Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KISIWA CHA MAUTI – Sehemu ya 2

KISIWA Pict

KWA KIFUPI

“Wewe una ushahidi gani kuwa hizo nyumba ulizotaja ni zake?”

“Aliwahi kuniambia mwenyewe na aliwahi kunionesha baadhi ya hati za nyumba hizo zikiwa na jina lake”

“Na  hizo hoteli ulizosema ni zipi?”

“Moja ni New Star. Ipo Masaki. Nyingine pia inaitwa hivyo hivyo ipo Kibaha. Mwanza anazo hoteli mbili. Hizo hoteli zote nilishafika na nilishalala”

SASA ENDELEA...


Nilinyamaza kidogo nikawaza, kisha nikamuuliza.

“Sasa wewe ulitaka nini?”

“Nilitaka hizi habari ziandikwe kwenye gazeti.”

“Kwamba anamiliki mali nyingi ambazo hazilingani na mshahara aliokuwa akiupata?”

“Ndiyo.”

“Unajua kuna kazi kubwa ya kuthibitisha kwamba hizi mali ulizotaja ni zake?”

“Ni zake?”

“Wewe unajua kwamba ni zake, lakini yeye anaweza kukataa. Lazima na sisi tuwe na vigezo vya kuonyesha kwamba ni kweli mali hizo ni zake.”

“Sasa vitafute wewe. Mimi nimeshakupa kazi.”

“Ulisema kwamba mke wake wa kwanza aliachana naye?”

“Ndiyo, aliachana naye.”

“Wewe unamfahamu vizuri?”

“Nilikuwa namfahamu, lakini alishakufa.”

“Kumbe alishakufa?”

“Alikufa, na kifo chake pia kilikuwa cha utata. Yule mama, baada ya kuachwa, alifungua kesi mahakamani ya kudai kugawana mali. Alikuwa ameorodhesha mali zote za Makita. Kabla ya tarehe iliyopangwa kusikilizwa kesi hiyo, gari la yule mama lilipinduka pale Chalinze. Alikuwa anakwenda Morogoro. Yule mama alikufa hapo hapo. Lakini mwili wake ulipochunguzwa, ulikutwa na tundu la risasi ya bastola kichwani. Dereva wake alitoweka mpaka leo hajulikani alipo.”

Ile habari ilinishitua kidogo. Nikamuuliza.

“Una maana kwamba aliuawa?”

“Aliuawa. Ile ajali ilikuwa geresha tu, halafu dereva wake aliyekuwa akimuendesha alikimbia. Hajapatikana.”

“Atakuwa anahusika na kifo chake kwa namna moja au nyingine. Sasa ile kesi yake ikawaje?”

“Kesi haikuweza kuendelea tena kwa sababu mlalamikaji hayupo. Wakili wa yule mama naye alijitoa kwenye kesi hiyo.”

“Makita hakuwahi kuitwa mahakamani?”

“Hakuwahi, na wakati yule mama anakufa yeye alikuwa Marekani.”

“Lakini wewe ulikuwa naye kiuhusiano?”

“Ndiyo, tulikuwa tumeshaanzana.”

“Uligundua nini au Makita alikueleza nini kuhusu tukio hilo?”

“Makita aliniambia kwamba huenda mtalaka wake huyo aliuawa na dereva wake kwa sababu zao wenyewe.”

“Na kuhusu ile kesi alikwambia nini?”

“Kwanza hakutaka nijue lolote kuhusu kesi hiyo. Nilichofahamu ni kuwa yule mama alikuwa amempa nyumba moja pale Sinza ambayo hivi sasa anaishi kijana mmoja ambaye ni mtoto wa dada yake anayeitwa Kabwe.”

“Hiyo nyumba unaifahamu?”

“Ninaifahamu.”

“Huyo mama hakuwa na mtoto?”

“Hakuwahi kuzaa.”

Baada ya ukimya mfupi nikamwambia yule msichana:

“Kunahitajika uchunguzi kidogo ili tuweze kuipata hii habari vizuri. Kwa hiyo acha nifanye huo uchunguzi. Nikiona nimepata vigezo ninavyovihitaji, sitasita kuiandika, ila ujue kuwa nitahitaji ushirikiano wako.”

