KISIWA CHA MAUTI - 16
ILIPOISHIA
Wakati nazungumza na Edda akaja yule mrakibu wa polisi na kuniita ofisini kwake.
Tulipoingia ofisini kwake akanikaribisha kwenye kiti. Muda ule sauti yake ilikuwa ni ya kawaida. Haikuwa kali kama ile aliyokuwa nayo juzi na jana yake. Bila shaka ni baada ya kuona sikuwa na kosa.
Akajidai kuniuliza.
“Wamekuachia saa ngapi?”
“Mimi sijui kama wameniachia” nikamwambia.
SASA ENDELEA...
“Si nimekukuta mbele ya Si nimekukuta mbele ya kaunta ya polisi unazungumza?”
“Nilitolewa mahabusi nikaambiwa nikae pale, lakini sikupata maelezo yoyote.”
Mrakibu akajidai kucheka.
“Ndiyo, umeachiwa hivyo. Kama bado ungekuwa mtuhumiwa, ungekuwa mahabusi.”
“Ilitakiwa nielezwe kama nimeachiwa na ikiwezekana nielezwe kwa nini nimeachiwa wakati nilikuwa mtuhumiwa wa mauaji.”
“Ni kweli. Kusema kweli, tulitaka kukuachia tangu jana usiku, lakini tulifikiria usiku huo tukikuachia utakwenda wapi. Tukaona tukuachie hii asubuhi,” Mrakibu akaniambia na kuongeza:
“Tumekuachia baada ya uchunguzi wetu kuonesha kuwa hukutenda kosa ulilokuwa unatuhumiwa, isipokuwa ulitengenezewa kesi na bosi wa ile hoteli akishirikiana na meneja wake.”
“Kwa hiyo mmeamini kuwa niliwekewa dawa ya kulevya kwenye bia?”
“Sasa tumeamini. Wale watu ni wabaya sana, na niliwagundua tangu jana. Kwanza walituambia aliyeuawa alikuwa Edda. Kwa bahati njema, Edda naye alifika hapa kituoni. Baadaye wanatuambia aliyeuawa ni mfanyakazi mwingine. Yaani wanatubabaisha, kumbe hakuna aliyeuawa. Wamekwenda kuiba maiti hospitalini….”
Mrakibu huyo aliposema aligundua tangu jana yake kuwa watu hao walikuwa waongo, sikubakiana naye. Mpaka hiyo jana alikuwa upande wao, akinikandamiza mimi.
Na ile ilikuwa ndiyo tabia ya baadhi ya polisi. Muda ule alikuwa anajikosha tu baada ya ukweli kubainika.
Wakati Mrakibu akinieleza hivyo, simu iliyokuwa juu ya meza yake ikaita. Akakiinua kiwiko cha kusemea na kukiweka mdomoni mwake.
“Hello! Central Police hapa, naweza kukusaidia.”
Akasikiliza kidogo kisha akasema:
“Ndiyo, tulishamuachia, lakini bado tunaye hapa.”
Ingawa sikuweza kujua ni nani aliyekuwa anaongea upande wa pili, niligundua kuwa nilikuwa ninaongelewa mimi.
“Sawa, afande,” Mrakibu huyo akasema baada ya kupata maelezo ambayo sikuweza kuyasikia, kisha akakirudisha kiwiko cha simu mahali pake.
“Hawa watu walikuwa wanajaribu kutumia mbinu chafu kukuzima, lakini kibao kimewageukia,” akaniambia kisha akainuka kwenye kiti.
“Twende tukaongee nje ya kituo.”
Sikuweza kujua ni kwa nini aliniambia vile. Nikahisi pengine ndivyo alivyoagizwa kwenye simu.
Tukatoka nje ya kituo. Nilimkuta Edda bado amekaa kwenye benchi akinisubiri.
Vile tunatoka tu, nikamuona mhariri wangu akishuka kwenye gari na kuchanganya mwendo kuja kwenye lango la kituo cha polisi. Aliponiona akaanza kutabasamu.
