KISIWA CHAMAUTI - 34
ILIPOISHIA
“Kumbe na sisi tungekuja kufa!” Mzanzibari naye aling’aka.
“Ndiyo maana niliwambia mwanzo kuwa mshukuru kwa kufika katika kisiwa hiki katika kipindi cha usalama” Yasmin akawambia.
“Sasa kule nyumbani Comoro wanajua uko wapi?” Yule Mzanzibari alendelea kumuuliza Yasmin.
“Wao hawajui niko wapi na kwa sasa wanaamini kuwa nimeshakufa”
SASA ENDELEA...
“Je, wakikuona tena itakuwaje?”
“Itakuwa mshangao mkubwa. Wazazi wangu hawataamini.”
“Ni mkasa wa kutisha kweli na unastahili kuandikwa katika historia ya Comoro.”
“Hapo ni kama tutanusurika na nitarudi kwetu, kwani kama nilivyowambia mwanzo, hapa hatutarajii kupata msaada wowote. Hatima yetu tumemwachia Mwenyezi Mungu.”
Wakati tunazungumza, tulikuwa tumeshaondoka katika ile nyumba aliyouawa Shazume na tulikuwa tunaelekea ufukweni mwa bahari. Tulipofika ufukweni, Yasmin akataka tukae kidogo tupumzike, kwani tulikuwa tumetembea mwendo mrefu.
“Tangu niletwe katika kisiwa hiki, nyinyi ni wageni wangu wa pili kufika hapa,” Yasmin aliwaambia wale watu wakati tumeketi.
“Wa kwanza walikuwa kina nani?” Mzanzibari akamuuliza.
“Wa kwanza walikuwa ni hao watu saba ambao waliuawa na Harishi na kubaki mtu mmoja mliyenikuta naye.”
Yasmin alinionyesha mimi.
“Ulikuwa unakula nini?”
“Harishi alikuwa akiniletea chakula.”
“Yeye alikuwa anakipata wapi?”
“Anaiba kwenye masoko. Harishi ni mwizi na anatembea sehemu nyingi kuanzia kwetu Comoro hadi Afrika Mashariki.”
Tulikaa pale ufukweni tukazungumza na wale wageni hadi Yasmin aliposema kuwa anahitaji kurudi nyumbani.
Wakati tunarudi, yule Mzanzibari aliyekuwa pamoja na wale wazungu alituambia kuwa boti waliyokuwa wakitalii nayo ilipopigwa na dharuba, waliweza kupiga simu Zanzibar kuomba msaada, lakini baadaye mawasiliano yalikatika.
“Boti ya polisi wanamaji inaweza kuwa inatutafuta baharini,” akatuambia.
“Lakini haitawapata, mmeshafika huku,” Yasmin akamwambia.
“Ni vizuri kama tungeendelea kukaa ufukweni ili tuangalie vyombo vinavyopita. Tunaweza kuwaona.”
“Sawa. Mnaweza kwenda kukaa. Tutawafuata baadaye.”
Mzanzibari huyo alizungumza na wale wazungu na kukubaliana kuwa wabaki kule kule ufukweni. Tukawaacha na kurudi kwenye lile jumba.
“Unajua ni kwa nini nimetaka turudi?” Yasmin akaniuliza.
“Sijui.”
“Ninataka kupika.”
“Ukipika tutawapelekea chakula na wale jamaa?”
“Tutawapelekea. Wameshakuwa wageni wetu.”
“Nilitaka kujua hilo tu.”
“Jibu umeshalipata?”
“Nimelipata.”
“Sawa.”
Yasmin akaanza kushughulika. Baada ya masaa mawili akawa ameshaivisha wali na mboga ya uyoga.
“Unaonaje ukaenda kuwaita tuje tule nao hapa?” Yasmin akaniuliza.
“Ni sawa. Ngoja nikawaite.”
Nikatoka. Wakati nachanganya mwendo kuelekea ufukweni, nilisikia mlio wa helikopta. Ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kusikia mlio kama huo tangu tulipofika katika kisiwa hicho. Nikashituka na kutazama juu. Niliona helikopta ikipita chini chini. Ilinipita ikaendelea kwenda na kupotea mbele yangu.