“Unadhani itachukua muda gani?”

“Usijali muda. Hii habari imeingia mikononi mwangu, acha niifanyie kazi, lakini tutaendelea kuwasiliana. Sawa?”

“Sawa.”

Nikainuka.

“Sasa dada yangu, acha nirudi. Jua limechwa sana.”

“Utanisamehe, sijakupa hata soda kaka yangu,” msichana akaniambia huku naye akiinuka.

“Soda ya nini wakati nipo kazini, dada yangu?”

“Nitakukaribisha siku nyingine utakayokuja kunitembelea. Kwa vile nyumba umeshaijua, naamini utakuja tu siku yoyote.”

Tulikuwa tumeshatoka nje ya ile nyumba. Msichana huyo aliwaambia wale wenzake kuwa ananisindikiza. Tukaondoka. Alinipitisha tena kwenye vichochoro.

“Huku siwezi kufika peke yangu. Lazima nitapotea tu,” nikamwambia.

“Siku utakapokuja, ukishuka kwenye daladala, nipigie simu. Nitakuja kukuchukua.”

“Labda iwe hivyo, lakini kwangu mwenyewe kuja huku itakuwa ngumu.”

“Tumetoka katika nyumba nzuri na maeneo mazuri, tumekuja huku.”

“Ndiyo maisha. Usijali. Unaweza kupata bwana mwingine akakurudisha Masaki, huwezi kujua.”

Nilipomwambia hivyo msichana alicheka sana.

“Hivi nilivyokwisha, kweli naweza kupata mwanaume wa kuniweka Masaki?” akaniuliza.

“Unaweza. Mbona bado uko vizuri tu?”

“Kweli?”

“Wasiwasi wako tu. Bado uko vizuri.”

“Basi niombee nimpate huyo mwanaume anayeishi Masaki, lakini kwanza nataka hili suala la huyu mtu tulimalize.”

“Hili litamalizika tu. Subiri tulifanyie kazi.”

“Sawa. Nitashukuru sana.”

Msichana alinisindikiza hadi kwenye kituo cha daladala. Kwa bahati, wakati tunafika tu, daladala ilikuwa inapita. Nikaagana naye na kujipakia.

Nilipofika nyumbani kwangu Kinondoni, nilioga kisha nikapumzika kwenye kochi. Wakati huo ndipo nilipoanza kuyatafakari kwa kina maelezo ya yule msichana.

Baada ya kuyachambua, nikahisi ningeweza kuibua habari zaidi ya moja kama maelezo yake yangekuwa na ukweli.

Ili kupata huo ukweli, nikajiambia, ni lazima nifanye uchunguzi juu ya madai yake pamoja na mfululizo wa maelezo yake. Ikithibitika kuwa kuna ukweli, nitaibuka na habari ya maana sana.

Tangu nilipoanza kazi hii ya uandishi wa habari, nimejifunza kwamba kufanya uchunguzi unapopata habari ni jambo muhimu sana kuliko kukimbilia kuandika habari ambayo hujaifanyia utafiti. Mara nyingi matokeo yake ni kuja kufedheheshwa na wahusika na pengine kuburuzwa mahakamani.

Lakini mimi nilikuwa makini. Baadhi ya waandishi wenzangu walikuwa wanaona kama ninajipa kazi isiyo na umuhimu, kuifanyia uchunguzi habari kwa siku kadhaa.

Mwandishi mmoja aliwahi kuniambia kuwa kitu muhimu ni kuiwekea mizani habari yako, kwa maana kwamba nimfuate mlalamikiwa na kumweleza anacholalamikiwa. Eti yeye ndiye atakayeeleza kila kitu.

Niligundua kuwa bila kuwa na data kamili, mlalamikiwa anaweza kukutoa nje akajifanya hajui chochote. Na hapo utakuwa hujafichua kitu.