Alipotufikia alinipa mkono kisha akampa mkono Mrakibu wa polisi.
“Natumaini mko wazima?” akatuuliza.
“Kwa upande wangu namshukuru Mungu,” nikamwambia.
“Na mimi pia namshukuru Mungu,” Mrakibu naye akawambia.
“Natumaini mmeshamuachia mwandishi wangu?”
“Tumemuachia mapema sana,” Mrakibu akamjibu na kuongeza:
“Tulikuwa hapa nje tunapiga stori.”
“Kosa lenu polisi ni kwamba mlikubali kudanganyika,” Mhariri wangu akamueleza wazi Mrakibu wa polisi.
Mrakibu aliruka kimanga.
“Hapana. Sisi polisi hatuna kosa. Sisi kazi yetu ni kupokea malalamiko na kuyashughulikia. Mtu anapotuambia umeua, ni lazima tukukamate, tukuweke ndani kisha tuanze kuchunguza ilikuwaje.”
“Kama mimi nisingeandika hii habari kwenye gazeti la leo, mngemuachia kijana wangu?”
Mrakibu akajifanya hajui kilichoandikwa.
“Kwani mmeandika habari gani?”
“Una maana hamjasoma gazeti letu?”
“Bado sijasoma.”
Kama vile aligundua kuwa Mrakibu huyo hakuwa akisema ukweli, Mhariri wangu alicheka.
“Kama hujasoma, utakaposoma utaona tumeandika nini.”
Vile anavyomueleza hivyo, gari la polisi likasimama mbele ya kituo. Sote tukageuka na kulitazama.
Kwa namna ambayo ilitushitua, tukamuona Makita pamoja na meneja wake wakishushwa kutoka kwenye gari hilo. Wote wawili walikuwa wametiwa pingu kama wahalifu.
Wakati wanaongozwa na polisi sita kuelekea kwenye lango la kituo, Makita na meneja wake walitupa macho na kuniona, halafu wote wawili waligeuza macho haraka na kuyaelekeza walikokuwa wanapelekwa. Nilijua walikuwa wamepata aibu kuona nimewaona walivyokamatwa na kutiwa pingu.
“Mzee Makita, utanyea debe!” nikamwambia Makita kutokana na uchungu niliokuwa nao.
Makita hakugeuka, aliendelea kwenda akijifanya hakunisikia.
“Haifai, acha tu,” Mhariri wangu akanionya akidhani ningeendelea kumpakazia.
Makita na meneja wake wakaingizwa ndani ya kituo. Mrakibu wa polisi alikuwa anawatazama huku anatabasamu.
Edda alipowaona waliokuwa mabosi wake wakiingizwa kituoni aliinuka akatufuata.
Ndipo Mhariri wangu alipomuona.
“Oh, Edda! Kumbe upo?” akamuuliza.
“Nilikuwa nimekaa pale.”
Edda alionesha kwenye benchi alipokuwa ameketi.
“Nilikuwa sijakuona. Nakushukuru kwa mara nyingine kutokana na ushirikiano wako,” Mhariri alimwambia kisha akanitazama mimi.
“Jana nilikutana naye tukazungumza sana.”
“Nimeona kwenye gazeti,” nikamwambia.
“Oh, kumbe umesoma zile habari?”
“Nimesoma. Aliniletea yeye Edda. Alipokuja nilikuwa nimeshaachiwa.”
“Jana na juzi tulihangaika sana kutafuta ukweli wa hii habari. Tuliingiza gazeti mitamboni usiku mwingi kwa ajili yako.”
“Sasa kijana, njoo uchukue vitu vyako. Huna sababu tena ya kuwa hapa,” Mrakibu wa polisi akaniambia na kutangulia kuingia kituoni. Nikamfuata.
Alikwenda kunipa simu yangu, mkanda wa suruali na pesa zangu ambazo walizishikilia wakati wananiweka ndani.
