Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KISIWA CHAMAUTI - 30

KISIWA 29 Pict

ILIPOISHIA

Wakati tumepumzika Shazume akawa anahimiza tuondoke.

“Tumeshakunywa uji sasa tunaweza kwenda”

“Tusubiri kidogo nifikirie pa kuwapeleka” Yasmin akamwambia.

Baada ya kusubiri kwa muda kidogo Yasmin akatuambia. “Haya twendeni tukatafute nyumba nyingine”

Tukatoka na Yasmin. Niliona wazi kuwa Yasmin alikuwa na wasiwasi. Alikuwa akitupeleka katika nyumba nyingine lakini hakuwa mtu aliyeonesha matumaini.

SASA ENDELEA...


Tulizunguka sana kutafuta nyumba nyingine ambayo ingeweza kutufaa kumkwepa Harishi. Tulikuta nyumba moja iliyokuwa ufukweni mwa bahari, iliyokuwa na hali nzuri kidogo.

“Mnaionaje nyumba hii?” Yasmin akatuuliza huku akituonyesha nyumba hiyo.

“Hii inafaa,” nikamwambia, kisha nikamtazama Shazume ili nipate mawazo yake.

“Unaionaje, Shazume?”

“Hapa pamejificha kidogo, panafaa,” akaniambia, ingawa sauti yake haikuwa na nguvu.

Tukaingia katika ile nyumba. Humo ndani ilikuwa kama stoo iliyosahauliwa. Vitu vilikuwa vimerundikwa ovyo. Ubuibui na vumbi vilikuwa vimetanda pande zote.

Binadamu mwenye akili zake timamu asingeweza kukaa ndani ya nyumba ile, labda wadudu kama vile nyoka na tandu. Lakini sisi hatukuwa timamu. Tulikuwa tumetingwa. Tungeweza kukaa.

Kama tungehitaji kufanya usafi ili nyumba hiyo iweze kukalika, tungelazimika kutoa nje vitu vyote vilivyokuwa ndani na kuanza kufagia, kupiga deki na kusafisha kuta. Ingekuwa kazi kubwa. Ingetuchukua hata siku mbili.

Tuliingia katika chumba kimoja, tukatenga vitu na kupata upenyu mdogo ambao tuliusafisha na kuamua kukaa hapo.

Kusema kweli, siku ile sisi sote hatukuwa na furaha. Tulikaa chini pamoja na Yasmin. Tukawa kimya. Kila mtu akiwaza lake.

Mimi nilikuwa nikiomba usiku usifike, kwani karibu wenzetu wote waliuawa usiku.

Sikujua Yasmin na Shazume walikuwa wakiwaza nini. Lakini kila nilivyomuangalia Shazume, niliona mawazo yake yalikuwa mbali sana. Nilikisia kwamba alikuwa akikumbuka kwao Pemba, akiwakumbuka wazazi wake na ndugu zake. Pengine hakuwa na matumaini ya kuwaona tena.

Bila shaka Yasmin alikuwa akiwaza kwamba kama tutauawa, atakosa wenzake wa kuzungumza nao na ataendelea kuwa mkiwa.

Mimi, licha ya kuwa na hofu, nilishajitolea kufa kupona. Sikupenda kujipa tamaa moja kwa moja kuwa nitapona na sikutaka kujikatisha tamaa.

Ghafla Shazume akaanza kuimba kwa sauti ya huzuni. Ulikuwa wimbo maarufu uliokuwa ukiimbwa na vikundi vya ngoma za kiasili.

“We Yauledi, we niletee mashua twende Unguja! We Yauledi, niletee mashua twende Unguja!”

Na mimi nikamuitikia. “Ukipamba mke nawe ujipambe, ndiyo suna. Usipojipamba watu hukwambia umetumwa! We Yauledi, niletee mashua twende Unguja!”

Shazume aliendelea kuimba ubeti wake kwa kughani, huku na mimi nikimuitikia.

Sauti ya wimbo huo ilikuwa ya huzuni, lakini ilituchangamsha. Yasmin alikuwa akitutazama. Wakati ninamuitikia Shazume, Yasmin alikuwa akinifuatisha ninavyoimba.

Pengine tulikuwa tunajifariji kwa siku yetu ya mwisho, kwani tangu tufike katika kisiwa kile, kila siku mwenzetu mmoja aliuawa na Harishi. Hakukuwa na siku yoyote ambayo hakukutokea kifo.