Laiti ningekuwa na uwezo wa kuisimamisha, ningeisimamisha, lakini sikujua ningeisimamishaje. Nikabaki kuikodolea macho huku nikisikitika.
Mlio wa helikopta hiyo ulikuwa bado ukisikika masikioni mwangu. Ilikuwa kama inayozunguka kwenye hicho kisiwa. Ghafla nikausikia tena mlio huo ukitokea kwa nyuma yangu. Nikageuka na kuitazama. Ilinipita tena na kuendelea kuzunguka.
Ghafla, kwa mbele yangu, nikasikia kelele za watu zikitokea kwenye miti. Baadaye kidogo nikawaona wale wazungu pamoja na yule Mswahili wamevua mashati wakiifukuza ile helikopta huku wakiipungia mashati yao.
Ile helikopta ilirudi tena upande niliokuwa mimi. Sasa mwendo wake ulikuwa wa taratibu na ilikuwa chini chini sana. Ilitafuta sehemu iliyokuwa wazi ikatua. Kitendo cha kutua kwa helikopta hiyo kilinipa furaha na kunirudishia matumaini. Nikajua msaada umeshapatikana. Nilitaka nirudi mbio nikamchukue Yasmin, lakini naye alishausikia mlio wa helikopta hiyo. Alitoka na kuja mbio.
Ndani ya ile helikopta walishuka watu watatu. Mmoja alikuwa na mavazi ya kipolisi, lakini sikuweza kujua alikuwa polisi wa wapi na pia sikuweza kujua ile helikopta ilitokea wapi na ilikuwa inatafuta nini kwenye kile kisiwa.
Watu hao waliposhuka, walitutazama. Yule polisi akauliza.
“Ninyi ndio ambao mliripoti kuwa chombo chenu kinazama?” Alikuwa akimtazama yule Mzanzibari aliyekuwa amevua shati pamoja na wale wazungu.
“Ndiyo, sisi,” Mzanzibari huyo akajibu haraka.
“Na hao watalii wa Kifaransa ndio hawa mabwana?”
Aliwaonyesha wale wazungu.
“Ndiyo, hawa niliokuwa nao kwenye boti. Tuliogelea hadi kwenye kisiwa hiki.”
“Tumezunguka sana baharini kuwatafuta bila mafanikio. Huku tulikuja kubahatisha tu, ndio tunaona watu wanatupungia. Poleni sana.”
“Tunashukuru sana kwa msaada wenu.”
“Tuliambiwa mlikuwa watu watatu, na hawa watu wengine ni kina nani?”
“Ndiyo wenyeji wetu tuliowakuta hapa kisiwani, hakuna watu wengine.”
“Ninachofahamu mimi ni kuwa hiki kisiwa kilihamwa na watu. Sasa hawa wametokea wapi?”
“Wametueleza habari ya kusisimua sana. Huyu msichana ni binti wa Rais wa Comoro. Aliletwa katika kisiwa hiki katika mazingira ya kutatanisha, mwenyewe akiwa hajifahamu. Na ameishi hapa kwa zaidi ya mwaka mmoja akiwa peke yake.”
Watu hao watatu waliotoka kwenye helikopta walipatwa na mshangao waliposikia habari ile.
“Eti ni kweli?” Yule polisi akaniuliza.
“Ni kweli,” Yasmin akamjibu.
“Wewe ni binti wa Rais wa Comoro?”
“Ndiyo.”
“Ulifikaje katika kisiwa hiki kisichokuwa na watu na ulikuwa unaishije?”
Yasmin akaeleza kisa chake kuanzia alivyokumbwa na Harishi katika siku ya harusi yake hadi kuletwa katika kisiwa kile.
Akaeleza jinsi alivyokuwa anaishi.
“Wageni wangu wa kwanza kufika katika kisiwa hiki ni huyu kaka na wenzake.”
Alinionyesha mimi.
“Wenzake wote waliuawa na Harishi na kubaki yeye peke yake. Siku yake ya kuuawa ilikuwa ni leo, lakini Mungu mkubwa, amenusurika,” Yasmin akaeleza.
Alieleza tukio zima la kumfungia Harishi kwenye chupa lililotokea usiku uliopita.
“Hatukudhani kuwa ungekuwa mwisho wake. Sisi sote tulikuwa tumeshapanga kufa.”