“Leo tunakuruhusu, lakini kesho asubuhi utafika ili tuandikishe maelezo yako,” Mrakibu akaniambia.
“Maelezo mengine tena?”
“Yale uliyoandikisha jana uliyaandikisha kama mtuhumiwa. Kesho utaandikisha maelezo kama shahidi.”
“Sawa.”
“Sasa unaweza kwenda zako.”
“Asante.”
Nikajifunga mkanda wangu wa suruali kisha nikageuka na kutoka.
“Ulikwenda kupewa vitu gani?” Mhariri wangu akaniuliza nje ya kituo.
“Ni simu yangu na huu mkanda wa suruali. Walikuwa wamevishikilia wao.”
“Kuhusu ile pikipiki yetu wamesemaje?”
“Oh, nimeisahau.”
Nikarudi tena ofisini kwa Mrakibu wa polisi.
“Nimesahau pikipiki yangu.”
“Utapewa pikipiki yenu. Sisi hatuna kazi nayo.”
Mrakibu akainua mkono wa simu na kumuagiza polisi aliyepokea simu nipewe pikipiki yangu.
“Nenda, utapewa pikipiki yako.”
Nilitoka nje ya kituo. Baada ya muda kidogo pikipiki ikatolewa.
“Si unakuja ofisini au…?” Mhariri wangu akaniuliza nilipopewa pikipiki.
“Kwanza nakwenda nyumbani nioge, nibadili hizi nguo,” nikamwambia.
“Sawa. Basi mimi natangulia ofisini.”
“Sawa, tutakutana huko baadaye.”
Mhariri wangu akaenda kujipakia kwenye gari lake na kuondoka.
Nikamtazama Edda.
“Sasa inakuwaje?” nikamuuliza.
“Unataka kuondoka?”
“Sio kama nataka kuondoka. Nataka tuondoke.”
“Twende,” akaniambia.
Nikapanda pikipiki na kuiwasha.
“Kaa,” nikamwambia Edda ambaye alijipakia nyuma yangu.
Nikaenda naye nyumbani kwangu.
Wapangaji wenzangu waliponiona wakashangaa.
“Imekuwaje?” mpangaji mmoja akaniuliza.
Sikuona soni wala aibu kueleza yaliyonitokea. Wapangaji wengine wakajisogeza kunisikiliza na kunisikitikia.
“Kila kazi haikosi changamoto,” mpangaji mmoja akaniambia.
“Ni changamoto kubwa, lakini namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunivusha,” nikasema.
“Na huyo mzee inaelekea ni mshenzi kweli. Alitaka kukumaliza kabisa!” mpangaji mwingine akasema.
“Ushenzi wake umeishia mikononi mwa polisi. Waswahili wanasema mchimba shimo huingia mwenyewe. Ndio yeye.”
Baada ya kuzungumza na wapangaji hao nikaingia chumbani mwangu. Edda alikuwa ameshaingia akinisubiri humo ndani.
Kitu cha kwanza nilikwenda kuoga. Nilipotoka bafuni nilivaa nguo nyingine.
“Edda, ninachoweza kukwambia ni kuwa nakushukuru sana. Najua umepoteza kazi yako kwa ajili yangu, lakini kuna kitu kingine kizuri ambacho utakipata kwangu,” nikamwambia Edda baada ya kuvaa.
Nikatoa pochi yangu na kumpa Edda noti ya shilingi elfu kumi.
“Mimi narudi kazini. Haitafika saa kumi nitakuwa nimesharudi. Wewe nenda sokoni kanunue unachofikiria kwamba utakipika na tutakula mimi na wewe nitakaporudi. Sawa?”
“Una maana nitashinda hapa?”
“Ndiyo maana yake. Moyo wangu hautaki nikuache mapema.”
“Sawa. Nimekuelewa.”
Nikamuonesha Edda jiko lilipo, kabati la vyombo na vitu vingine ambavyo angehitaji kuvitumia akiwa hapo nyumbani.