Kwa hiyo, hatukujua usiku wa siku ile atakufa nani kati yangu na Shazume.

Shazume aliendelea kuimba kwa huzuni. Mimi nilikuwa nimenyamaza. Yasmin akawa anamuitikia.

Shazume alipoona mimi nimenyamaza, na yeye akaacha kuimba, tukawa kimya. Baada ya muda kidogo, nilipata wazo.

“Tuombeni dua,” nikawaambia wenzangu.

“Tulikuwa tumejisahau kidogo,” Shazume akasema.

Nikasoma dua ndefu. Shazume na Yasmin wakawa wanaitikia, “Amin.”

Nilipomaliza, nilimwambia Shazume aombe na yeye. Shazume akaomba dua ndefu, sisi tukamuitikia, “Amin.”

Alipomaliza, nikamwambia Yasmin, “Omba na wewe.”

Yasmin naye akaomba dua.

Kwa muda wa nusu saa hivi, mahali hapo pakawa kama madarasa kutokana na kurindima visomo vyetu vya dua.

“Pia tungekuwa tunaswali,” Shazume akatukumbusha.

Siku zote binadamu humkumbuka sana Mola wake pale anapofikwa na matatizo. Siku zote hizo tulikuwa hatukumbuki kuswali, ila ni kwa siku ile ambayo tuliona tutamalizika.

“Pia ilitakiwa leo tufunge,” na mimi nikawakumbusha.

“Ni kweli,” Shazume akanikubalia na kuongeza, “Lakini tumeshakunywa uji.”

“Kama tutanusurika leo, tutafunga kesho. Umesikia, Yasmin?”

“Nimesikia,” Yasmin akanijibu.

“Sasa sisi hatuko tohara, tutaswali vipi?” nikawauliza wenzangu.

“Twendeni tukaoge baharini, tujitoharishe,” Shazume akasema.

“Hizi nguo zetu pia hazina tohara.”

“Tuoge na nguo zetu ziweze kutoharika, zikikauka tutaswali.”

Tukakubaliana.

Tukaamua sasa twende baharini tukaoge. Tukaenda sote watatu, mimi, Shazume na Yasmin. Yasmin alipotuona sisi tunajitosa kwenye maji, na yeye akajitosa. Tukawa tunaoga na kuogelea pamoja.

Tuliendelea kukaa kwenye maji kwa muda kidogo ili kujisahaulisha matatizo yaliyokuwa yanatukabili.

Asubuhi ile maji yalikuwa matamu kwa mtu ambaye alikusudia aogelee kwa starehe, ila kwa sisi ilikuwa starehe ya kujilazimisha. Mawazo mabaya yalituepuka kwa muda, yakitusubiri tumalize kuogelea.

Tulitamani tusitoke ndani ya maji, lakini nilipomuona Yasmin, aliyekuwa akiogelea karibu yangu, anarudi ufukweni, na mimi nikaamua kurudi.

Tukakaa ufukweni na kumsubiri Shazume. Naye alipotuona tumerudi ufukweni, akatufuata.

Tukakaa kuota jua. Nguo zetu zilikuwa zimetota. Kitendo cha kuogelea na nguo zetu hakikuwa cha maana sana, kwani mzizimo ungeweza kutuletea madhara ya kiafya, lakini hatukuwa na la kufanya.

Yasmin, ambaye alikuwa na nguo za kubadili alizokuwa akiletewa na Harishi, alikuwa akifuata mkumbo tu. Haikumpasa aloweshe nguo zake, ila alipotuona sisi tunaoga, na yeye akajitosa.

Tulikaa kwa muda kwenye ufukwe tukiangalia bahari na ndege waliokuwa wakiruka-ruka. Ili miili yetu isisinyae, tuliamua kufanya mazoezi ya kukimbizana.

Tulikimbizana mpaka tulipochoka, tukarudi kwenye ile nyumba. Tukapanga kwamba itakapofika saa saba, tuanze kuswali swala ya adhuhuri. Yasmin alituaga, akatuambia kuwa anakwenda kupika chakula cha mchana.

Kwa mustakabali wetu, tatizo la chakula halikuwepo. Chakula kilikuwepo kwa Yasmin.

