya nguo za mwanangu?”
“Maelezo ya yule mlinzi hayaeleweki na yanatia shaka. Inaonekana kama kuna kitu anatuficha.”
“Ni lazima polisi muwe wakweli. Lazima mtambue kuwa liko tatizo. Msije mkawaacha wauaji na kupeleka tuhuma kwa yule kijana. Mtakuwa hamjafanya jambo lolote!” Almasi alisema kwa jazba.
“Huwezi kutufundishs kazi yetu. Sisi tunajua tunafanya nini. Acha tu tumuweke ndani.”
“Hii si mara ya kwanza kwa mwanangu kuuawa. Huyu ni mwanangu wa pili kuuawa na nyinyi wenyewe mmesema kwamba wauaji ni wale wale wa kwanza. Sasa nashangaa unaponiambia kuwa mmemuweka ndani yule mlinzi.”
“Ni kawaida. Kama yeye ni mlinzi wa mahali hapo, halafu kuna mtu anauawa hapo hapo na anashindwa kutupa maelezo ya kutosheleza tutamtuhumu nani?”
“Lakini wauaji si ndio wale wale wa mwanzo?”
“Mzee acha tuendelee na uchunguzi wetu. Uchunguzi utabainisha kila kitu. Usiwe na wasiwasi. Kama tutaona hana kosa tutamuachia. Tafuta mlinzi mwingine kwa sasa.”
“Sawa. Mimi siingilii kazi zenu. Nilikuwa ninatoa mawazo yangu tu.”
“Ninajua. Nadhani nimekuelimisha kuhusu kazi zetu. Sisi polisi tuna sheria zetu na taratibu zetu. Sasa tuliache hilo la mlinzi. Nilitaka kukueleza kwamba tumeshaanza uchunguzi wetu wa kuwatafuta wale watu watatu.”
Almasi alimtazama Amour kwa macho makali kabla ya kumuuliza.
“Ule uchunguzi wa mara ya kwanza uliishia wapi?”
Amour alikwama kujibu. Akaupeleka uso wake kwenye ukuta mmoja wa chumba hicho.
Almasi alikuwa amemtumbulia macho Amour aliyeonekana kupatwa na fadhaa iliyomfanya ainuke kwenye kiti na kuanza kuranda mle ofisini huku uso wake ameuinamisha chini.
“Uchunguzi wa mara ya kwanza bado unaendelea.” Amour akasema akiwa amempa mgongo Almasi akizunguka ofisi yake.
Akaendelea “Uchunguzi ni uchunguzi tu, unaweza kuwa wa muda mfupi au wa muda mrefu. Lakini tunakwenda kidogo kidogo mpaka tunawapata wale watu tunaowatafuta. Wako wahalifu waliofanya uhalifu miaka mitatu iliyopita lakini ghafla tunakuja kuwakamata.” Amour aliendelea kuranda randa.
“Ni rahisi kumkamata mhalifu aliyefanya uhalifu wake siku za nyuma kuliko aliyefanya uhalifu wake hii leo. Mara nyingi yule aliyefanya uhalifu siku za nyuma anakuwa amejisahau. Na anadhani kuwa polisi nao wamemsahau. Kumbe sisi bado tunamtafuta kimya kimya.”
Amour alifika mwisho wa ofisi akageuka tena.
“Kwa hiyo mzee Almasi ninakuhakikishia kuwa hawa watu watakamatwa tu hata kama mwaka mmoja utapita. Najua una wasiwasi, una uchungu lakini ninakutaka uwe na subira. Siku zote nataka ujue kuwa mbio za kipofu uishia kwenye shimo au kukwaa jiwe!”
“Tangu alipouawa mwanangu wa kwanza naona siku zimesonga sana. Polisi hamjanieleza kitu. Mwanangu mwingine naye ameuawa. Mnadhani kweli nitaweza kuwa na subira?” Almasi akasema kwa uchungu.
“Polisi ni binaadamu na uwezo wao ni wa kibinaadamu. Tumechukua muda mrefu lakini bado tuko kwenye uchunguzi. Uchunguzi ule wa kwanza tutauunganisha na uchunguzi huu wa sasa. Ninaamini kuwa hautapita muda mrefu wale watu tutawakamata. Nataka na wewe utuamini.”
Almasi akanyamaza kimya kama vile alikuwa akiyatafakari maneno ya Inspekta Amour.
Katika ukimya huo Amour aliona amemaliza kazi ya kumuelimisha mzee huyo, akarudi kwenye kiti.
Kukaa kwake kukamzindua Almasi.
“Halafu kuna kitu kingine nimekuwa nikijiuliza bila kupata jibu.” Almasi akasema ghafla.
“Kitu gani?”
“Huyu mtu ambaye anaelezwa kuwa shingo yake imechinjwa na kichwa chake kinaning’inia, ni mtu wa aina gani?”
Amour hakujibu kwa haraka.
“Kama nilivyokwambia bado tuko kwenye uchunguzi. Kwa sasa hatuwezi kueleza mtu huyo ni wa aina gani bali tunaweza kukisia tu kwamba anaweza kuwa amevaa kinyago ili kuficha sura yake halisi.”
“Kwa hiyo kinyago ndicho kilichochinjwa?”
“Inaweza kuwa kinyago hicho kiko katika muundo huo wa kuchinjwa.”
Almasi hakuuliza kitu tena mpaka alipoambiwa na Inspekta Amour.
“Mnaweza kwenda kuuchukua mwili wa marehemu mtakapohitaji kufanya hivyo kuanzia saa sita mchana.”
“Sawa.”
“Kwa mara nyingine ninawapa pole na ninawaomba muwe na moyo wa subira katika kipindi hiki cha msiba.”
Baada ya hapo Amour alimruhusu Almasi kuondoka.
Shughuli za mazishi zilifanyika nyumbani kwa Almasi siku iliyofuata.
Mwili wa James ulizikwa saa kumi jioni pembezoni mwa mahali alipozikwa kaka yake.
Usiku wa siku hiyo Almasi aliwaita wanawe waliobaki ambao walikuwa ni John, Alex na Benjamin.
“Miezi michache iliyopita tulimzika kaka yenu wa kwanza na leo tumemaliza kumzika kaka yenu wa pili. Sijui ni kwanini majambazi wametuandama sisi!” Almasi aliwambia wanawe.
“Labda wameona sisi ni matajiri sana?’ Benjamin akasema.
“Tuna utajiri gani wa kumshinda Bujuala anayemiliki viwanda vya saruji au tuna utajri gani wa kumshinda mfanyabiashara Marshal anayeingiza malori mia tano aina ya Scania kutoka Ulaya! Mimi sioni kama tuna utajiri wa kuwashinda watu hao lakini nashangaa kwamba majambazi wameniona mimi!”
“Tukio lile la kaka Martin na lile la juzi yana tofauti. Majambazi walimuua kaka na kumpora mamilioni ya pesa. Lakini kaka John ameuawa na kilichoibiwa hakijulikani!” Akasema Alex.
“Si wamepora masanduku yake.” Benjamin akamjibu.
“Sidhani kama wale majambazi walikuja nyumbani kwa kaka kufuata yale masanduku.”
“Kwanini hudhani wakati ndio waliyoyaiba baada ya kumuua?” Alex akamuuliza.