Mimi sikuwa hivyo. Nilishajifunza mengi kutokana na uzoefu wangu wa miaka michache. Mara nyingi sikuwa nikizingatia maadili tu, pia nilizingatia kuichunguza kwanza habari ninayoandika, hata kama itanichukua siku kadhaa. Nilipenda ninapotoa kitu kiwe cha uhakika.

Asubuhi ya siku iliyofuata, nilipofika ofisini, nikamweleza mhariri wangu kuhusu maelezo ya yule msichana.

Mhariri wangu, baada ya kunisikiliza kwa makini, alishituka.

“Kumbe yule bwana ana tuhuma nyingi! Kama alichokueleza huyo msichana ni ukweli mtupu, utakuwa na habari nzuri sana. Sasa wewe jaribu kuifanyia utafiti. Sijui itakuchukua siku ngapi?”

“Kiasi siku mbili au tatu tu, nitakuwa nimeshaupata ukweli wote.”

“Unadhani utahitaji kumpata nani na nani?”

“Kwanza nimefikiria nimpate huyo kijana anayeitwa Kabwe, nimuhoji. Nahisi atakuwa na mengi ya kunieleza kuhusu ile kesi ya mama yake mdogo.”

“Masha, huoni kwamba utajichanganya?”

“Sitajichanganya. Hizi zote ni habari na zinahusiana.”

“Sawa. Kwa hiyo nikuulize baada ya siku tatu?”

“Mimi mwenyewe nitakufahamisha ninavyoendelea.”

“Sasa utatoka muda huu?”

“Ndiyo, nitatoka kwenda kumuona yule kijana, lakini itabidi kwanza nimpigie Sofia ili anielekeze nyumba anayoishi huko Sinza.”

“Sawa. Shughulikia hilo suala.”

Nikaondoka ofisini kwa mhariri. Nikiwa katika chumba cha habari, nikampigia simu Sofia.

“Habari ya tangu jana, Sofia?” nikamsalimia mara tu alipopokea simu yangu.

“Nzuri, kaka Masha. Niambie?”

“Poa tu. Nilikuwa nataka kumuona yule kijana uliyeniambia anaitwa Kabwe ili nione kama atanipa maelezo zaidi kuhusiana na kesi ya mama yake mdogo ambaye alikuwa mke wa Makita.”

“Nilikwambia nyumba yenyewe iko Sinza. Sasa ngoja nikupe maelekezo…”

Sofia akanielekeza.

Dakika arobaini na tano baadaye, nikawa nimesimama mbele ya geti la nyumba moja iliyokuwa katika mtaa mmoja wa Sinza Mori, nyumba ambayo nilielekezwa na Sofia.

Baada ya kubisha geti hilo, nilisikia hatua za mtu aliyekuwa akija kulifungua. Nikadhani alikuwa Kabwe ambaye niliambiwa alikuwa akiishi katika nyumba hiyo.

Baada ya geti kufunguliwa, nilikutana na uso wa msichana mrembo aliyeonyesha wazi kunishangaa.

“Karibu,” akaniambia huku akinitazama kwa udadisi.

“Asante. Habari yako, dada yangu?”

“Nzuri. Unamtaka nani?”

Swali lake likanirahisishia kazi ya kumuuliza kijana niliyekuwa ninamtaka. Nikamwambia:

“Namuulizia Kabwe. Nafikiri anaishi hapa.”

“Ndiyo, anaishi hapa.”

“Yupo?”

“Yupo. Sijui nimwambie nani anamuulizia?”

Kabwe mwenyewe hatujuani! Hata nikimtajia jina langu hatanielewa. Hata hivyo, nikamjibu:

“Mwambie Masha.”

Msichana akafunga geti kisha akarudi ndani. Kitendo hicho kiliniudhi kidogo, ingawa kilikuwa cha kiusalama.

Nikasimama kwa karibu dakika tatu hivi kabla ya geti kufunguliwa tena. Aliyefungua geti alikuwa msichana yule yule.

“Anakwambia upite ndani,” akaniambia huku akinipisha kwenye mlango wa geti.