“Sasa ikawaje?” Polisi aliendelea kumuuliza kwa shauku.
“Harishi alishindwa kutoka ndani ya chupa na leo asubuhi tukaenda kuizamisha baharini.”
“Ni habari kubwa na ya kushangaza kwa kweli. Unaweza kwenda kutuonyesha nyumba uliyokuwa unaishi?”
“Ninaweza. Twendeni.”
Yasmin akaliongoza kundi hilo la watu kuelekea katika lile jumba alilokuwa anakaa.
Watu hao waliingia ndani na kujionea jumba hilo lilivyokuwa. Yasmin aliwatembeza sehemu zote za jumba hilo hadi katika chumba alichokuwa analala.
Watu hao walimpa pole na kumsifu kuwa alikuwa msichana jasiri aliyeweza kuishi katika mazingira kama yale.
“Leo imekuwa ni siku yako ya uokozi, wewe na mwenzako,” polisi aliyetoka kwenye helikopta alimwambia na kuongeza.
“Washukuru hawa watalii ambao chombo chao kilizama, kwani wao ndio sababu ya sisi kufika hapa na kuwagundua nyinyi.”
“Nawashukuru nyote kwa jumla, hawa watalii na nyinyi mliokuja kutuokoa,” Yasmin akawambia watu hao huku akitabasamu.
“Sasa twendeni tukajipakie tuondoke,” polisi huyo akatuambia.
Yasmin akanitazama.
“Hatutakula tena?” akaniuliza.
“Hata njaa yenyewe siioni, kwani wewe unahitaji tena kula?”
“Basi, ngojeeni nibadili hizi nguo zangu.”
Yasmin akaingia chumbani kwake haraka. Yule polisi akawambia wenzake.
“Unaona kama alikuwa anaishi maisha ya kawaida, kumbe alikuwa katika mazingira magumu.”
“Ameyazoea,” yule Mzanzibari akasema.
“Na pia ni jasiri sana,” na mimi nikatia kauli. “Mimi nimekaa hapa kwa siku chache tu, lakini nimeshachoka. Inakuwaje kwa yeye aliyekaa kwa zaidi ya mwaka?”
Wote wakatikisa vichwa.
Baada ya robo saa hivi, Yasmin alitoka. Alikuwa amebadili nguo na kuvaa vazi jingine lililokuwa limempendeza na kufanya aonekane kama malkia. Vazi hilo lilikuwa ni moja ya mavazi aliyokuwa akiletewa na Harishi. Alikuwa amejitia manukato yaliyokuwa yakinukia vizuri na nywele zake aliziweka katika mtindo wa Kikomoro.
Alikuwa ameshika mkoba wa kike mkono mmoja na mkono mwingine alishika begi kama msafiri.
“Hili vazi umelipata wapi?” Yule polisi akamuuliza.
“Nililipata kutoka kwa huyo jini. Alikuwa akiniletea nguo.”
“Na hilo begi na huo mkoba?”
“Vyote.”
Watu wote wakatazamana kwa mshangao.
Tulitoka katika lile jumba. Wakati tunatoka, Yasmin aligeuka nyuma akalitazama jumba hilo kwa mara ya mwisho. Sikujua alikuwa akiwaza nini. Baada ya kulitazama kwa sekunde chache, aligeuka mbele na kuendelea na safari.
“Lete begi nikusaidie,” nikamwambia.
Nilimpokea begi. Lilikuwa zito kiasi.
“Umetia nini?” nikamuuliza.
“Mna vitu vyangu.”
“Umeamua kuondoka navyo?”
“Nataka wazazi wangu wakavione.”
“Naamini watafurahi kukuona.”
“Na mimi nitafurahi kuwaona.”
Tulifika mahali ilipoachwa helikopta. Rubani akatufundisha jinsi ya kujipakia kwenye helikopta.
“Mnapotaka kupanda helikopta mnainama namna hii ili kukwepa mapangaboi na hata wakati wa kushuka mnainama,” akatuambia huku akituonyesha jinsi ya kuinama.
Yasmin ndiye aliyetakiwa ajipakie kwanza. Baada ya Yasmin kujipakia, tulifuatia sisi.