Tatizo lilikuwa ni la kuuliwa na Harishi. Kama si tatizo hilo, mahali pale pangekuwa pazuri pa kuishi. Sikuvutika na kisiwa hicho pekee, bali pia nilivutika na Yasmin. Nilifarijika sana kuona jinsi alivyokuwa akitupa moyo na matumaini, japokuwa hali ilikuwa tete.

Baada ya Yasmin kuondoka, tuliendelea kukaa, hatimaye tukapitiwa na usingizi.

Tulipokuja kuamka, yalikuwa majira ya saa nane. Tukaenda kutawadha kwenye maji ya bahari na kuswali swala ya adhuhuri.

Yasmin alikuja saa tisa akiwa amechukua kapu la chakula. Alikuwa amebadili nguo zake na kuvaa mavazi mengine.

“Mmepauka kwa chumvi. Mnasikitisha sana, kaka zangu,” akatuambia.

“Ndiyo hivyo, tutafanyaje sasa?” nikamwambia huku nikimpokea lile kapu.

“Mmeshaswali?” akatuuliza.

“Tumeswali. Na wewe umeswali?” Na mimi nikamuuliza.

“Mimi naswali kila siku kuomba nusura na kuwaombea na nyinyi. Sijui kama nyinyi mmekumbuka kuniombea.”

“Tumekuombea,” nikamdanganya. Tulikuwa tumemsahau.

“Mngesema mmesahau kuniombea, ningejua hamnipendi.”

“Tunakupenda sana. Umetuletea chakula gani?”

“Wali.”

“Roho zetu zimekinai, hatutamani hata kula,” Shazume akasema.

“Shazume, unaanza maneno yako!” Yasmin akamwambia Shazume.

“Unafikiri nakudanganya? Mimi sina hamu ya kula kabisa.”

“Mbona juzi na jana ulikuwa unakula?”

“Nilikuwa na matumaini.”

“Si vizuri hivyo. Kuleni, japokuwa kidogo, mpate nguvu. Mkiacha kula, mtakuwa mnajitesa wenyewe. Mimi pia sikula. Nimekuja huku nile na nyinyi.”

Yasmin alitoa kile chakula akakiweka chini. Akatoa tasa la maji, tukaosha mikono, kisha tukaanza kula.

Mimi pia sikuwa na hamu ya kula, lakini nilikula kumridhisha Yasmin.

Tuliendelea kula kidogo kidogo hadi Shazume alipomuuliza Yasmin.

“Yasmin, ukibaki peke yako itakuwaje?”

“Hatuombei hivyo. Tuombee tubaki sote. Ukiomba dua, uweke matumaini, isiwe unakata tamaa.”

“Ni kweli. Yasmin, huwezi kuomba kitu bila kukiwekea matumaini. Kama huna matumaini na kitu hicho, kwa nini unakiomba?” nikasema.

Shazume akaguna.

“Pamoja na kuomba kwetu, bado naona wakati wetu umekaribia sana,” Shazume akasema kwa hali ile ile ya kukata tamaa.

“Shazume, usiseme hivyo. Mnaweza kunusurika. Harishi ni kiumbe kama nyinyi.”

“Lakini mwenzetu amepewa uwezo.”

Yasmin naye akaguna. Pakawa kimya. Yasmin ndiye aliyeutanzua ukimya huo alipotuambia, “Jamani, tukinusurika nitawachukua Comoro. Nitamwambia baba yangu nyinyi ni ndugu zangu wa damu. Mtaenziwa kama watoto wa rais.”

“Sidhani kama hapa ni karibu na kwenu Comoro. Mimi nadhani kama tutapata msaada wa kuokolewa, tutapelekwa kwanza Zanzibar,” nikasema.

“Si vibaya, Zanzibar pia ni nyumbani, lakini baba akipata habari atatuma ndege siku hiyo hiyo ituchukue pamoja na nyinyi.”

“Itakuwa raha sana tukienda Comoro na kupokewa na rais,” nikasema.

Shazume alikuwa kimya akitusikiliza. Bila shaka alikuwa anaona tunajidanganya kujifariji. Kwa mawazo yake, sisi tulikuwa ni wa kufa tu.

“Si unajua mzazi aliyekwishamkatia tamaa mwanawe, halafu anaambiwa amepatikana, atafurahije?” Yasmin akaniuliza.